Muendelezo wa Mgogoro wa Spika Na CAG

Mgogoro huu unaokuzwa ulianza kufuatia kauli ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutumia neno “udhaifu wa bunge” wakati akihojiwa na idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani.

Hatua hiyo ilipelekea Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai kumuamuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Assad kuhudhuria mbele ya Kamati ya Haki, Maadili, na Kinga ya Bunge mnamo tarehe 21/01/2019 kujibu tuhuma zinazomkabili za ‘kuivunjia heshima’ taasisi hiyo ya kutunga sheria kufuatia kauli yake hiyo ya kuwa Bunge ni dhaifu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mara baada ya kufanyika mahojiano hayo, Kamati ya Haki, Maadili, na Kinga ya Bunge iliwasilisha maamuzi yake mbele ya Bunge na hatimaye Bunge likaazimia kutofanya kazi na Profesa Mussa Assad 2/4/2019, ambapo Mwenyekiti wa kamati hiyo Emmanuel Mwakasaka alisema “Profesa Assad wakati akihojiwa na kamati yake, hakujutia kosa lake na alisema maneno aliyotumia ni ya uhasibu na ataendelea kuyatumia’(Mtanzania 3/04/2019)

Kuna sababu kadhaa zilizopelekea kuibuka suala hili, kiasi cha kukuzwa kuwa kama mgogoro. Kuibuliwa sakata la Sh trilioni 1.5 kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/2017, ambapo kiasi hicho cha pesa hakikuonekana matumizi yake. Aidha, Mbunge Catherine Ruge, wa viti maalumu kupitia Chadema mkoani Mara alidai ubadhirifu mwingine wa trilioni 2.4, ikiwa ni kiwango kikubwa kabisa cha ubadhirifu kutokea tangu uhuru. Hiyo ilikuwa ripoti ya pili ya Professa Assad tangu awe CAG, na ripoti ya kwanza katika kipindi cha awamu ya tano ya Raisi John Magufuli. Aidha, ripoti ya karibuni zaidi 2017/2018 nayo imefedhehi ubadhirifu na uvurugaji wa hali ya juu wa fedha za Umma ikiwemo mashirika ya Umma kuendeshwa kwa hasara kubwa nk. Haya yote yanafedhehi serikali hii ambayo ilikuja kifua mbele kwamba inapambana na ufisadi. Si ajabu ikawa suala la mgogoro huu kuchapuzwa sasa unalenga malengo mawili. Kumtia shinikizo CAG ili aachie ngazi kwa khiyari, kwa kuwa amekuwa mwiba mkali dhidi ya serikali. Au kusahaulisha mjadala mkubwa na nyeti juu ya ufisadi na ubadhirifu mkubwa unaofanywa na serikali uliowekwa wazi katika ripoti ya CAG ya karibuni.

Kwa upande mwengine, si ajabu Spika Ndugai anautumia mgogoro huu kibinafsi, na kuukuza ili kujipendekeza kwa chama na kwa raisi ili apewe fursa ya kubakia katika nafasi yake au walau kupata fursa ya kugombea tena ubunge. Kwa kuwa kuna dalili za Naibu Spika, Tulia Ackson kuandaliwa kuwa Spika na Mbunge wa Mbeya Mjini mwaka 2020. Hii inamfanya Spika Ndugai kujaribu kufanya kila awezalo kutetea kiti chake ambacho kina kila dalili za kumponyoka. Spika Ndugai kwa upande mwengine, ana sababu ya kuifurahisha ikulu kwa kupambana na CAG ikiwa ni kulipa fadhila kubwa aliyopatiwa. Kwa mujibu wa taarifa zisizo rasmi Spika Ndugai aligharamikiwa na ikulu miezi mitano nchini India kwa ajili ya matibabu yake, akiwa na wasaidizi wawili, yeye binafsi alikuwa akilipwa $500 kwa siku, huku wasaidizi wake wakilipwa $450. Hivyo, binafsi alitumia takribani 174,015,000/=Tsh, kiasi ambacho kinaonekana ni kikubwa.

Suala la udini haliwezi kuepukika katika qadhia hii. Tangu ameingia madarakani Raisi Magufuli ameonesha wazi chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Amebadilisha na kuwatoa madarakani wengi katika Waislamu. Profesa Assad kuwa Muislamu ukiongeza na hayo yote tuliyotaja juu anakuwa ni kikwazo kikubwa katika utawala huu wa awamu ya tano.

Katika mafunzo ya sakata hili ni fedheha ya demokrasia kwa kile kinachoitwa mgawanyo wa madaraka na uwajibishaji, kwamba ni urongo wa wazi unaolezwa kwa Ummah, kujaribu kuwaonesha kwamba vitu viwili hivyo (mgawanyo wa madaraka na uwajibishaji) kuwa ni miongoni mwa mihimili miwili muhimu ya demokrasia. Lau kama ndani ya demokrasia kungekuwa na mgawanyo huo wa madaraka na uwajibishaji kikweli, basi Spika angemuacha Mkaguzi na Mdhibiti afanye majukumu yake bila ya kuingiliwa.

Zaidi ya hayo, sakata hili pia linadhihirisha uwongo mwengine mkubwa katika demokrasia, nayo ni uwepo wa ‘uhuru wa maoni’ (kujieleza). Maoni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kuhusu kutowajibika na udhaifu wa Bunge yalipaswa kuchukuliwa kama maoni yake binafsi, ambapo Spika angepaswa kuyaheshimu kama maoni binafsi, na hasa kwa kuzingatia unyeti wa afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu.

Pia tunaona wazi wazi namna ufisadi ulivyokuwa saratani iliyokita katika nidhamu ya kidemokrasaia, na makeke ya kupambana nao ni maneno matupu bila ya vitendo. Katika miaka ya karibuni kumeshuhudiwa wimbi kubwa la matumizi ziada ya serikali kama ununuaji wa ndege mpya, matumizi ambayo yapo kando ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge ambayo yanaweka mwanya ziada wa ufisadi.

Udhaifu wa sheria za kutungwa na wanadamu pia unadhihirika. Hilo linazifanya sheria hizo kuwa na mapungufu makubwa kabisa na uwepo wa mgongano. Kwa qadhia hiii kwa upande mmoja Ibara ya 143(6) ya Katiba ya Tanzania inatamka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kwa namna yoyote hatofungika na amri au maelekezo ya mtu yoyote au Idara ya serikali…..”Lakini wakati huo huo sheria kuhusu Kinga, Maadili na Haki ya Bunge inampa mamlaka Spika kumwita yoyote kumuhoji, kwa kile alichokitamka kuhusiana na Bunge. Huu ni mkanganyiko wa hali ya juu unaotoa ishara kuwa mwanadamu ni dhaifu na hawezi kutunga sheria zenye ufanisi, na hivyo hana budi mwanadamu huyo ila kujisalimisha kwa sheria za Muumba.

Katika Uislamu, viongozi hawana sifa za kimalaika, huwajibika kusimamia na kuyaangalia mambo ya Ummah ipasavyo, ilhali raia wote wana haki ya kuwahesabu/ kuwawajibisha, na kuwaangazia kwa makini utendaji wa viongozi hao kwa mujibu wa sharia ili kuhakikisha wanasimama juu ya mstari imara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Risala ya Wiki No. 37
17 Sha’aban 1440 Hijri /23 Aprili 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.