Ramadhani Iko Mbali Na Dhihaka Za Wanademokrasia

بسم الله الرحمن الرحيم

Ramadhani tayari imeingia, kama kawaida tunashuhudia dhihaka na dharau za wanademokrasia kwa mgeni huyu adhimu na Uislamu kwa jumla. Viongozi wa kidemokrasia katika madola makubwa kama Uingereza, Marekani, Ufaransa, Canada nk. na ndani ya nchi changa kama kawaida yao hujifanya kupaza sauti zao ati kutuma salamu za kuwatakia Waislamu kheri ya kuingia Ramadhani.
Aidha, hata hapa petu tunawasikia wengi kutoa salamu za Ramadhani Kariim. Si hayo tu bali pia tutaona maandalizi ya futari kutoka kwa viongozi hao ati kwa ajili ya Waislamu.
Tunasema hii ni dhihaka, dharau na shere kubwa kwa Ummah wa Kiislamu na mfumo wake, kwa kuwa madola kama Marekani na washirika wake na hata wafuasi wao katika nchi changa kila dakika wako mbioni kuangamiza Ummah wa Kiislamu na mfumo wao. Iweje kuwatakia Waislamu kheri katika ibada ya Ramadhani ilhali kile kinachoilinda na kudhamini ladha ya Ramadhani ambacho ni dola ya Khilafah wanaipinga kurejea kwake kwa nguvu na gharama zote?
Waislamu pia kupewa salamu kutoka mabunge ya kidemokrasia ni jambo la kushangaza sana, kwa kuwa imani ya kisekula ya mabunge ya kidemokrasia inapingana moja kwa moja na aqida ya Kiislamu, hasa ukitilia maanani kuwa Ramadhani ni mwezi ulioshushwa muongozo (Quran) kwa watu wote. (huda li-nasi)
Mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kidemokrasia kamwe hauthamini, haujali wala hauheshimu na hautoheshimu mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wao na mfumo wao ndio huruhusu na kudhamini kila aina ya uchafu na ufuska katika ulimwengu hata ndani ya kipindi cha mwezi mtukufu
Tunashuhudia dhulma zao za kiuchumi, uvamizi wa biladi za Waislamu kama, Palestina, Syria, Iraq, Somalia, Sudan, Kashmiri nk. na kuunga mkono kwao vibaraka wanaoangamiza Waislamu kama ndani ya Turkistan ya Mashariki, Myanmar, Palestina, Sudan, Kashmiri nk. Mfano hai wa kuhuzunisha wa karibuni, ni Waislamu kuanza Ramadhani ndani ya Ghazza na maeneo mengine ndani ya Palestina ilhali kwa kipindi cha karibu miezi mitano Waislamu zaidi ya 30,000 wameshauwawa na zaidi ya 70,000 majeruhi huku misikiti zaidi ya 600 imevunjwa kwa mabomu.
Aidha, upinzani wa nchi za magharibi dhidi ya ujumbe wa Uislamu uko wazi wazi, wakijizatiti kwa kila aina ya vita kijeshi, kifikra, kithaqafa na kisheria ili kufikia lengo lao la kuizima kabisa nuru yake. Bila ya kusahau kuwa wao ndio wanaozuiya ulinganizi wa Uislamu kwa propaganda, kuuwa, kutesa, kupoteza na kuwasweka majela walinganizi mukhlisina kwa kisingizio cha sheria ya ubaguzi ya ‘kupambana na ugaidi’, na badala yake kuwatumia wakala wao waovu ambao huusaliti Uislamu kwa thamani duni ya maisha ya dunia.
Ibada ya Ramadhaani ni ibada tukufu yenye hadhi kubwa ndani ya Uislamu, haimaliziki tu katika kualikwa vyakula vitamu na wanademokrasia. Jambo hilo ni kinyume na ibada yenyewe, na pia ni kinyume na taarikh yetu tangu zama za Mtume SAAW, masahaba na wema waliofuatia. Wao waliuchukulia mwezi huu kuwa ni kipindi adhimu cha kukithirisha amali zote za kheri kuanzia swaum, sala za sunnah, usomaji wa Quran, kutoa sadaka, kufanya ulinganizi wa Uislamu, kupigana jihad dhidi ya makafiri na hata kufungua miji.
Ramadhani ndio mwezi wenye fungamano na jambo kubwa la msingi kwa ukombozi wa mwanadamu kwa kuanza ndani yake kushuka wahyi kwa Mtume SAAW. Kubwa zaidi pia Ramadhani ikateuliwa na Allah SW kuwa ndio mwezi wa kushushwa muongozo wa Quran kutoka Bait-ul izzah mpaka kufikia wingu wa dunia. Kisha Quran kushushwa kidogo kidogo kufuatia matukio na minasaba mbalimbali kwa muda wa miaka 23 kupitia Mtume SAAW ili kwa muongozo huo awaongoze wanadamu wote.
Waislamu tuna wajibu wa kuchukua hadhari kubwa na mbinu na hadaa za maadui wa Uislamu ambazo ni hatari kwa Uislamu wetu na fikra zake. Aidha, tudharau na kufedhehi dhihaka za mfumo wa kibepari na wafuasi wake. Bali tuzidishe shauku yetu kwa mgeni huyu mtukufu (Ramadhani) na kuyakumbatia kwa mikono miwili aliyokuja nayo kuanzia thamani ya kinafsia na ya kisiasa.
Na mwisho tukumbuke tuna jukumu kubwa la kulingania Uislamu kwa jitihada kubwa ili kuleta mageuzi kwa msingi wa Uislamu, ili mwaka ujao mgeni huyu Insha Allah apokewe na mwenyeji wa kheri, yaani dola ya Kiislamu ya Khilafah ambaye ndie mlinzi wa matukufu yote ya Kiislamu na Waislamu.
Abdullah Juma
Risala ya Wiki No. 171
2 Ramadhan 1445 Hijria | 12 Machi 2024 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.