Arafa Itusukume Kuacha Ubaguzi na Kurudia Umoja wetu wa Asili

Ibada ya Kisimamo cha Arafa katika ibada tukufu ya Hijja ni wajibu mahujaji wote kuitekeleza. Amma kwa Waislamu wasiokuwa katika ibada ya hijja, wao huiadhimisha ibada hii kwa kufunga ndani ya siku hiyo.

Umuhimu na utukufu wa siku hiyo ni mkubwa kama alivyotueleza kwa kina Mtume (SAAW) katika hadithi mbalimbali.

Amali hiyo ya kusimama katika Uwanja wa Arafa kama zilivyo ibada nyengine ni katika ibada alizotuekea Allah Ta’ala ili kushibisha kiu yetu ya kumtumikia Yeye, kwa kuwa Yeye ndie aliyetupangia kuitekeleza ibada hiyo.

Ndani ya ibada hiyo, dhambi zetu husamehewa, kitu kinachothibitisha udhaifu wetu kama wanaadamu na kuhitajia kwetu msamaha  kutoka kwa Allah Ta’ala.  Kwa kuwa  Yeye pekee ndiye Anaesamehe dhambi (Al-Ghafir).

Zaidi ya hayo pia ndani ya ibada hiyo kuna mafunzo kadhaa likiwemo suala la kuikumbuka Siku kubwa ya Qiyama, kujiandaa nayo, suala la udugu baina yetu nk.

Aidha, katika ibada hii ni muhimu kujikumbusha tareekh, namna katika zama za jahilia kabla ya Uislamu na kabla ya kuja Mtume (SAAW) wakati ambapo waarabu walipokuwa wamezama katika kiza na upotofu. Katika hali kama hiyo maQureish walibobea katika masuala ya ubaguzi na kujitukuza kiasi kwamba katika ibada ya kisimamo cha Arafa walijihi kuwa kwa darja yao hawakustahili kujumuika na kuchanganyika na mahujaji wengine kutokana na fikra zao potofu za ubaguzi (‘asabiyya). Kwa dhana yao potofu kwamba wao ni watu bora na tofauti kabisa na mahujaji wengine.

Kuja kwa mfumo mtukufu wa Uislamu kulileta mapinduzi makubwa ya kifikra na kivitendo kwa kufinyanga aina thabiti ya fungamano baina ya wanaadamu ambalo ni fungamano la kimfumo pekee, kwani watu wote ni viumbe wa Mola Mmoja. Na hivyo kuondoa na kung’oa kabisa, kimsingi na kivitendo kila aina ya mabakibaki yote ya fikra za kibaguzi na kujitukuza kinyume na haki, na kuwaamrisha maQureish na wengine wote mara moja wajumuike pamoja na mahujaji wengine katika ibada hiyo ya Kisimamo cha Arafa.

ثُمَّ أَفِيضُوا مِنْ حَيْثُ أَفَاضَ النَّاسُ وَاسْتَغْفِرُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ

Kisha miminikeni pale wanapomiminika watu, na muombeni Allah msamaha. Hakika Allah ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu” [TMQ 2:199]

 Tangu kuangushwa dola ya Kiislamu ya Khilafah mwaka 1342 Hijri (1924 miladi), makafiri wamemakinisha fikra hatari za kiubaguzi wa kitabaka, rangi, jinsia na ‘taifa huru’ (japo uhuru huo ni wa bandia). Fikra zilizopenya kama mkuki mkali katikati ya  mwili wa Umma, kiasi cha kuota mizizi miongoni mwa baadhi ya Waislamu hadi kudhani hali hii ni ya kimaumbile. Na kwa bahati mbaya zaidi wakati mwengine hata wale wanaoulingania Uislamu huulingania kwa kutumia vipimo hivi vya kikafiri vya kiubaguzi kwa msingi wa utaifa na uzalendo. Ilhali inaeleweka wazi na bayana na kila Muislamu kwamba Umma wetu mtukufu ni Umma mmoja, Mola wake ni Mmoja, aqeedah yake ni moja, Kitabu chake ni kimoja, Kibla chake ni kimoja, vipimo vyake katika matendo ni vimoja, ardhi yake ni moja (pamoja na leo kugawanywa kwa mipaka ilioyochorwa na makafiri wakoloni ) na kila ajenda yake katika kila suala/qadhia nyeti ni pamoja. Na bila ya shaka suluhisho na ukombozi wake pia ni mmoja, yaani kurudia mfumo wake kikamilifu kwa kuungana chini ya bendera moja ya Khilafah ya Kiislamu inayounganisha biladi/nchi zote za Kiislamu na kuhukumu kwa Sheria moja ya Kiislamu.

إِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِي

“Hakika Umma wenu huu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu niabuduni”

[TMQ 21:92]

Ni wajibu katika wakati kama huu tunaoingia ndani ya ibada hii tukufu ya Kisimamo cha Arafa kuifungamanisha kwa udhati kabisa na suala la kung’oa kila aina ya ubaguzi na kuondoa kibri baina yetu, uwe ubaguzi kwa misingi ya rangi, kabila, kijografia nk. uliopandikizwa na makafiri wakoloni kwa lengo hatari   la ‘wagawe uwatawale’.

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُوا

“Na shikamaneni kwa kamba ya Allah nyote pamoja, wala msifarakiane” [TMQ 3:103]

Maoni hayajaruhusiwa.