Agenda Ya Ukoloni Mamboleo Ya Ujerumani Nchini Tanzania.

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Novemba 1,2023, Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini Tanzania, ziara iliyoanza Oktoba 30,2023. Ujumbe wa Rais Steinmeier ulijumuisha maofisa wa serikali ya Ujerumani na wawekezaji wa makampuni makubwa 12, ikilenga ziara hiyo kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kukuza biashara na uwekezaji.
Maoni:
Ujerumani iliikoloni iliyokuwa Tanganyika (sehemu ya Tanzania ya sasa) kuanzia mwaka 1885 hadi 1918 iliposhindwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia ambapo hatimaye ilipoteza makoloni yake, huku mengi ya makoloni hayo yakichukuliwa na Uingereza na Ufaransa chini ya Mkataba wa Versailles. Tangu wakati huo, yaani kuanzia mwaka 1919 Tanganyika ikawa chini ya ukoloni wa Waingereza huku Marekani ikifanya majaribio ya kuinyakua kutoka kwa Uingereza bila mafanikio.
Ziara ya Steinmeier inaonyesha kuwa Ujerumani inalenga kupanua wigo wake wa ushawishi nchini Tanzania katika kipindi hiki cha ukoloni mamboleo ambapo biashara ya kimataifa inatumika kama njia ya kufikia ajenda ya ukoloni kwa nchi masikini zinazokoloniwa za dunia ya tatu. Kupitia kile wanachokiita biashara huria, wakoloni wamezifanya nchi maskini kuwa soko la bidhaa zao na chanzo cha malighafi kupitia biashara isiyo na uwiano kati ya pande mbili.
Aina ya biashara kati ya Ujerumani na Tanzania bila shaka ni biashara ya kinyonyaji, isiyo na usawa na yenye maumbile ya kikoloni. Ujerumani pekee ndiyo inaweza kuwekeza Tanzania, na Tanzania kama yalivyo mataifa mengine maskini daima yamekuwa chanzo cha soko na uwekezaji kwa Ujerumani. Katika ziara hii, kulikuwa na ujumbe wa makampuni 12 ya biashara ambapo kongamano la biashara kati ya wadau wa biashara wa Tanzania na Ujerumani lilifanyika.
Wakati Tanzania haina uwezo wowote wa uwekezaji wa kidhati nchini Ujerumani, kuna uwekezaji mkubwa wa Ujerumani nchini Tanzania kwa miaka mingi. Hadi kufikia Agosti 2023, miradi 178 yenye thamani ya dolari milioni 408.11 kutoka kwa wawekezaji wa Ujerumani ilikuwa imesajiliwa Tanzania Bara na miradi 15 yenye thamani ya dolari milioni 300 zilisajiliwa Zanzibar. Pia kuna uwekezaji mwingine mwingi kama vile kiwanda cha Saruji cha Twiga kilichopo jijini Dar es Salaam ambacho kinaendeshwa kwa ushirikiano na kampuni ya Kijerumani ya Scancem International. Ujerumani imewekeza katika sekta mbalimbali za kimkakati nchini Tanzania kama vile maji, afya, fedha na utalii.
Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Tanzania inasafirisha bidhaa zenye thamani ya dolari milioni 42.04 kwenda Ujerumani, nyingi zikiwa ni tumbaku, kahawa, pamba, asali, samaki, nta na madini ya vito. Kila mwaka, Tanzania inaagiza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 237.43 kutoka Ujerumani, mara nyingi zikiwa ni madawa, vifaa tiba, uturi, magari na vifaa vya umeme.
Mataifa yanayoendelea kama Tanzania daima yamekuwa yakitawaliwa na kunyonywa na nchi za kikoloni za Magharibi kama Ujerumani chini ya ubepari ambao ukoloni ulibakia kuwa ni mbinu yake isiyobadilika ya kufikia lengo lake ambalo ni unyonyaji.
Pindi serikali ya kiulimwengu ya Kiislamu, yaani Khilafah, itakaporejeshwa tena, tofauti na wakati huu ambapo Afrika ilipo chini ya ubepari, wakati huo, Afrika na dunia kwa ujumla itafurahia biashara ya haki, yenye tija na yenye matunda kama ilivyokuwa kabla ya ukoloni kuingia mwishoni mwa karne ya 19.
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mjumbe wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.