Wakati Tukianza Mwaka Mpya wa Kiislamu Tuukumbukeni Usiku wa ‘Aqaba ya Pili’

بسم الله الرحمن الرحيم

Ukiangalia kwa makini historia ya Mitume As. waliotangulia utaona kuwa ujumbe waliopewa ulikuwa umefungika kimaeneo na jamii ya watu wao, lakini ujumbe wa Mtume Muhammad SAAW umeletwa kwa watu wote na wa kiulimwengu. Kwa hali hiyo ulilazimu awe na nguvu thabiti ya kuifikisha ajenda ya Uislamu ulimwengu mzima.
Tukio la Hijra ni kielelezo tosha cha namna Mtume SAAW alivyofanya harakati zake kwa lengo la kuwa na nguvu kwa ajili ya kutekeleza, kulinda, kuhifadhi na kutangaza ujumbe wa Uislamu. Ndio maana licha ya unyeti na umuhimu wa matukio mbalimbali katika tareekh, tukio lilopewa nafasi kubwa katika historia ya Uislamu lilikuwa ni tukio la Hijra kutoka Makka kwenda Madina.
Tukio hili ndio nukta ya mageuzi katika historia ya Uislamu na pia itakumbukwa kuwa wakati wa Khilafah ya Umar ra. pindi maswahaba walipotaka kuhesabu tarekh ya Kiislamu ianze wakati gani, baada ya mjadala mrefu waliwafikiana kuanzia tukio la Hijra.
Asili ya tukio la Hijra ni kikao cha siri cha Aqaba ya Pili kilichofanyika usiku wa manane ndani ya mwezi wa Dhulhijja katika ‘Masiku ya Tashriq’ (Ayamu Tashriq) hususan tarehe 13 Dhulhijja.
Kikao hicho kilikuwa baina ya Mtume SAAW kwa upande mmoja, na upande wa pili walikuwa majemadari wakubwa na viongozi wenye ushawishi mkubwa kutoka makabila mawili makubwa ya Aus na Khazraj ya Madina. Wawakilishi wao wa Madina walikuwa sabini na tatu, wakiwemo wanawake wawili ambao ni bi. Nusayba na bi Asmaa ra.
Wakati wa kikao hicho nyeti Mtume Muhammad SAAW aliamrisha asiamshwe yoyote aliyelala wala asingojewe aliyechelewa. Miongoni mwa waliohudhuria upande wa Mtume SAAW ni bwana Abass ra, Ammi yake Mtume SAAW alihudhuria kama mzazi ili kushuhudia tukio hilo adhimu.
Bwana Abbas akawa wa mwanzo kuzungumza ambapo alisema:
“Enyi mkusanyiko wa Aus na Khazraj, hakika Muhammad (SAAW) kwetu kama namna mnavyojua tumemuhami dhidi ya watu wetu kwa namna mlivyoona, hakika ni mtu mtukufu kwa watu wake, na ni mwenye ulinzi kwenye mji wake, na hakika yeye amekataa isipokuwa kuja kwenu na kukutana na nyinyi. Ikiwa nyinyi mtaona mtatekeleza yale aliyokuiteni kwayo na mtamlinda dhidi ya wale wenye kumpinga na yale mtakayoyabeba (ni vizuri)…. lakini mkiwa mtakuwa tayari kumsalimisha kwa maadui zake na kumuacha mkono baada ya kutoka hapa, basi mwacheni “
Baad ya Aus na Khazraj kusikia maneno ya Abbas ra. wakamwambia Abbas tumekusikia uliyoyasema sasa, zungumza Mtume (SAAW) yale unayotaka wewe na Mola wako.
Hapo Mtume SAAW akazungumza baada ya kuwasomea Quran na kuonyesha uzuri wa Uislamu akawaambia :
“Nipeni baia (kiapo cha nguvu, utii na ulinzi) kama mnavyowalinda wake zenu na mali zenu”
Basi akanyoosha mkono bwana Baraa kwa ajili ya kumpa ba’ia (kiapo cha utii) Mtume SAAW, kisha bwana huyo akasema :
‘ Pokea kiapo cha utii ewe Mtume Muhammad (SAAW), hakika sisi ni watoto wa wapiganaji wa vita vya mzunguko, tumerithi toka vizazi vyetu vya nyuma”
Baada ya mazungumzo na mjadala mrefu, watu wa Madina wakanyoosha mkono kwa pamoja kumpa baia/kiapo Mtume Muhammad SAAW kwa kusema :
‘Tumekupa kiapo cha utiifu ewe Mtume wa Allah (SAAW) juu ya kukusikiza na kukutii katika uzito na wepesi, kwa (tutayoyaona) yanatupendeza na yanayotukera na kukupendelea kuliko nafsi zetu, na kusema ukweli, hakuna kuogopa lawama ya mwenye kulaumu.
Baada ya kumaliza baia/kiapo, Mtume Muhammad SAAW akawaambia toeni wawakilishi kwenu watu kumi na mbili ili wawe wawakilishi kwa watu wenu, basi wakachagua watu tisa kutoka Aus na watatu kutoka Khazraj, kisha akasema SAAW nyinyi ni wawakilishi kwa watu wenu kama walivyokuwa wanafunzi wa Issa As. wawakilishi kwa watu wao, na mimi ni mwakilishi kwa watu wangu. ( Seerah ibn Hisham)
Baada ya tukio hilo wahusika wakarudi kulala kwenye matandiko yao, na Mtume SAAW akawaamrisha maswahaba zake kuanza kuhama kwenda Madina.
Tukio hili ndilo lililopelekea Hijra ya Mtume Muhammad SAAW kwenda Madina kuasisi dola ya mwanzo ya Kiislamu baada ya kupata nguvu za kivitendo (nusra) katika usiku wa Aqaba. Tukio la Hijra halikuwa kwa ajili ya kukimbia maudhi ya maqureishi kama wengi wanavyodhani kwani Mtume SAAW alikaa Makka kwa muda mrefu na maudhi kwake hayakuwa yenye kumzuiya kufanya ulinganizi, licha ya kuwa jamii ya Makka ilikuwa ngumu. Bali Hijra ilikuwa ni kuhama kutoka Dar ul kufr (nchi isiyoendeshwa Kiislamu) ambayo ilikuwa Makka kwenda Daar ul Islam ambayo ni Madina. Kama alivyosema Mtume SAAW katika Hadith aliyoipokea Imam Muslim:
“Nimeamrishwa kuhama kwenye mji ambao unakula miji (unaingiza miji mingine kwenye himaya yake) na ni mji ambao wanauita Yathriba (Madina).” Hadithi hii inasadifu maneno ya Mola katika Quran:
وَقُلْ رَبِّ أَدْخِلْنِي مُدْخَلَ صِدْقٍ وَأَخْرِجْنِي مُخْرَجَ صِدْقٍ وَاجْعَلْ لِي مِنْ لَدُنْكَ سُلْطَانًا نَصِيرًا (الإسراء: 80).
“Na Sema (Muhammad) niingize mwingizo mwema (Madina) na nitoe kwa utokaji mwema (Makka) na unipe kutoka kwako ulinzi wenye nusra” (TMQ 17: 80)
Huo ndio usiku wa Aqaba uliopelekea kupatikana kwa tukio la Hijra punde baada ya Mtume SAAW kupata nusra kutoka kwa viongozi wenye ushawishi wa kisiasa (ahlu alhal wal aqd) kutoka makabila mawili makubwa ya Madina.
Mara baada ya tukio hilo Ibilis (laanatu llah) alipiga kelele kubwa kwa huzuni kuashiria kushindwa kwake kuizuiya nuru ya Allah SW. Kwa kuwa mawafikiano hayo yalilenga kuinua hali ya Uislamu katika kiwango cha dola na utawala. Tukio la Hijra lililojiri baada ya makubaliano ya Aqaba lilikuwa chachu ya kuubadilisha ulimwengu kwa kuubeba Uislamu kimfumo na kiutawala tofauti na awali.
Tukio hili liwe na mazingatio makubwa kwa Waislamu, lakini pia liwe bishara njema kwamba licha ya mashaka, mateso, mauwaji, kufungwa jela na idhilali kama zinazojiri Kashmiri, China, Syria, India nk. mwisho wa yote nusra itarudi tena na hasa ukizingatia kuwa mfumo uliopo wa kibepari umeshindwa kumsimamia mwanadamu ipasavyo. Basi tufanyeni kazi ya ulinganizi huku nyoyo zetu zikiwa na utulivu
Amesema Mola katika Quran:
وَتِلْكَ الأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ
“Na hayo masiku tumeyapanga kwa zamu baina ya watu” (TMQ 3:140)
وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ (الروم: 4)
“Na siku hiyo watafurahi Waumini” (TMQ 30:4)
Ust. Issa Nassib
Risala ya Wiki No. 161
15 Muharram 1445 Hijria / 02 Agosti 2023

Maoni hayajaruhusiwa.