Ni Uislamu Tu Ndio Wenye Suluhisho la Kweli kwa Usalama wa Chakula kwa Afrika

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:

Kuanzia Septemba 5 hadi 8, 2023 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 13 wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika. Mkutano huo ulioendeshwa ana kwa ana, na mtandaoni ulikuwa na wazungumzaji zaidi ya 350, zaidi ya wahudhuriaji 3,000 kutoka zaidi ya nchi zaidi 70. Mkutano huo ulibeba kauli mbiu: “Huisha, Tengeneza, Chukua hatua kwa Suluhisho la Afrika kwa Mabadiliko ya Mifumo ya Chakula”. Mkutano huo ulilenga kurudisha mifumo bora ya chakula na kujitosheleza ukiwalenga vijana na wanawake kama sehemu muhimu.

Maoni:

Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika – AGRF ni jukwaa kuu la Kiafrika la mifumo ya kilimo na chakula, linaloleta pamoja wadau  kuchukua hatua za kivitendo na kujifunza kwa pamoja jinsi ya kuimarisha na kupeleka mbele mifumo ya chakula ya Afrika.

Kwa mujibu wa kaulimbiu ya jukwaa hilo la AGRF, tamko ‘Kuhuisha’, linamaanisha kutandika mikakati thabiti na hatua za kivitendo za kujenga upya mifumo ya chakula, ‘Kutengeneza’ kunakusudiwa uwepo wa haja ya kuzalisha upya rasilimali asilia kivitendo, uvumbuzi, na teknolojia kwa ajili ya uzalishaji endelevu wa chakula katika mazingira ya mabadiliko ya hali ya hewa. Amma tamko ‘Kuchukua hatua’ kunalenga kujifunga na hatua za haraka kuharakisha gurudumu la mabadiliko ya mifumo ya chakula kupitia sera bora, kwa matendo na uwekezaji.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika, Afrika ina takriban hekta milioni 874 za ardhi ambayo inafaa kwa kilimo, 83% ina udongo wenye rutuba ya kutosha na wenye uwezo wa kufikia uzalishaji wa hali ya juu na endelevu. Pia, (Afrika) ina zaidi ya mito 67 mikubwa na mabonde 63 ya mito inayovuka mipaka. Kwa ufupi, 65% ya ardhi inayolimwa duniani na 19% ya maji safi yanayoweza kuregeshwa duniani yanapatikana barani Afrika.

Kuhusiana na vyakula vya baharini, nchi 27 za Afrika zinapakana na Bahari ya Atlantiki, 13 zinapakana na Bahari Hindi, 5 zinapakana na Bahari ya Mediterania na 4 zinapakana na Bahari Nyekundu.

Kwa upande wa rasilimali watu, Afrika ni makaazi ya watu bilioni 1.3 miongoni mwao karibu 70% ni vijana chini ya miaka 30. Zaidi ya hayo Afrika ina 40% ya dhahabu duniani, 90% ya madini ya kromiamu na platinamu na mrundikano mkubwa wa akiba kubwa ya kolbati na urani inapatikana katika Afrika.

Licha ya rasilimali zote hizo, Afrika bado inakabiliwa na uhaba wa chakula, njaa na ukame.  Zaidi ya watu milioni 140 barani Afrika wana njaa, Somalia hivi karibuni imefikia kiwango cha kutisha ikikadiriwa kuwa na watu milioni 6.5 wanaokabiliwa na shida ya chakula, watu milioni 17.5 hawana chakula cha kutosha nchini Nigeria, nchini Madagascar watu milioni 7.8 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, na watu milioni 22.7 nchini Ethiopia hawana uhakika wa chakula. Ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni mojawapo ya sehemu hatarishi katika majanga ya chakula yanayotisha zaidi katika miongo kadhaa ambapo takriban watu milioni 146 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Katika bara la Afrika, njaa inachangia hadi 45% ya vifo vya watoto.

Mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika, kama yalivyo majukwaa mengine halitofanikiwa kulinda Afrika na dunia kutokana na njaa na uhaba wa chakula, kwa sababu mipango yote haijafikia chanzo halisi cha mgogoro wa chakula barani Afrika. Na lau mipango hiyo ingefikia chanzo (cha tatizo) basi wangeweza kuja na suluhisho muwafaka. Badala yake wanapendekeza masuluhisho ya kibepari na kufikiria ndani ya mipaka ya ubepari, kutegemea masuluhisho ya kikoloni ya Wamagharibi kutatua matatizo yaliyoletwa na hao (Wamagharibi).

Mabadiliko ya hali ya hewa barani Afrika yanachangiwa sana na viwanda vya kibepari vya wakoloni wa Magharibi vinavyosababisha hali mbaya ya hewa na kusababisha majanga yanayoathiri mfumo wa chakula ambayo kwa sasa yanatokea kila baada ya miaka 2.5, hali hii ni mara nyingi zaidi kuliko hapo awali.

Afrika inakabiliwa na ongezeko la bei ya chakula, na bei ya chini na duni kwa bidhaa zao za kilimo katika soko la dunia kutokana na mfumo wa kiuchumi wa kikoloni ambao Afrika imefanywa kuwa shamba la Wamagharibi ambapo wakoloni huja na kunyonya rasilimali na kuendelea kuifanya Afrika kuwa maskini zaidi duniani.

Iwapo Afrika itasimamiwa vyema, sekta yake ya kilimo inaweza kutatua sio tu mgogoro wa chakula ndani ya Afrika, bali ulimwengu kwa jumla, na hilo linawezekana tu kupitia Uislamu pekee.

Chini ya dola ya Kiislamu (Khilafah), mataifa ya kikoloni ya Magharibi hayatokuwa na fursa yoyote ya kudhibiti sera, mipango na programu zetu za kilimo. Sera za Kiislamu za kilimo kama vile kuzingatia kulisha wahitaji kuwa jambo la lazima (faradhi), kufufua ardhi zilizokufa, usambazaji thabiti wa chakula, kufadhili miradi midogo na mikubwa ya kilimo nk. Sera hizo za kujitegemea, zisizotegemea nchi za Magharibi zitahakikisha uzalishaji wa chakula kwa wingi, kuongeza uwezo wa kilimo wa Ummah kama vile viwanda vya kusindika mazao ya mifugo na kilimo, kwa ajili ya kulisha wenye njaa na kutengeneza ajira.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mjumbe wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.