Kampeni Ya Ramadhani Ndani Ya Tanzania

بسم الله الرحمن الرحيم

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Jana Ijumaa 05 Ramadhani 1445 H / 15 Machi 2024 M wanaharakati wa Hizb ut Tahrir Tanzania katika baadhi ya maeneo walifanya Kampeni Maalum ya Ramadhani chini ya kaulimbiu ya ‘Ramadhani ni Kielelezo cha Umoja wa
Ummah’
Maandamano baridi yalifanywa katika jiji la Dar es Salaam na Zanzibar, ambapo ndani ya Dar es Salaam yalifanyika nje ya Masjid Dar us Salaam, Kigamboni, pia yalifanyika nje ya Masjid Idrissa, Kariakoo. Kwa Zanzibar maandamano baridi yalifanyika eneo la wazi karibu na Soko la Darajani.
Kampeni ilifafanua bayana kwamba mwezi wa Ramadhani unawasilisha umoja wa Ummah wa Kiislamu kuwa kitu kimoja, wenye shakhsiaya moja, pia wenye muongozo mmoja, ambapo kutokana na muongozo huo ndio imepatikana amri hiyo ya Swaumu ya Ramadhani.
Hata hivyo kampeni hiyo iliwahadharisha Waislamu kwamba umoja wa Kiislamu haupaswi kujifunga katika masuala ya ibadati za kiroho tu, bali lazima umoja huo utanuke kwa upana hadi kuwa na umoja wa kisiasa chini ya dola ya kilimwengu ya Khilafah ambayo itasimamia mambo ya Waislamu.
Kuweza kuufikia umoja wa aina hiyo (wa kisiasa) kampeni imewahamisha Waislamu kushiriki kikamilifu katika jukumu la kurejesha tena dola ya Khilafah kwa Manhaj ya Utume inayopaswa kuanzia katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa dola hiyo umoja wa kweli wa kisiasa utafikiwa na utaweza kuhifadhiwa.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Kumb: 1445/05
Jumamosi,06 Ramadhani 1445 Hijria 16/03/2024 M

 

Maoni hayajaruhusiwa.