Mabalozi katika Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuhu Sheikh wetu mpendwa

Namuomba Mwenyezi Mungu akupe nguvu, akupe afya na umri mrefu na akujaalie kushuhudia kurudi kwa Khilafah na utuongoze, Amin.

Nina swali kuhusiana na rasimu ya katiba ya Hizb. Katika ibara ya 7 kifungu cha F inasema: “Dola itatabikisha hukmu zote za Sharia na mambo yote ya Shari’ah ya Kiislamu, kama vile miamala, kanuni za adhabu, ushahidi, mifumo ya utawala na uchumi miongoni mwa mengine kwa usawa juu ya Waislamu na Wasiokuwa Waislamu, Dola pia itatabikisha hayo hayo juu ya wale walio na mkataba, wanaomba hifadhi na wale wote walio chini ya mamlaka ya Uislamu kwa njia hiyo hiyo. Inatabikisha kwa wanajamii wote isipokuwa kwa mabalozi, wajumbe na mithili yao kwa kuwa wana kinga ya kidiplomasia.”

Swali langu ni kuhusu hoja kuhusu Mabalozi. Uhalisia ni kwamba wakati mwingine kuna mabalozi wa muda ambao hukaa kwa muda tu kisha kurudi kwenye nchi zao na mabalozi wa kudumu ambao hukaa ndani ya Khilafah kwa kudumu. Je, kifungu hiki kinahusu aina zote mbili za mabalozi?

Pia, endapo mmoja wa balozi atafanya uhalifu au kufanya shughuli isiyo halali nje ya mipaka yao kama mabalozi, je, wote wawili watahukumiwa na kuadhibiwa ipasavyo na Khilafah? Au mabalozi wa muda na wa kudumu wanachukuliwa tofauti katika jambo hili.

Jazakumullahu Khairan.

Kutoka kwa: Saifudeen Abdullah

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

Baraka za Mwenyezi Mungu ziwe nawe kwa dua yako nzuri kwangu, pia namuomba Mwenyezi Mungu akupe kheri.

1- Kuhusiana na swali lako kuhusu mabalozi wa kudumu na wa muda. Hakuna tofauti baina yao katika mtazamo wa Shariah, maadamu maana ya neno (mjumbe) inatumika kwa mtu huyo, anakuwa na kinga ya kidiplomasia wakati wa kukaa kwake ndani ya dola ya Khilafah, bila ya tofauti yoyote… Hapo awali, katika zama za Mtume (saw), Maswahaba na zama zilizofuata, hapakuwa na mabalozi wa kudumu na wakaazi. Badala yake, wajumbe walitumwa kufikisha ujumbe na kisha kurudi katika nchi yao, yaani, walikuwa, kulingana na usemi wako (mabalozi wa muda / wajumbe wa muda) … Kisha mabalozi na afisi za mabalozi za kudumu duniani zikaanzishwa kutokana na uzito wa mahusiano na haja ya mawasiliano ya kudumu kati ya nchi na uwepo wa raia wa ubalozi wa nchi hizo ndani ya nchi husika. Kwa hiyo, dola zilianza kukubali kufunguliwa kwa afisi za ubalozi za kudumu za nchi nyingine katika ardhi zao na kukubali kibali cha mabalozi wa nchi hizo wanaoishi ndani yake… Zamani balozi au mjumbe alikuwa akienda mara moja tu kupeleka ujumbe mahususi… Hili ndilo linalofahamika kutoka kwa Hadith tukufu kuhusiana na wajumbe, kama alivyosimulia Ahmad kutoka kwa Ibn Masoud ambaye amesema:

«جَاءَ ابْنُ النَّوَّاحَةِ وَابْنُ أُثَالٍ، رَسُولاَ مُسَيْلِمَةَ إِلَى النَّبِيِّ ، فَقَالَ لَهُمَا: أَتَشْهَدَانِ أَنِّي رَسُولُ اللَّهِ؟ قَالاَ: نَشْهَدُ أَنَّ مُسَيْلِمَةَ رَسُولُ اللَّهِ، فَقَالَ النَّبِيُّ : آمَنْتُ بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ، لَوْ كُنْتُ قَاتِلاً رَسُولاً لَقَتَلْتُكُمَا، قَالَ عَبْدُ اللَّهِ: قَالَ: فَمَضَتِ السُّنَّةُ أَنَّ الرُّسُلَ لاَ تُقْتَلُ»

Ibn Nawwaha na Ibn Uthal walikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kama wajumbe Musaylama – mrongo – na Mtume wa Mwenyezi Mungu akawaambia: “Je, mnashuhudia kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Wakasema: “Tunashuhudia kwamba Musaylama ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.” Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Mimi ninamuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. “Mimi nakupeni usalama kupitia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kama ingekuwa mimi ni mwenye kumuua mjumbe ningekuuweni nyinyi wawili.” Abdullah amesema: dhihirisho la sunna hii ni kwamba wajumbe hawauwawi.” (Imepokewa na Ahmad na kutangazwa kuwa ni Hasan na Al-Haythami).

Ni wazi kutokana na Hadith hii kwamba hotuba hiyo inahusu wajumbe wawili waliotumwa kutoka kwa Musaylamah, mrongo.

2- Kuhusu uulizaji wako kuhusu adhabu kwa mabalozi na wajumbe, jibu lake linapatikana katika maelezo ya kilma “na” cha Ibara ya 7 katika kitabu, Utangulizi wa Rasimu ya Katiba, na haya ndiyo maandishi yake:

Ama Ibara F, ushahidi unaohusiana na utekelezaji wa kanuni zote za Uislamu unatokana na yale yote ambayo yametajwa hivi punde kwamba kafiri ana wajibu wa kushikamana na misingi na matawi, hivyo basi, ameamrishwa kujisalimisha kwa sheria zote za Uislamu. Hii ni jumla, na inajumuisha Dhimmi na asiyekuwa Dhimmi kutoka miongoni mwa wale wanaoishi chini ya mamlaka ya Uislamu. Kwa hivyo, makafiri wote wanaoingia Dar Al-Islam lazima wakabiliwe na sheria za Uislamu isipokuwa mambo ya ́Aqidah, hukmu zinazohusiana na mambo ya ́Aqidah na kitendo chochote ambacho Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwaruhusu kufanya iwe makafiri hawa ni Dhimmi, wako chini ya mkataba au wanaotafuta hifadhi. Hata hivyo, mabalozi na mfano wao wametengwa kutokana na hili na hukmu za Uislamu hazitatabikishwa juu yao kwani watapewa kile kinachojulikana kama kinga ya kidiplomasia. Hii ni kwa sababu Ahmed amepokea kutoka kwa Ibn Masoud ambaye amesema:

«جَاءَ ابْنُ النَّوَّاحَةِ وَابْنُ أُثَالٍ، رَسُولاَ مُسَيْلِمَةَ إِلَى النَّبِيِّ ، فَقَالَ لَهُمَا: أَتَشْهَدَانِ أَنِّي رَسُولُ اللَّهِ؟ قَالاَ: نَشْهَدُ أَنَّ مُسَيْلِمَةَ رَسُولُ اللَّهِ، فَقَالَ النَّبِيُّ : آمَنْتُ بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ، لَوْ كُنْتُ قَاتِلاً رَسُولاً لَقَتَلْتُكُمَا، قَالَ عَبْدُ اللَّهِ: قَالَ: فَمَضَتِ السُّنَّةُ أَنَّ الرُّسُلَ لاَ تُقْتَلُ»

“Ibn Nawwaha na Ibn Uthal walikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kama wajumbe Musaylama – mrongo – na Mtume wa Mwenyezi Mungu akawaambia: “Je, mnashuhudia kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Wakasema: “Tunashuhudia kwamba Musaylama ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.” Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Mimi ninamuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. “Mimi nakupeni usalama kupitia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kama ingekuwa mimi ni mwenye kumuua mjumbe ningekuuweni nyinyi wawili.” Abdullah amesema: dhihirisho la sunna hii ni kwamba wajumbe hawauwawi.” (Imepokewa na Ahmad na kutangazwa kuwa ni Hasan na Al-Haythami). Kwa hivyo, riwaya hii inaashiria kwamba hairuhusiwi kuwauwa wajumbe wa makafiri na wala kuwawekea adhabu (Uqubat). Hata hivyo, hii inatumika pekee kwa wale ambao wana nafasi ya mjumbe kama vile balozi na “Charge d’affaires” na kadhalika. Ama wale ambao wadhifa wa mjumbe hauwahusu kama vile mwakilishi (consul) na Mwambata wa Biashara (Commercial Attaché) na mfano wake, hawatakuwa na kinga yoyote kwa kuwa hawana wadhifa wa mjumbe. Jambo hili linapaswa kuregeshwa kwenye mkataba wa kimataifa kwa sababu ni maelezo ya istilahi ambayo uhalisia wake unapaswa kueleweka kwa kuuangalia mkataba na je ni sehemu ya kuthibisha Manat (uhalisia); kwa maana nyengine, kuthibitisha kama wanachukuliwa kuwa wajumbe au la] Mwisho wa Nukuu kutoka kwa maelezo kutoka katika kitabu, Rasimu ya Katiba.

Uharamu wa kutoa adhabu ya kifo na adhabu nyenginezo unatekelezeka kwa balozi wa kudumu, kwa balozi na mjumbe wa muda maadamu uhalisia wa “mjumbe” unawahusu. Hakuna tofauti katika suala la kutotoa adhabu kwa balozi wa kudumu na kwa balozi wa muda, kwani wote wawili ni wajumbe ambao sheria za mjumbe zinawahusu katika suala la adhabu.

Ama sehemu ya mwisho ya swali lako: (Pia, iwapo mmoja wa balozi atafanya jinai au atafanya kitendo kisicho halali zaidi ya mipaka yake kama balozi, je, wote wawili wanahukumiwa na kuadhibiwa ipasavyo na Khilafah? Au mabalozi wa muda na wa kudumu wanatendewa tofauti katika suala hili.)

Hatukueleza kwa undani uhalisia wa adhabu zinazojumuishwa chini ya kinga na zile ambazo hazijumuishwi, bali tutalieleza hili kwa kina katika kanuni za utendaji za vifungu vya katiba tulizoanza nazo, na tunamuomba Mwenyezi Mungu atusaidie katika kuzikamilisha kwa wakati muafaka, Mwenyezi Mungu akipenda.

Natumai kuwa haya yanatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi Hekima.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

6 Safar Al-Khair 1445 H

22/8/2023 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa  Amiri wa Facebook page.

Maoni hayajaruhusiwa.