Ramadhani Inatuonesha Matamanio Yanazuilika

بسم الله الرحمن الرحيم

Quran Tukufu inasema:
أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَى نِسَائِكُمْ هُنَّ لِبَاسٌ لَكُمْ وَأَنْتُمْ لِبَاسٌ لَهُنَّ ……..
“Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao”.
Moja katika mazingatio makubwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kule Uislamu kutambua kwamba matamanio ya kijinsia ni kitu kinachozuilika. Ramadhani inatuonesha wazi kuwa katika mazingira fulani ya ibadat hulazimu matamanio ya kijinsia baina ya mke na mume yawekwe pembeni kwa lengo la kubeba majukumu mengine nyeti kwa wakati husika. Hii haina maana kwamba matamanio hayo sio muhimu kwa mwanadamu. Bali tunafundishwa kuwa yanazuilika na kuna mazingira ambayo hulazimu kutanguliza hisia za kiibada mbele zaidi na kuyawacha matamanio hayo pembeni kwa muda.
Kwa bahati mbaya kuna wanaodhani kwa ujinga au kwa kuathirika na fikra za kimagharibi kwamba kushibisha matamanio ya kijinsia ni jambo la lazima na kukosekana kwake humpelekea mwanadamu kudhurika. Katika hali kama hiyo si ajabu kuwasikia wengine wakisema siwezi kujizuilia. Hata hivyo ndani ya Ramadhani tunawaona kusita hata wale ambao katika miezi ya kawaida hujitosa katika uovu wa zinaa.
Ufahamu kwamba matamanio ya kijinsia hayazuiliki si sawa. Kwa kuwa Allah Taala ametangaza kuwa asiyeweza kuoa ajizuilie. Pia tumekatazwa kuwa na mahusiano ya kijinsia baina ya mke na mume katika mchana wa Ramadhani, katika ibada ya itikafu, Hijja nk. Katazo hili la kutoyatumia matamanio ya kijinsia kutoka kwa Allah Taala kwa asiye na uwezo wa kuoa au aliyekuwa hajaolewa na katika baadhi ya ibadaat maana yake ni kuwa matamanio haya yanadhibitika, lau una dhamira ya kweli kuyadhibiti.
Kwa kuwa Allah Taala ni Muadilifu hamuamrishi mwanadamu kutenda au kuwacha kutenda jambo ambalo katika maumbile ya mwanadamu haliwezekani. Na zaidi ni Yeye Allah Taala ndie aliyemuumba mwanadamu, na ni Yeye ndie aliyeyaumba hayo matamanio ya kijinsia.
Wamagharibi wamekwenda kombo juu ya mtazamo wao kwa matamanio ya kijinsia. Kiasi kwamba baadhi ya wanafikra wao kama Abraham Maslow amefurutu ada kiasi cha kuyapandisha darja matamanio ya kijinsia kuwa ni mahitajio ya lazima ya kimwili (physiological needs) kwa mwanadamu. Jambo hili huwasukuma watu wao na wanaobeba fikra zao kuvamia katika kushibisha matamanio yao ya kijinsia kama manyani porini, kana kwamba ni suala la kufa na kupona.
Hii ni kwa sababu ya kujengwa fikra zao kuwa ni jambo la lazima. Mtazamo huu ni butu na umetokana na fikra zao potofu za uhuru (freedoms) zinazohamasisha kila aina ya vichocheo vya uchafu wa zinaa. Na kutokana na kueneza vishawishi vingi na vichochezi vingi vya kuhemua matamanio ya kijinsia imewapelekea kuamini na kuchukulia kuwa jambo hilo ni suala la ulazima ilhali sio hivyo. Jamii zao leo ni jamii za wanyama waliobakiwa tu na sura za kibinaadamu.
Uislamu unamuangalia mwanaadamu kwamba ana mahitajio ya kibaologia (organic needs) kama chakula, maji, hewa nk. Mahitajio haya huwa lazima mwanaadamu ayapate au atafariki. Pi ana hisia za kimaumbile (ghariza/instincts), ambazo hupaswa na ni vyema zishibiswe kwa utaratibu maalum. Lakini hizi si katika mahitaji msingi ya kibaologia kama chakula na mengineyo. Miongoni mwa ghariza/hisia za kimaumbile alizonazo mwaadamu imo ‘hisia ya kuendeleza kizazi’ ambayo humsukuma wanadamu kuvutika baina ya mwanamke na mwanamumu, kuwapenda ndugu, kuwa karibu na jamaa zake, kutaka awe na watoto nk. Msukumo wa ndani wa hisia hii ndio hupatikana matamanio ya kijinsia.
Licha ya matamanio haya kuwemo ndani ya maumbile ya mwanaadamu lakini kamwe hayawezi kuripuka wala kumuhemua mtu bila ya msukumo wa vishawishi vya nje, iwe kwa njia ya kusikia , kugusa au kuona vishawishi fulani. Pale vishawishi hivyo vinapohudhurishwa akilini, ndio matamanio ya mtu huripuka na kuhitaji kushibishwa. Kinyume na hivyo matamanio ya kijinsia hubakia katika hali ya kuwapo tu (dormant) ndani ya nafsi ya mwanadamu, bila ya mripuko wala harara yoyote hata kama mtu huyo atakula vyakula vizuri vya aina gani.
Ndio maana Uislamu ukazuiya kila aina ya vishawishi na kamwe haukuziya aina ya vyakula. Na kwa kuwa matamanio ya kijinsia haya ni muhimu katika kufikia lengo la ustawi wa mwanadamu katika kuendeleza kizazi cha mwanaadamu Uislamu ukahimiza sana ndoa kwa mwenye uwezo na ukahimiza kukuzwa hisia hizi baina ya mke na mume.
Huo ndio mtazamo sahihi wa Kiislamu juu ya matamanio ya kijinsia baina ya mwanamke na mwanamume ambapo mwezi wa Ramadhani unatuonesha wazi wazi. Na huu ndio mtazamo unaowafanya wanadamu kuwa madhubuti wasiokuwa mateka wa matamanio yao ya kijinsia. Kinyume na wamagharibi leo chini ya nidhamu yao potofu ya kikafiri ya kidemokrasia. Kwa hakika wameshasalimu amri kikamilifu kwa matamanio yao ya kijinsia, kiasi kwamba huyashibisha matamanio hayo hadharani kama wanyama au zaidi. Wamekua mateka katika dunia hii, na kesho akhera ni majuto upande wao.
قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ
“Watasema : Mola wetu tulishindwa na matamanio yetu na tukawa tuliopotea (TMQ 23:106)
Risala ya Wiki No. 177
25 RamadhanI 1445 Hijria | 04 Aprili 2024 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.