Bilal Bin Rabaah: Sahabah Mwenye Nuru Yenye Mafundisho Kwa Ummah

بسم الله الرحمن الرحيم

Mmojawapo ya swahaba ambaye tareekh ya maisha yake inasisimua sana ni Bilal bin Rabaah. Asili ya Sahaba huyu ni mhabeshi aliyekuwa mtumwa wa kabila la Banu Jumah ndani ya Makka. Maisha yake yalikuwa ya kinyonge na udhaifu kama mtumwa yeyote wa kawaida pale Makka, hakuwa na uwezo, hadhi wala uhuru wowote isipokuwa kuwatumikia mabwana zake wa kabila la Banu Jumah
Bilal alimilikiwa na bwana Umayya bin Khalaf, mmoja wa mabwanyenye wa Makkaa kutokana na kabila la Banu Jumah. Pia mama mzazi wa Bilal bi. Hamamah naye pia alikuwa mtumwa wa kabila moja na mwanawe.
Daawa ya Uislamu ilipoanza kutoka wazi ndani ya Makka ilimvutia Bilal. Alipata ulinganizi wa Uislamu kupitia kwa Abubakar Al-Siddiq (ra.) aliyekuwa kila anapopata fursa anakwenda kumlingania Bilal na watu wengine. Bilal na Abubakar Siddiq walikuwa na mahusiano mazuri kabla Bilali ya kuwa Muislamu, na kupitia mahusiano hayo iliwezekana kwa Ababukar kumfikishia Bilal ujumbe wa Uislamu kiurahisi.
Bilal (ra.) alifuatana na Abubakar (ra) mpaka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na kuzitamka shahada mbili mbele yake.
Bilal alikuwa miongoni mwa Waislamu wa kwanza kupata misukosuko katika daawa na Uislamu kiujumla. Watumwa wengine ambao nao walisilimu na kupata misukosuko na mateso ni bi Sumaiyya, mume wake Yassir na mtoto wao Ammar (ra.) hawa walikuwa na asili ya Yemen.
Bilal, familia ya Yassir na wengine walipata misukosuko kwa kusilimu kwao na walikuwa wakiadhibishwa sana, na kila Mtume (SAW) anapopita alikuwa akiwabashiria na kuwafariji. Kwa mfano, alikuwa akiwaeleza familia ya Yassir:
“Kuweni na subira enyi watu wa nyumba ya Yasir, kwani hakika ahadi yenu ni Pepo”.
Bi. Sumayya (RA) alifariki kwa mateso na akapata bahati njema ya kuwa shahid wa mwanzo katika dini ya Kiislamu.
Kwa upande wa Bilal (ra.), naye alipata sehemu kubwa ya adhabu, kwani bwana wake Umayya bin Khalaf alikuwa mtu khabithi na muovu sana, bwanyenye huyu wa Makka alikuwa akimtoa Bilal nje wakati wa jua kali linalounguza mwili na kumvua nguo zake kisha kumlaza juu ya mchanga wa jangwani unaounguza na kumwekea jiwe kubwa sana juu ya kifua chake huku akimwambia;
“Utabaki hivyo hivyo mpaka ufe isipokuwa kama utamkanusha Muhammad na kumtukana, kisha urudi tena kuiabudu miungu ya Latta na Uzza”.
Bilal (ra.) alikuwa akijibu kwa kusema “Ahadun Ahadun”. Bilal (ra.) akawa anaendelea kuadhibiwa lakini akabaki katika mstari wa subra na istiqama mpaka bwana wake Umayya akashindwa kumdhibiti, kwani kila siku licha ya kumtesa kwa jua la mchana, pia alikuwa akimfunga kamba shingoni na kuwakabidhi watoto wadogo na majahili wengine ambao wakimburuza Bilal (RA) na kuzunguka naye mjini Makka, huku wakimzomea, kumkebehi na kumpiga lakini Bilal hakutetereka msimamo wake juu ya Uislamu.
Aliwahi kuulizwa sahaba Bilal; “Kwanini ulipokuwa ukiteswa ulikuwa ukiendelea kusema matamshi ya “Ahadun Ahad”. (mmoja tu, mmoja tu), na hali unajua kuwa maneno hayo yanawaghadhibisha (makafiri) na kwa ajili hiyo wataendelea kukuadhibu?”Akajibu;”Wallahi kama ningekuwa nalijua neno jingine lolote linaloweza kuwakasirisha zaidi kuliko hilo, basi ningelilitamka”.
Mtume (saw) alikuwa anahuzunika na kuumia sana juu ya matendo ya mateso kwa masahaba wake akiwemo Bilali, lakini hata siku moja hakuamuru wafuasi wake waanzishe vurugu ndani ya Makka. Hatimae alimuamuru Abubakar amkomboe Bilal kwa kwa fidia ya fedha ili awe huru, na Abubakar akamlipa fedha Ummaya ibn Khalaf (bwana wa Bilal) na Bilal akawa huru.
Bilal daima atakumbukwa katika Uislamu kwa ujasiri, uimara na subra yake, na hakumuogopa yoyote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Baadhi ya wanatariikh wamediriki kusema kuwa Bilal alichangia sana kuwadhoofisha makafiri wa Makka kisaikolojia, kwani uwezo wake wa kuhimili mateso uliwaathiri sana Maqureishi wa Makka na kuanza kuhisi kwamba siku moja watashindwa na Waislamu.
Baada ya ushindi wa Waislamu Bilal alipewa hadhi na heshima kubwa na Mtume (Saaw) kwa kuwa muadhini wa kwanza wa Mtume (saw) ndani ya Madina. Aidha, katika medani ya kivita Bilal daima alikuwa akisimama kidete kwa ushupavu katika kupambana na makafiri, kutetea na kuilinda serikali ya Kiislamu.
Katika maisha ya Bilal pamoja na mengi tunajifunza namna Mtume Muhammad (saw) alivyoweza kuwajenga masahaba wake kwa uimara na ushujaa mpaka wakaweza kuiathiri Makka kwa ulinganizi ambao ulikuwa hautumii nguvu, silaha wala mabavu mpaka akaweza kusimamisha dola ya mwanzo ya Kiislamu katika mji wa Madina.
Pia, sahaba kisa cha Bilal kinatufundisha tujitoee muhanga kwa kila namna kwa ajili ya Uislamu. Muhanga huo unahitajika leo kuliko wakati wowote ili kurejesha tena maisha ya Kiislamu kupitia manhaji ya Mtume (saw) kwa kurejesha tena serikali ya Kiislamu (Khilafah) inayopaswa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu ili iwakomboe Waislamu na wanadamu kwa ujumla.
Basi kwa kila Mumumi anayetaka na kutamani kuungana na sahaba Bilal peponi ni wajibu ajifunge kwa uimara, ushujaa, ushupavu na subra ya sahaba huyo aliyoitoa kwa ajili ya Uislamu.
Risala ya Wiki No. 163
17 Safar 1445 Hijria / 02 Septemba 2023 Miladi

Maoni hayajaruhusiwa.