Makusanyo Makubwa ya Kodi Tanzania si Jambo la Kujifakhiri nalo

0

Habari:
Vyombo vya habari vya Tanzania na nje vimeripoti juu ya taarifa ya kupanda kwa makusanyo makubwa ya kodi yaliyofanywa na Mamlaka ya MapatoTanzania (TRA) kwa miezi michache iliyopita mpaka kufikia asilimia 8.45. Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa kodi bwana Richard Kayombo amewashukuru walipakodi kwa kuiwezesha TRA kukusanya kiasi hicho, na akasema TRA ina kampeni ya nchi nzima kusajili bure namba ya utambuzi kwa mlipa kodi (TIN) kwa lengo la kurahisisha mchakato wa ukusanyaji wa kodi.

Maoni
Kodi (za dhulma) ni mfumo utumiwao na serikali za kibepari kupata fedha za matumizi ya serikali na kwa huduma nyinginezo, na mapato ya serikali za kibepari/kidemokrasia yatokanayo na kodi ni zaidi ya asilimia 90%. Ni dhahir shahir kwamba utaratibu huo wa mfumo wa kibepari tangu kuzaliwa hadi kuzikwa kwake kamwe kwa namna yoyote hautaweza kuwaletea raia maisha bora.

Kodi katika uchumi wa kibepari huzalisha matatizo lukuki kama vile kuvuruga mgawanyo wa mali, kufifisha uwekezaji, kupunguza fursa za ajira, kuchochea mfumuko wa bei, kupaisha gharama za maisha na kuondosha mizania  kwa kijamii kuongeza pengo la kipato baina ya masikini na matajiri, huku mzigo wa kodi huwaelemea zaidi wanyonge na masikini ilhali matajiri hupatiliza mianya ya kijanja kulipa kodi kidogo, rushwa au kusahaulisha na kutorosha fedha zao katika sehemu salama na kodi.

Zaidi ya hayo, kupatikana makusanyo makubwa ya kodi  haimaaanishi  kwamba fedha zote hizo zitakwenda katika matumizi sahihi kama inavyodaiwa. Katika mfumo wa kibepari mara nyingi fedha huvurugwa na kuingia katika mikono miovu ya mafisadi, na  kiwango kidogo kilichobakia ndio huangukia katika katika matumizi muwafaka.

.Licha ya Tanzania kujigamba kupata mafanikio katika ukusanyaji wa  kiasi kikubwa cha kodi,  ripoti ya karibuni ya  Shirika la Fedha la Kimataifa ( IMF) imeionya Tanzania juu ya hali ya mporomoko wa kiuchumi, shirika hilo likiitaka serikali ya Tanzania kuchukua hatua muhimu kuidhibiti hali hiyo ambayo kwa juu juu inaonesha kana kwamba uchumi umeimarika, ilhali kiuhalisia kuna mdororo mkubwa wa harakati za kiuchumi.

http://www.xinhuanet.com/english/2018-01/13/c_136891878.htm

Katika Uislamu kuna malipo ya zakat asilimia 2.5 kwa kiwango maalum cha mali iliyofikiwa na kipindi cha mwaka mmoja, hii hupelekea kupatikana fedha za ziada katika mzunguuko wa kiuchumi ambao natija yake hupelekea watu wengi kuingia katika shughuli za uzalishaji, kutengeneza zaidi  fursa  za ajira, kisha kuzidisha upatikanaji  zaidi wa bidhaa  na huduma na kuchochea uwekezaji. Hali hii ni kinyume kabisa na nidhamu ya kibepari iliyotungwa na binadamu ambayo imekosa uadilifu, huleta dhulma, rushwa na kuwafanya watu na mataifa dhaifu kubakia kana kwamba ni watumwa.

Ni kwa Uislamu pekee ndipo uadilifu wa  kiuchumi hupatikana kwa watu wote na kusimamiwa vyema maisha yao. Kwa mapato ya serikali ya Khilafah kama kharaj, ngawira na nyenginezo kwa pamoja na mali za Ummah kama gesi, mafuta, madini  yatatumika kuwanufaisha raia wote wa dola ya Khilafah bila ya kuwazingatia dini zao.

Imeandikwa na Ramadhan Said Njera
Mjumbe wa Afisi ya Habari  Hizb ut Tahrir Tanzania

Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.