‘Kukomeshwa Adhabu ya Kifo’ Dhihirisho la Mgongano Katika Mfumo wa Kidemokrasia

Makala hii iliandikwa miaka kadhaa iliyopita tunaiweka tena kwa munasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kukomeshwa adhabu ya Kifo (10 Oktoba 2018)

Tangu mwaka 2003, siku ya tarehe 10 Oktoba ya kila mwaka imechaguliwa kimataifa kuwa siku ya kampeni ya kukomeshwa kwa adhabu ya kifo duniani. Kampeni hii hufanywa dunia nzima ikiungwa mkono na baadhi ya nchi, majukwaa ya haki za raia na taasisi mbali mbali hususan zinazoitwa na kujishughulisha na masuala ya ‘haki za binaadamu’. Dhamira ya kampeni hii ni kuhakikisha kwamba adhabu hiyo inafutwa kabisa katika uso wa dunia.

Adhabu hii ni miongoni mwa adhabu ya kale na imekuwepo tangu katika zama za sheria za mayunani (wagiriki) zilizobuniwa na Draco katika miaka ya 621 BC. Katika bara la Asia nchi kama China ilikuwa sheria maarufu hadi kusitishwa kwa muda katika zama za Utawala wa Tang (Tang Dynast) katika mwaka wa 747. Kwa upande wa baadhi ya nchi nyingine za Ulaya ilitumika kiasi kwamba hata katika baadhi ya mizozo yao ya kikabila(vendetta) ikiwa kama chombo cha fidia au njia ya utatuzi wa migogoro yao hususan katika zama za Viking. Kwa upande wa dini, wakatoliki waliitumia sana kwa kufuata mafunzo ya Thomas Aquinas, hadi kufikia kuruka mipaka katika historia dhidi ya wanaopinga mafundisho ya kanisa hilo. Pia katika mfumo wa Uislamu ambao ndio mfumo wa haki na ambao sheria zake ni za wahyi nao umeweka adhabu ya kifo katika baadhi ya makosa ya ‘Hadd’ kama vile kwa anaeacha dini ya Uislamu na akakataa kutubu (murtad), mzinifu alieowa au kuolewa, vitendo vya liwati, ujambazi (ihrab), na mauwaji ya makusudi kama mawalii (ndugu) wa aliyeuliwa hawakusamehe au kukubali kulipwa fidia. Kadhalika adhabu hiyo inaweza kutumika katika upande wa adhabu za ‘Taazir’ kama itakuwa ipo haja ya kutoa adhabu hiyo kwa mujibu wa ‘ijtihadi’ ya kadhi.

Adhabu ya kifo bado ilishika hatamu hata katika karne ya 18 na baada. Kwa mfano, nchini Uingereza ilishtadi sana kati kati ya karne hiyo na baada, kiasi kwamba chini ya sheria yao iliyoitwa ‘Waltham Black Acts’ kwa kipindi cha karibu miaka mia kutoka 1740 mpaka mwaka 1834 iliwanyonga watu 8,753 katika England na Wales, huku idadi ya watu wao (population) kwa kipindi hicho ilikuwa haizidi watu Milioni 9. Urusi nayo iliwanyonga raia wake karibu 158,000 waliosaliti katika Vita vya kwanza vya dunia.

KUIBUKA KAMPENI YA KUKOMESHWA KWAKE.

Ingawaje adhabu hii iliota mizizi na kumakinika kwa muda mrefu katika jamii mbalimbali hususan katika Ulaya na sehemu nyingine kwa karne nyingi, lakini mwishoni mwa karne ya 18 kuliibuka vuguvugu na kampeni kabambe kutaka ikomeshwe kwa kuonekanwa ni ya kikatili, si ya kidemokrasia na inamnyima mwanaadamu uhuru wake wa kuishi.

Ikumbukwe kwamba kipindi hiki Ulaya ilikuwa ikipita katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya kimfumo kutoka katika hali ya kutawaliwa na mabwanyenye kwa kushirikiana na kanisa kuelekea katika mfumo mpya wa kidemokrasia uliokuwa ukihubiri fikra ya demokrasia na uhuru (freedoms). Miongoni mwa wanafikra wao wa mwanzo kuibuka na kampeni hii alikuwa mtaalamu wa sheria wa kitaliano (jurist) Cesare Beccaire katika mwaka 1764 alipoandika katika kitabu chake ‘Dei Delitti e Delle Pene’ (‘On crimes and Punishments’) kadhalika mwanafalsafa maarufu wa kifaransa Voltare alihamasisha dhidi ya adhabu hii, na wengi katika wanafikra (thinkers) wa Ulaya na wajuzi wa sheria kama vile waingereza Jeremy Bentham na Samwel Romily. Wote hao walitoa mwito wa kukomeshwa kwa adhabu hiyo.

Kufuatia kampeni hiyo baadhi ya nchi zilipiga marufuku mapema zaidi kama vile Jamhuri ya Rome (The Roman Republic) katika mwaka 1849, Ureno mwaka wa 1867 na Venezuela mwaka wa1863. Hata hivyo baadhi ya nchi waliendelea nayo kwa muda na baadhi wanaendelea nayo mpaka leo. Kwa mfano, Uingereza ilipiga marufuku rasmi katika mwaka 1965, Ufaransa mnamo mwaka 1981, Canada katika mwaka 1976 na Marekani ni majimbo yake (states) 15 tu, ndio yaliokomesha adhabu hiyo, na lililotangulia mapema zaidi ni Jimbo la Michigan tangu Mei 18 mwaka 1846.

‘Tamko la haki za binaadamu’ la mwaka 1948 lilichangia na kuongeza msukumo mkubwa katika kutilia nguvu harakati ya kukomeshwa adhabu ya kifo. Hii ni kutokana na kule kuweka bayana katika ibara yake ya tatu (Article 3) kwamba haki ya kuishi ni haki ya msingi ya mwanaadamu, na jambo hilo likakoleza msimamo ziada kwa wakereketwa wa demokrasia kupata nguvu katika kampeni hii. Hata hivyo kampeni hii imekuja kupata nguvu na kushtadi zaidi na zaidi kufuatia kuanguka kwa Ukomunisti, kwa vile mfumo wa kidemokrasia umebakia peke yake katika uwanja wa kimataifa.

Wakati vugu vugu la kampeni dhidi ya adhabu ya kifo zikiririma, Shirika la Gallup (Gallup International Poll) linaonesha katika tafiti zake kwamba katika mwaka 2000 asilimia 52% ya watu wote duniani waliunga mkono adhabu hiyo, pia tafiti ndani ya Marekani zinaonesha katika Mei 1966 walipoulizwa raia kutoa maoni yao kuhusu adhabu hiyo asilimia 42% waliunga mkono, asilimia 47% walipinga na asilimia 11% hawakuwa na maoni. Lakini walipoulizwa tena miaka 40 baadae katika mwaka 2006 kiwango cha asilimia 65% waliunga mkono na asilimia 28% walipinga adhabu hiyo.

Amma ndani ya Uingereza takwimu zao zinaonesha kwamba tangu mwaka 1964 ilipokomeshwa rasmi adhabu hiyo idadi ya mauwaji imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutoka watu 300 katika mwaka 1964 hadi kufikia watu 563 katika mwaka 1994 na kuzidi mpaka idadi ya 833 katika mwaka 2004.

Licha ya yote hayo yanayoashiria kuhitajika adhabu hiyo katika nchi za magharibi na kuelewa kwa kina kwamba kwa waislamu adhabu hiyo hufungamana na imani yao kwa kuwa ni adhabu iliyoletwa kwa wahyi, bado wakereketwa na wanasiasakali wa kidemokrasia wamekuwa waking’ang’aniza na kwenda mbio usiku na mchana kuhakikisha adhabu hiyo inapigwa marufuku na kukomeshwa kabisa dunia nzima.

Katika kulifikia lengo la kuikomesha adhabu hiyo wanaharakati wake wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kama vile Jumuiya isiyokuwa ya kiserikali ya World Congress Against Death Penalty iliyotowa Tamko rasmi la Strasborg (Strasborg Declaration) katika mwezi wa Juni mwaka 2002 kuzitaka Jumuiya mbali mbali wadau wa zinazoitwa ‘haki za binaadamu’ kama vile Amnesty International, Human Rights Watch, Vyama vya wafanyakazi na Jumuiya mbali mbali zisizokuwa za kiserikali (NGO’s) kuungana pamoja kukomesha adhabu hiyo.

Katika mwezi wa Mei mwaka huo huo wa 2002 iliundwa Jumuiya ya Muungano wa pamoja dhidi ya adhabu ya kifo iliyoitwa (World Coalition Against Death Penalty) na kupata baraka moja kwa moja na kwa kuungwa mkono kwa dhati kabisa na Tume ya haki za binaadamu ya Jumuiya ya Ulaya, hali iliyoipelekea Jumuiya hiyo kutangaza rasmi kuanzia mwaka wa 2003 kwamba kila Oktoba 10 ya kila mwaka itakuwa siku ya kukomeshwa adhabu hiyo.

Umoja wa mataifa kwa upande wake katika kikao chake cha 62 cha Baraza Kuu katika mwaka 2007 ulipitisha Azimio kutoa mwito wa kukomeshwa adhabu hiyo kilimwengu (Universal Ban) kwa kuzitaka nchi zote kuipiga marufuku na kukomeshwa kabisa adhabu hiyo. Mashirika mbali mbali ya kimataifa ya ‘haki za binaadamu’ na ya nchi, nayo yakaweka misimamo thabiti na kutabanni (kushikilia msimamo) sera makhsusi katika kupambana na adhabu hii. Kwa mfano, mashirika kama Human Right Watch, Amnesty International na mengineyo yote huiegemeza na kuichukulia adhabu hii kama ni uvunjifu wa wazi wa haki ya kimsingi ya kibinaadamu (Ultimate denial of Human Rights).

Kwa upande wa Jumuiya ya Ulaya wakajifunga (adopt) kwamba kukomeshwa kwa adhabu hiyo ni sharti msingi la kwa nchi inayotaka kujiunga na Jumuiya hiyo. Mikataba ya kimataifa na taasisi zaidi za kupigania ‘haki za binaadamu’ kimataifa, kimajimbo (regional) na kimaeneo (local) kama vile katika waraka wa mkataba unaoitwa (Second Optional Protocol to the ICCR 1990) pia nyaraka ya mkataba wa haki za binaadamu wa Afrika (African Charter on Human and Peoples Right 1981)’zote hizo zinasisitiza kwa nchi wanachama na wasiokuwa wanachama kushikamana na maazimio ya kimataifa kwa kuikomesha adhabu ya kifo. Pia zinatoa mwito kwa nchi kujizatiti katika kuunga mkono maazimio ya kimataifa juu ya qadhia hii, ambayo tayari baadhi ya maazimio hayo yameingizwa katika katiba (entrenched) za nchi mbali mbali katika kifungu cha haki maalum za raia (Bill of Rights). Kwa hakika kampeni hii imezaa matunda na karibu nchi 94 duniani zimeshaikomesha kabisa adhabu hii.

Inaendelea

#UislamuniHadharaMbadala

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.