Walinganizi Waelewe Upinzani Wanaokabiliana Nao

0

Walinganizi wana wajibu wa kuelewa kwa kina ulimwengu wanaofanyia ulinganizi wao ili waweze kubeba jukumu lao la wajibu huku wakiukabili uhalisia wa mambo kama ulivyo bila ya kutetereka.  Allah SW anasema:

” Yeye ndie ambae amewaumba nyinyi, basi (mupo makundi mawili tu) miongoni mwenu wamo Waislamu, na miongoni mwenu wamo makafiri”

Kwa ufahamu wa aya hiyo, walinganizi  wanapofanya ulinganizi wanatakiwa wajue wanakutana na watu wa makundi mawili. Wapo watakaoukubali ulinganizi wao na pia wapo watakaoupinga, ila walinganizi  wasichoke wala kukata tama kwa kuwa lengo kuu ni kupata radhi za Allah SW na si kinginecho.

Tukumbuke hali ya upinzani wa inadi aliyokutana nayo Mtukufu wa daraja Mtume SAAW, Ila hakufanya ulinganizi kwa kumridhisha yoyote bali aliyemtuma tu.

Miongoni mwa matukio ambayo yanayoonesha jinsi gani upande wa pili unapofikiwa na ujumbe, wapo wanaopinga kwa ujinga, lakini pia wapo wanaopinga kwa inadi/ makusudi. Na mifano ya inadi ni kama ifuatayo:

Tukio la kwanza, pale Mtume SAAW alipowalingania Mughira Ibnu Shuuba pamoja na wenzake. Katika tukio hilo pia alikuwepio Abu Jahal  ambaye alimtolea Mtume SAAW maneno makali kiasi cha kumfanya Mtume SAAW aondoke.

Baada ya Mtume SAAW kuondoka Ibnu Shuuba alimuuliza  Abu Jahal kuhusu utume wa Mtume SAW, na Abu Jahl kujibu kuwa anakubali kwa dhati kuwa Muhammad SAAW ni Mtume, ila wao wanalingana na Banu Hashim kwa kila kitu, sasa wao wataupata wapi utume?

Tukio la pili ni baada ya kusilimu aliyekuwa mwanazuoni mkubwa wa kiyahudi Abdallah bin Salaam, ambapo wanazuoni wengine wa kiyahudi waliitwa na Mtume SAAW kwa ushauri wa Abdallah ibnu Salam, ili kumuonesha Mtume SAAW uovu wa mayahudi. Baada ya Mtume SAAW kuwaita wanazuoni wale wa kiyahudi na kuwauliza juu ya Abdallah bin Salaam na baba yake. Kongamano lile la mayahudi wakajibu kuwa yeye (Abdallah ibnu Salaam) ni mtukufu wao zaidi, ni alim zaid kwao, yaani ni msomi mkuu. Kisha Mtume SAAW akawauliza mayahudi: je mutanikubali ikiwa yeye Abdallah bin Salaam amenikubali na kusilimu? Wanazuoni wa kiyahudi wakasema hilo hawezi kulifanya. Abdallah ibn Salaam kusikia kauli yao akajitoa alipojificha na kutangaza Uislamu wake kwao. Hapo hapo wanazuoni wale wa kiyahudi wakageuza maneno na kumwambia Mtume SAAW kwamba, Abdallah Ibnu Salaam ni mpumbavu na mjinga zaidi katika jamii  yao kama alivyokua baba yake.

Tukio la tatu ni kisa cha myahudi aliyekuwa akimuuguza mwanawe mgonjwa huku akimliwaza kwa kumsomea Taurat, kwa bahati Mtume SAAW alipita na kusikia kisomo kile cha Taurat, akamfuata yule baba na kumuuliza kuhusu kubashiriwa kwake SAAW ndani ya Tauraat, kwa inadi yule baba akajibu kuwa hamna wala hajaona kubashiriwa huko kwa Mtume SAAW, kwa bahati yule mtoto mgonjwa anaeuguzwa, palepale akajibu na kumwabia Mtume SAAW kuwa habari za utajo wake zimo.  Kijana yule mgonjwa alisilimu na alipofariki dunia kufuatia maradhi aliyokuwa nayo, Mtume SAAW alikwenda kumchukua na kumzika Kiislamu.

Walinganizi tujue ya kuwa katika ulinganizi kuna watu wataijua haki na ukweli na hawatoibeba kwa sababu zao wenyewe, na wataamua kupambana na daawah kwa sampuli tafauti.

Ni hatari kwa walinganizi kuielekeza daawa kutaka kuwaridhisha watu fulani au kundi Fulani, kwani kufanya hivyo watakengeuka katika njia. Aidha, hatari zaidi ni kuanza kuufikiria upande wa pili unapanga nini juu ya ulinganizi, kwani jambo hilo pia litawarudisha nyuma walinganizi wasifanye daawa kwa kuchelea kuwaudhi au kuhisi kila ujumbe wanaoufikisha ni mkali au haujafika muda wake.

 

Afisi ya Habari –   Hizb ut- Tahrir Tanzania

 06 Jumada al-thani 1439 Hijri   | 22-02-2018 Miladi

                        

 

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.