Waislam na Wanadamu izingatieni Vyema Siku Hii

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

             Tumeingia katika Siku tukufu ya  Eid ul-udh- hiya. Licha ya majeraha makubwa yaliotusibu ndani ya  Ummah wetu, tunamshukuru Allah Taala kwa kila hali.

Enyi Waislamu:

Kwa hakika Eid hii kubwa imeshikamana na kumalizika ibada tukufu ya Hijja. Ibada aliyopewa agizo Nabii Ibrahim (As) awatangazie watu ili waende Makka kuhiji.  Aidha, Eid hii inaambatana na tukio kubwa la muhanga wa Nabii Ibrahim (As) kumtoa muhanga mwanawe Nabii Ismail (As) kwa amri ya Allah Taala.

Tukio la Nabii Ibrahim (as) kutekeleza agizo la kuwatangazia watu Hijja, tena watu asiowaona wala wao kusikia sauti yake ni dalili tosha kuwa katika utekelezaji wa maagizo ya Allah Taala, akili zetu huwa hazina maamuzi wala haifai kupima matokeo/ natija. Bali mara baada ya kufahamu tulichoagizwa ni kutekeleza tu.

Aidha, tukio la muhanga wa Nabii Ibrahim (As) kuwa tayari kumchinja mwanawe Nabii Ismail (As) ni funzo kubwa kwetu la kujitolea muhanga katika hali zote, na katika utekelezaji wa amri za Muumba haifai kutanguliza maslahi wala kupima kwa vipimo vya akili zetu. Kwa kuwa Nabii Ibrahim (As) angeweza kuhoji kiakili kwanini amchinje mwanadamu, tena mtoto mdogo wa pekee kwa muda huo. Lakini hakufanya hayo ila alinyenyekea, kwa kuwa ilikuwa ni amri kutoka kwa Muumba.

Enyi Waislamu :  

Eid hii yetu ya leo tunayoisherehekea kihakika haina furaha kamilifu, bado sehemu ya Ummah wa Kiislamu na wanadamu kwa jumla wamo katika mashaka, idhilali, misiba, majonzi na huzuni kubwa.  Kama vile ndugu zetu wa Syria, Palestina, Iraq, Misri, Afghanistan, Somalia, Yemen nk. Ambapo madola makubwa ya kibepari yakiongozwa na Marekani kwa kushirikiana na watawala madhalimu na vibaraka katika miji ya Waislamu wanaua bila ya huruma hata watoto wadogo wa shule wasio na hatia yoyote. Aidha, maeneo yetu ya Afrika Mashariki vitendo vya ukatili, mateso, idhilali na kusekwa Waislamu ndani ya majela vinaendelea kupamba moto usiku na mchana kwa kisingizio cha sheria ya kibaguzi ya ‘Ugaidi’ na kutokamilika kwa ushahidi.

Enyi Waislamu na Wanadamu kwa jumla:

Katika Hijja ya mwisho ya Mtume SAAW, katika kulinda na kutetea ustawi wa mwanadamu alihadharisha kujiepusha na mambo mengi, kama umwagaji damu, uchumi wa riba, kudhulumu pia suala la ubaguzi , sehemu ya khutba ya Mtume SAAW katika Hijja hiyo alisema:  “Hakuna mbora kati ya muarabu na asiyekuwa muarabu, wala mweupe kwa mweusi. Au mweusi kwa mweupe ila kwa ucha Mungu’.

Leo chini ya mfumo wa kibepari mambo yote tuliyohadharishwa, na mengine mengi mfano wake yameenea kila mahala kiasi cha kuangamiza ustawi wa binadamu katika kila kipengee iwe siasa, uchumi, jamii nk.

Kwa wasiokuwa Waislamu ni muda muwafaka sasa kutafiti na kuchunguza Uislamu kwa jicho la uadilifu na kuyapokea mafundisho ya Mtume SAAW kuwa ukombozi wa kweli kwa ubinadamu. Tunakuombeni itumieni siku hii tukufu kulitafakari jambo hilo. Kwa Waislamu, yabebeni mafundisho hayo kwa ukamilifu kwa kufanya kazi ya kurejesha chombo cha kuyasimamia, nacho ni dola ya Khilafah Rashidah inayopaswa kuasisiwa katika  ardhi kubwa za Waislamu kwa kutumia njia ya mvutano wa kifikra na kisiasa bila ya kuhusisha utumiaji nguvu, silaha wala mabavu, kisha dola hiyo kuenea  maeneo yote.

Mwisho, tunawapa Umma wote wa Kiislamu mkono wa Eid hii kubwa na tukufu
                                 KULU AMMU WA ANTUM BILKHAIR   –           EID MUBARAK

#UislamNiHadharaMbadala

 

Dhul-hijjah 1439 Hijria

Front Page

https://web.facebook.com/HtTanzaniaa/

Maoni hayajaruhusiwa.