‘Usomi’ Mzigo Kwa Ummah

Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2018 kama yalivyokwishatangazwa, yamepokewa kwa hali mbili tofauti ikiwemo furaha na huzuni, matumaini na kukata tamaa. Waliofanya ‘vizuri’ pamoja na shule zao husifiwa na kusemwa ni wajuzi wenye akili. Waliofanya ‘vibaya’ hujiona na kuonwa ni “vilaza” wasiokuwa na akili ambao wamekwisha kwama kimaisha.

Hapana shaka kuwa elimu ni nyenzo msingi ya kuinua ustawi wa kiutu kibinafsi na jamii yake kwa jumla. Na juhudi zinafanyika kwa kuweka mikakati madhubuti na ya kipaumbele kwa kila taifa kuelimisha watu wake. Lakini jitihada hizo hazigusi uhalisia, bali zimebaki kuwa ndoto na zisizokuwa na matunda mazuri.

Baada ya matokeo hayo, waliofaulu ndio hupewa nafasi za kuendelea na masomo kwa ngazi za juu wakiwaacha waliofeli mitaani wakiendesha maisha na kuwatumikia walio ‘faulu’. Lakini wasomi hao wanaoendelea na masomo watakuwa na tija kwa jamii kwa ujumla? Bila ya shaka hawatokuwa, kutokana na mfumo huu wa kielimu kukosa fungamano la kweli la maisha haya na maisha yajayo.

Ajabu ni kwamba ‘watawala’ na wasimamizi wa mifumo ya elimu hawataki kukubali uhalisia kwamba ufaulu unaoshangiliwa hauakisi yanayoshuhudiwa katika jamii.

Wasomi hao ambao baada ya masomo katika ngazi za juu hatimaye huajiriwa na kuwa wataalamu na viongozi wa jamii kuwaongoza na kuwasimamia walio ‘feli’. Lakini baadhi wakifika vyuo vikuu kama wanafunzi hukubali kujidhalilisha miili na utu wao kwa ngono ili waendeleze sifa ya ‘kufaulu’.

Ndio wasomi hao watapokuwa walimu (wahadhiri) katika vyuo vikuu baadhi yao huhusianisha alama (marks) za ufaulu na udhalilishaji wa kingono (SAM-Sexually awarded marks). Yaani humtambulisha kuwa na akili (aliyefaulu) mwanafunzi aliyekubali kujidhalilisha kwake kingono.

Ndio wasomi hao baadhi yao kwa ‘utaalamu’ wao wakipewa vitengo vya Ummah hutoa maamuzi ya kudhuru jamii, mradi tu yana ‘manufaa’ kwao binafsi. Watachakachua miradi ya barabara, madaraja na vyombo vya usafiri na kuruhusu (kwa makusudi au kwa kutokujua) vitu ambavyo ni vibovu kuingia na kutumika katika jamii, kisha kuleta maafa.

Ndio wasomi hao baadhi yao wakipewa nafasi za kiuongozi hufanya maamuzi ya hovyo ambayo ni maumivu ya kudumu kwa jamii. Wakashindwa kutumia ‘elimu’ yao kusaidia Ummah bali uongo na hadaa ikawa ni sehemu muhimu ya ‘mafanikio’ yao. Hutoa maamuzi ya na maagizo ambayo utekelezaji wake huongeza kiza kwa Ummah.

Ndio wasomi hao baadhi yao hukataa kuingia katika ndoa (uundaji wa familia kiutu) na wachache watakaoingia watakuwa wauwaji wa watoto wao ili wasiingie duniani ati kujaza mesi zao. Wakawa na watoto wawili, mbwa watatu, walinzi na wafanyakazi zaidi ya 3. Na wakiwa madaktari hushawishi na kusaidia wengine ufungaji uzazi na kutoa mimba.

Kama alivyowahi kusema Shaikh Abdul Alaa Maududi alipokuwa akizungumza na wahitimu Waislamu katika chuo kimoja huko Pakistani waliomualika kama mgeni rasmi katika mahafali yao kwamba:

“Japokuwa mnafuraha lakini mimi ninawatazama kama watu mahututi sana waliomo miongoni mwa maiti wengi kwa kuwa tu bado mnapumua kwa mbali. Ni kwasababu elimu mnayosoma imewatoa katika uhalisia wa ubinadamu wenu kama inavyokuwa kwa mmea unapohamishwa kutoka udongo wake wa asili katika kitalu”.

Athari za elimu yoyote ni zao la fikra msingi (aidilojia tawala) inayoongoza jamii husika na ambapo mfumo wa elimu umeundwa kwayo.

Kwa bahati mbaya ulimwengu leo upo chini ya mfumo wa kibepari, ambao kigezo cha mafanikio ni kiwango cha mtu binafsi na jamii kukusanya maslahi. Pia upo chini ya tawala za kidemokrasia ambapo fikra na mawazo ya watu ndio hutumika kuwapangia na kuwaongoza watu kuishi kwa mujibu wa hayo. Matokeo yake elimu chini ya mfumo huo imetenganisha kabisa kando utu kutoka katika akili, ukaifanya akili ijengeke katika unyama. Mtu akakuzwa kinyume na uhalisia wa utu wake, akajikuta aliyojazwa kichwani humfanya adhalilike na kuwa mzigo kwa jamii badala ya kuwa suluhisho.

Mbadala wa ubepari ni Uislamu. Elimu katika Uislamu inajenga akili katika kuzidi kuutambua zaidi uasili wa mtu na utu wake.
Allah Taala Anasema:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ (العلق: 1

Soma kwa Jina la Mola wako Ambaye Ameumba (kila kitu).” (TMQ 96: 1)

Elimu kwa namna hii kila ukijifunza ndivyo utambuzi wako hukua. Humpa mtu mwanga wa wazi kwamba asili yake ni kiumbe cha Mungu, Muumba. Kukua kwa utambuzi kimsingi ni kukua katika kutambua nafasi msingi kila mtu aliyonayo duniani. Na kwamba kusoma na kufaulu hakumaanishi ubora kwa wengine bali ni kuongezeka jukumu kwa Ummah. Jukumu la kuufanya Ummah uishi kwa mujibu wa matakwa ya Muumba wao.

Hamza Sheshe

#UislamuNiHadharaMbadala

Maoni hayajaruhusiwa.