Tumuenzi Mtume (Saaw) Kwa Kujipamba Kwa Sifa Zake

 (15:قَدْ جَاءَكُمْ مِنْ اللَّهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُبِينٌ (المائدة

Bila ya shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na kitabu chenye kubainisha (kila kitu)(TMQ 5:15)

Katika mwezi huu wa Rabil awwal, mamilioni ya Waislamu ulimwenguni kote huadhimisha mazazi/uzawa ya kipenzi chetu Mtume SAAW. Wakati kama huu ni muhimu kujikumbusha sifa na mwenendo wake hususan sifa kubwa na nyeti ya kubeba risala tukufu ya Uislamu aliyotumwa nayo kwa ajili ya walimwengu wote.

Katika kufanya kazi ya kuibeba, kuilinda na kuitetea risala aliyotumwa nayo Mtume SAAW alijipamba na sifa mbali mbali tukufu.

Miongoni mwao ni huruma, ushujaa, subra, muhanga na ujasiri. Sifa zake hizi zimedhihirika katika matukio mbali mbali kiasi cha kutambulika na kila mtu hata na maadui zake.
Amma kuhusu huruma yake, inaonekana waziwazi pale mtoto mmoja ndani ya Madina wakati alipofiliwa na ndege wake wa kufuga, na akajawa na majonzi na huzuni kubwa kwa kumkosa ndege wake huyo aliyemzoea sana. Mtoto huyu akaaamua kwenda kwa Mtume SAAW kupata faraja na maliwazo. Akaanza mtoto huyu kumsimulia kisa chote kwa Mtume SAAW. Nae Mtume SAAW akamliwaza mtoto huyo kwa mkasa huu uliomfika, na akaamua kuzunguka nae mtoto huyu katika mitaa ya mji wa Madina kama mbinu ya kumpa maliwazo na kumuondolea huzuni na majonzi yaliyomgubika.

Katika kitendo hiki cha Mtume SAAW kunadhihirika mambo mawili makubwa: Kwanza, mahusiano yake mazuri na ya karibu kwa watu wa marika yote hata watoto wadogo. Pili, huruma yake ya kiwango cha juu kwa Ummah wake, hata kwa watoto wadogo kama hawa. Hebu leo tafakari Mtume SAAW angekuwa na huruma kiasi gani kwa watoto wanaolia usiku na mchana kwa huzuni na majonzi ndani ya Syria, Palestina, Iraq , Afghanistan, Somalia, Pakistan, Burma, Misri nk, huku wakiona maiti za wazazi wao na kudhuriwa wao binafsi kwa mabomu na dhulma ya wazi kutoka kwa mayahudi na madola mengine ya Magharibi kama Marekani, Uingereza na wasaidizi wao?

Ikiwa Mtume SAAW aliacha shughuli zake na kujishughulisha kumliwaza mtoto mmoja alieondokewa na ndege wake, jee angeliwaacha watoto hawa bila ya huruma, kuwalinda na kuwatetea watoto hawa wa kiislamu wanaogubikwa na dhiki kuanzia ya vita na majanga ya kimaumbile kama njaa, matetemeko, mafuriko nk. kama wanavyofanya viongozi waovu vibaraka katika ulimwengu wa kiislamu. Na uovu na lakutia uchungu mkubwa zaidi, vibaraka hawa wanashirikiana kamwe na makafiri kuwapa msaada wa kijeshi, kisiasa na kistretejia kuendelea kuvamia na kukalia kimabavu biladi za kiislamu na kusababisha maafa kwa ummah mzima. Ni wapi na wapi hali zao na huruma ya kipenzi chetu Mtume SAAW?

Kuhusiana na sifa ya ushujaa, tunamuona Mtume SAAW katika Vita vya Hunain namna alivyosimama kidete, baada ya Waislamu kughurika na idadi ya jeshi lao kubwa na kujawa na matumani ya ushindi dhidi ya maadui zao Bani Hawazin. Ghafla mambo yakawageuka na wakavamiwa kwa mishale kama mvua na wakaanza kukimbizana na kuuwacha uwanja wa mapambano na Wislamu wachache! Mtume SAAW kwa ushujaa mkubwa akaamrisha Waislamu waitwe warudi katika medani na yeye binafsi akasimama akajinadi katika kurejesha morali ya mujahidinna, kwa kusema:

“Mimi ni Mtume wa Allah wala si urongo, mimi ni mwana wa Abdul- Muttalib!”

Mtume SAAW alichukua hatua hiyo ambayo ni ya aina yake katika tareekh ya wanaadamu! tahamaki, Waislamu waliokimbia vita wakaanza kukumbuka ahadi waliochukuwa kwa Mtume SAAW kwamba watakuwa nae katika raha na shida na hapo wakaanza kurudi tena katika medani ya vita. Waislamu wakapigana kwa ushujaa na ujasiri hatimae wakaweza kuwashinda maadui zao. Hii ni sifa tukufu isiyo na kifani kutoka kwa kiongozi wetu. Kwa bahati mbaya, na kwa masikitiko makubwa watawala katika ulimwengu wa Kiislamu leo ni kinyume kabisa na hali hii. Wangekuwa na ushujaa kama huu, makafiri wasingethubutu kuwapiga Waislamu na kuzivamia biladi zetu wakiingia na kutoka kama majumbani mwao. Au kijidola dhaifu cha mayahudi kilichozingirwa na pande zake zote na Waislamu kingekuwa kimeshasahauliwa katika kifusi cha historia. Lakini ushujaa wa vibaraka katika ulimwengu wa Kiislamu ni katika kuwatoa kafara raia wao na ardhi zao kwa makafiri maadui wa Allah SW na Mtume wake SAAW, kama inavyofanya Pakistan na Sudan kuitoa muhanga Sudan ya Kusini. Na huku vibaraka hao hujifanya wamahiri wa kuropokwa uwongo ati kughilibu Umma, ilhali hawaghilibu ila nafsi zao.

Na mwisho, sifa ya subra, muhanga na ujasiri wa Mtume SAAW, zinadhihirika katika matukio mbalimbali. Mfano mzuri ni katika vita vya Ahzab katika mwaka wa sita Hijria. Katika maandalizi ya vita hivyo masahaba walilalama na kushtakia njaa kwa Mtume SAAW, na kila mmoja wao akafunua na kuonesha jiwe alilolifunga kwenye tumbo lake kwa ajili ya kupata uzito, mara Mtume SAAW akafungua tumbo lake wakamkuta nae amefunga mawe matatu! Hapa inadhihirika subra, muhanga na ujasiri usio na mfano kwa ajili ya haki. Aidha, tukio hili ni kielelezo cha siasa ya kiongozi mkweli na muadilifu, kwa kuwa yeye huwa wa kwanza kutaabika ili raia wake wapate amani na utulivu, kinyume na viongozi tulionao katika siasa potofu za kibwanyenye za kidemokrasia, wao hutanguliza matumbo na mifuko yao, familia zao na wapambe wao bila ya kujali wala kubali raia wanaowatumikia. Na kubwa zaidi viongozi hawa hufurahi kamwe kuwaona raia wanadhikika, na huwatia katika dhiki kwa kuwaongezea mzigo wa kodi na mengineyo wanapoona wananufaika na kufarajika.

Tunapoendeleaa kukumbuka mazazi ya Mtume wetu SAAW, haitoshelezi tu kutaja sifa zake njema kwa malengo ya kujifurahisha na kujiburudisha. Bali lazima tumuangalie yeye kama ruwaza/kigezo njema katika maisha yetu yote huku tukiambatanisha kuienzi kwa kuifanya kazi tukufu aliyoifanya ya kuunusuru ubinaadamu. Aidha, tukumbuke kwamba tumeamrishwa na sheria kuchukua yote aliyokuja nayo na kuyawacha yote aliyotukataza.

وَمَا آتَاكُمْ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ).

“Na yote mliyopewa na Mtume chukuweni, na anachowakatazeni kiwacheni. Na mcheni Allah, kwani ni Mkali wa kaudhibu” (TMQ 59:7)

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

09 Rabi al awwal 1440 Hijri | 17-11- 2018 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

 

Maoni hayajaruhusiwa.