Watoto Katika Uislamu

    Uislamu ni dini iliyoteremshwa na Allah (swt) kwa wanadamu wote, kila sehemu, na kila zama. Kwa ajili hiyo, Uislamu uko wazi kwa kila mtu na unatilia maanani umuhimu wa heshima, haki, na majukumu. Aya za Quran na Hadith sahih za Mtume Muhammad (saw) zina jumuisha haki na majukumu kutoka Allah (swt) kwa wanadamu. Kamwe hayategemei matamanio na matakwa ya wanadamu, wake kwa waume, hivyo basi hayabadiliki. Haki hizi za kipekee zilizo tajwa na Uislamu hujumuisha pia haki za watoto. Haki za watoto hazikudhaminiwa na wazazi wao, jamii, serikali au hata mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali. Bali Allah (swt) mwenyewe ndiye Aliyedhamini haki hizi za watoto.

Uislamu umeweka mpangilio wa kisheria, na mkusanyiko wa maadili, yaliyoundwa kulinda haki za mtu binafsi ikiwemo haki ya kuishi ndani ya mujtama salama. Kwa watoto, usalama una umuhimu mkubwa. Haki za watoto zinaanza hata kabla ya kuzaliwa; kihakika huanza kabla ya utunzi wa mimba. Qur’an na hadith sahih za Mtume Muhammad (saw) zinaweka wazi kuwa watu wawili hawapaswi kuingia katika ndoa kiholela. Mazingatio na matayarisho makubwa ni muhimu kabla mume na mke kujitolea kukaa pamoja na kwa familia ambayo itatokamana na fungamano lao.

Kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, Mtume (saw) amesema:

روى أبو داود والنسائي عن أبي هريرة رضي الله عنه: قال النبي صلى الله عليه وسلم: تنكح المرأة لأربع لمالها ولحسبها ولجمالها ولدينها فاظفر بذات الدين تربت يداك

“Mwanamke huolewa kwa ajili ya mambo manne: kwa ajili ya mali yake, nasaba yake, urembo wake, na dini yake, chagua dhati ya dini mikono yako itajifunga (kutokamana na fitna).”

(Abu Dawud)

Ikiwa mume na mke wote wamejitolea maisha yao kumuabudu na kurimdhisha Muumba wao, basi wanapaswa kutambua kwamba haki za watoto wowote watakao kuwa nao kiasili zimedhaminiwa. Kumuabudu Allah (swt) humaanisha kutii maamrisho yake; na miongoni mwa maamrisho yake ni kuhifadhi haki za mtoto. Kupitia ndoa kinyume na uhusiano haramu wa zinaa wanandoa huwa tayari wameanza safari ya kuhifadhi haki za watoto wao wa siku za usoni ikiwa ni haki ya mtoto kuifahamu nasaba yake. Mimba ya mtoto pindi inapotungwa, ina haki ya kuishi. Qur’an imeweka wazi kuwa maisha ya kiumbe ni matukufu. Kamwe hairuhusiwi kuavya ‘kutoa’ mimba kwa hofu ya kutoweza kusimamia mahitaji ya kifedha ya mtoto au mtoto wa pili. Allah (swt) pekee ndiye mwenye kuruzuku na kuhuisha katika maisha.

Allah (swt) asema:

وَلا تَقْتُلُوا أَوْلادَكُمْ مِنْ إِمْلاقٍ نَحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ

...wala musiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunawaruzuku nyinyi na wao.

[Al- An’aam: 151]

Mtu anapofanya uamuzi wa kuavya ‘kutoa’ mimba ni muhimu kukumbuka kwamba kupata mtoto ni Baraka kutoka kwa Allah (swt) na Baraka zote mfano wa hii hazina budi kupokewa kwa furaha na shukrani. Kuna watu wengi ulimwenguni leo ambao hawana uwezo wa kupata watoto, hivyo basi ikiwa Allah (swt) ataibariki familia kwa mtoto, inatakiwa iwe ni sababu ya sherehe na furaha. Licha ya hayo watoto sio vinyago wala mali tu za kumilikiwa; kupata mtoto huja na jukumu kubwa nyuma yake.

Qur’an na hadith sahih za Mtume Muhammad (saw), zinazungumza waziwazi kuhusu jukumu la malezi ya mtoto. Ni wajib juu ya Waumini kuwalea na kuwajali watoto wao kwa kuwakuza kuwa watu wenye maadili mema na uchaji Mwenyezi Mungu. Kujenga utambuzi kwao kuwa wao ni miongoni mwa wanadamu wenye thamani kwa watu jumla na hususan kwa familia zao. Kupuuza jukumu hili hupelekea kumtoa mtu katika njia ya wema na kumueka mbali na radhi za

Allah (swt):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَئِكَةٌ غِلَظٌ شِدَادٌ لَّ يَعْصُونَ اللََّ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

Enyi mulioamini! Ziokoeni nafsi zenu na za jamaa zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Juu ya Moto huo kuna Malaika wakali wenye nguvu, hawamuasi Allah kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa.

 [At- Tahriim: 6]

Kutoka kwa Abdullah ibn ‘Umar amesema: nimemskia Mtume (saw) akisema:

عَنْ عَبْدِ اللَِّ بْنِ عُمَرَ يَقُولُ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَِّ صَلَّى اللَّ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ…: وَالرَّجُلُ رَاعٍ فِي أَهْلِهِ وَهُوَ مَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالْمَرْأَةُ   اعِيَةٌ فِي بَيْتِ زَوْجِهَا…وَمَسْؤولَةٌ عَنْ رَعِيَّتِهَا

…na mume ni mchungaji kwa watu wa familia yake na ataulizwa kutokana na anao wachunga, na mke ni mchungaji katika nyumba ya mumewe na ataulizwa juu ya anavyo vichunga

(Bukhari na Muslim)

Kuwajali na kuwalea watoto katika njia inayostahili ni jukumu kwa wazazi na daima si jambo rahisi hususan leo chini ya mfumo batili wa kimagharibi wa kirasilimali pamoja na maadili yake yaliyooza kama fikra za uhuru. Kihakika, Allah (swt) anatukumbusha katika Qur’an kuwa watoto huenda wakawa mtihani mkubwa kwa wazazi wao. Ushindi na majaribio katika maisha ni katika mitihani na watoto ni sehemu yake. Wanaweza kuleta furaha na huzuni kubwa vile vile. Allah (swt) asema:

إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَدُكُمْ فِتْنَةٌ وَاللَُّ عِنْدَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ

Hakika mali zenu na watoto wenu ni fitna. Na kwa Allah upo ujira mkubwa (Pepo).

[At-Taghaabun: 15]

Kufuata mafundisho ya Uislamu humwezesha Muumini kukabiliana na matukio yote ya kimaisha ikiwemo mitihani, fitna na ushindi. Nasaha sahihi ya Kiislamu juu ya malezi na kuwakuza watoto inajumuisha Nyanja zote za maisha. Ni nasaha tukufu kama ulivyo Uislamu wenyewe. Kuimarika upande wa kimwili, hisia na kiroho vyote vina umuhimu sawa. Ni muhimu kutilia maanani kuwa Uislamu daima umejumuisha haki za watoto. Mtazamo wa Uislamu kuhusu utoto unaeleza kuwa ni kipindi cha kipekee katika uhai wa mtu. Hii ni kinyume na mtazamo wa mfumo wa batil wa kimagharibi ambapo fikra ya utoto haikuzungumziwa mpaka katika karne ya 16. Sio kuwa wamagharibi hawakuwa na watoto au vijana bali waliwachukulia kuwa watu wazima wachanga walio na mahitajio na matakwa sawa na watu wazima wapevu.

Katika historia yote ya Uislamu na katika fasihi ya Kiislamu haki na majukumu yanayo husiana na watoto yamefafanuliwa kwa uwazi. Wazazi, familia, na jamii wana majukumu maalumu juu ya watoto. Mengi yao yakiwa ya wajib, na siku ya Qiyama, Allah (swt) atawauliza watu wazima kuhusu jinsi walivyo watendea watoto wao.

Watoto wetu ni amana tuliyopewa na Allah (swt). Hivyo basi, kwa muktadha huu, wanatakiwa wapewe lishe bora, wavishwe vizuri, waongozwe kiroho na wafuatiliwe kwa makini katika fahamu zao (Aqliyya) na utendaji wao (Nafsiyyah). Wanapaswa kukuzwa kwa thaqafa imara ya Kiislamu ili kuzalisha ndani yao utambulisho ‘shakhsiyya’ wa Kiislamu wenye uwezo wa kuubeba Uislamu kama fikra na njia, na kuwatayarisha katika njia hiyo, kwa jukumu kubwa la ubebaji ulinganizi wa kuregesha tena maisha kamili ya Kiislamu kupitia kusimamisha tena dola ya Khilafah kwa Njia ya Utume.

Masoud Salim Mazrui

Mwanachama wa Hizb ut Tahrir

Kenya

Inatoka Jarida la Uqab: 10

https://hizb.or.tz/2017/11/01/uqab-10/

Maoni hayajaruhusiwa.