Mkataba wa Hilf Al-Fudhoul Utuongeze Hima Kuendelea Kutetea Mahabusu

بسم الله الرحمن الرحيم

Katika zama za Jahilia wakati Mtume SAAW kabla hajapewa Utume baadhi ya makabila makubwa ndani ya Makkah walifanya makubaliano ya mkataba unaoitwa Hilf al-Fudhoul wenye lengo la kupambana na dhulma na kuwatetea wanyonge, wageni na wanaodhulumiwa. Mkataba huo ulifanyika wakati Mtume SAAW akiwa bado kijana sana akijumuika na ami yake kwa kushiriki kikamilifu katika kikao kilichopelekea makubaliano ya mkataba huo.
Na mara baaada ya Mtume SAAW kupewa Utume aliyataja, kuyasifu na kuunga mkono kwa dhati makubaliano hayo. Mazingira yaliyopelekea makubaliano ya mkataba huo yalikuwa kama hivi :
Mfanyabiashara mmoja wa Yemen kutoka kabila la Zabid alileta bidhaa na biashara zake ndani ya mji wa Makkah akampatia bidhaa zile mmoja katika mabwanyenye wa Makka kwa jina la Ass bin Wail Al-Sahm (baba wa sahaba mkubwa Amr ibnul Ass). Bwana huyu kwa kujiona ni katika watu wenye athari na ushawishi mkubwa ndani ya Makka na kuona kwamba mfanyabiashara huyu ni mnyonge na mgeni mjini pale hana wa kumtetea alikataa kumpatia malipo ya bidhaa alizochukua kutoka kwake.
Mfanyabiashara yule kutoka Yemen akajaribu kila hali kumshawishi bwana Ass bin Wail ampatie haki yake lakini akakataa kumpatia haki yake hiyo. Mfanyabiashara huyo kutoka Yemen akajaribu kupita huku na kule kutaka kuungwa mkono na Makureishi na kutoa kilio chake kwa watu wa Makka ili wamsaidie ili aweze kupata haki yake lakini ilishindikana.
Hata hivyo, mfanyabiashara huyo bado alifanya ujasiri hakukata tamaa katika kutafuta haki yake aliendelea kufanya jitihada kwa kupanda juu ya mlima unaoitwa Abu Qubays karibu na Masjid Haram, hapo akanadi tena na tena kwa mashairi akipaza sauti ya kilio na masikitiko yake juu ya dhulma aliyofanyiwa katika biashara yake.
Hatimaye ami wa Mtume SAAW bwana Al-Zubayr bin ‘Abd al-al-Muttalib akaguswa na kilio na hali ya dhulma aliyotendewa mfanyabiashara yule akaona kuna haja ya kuchukua hatua ya kumpigania haki yake na kuzuiya dhulma kama zile zisitokee.
Bwana Al-Zubayr bin ‘Abd al-Muttalib akayakusanya baadhi ya makabila mashuhuri ndani ya Makka, kama vile: Banu Hashim, Banu l-Muttalib, Banu ‘Abd Manaf, Banu Zuhra bin Kilab, Banu Taym bin Murra, Banu Asad bin Abd al-‘Uzza bin Qusay na kuitisha kikao maalum katika nyumba ya bwana Abd Allah bin Jud’an al-Taymi kuzungumzia namna ya kumsaidia mfanyabiashara yule lakini pia kuja na maazimio ya kutowadhulumu watu haki zao.
Maazimio muhimu ya kikao kile yalikuwa:
a. Mtu yoyote hususan mgeni asidhulumiwe haki yake kwa namna yoyote.
b. Lau kuna mtu kadhulumiwa na kuna mtu hataki kumpa haki aliyemdhulumu, makabila ya mkataba huo yasimame dhidi ya dhalimu, kwa ajili ya kumtetea aliyedhulumiwa.
Mkutano ule ndio uliozaa mkataba wa makubaliano adhimu (Hilf alfudhoul) ambayo Mtume SAAW baada ya kupewa Utume aliyasifu na kuyaunga mkono kwa kusema:
“Nilishuhudia makubaliano katika nyumba ya Abd Allah bin Jud’an ambayo kamwe nisengependa kuyavunja hata kama nikipewa ngamia wote wekundu. Lau leo ningeitwa tena ( kwa makubaliano kama yale) basi ningekubaliana nayo.”
Mafundisho matatu makubwa yanapatikana katika tukio na mchakato wa kupatikana mkataba huu:
Kwanza, lau mfanyabiashara wa Yemen aliyeleta bidhaa zake Makka na kudhulumiwa angekata tamaa na kwa kujiona mnyonge, dhaifu na mgeni pale Makka bila ya kupaza sauti yake kupigania haki yake na kupambana na dhulma basi angemalizia kwa kukosa haki yake daima.
Pili, wakati wote katika maisha ya wanadamu kuna watu ambao huguswa na kuchukizwa na dhulma kwa misingi ya ubinadamu, na huwa wako tayari kwa hali zote kusimama kidete kuwasaidia wanaodhulumiwa dhidi ya madhalimu.
Tatu, ni namna Uislamu usivyopenda dhulma, na ndio maana Mtume SAAW akasema hata angeitwa tena katika mkataba ule wa kupambana na udhalimu basi angeunga mkono makubaliano yale. Hilo ni fundisho la kudumu kwetu kusimama imara kuwatetea waliodhulumiwa na kuwapinga madhalimu.
Tukio hili lizidishe hima na ghera yetu kusimama kukataa dhulma kwa sura zake zote. Na katika kipindi hiki liwe chachu ya kutia nguvu kutetea ndugu zetu walioko mahabusu, ili kesi zao zisikilizwe, wapate dhamana au waachiwe huru.
Risala ya Wiki No. 82
29 Dhu al-Qi’dah 1441 / 20 Julai 2020 Miladi

Maoni hayajaruhusiwa.