Je, Yajuzu kwa Mwanamke Kafiri Kutawalishwa Ukadhi wa Shariah?

بسم الله الرحمن الرحيم

Msururu wa Maswali Yaliyo Wasilishwa kwa Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut Tahrir katika ukurasa wake wa Fiqhi wa Facebook

Jibu la Swali

Je, Yajuzu kwa Mwanamke Kafiri Kutawalishwa Ukadhi wa Shariah?

Kwa: Husam Y Dawoud

Swali:

Assalam Aleykum wa Rahmatullah wa Barakatuh. Sheikh mpendwa, natumai Mwenyezi Mungu atakamilisha amri yake mikononi mwenu na atukirimu kwa Dola ya Khilafah karibuni, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu juu ya hilo… na hapa nina hamu ya kujua hali katika kusimama Dola yetu je, tutampa mwanamke kafiri mamlaka ya kuwa Kadhi wa Shariah?

Niko na swali, imetajwa katika kitabu cha Nidhamu ya Kijamii ukurasa 91 kwamba yajuzu kwa mwanamke kuwa na mamlaka ya kuhukumu kwa lafdhi ya hadith ambayo ni jumla,

«لنْ يُفْلِحَ قومٌ ولَّوا أمرَهُمُ امرأةً»

“Hawatafaulu watu watakaompa mwanamke mamlaka ya mambo yao”, na kikasema hii ni dalili ya kujuzu kwake kuwa kadhi… imenipitikia mawazoni mwangu; kwamba mwanamke kafiri au katika watu wa kitabu yajuzu kwake kuwa na mamlaka ya kuhukumu… wala sijawahi kupata andiko kuwa mwanamke asiyekuwa Muislamu alitawalishwa ukadhi katika Uislamu kwa wale waliotangulia… ni nini maana ya hilo? Na je, yajuzu kwa mwanamke kafiri kuwa na mamlaka ya kuwa kadhi wa Shariah? Na hapa nakusudia (sheria ya) hali za kibinafsi; ndoa, talaka… na tumefafanua maana ya ukadhi kuwa ni ujulishaji hukmu kwa njia ya ulazima… na je, kutoitakidi hukmu ni njia ya ulazima? Na kuhitimisha nataraji utakuwa na subira kwa swali hili na utanifikishia jibu la kutosheleza. Na daima muwe katika kheri elfu moja na namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwingi wa uwezo awahifadhi kutokana na kila ovu.

Husam Dawoud / Palestina

Jibu:

Waaleykum salaam wa rahmatullah wa barakatuh,

Inaonesha kana kwamba unaashiria andiko lifuatalo katika kitabu, Nidhamu ya Kijamii mlango “Kazi za Mwanamke”:

(… Isipokuwa kwamba haijuzu kwa mwanamke kuchukua wadhifa wa utawala, hasi hawezi kuwa raisi wa dola, wala Mu’aawin (msaidizi) wake, wala Wali (gavana), wala ‘Aamil (meya wa mji), wala kazi yoyote inayo chukuliwa kuwa ya utawala, kutokana na yale yaliyo simuliwa kutoka kwa Abu Bakrah aliyesema: Pindi habari zilipomfikia Mtume (saw) kwamba watu wa Fursi wamemtawaza ufalme binti ya Kisra alisema:

«لنْ يُفْلِحَ قومٌ ولَّوا أمرَهُمُ امرأةً»

“Hawatafaulu watu watakaompa mwanamke mamlaka ya mambo yao”, [Imepokewa na Bukhari]. Na hii iko wazi katika katazo la kumpa mwanamke utawala kwa kuwashutumu wale wanaotawalisha mambo yao kwa wanawake. Na mtu mwenye mamlaka (Wali al-amr), ni mtawala asema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ﴿

“Enyi mlio amini! Mt’iini Mwenyezi Mungu, na mt’iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi”. [An- Nisaa`: 59]

Hivyo basi mamlaka ya utawala hayajuzu kwa wanawake, ama usiokuwa utawala yajuzu kumpa mamlaka hayo mwanamke. Kwa hayo, yajuzu kwa mwanamke kuteuliwa katika nyadhifa za utumishi wa umma katika dola, kwa sababu hizi sio katika utawala bali zinaingia katika mlango wa ajira, hivyo basi mfanyikazi huyo ni mwajiriwa wa kibinafsi wa serikali, na yeye ni kama mwajiriwa wa mtu au shirika lolote, na inajuzu kwake kuwa kadhi kwa sababu kadhi si katika watawala bali yeye huondoa utesi baina ya watu, na huwajuza hukmu ya kisheria wanaozozana kwa njia ya ulazima. Hivyo basi ufafanuzi wa ukadhi ni ujulishaji hukmu kwa njia ya ulazima. Hivyo basi kadhi ni mfanyikazi na sio mtawala, yeye ni mwajiriwa wa dola kama waajiriwa wengine. Na imesimuliwa kutoka kwa Umar bin Al-Khattab kwamba alimpa mamlaka al-Shifa – mwanamke katika jamaa zake – ya soko yaani kadhi wa masoko (Qadhi al-Hisbah ambaye anahukumu juu ya ukiukaji wote. Na kwamba suala la mwanamke kujuzu kuwa kadhi linahusiana na andiko la hadith hiyo na kutekelezeka juu ya uhalisia wa wadhifa wa kadhi. Ikiwa hadith ya katazo la kumpa mwanamke utawala inatabikika juu ya ukadhi basi kumpa mamlaka hayo ya ukadhi itakuwa haijuzu, na ikiwa haitabikiki juu yake basi hadith hii haitasihi kuwa ni dalili ya kumkataza kuwa kadhi. Na tunapoiangalia hadith hii tunapata kuwa Mtume (saw) aliwashutumu watu waliotawalisha mambo yao kwa mwanamke, kama jibu kwa yale yaliyomfikia kwamba watu wa Fursi wamemtawaza ufalme mwanamke juu yao, hii ni taaliki juu ya habari, na mahali pa jibu la swali. Hivyo hii ni maalum kwa maudhui ya uraisi wa dola, na maana yake ni utawala. Hii ni kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine katazo limenasibishwa na utawala jumla, kwa sababu huo ndio utawala wa mambo (ya watu). Hii ndio maana ya hadith hii na lile inalofahamisha. Ama maudhui ya ukadhi ni kazi ambayo yatofautiana na kazi ya Khalifah na Wali (gavana). Kazi ya Khalifah na Wali ni utekelezaji hukmu moja kwa moja kwa upande wake, sawa iwe kadhia imeletwa kwake, au kuletwa kwa kadhi, au iwe kadhia haikuletwa kwake na yeyote, lakini akaona kuwa kuna ukiukaji wa sheria, basi atahukumu ukiukaji huo pasi na kuwepo mlalamishi na atatekeleza hukmu juu yake kwani yeye ni mtekelezaji. Ama kadhi yeye hana uwezo wa kuhukumu isipokuwa inapopatikana kesi, kupitia mlalamishi kumpelekea kesi, na kukawa na watesi wawili. Basi atahukumu kesi hiyo. Na hakuna atakalofanya endapo hakutakuwepo na mlalamishi. Na kwa mtazamo wake wa kadhia, atajulisha hukmu ya kisheria katika kadhia hiyo kwa njia ya ulazima, wala kamwe hana mamlaka ya utekelezaji, isipokuwa ikiwa ameteuliwa kama mtawala na kadhi wakati huo huo, basi hapo atatekeleza kwa sifa yake kama mtawala na atahukumu kwa sifa yake kama kadhi. Na kwa hilo, uhalisia wa ukadhi sio uhalisia wa utawala, hivyo hadith hii haitabikiki juu ya kadhi…” Mwisho.

Swali lako ndugu yangu haliko wazi na ndani yake mna mambo yaliochanganyika, je unauliza kuhusu hukmu ya kumpa mamlaka ya ukadhi wa Kisheria mwanamke kafiri katika upande wa kuwahukumu baina ya Waislamu? Au unakusudia hukmu ya kumpa mwanamke mamlaka ya ukadhi kuhukumu baina ya makafiri katika watu wa dini yake katika mambo ya ndoa na talaka ambayo Shariah imejuzisha kuhukumu kwao katika mambo hayo kwa mujibu wa dini zao?

1- Ama kuhusu hali ya kwanza nayo ni kuhukumu baina ya Waislamu, hiyo haijuzu kwa mwanamke kafiri kuwa kadhi baina ya Waislamu katika swala lolote kama ambavyo haijuzu kwa mwanamume kafiri kuwa kadhi baina ya Waislamu katika suala lolote na hilo ni kwa sababu masharti ya kadhi wa kisheria ni awe ni Muislamu sawa awe ni mwanamume au mwanamke, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

  وَلَنْ يَجْعَلَ اللَّهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلاً﴿

“…Wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini. [An-Nisa: 141]. Hivyo ndani yake kuna katazo la kukatikiwa kwa sababu semi hii ina herufi “Lan (kamwe)” ambayo inaashiria mwiko, ni maelezo kwa maana ya ombi, na maadamu Mwenyezi Mungu ameharamisha kafiri kuwa na mamlaka juu ya Waumini basi ameharamisha kumjaalia kafiri kuwa kadhi anayehukumu baina yao, kwani katika kuhukumu ni kuwa na mamlaka juu ya Waislamu. Na tumetaja sharti la Uislamu upande wa kadhi katika zaidi ya sehemu moja katika vitabu vyetu, kwa mfano:

– Katika kitabu cha Taasisi za Dola ya Khilafah mlango “masharti ya makadhi”:

(Ni sharti kwa yeyote anayechukua wadhifa wa ukadhi awe: Muislamu, mtu huru, aliye baleghe, mwenye akili timamu, mwadilifu, msomi wa fiqhi, mjuzi wa kuvua hukmu juu ya uhalisia.) Mwisho.

– Katika kitabu cha Utangulizi wa Katiba, Juzuu ya kwanza:

(Kifungu cha 78: ni sharti kwa yeyote anaye chukua wadhifa wa ukadhi kuwa: Muislamu, mtu huru, aliye baleghe, mwenye akili timamu, mwadilifu, msomi wa fiqhi, mjuzi wa kuvua hukmu juu ya uhalisia. Ni sharti kwa yeyote anaye chukua wadhifa wa kadhi mwenye kutatua dhulma za watawala kwa raia (Kadhi al-Madhaalim) awe na masharti ziada ya haya awe mwanamume na awe Mujtahid.

Dalili zake ni dalili iliyo tangulia ya kadhi mkuu, isipokuwa si sharti kwa kadhi anaye tatua tetesi wala kadhi wa masoko awe mwanamume, bali yajuzu kuwa mwanamke; kwa sababu yeye si mtawala bali ni kadhi, yaani yeye ni mjulishaji tu wa hukmu ya kisheria na sio mtekelezaji wake; na kwa hilo hadith:

«لَنْ يُفْلِحَ قَوْمٌ وَلَّوْا أَمْرَهُمُ امْرَأَةً»

“Hawatafaulu watu watakaompa mwanamke mamlaka ya mambo yao”, iliyo pokewa na Bukhari haitabikiki juu yake, kwani hiyo ni katika mamlaka ya utawala, na sababu ya hadith hii ni tukio la watu wa Fursi kumtawaza ufalme mwanamke juu yao. Kutoka kwa Abu Bakrah amesema: Pindi ilipomfikia Mtume (saw) kwamba watu wa Fursi wamemtawalisha ufalme binti wa Kisra alisema:

«لَنْ يُفْلِحَ قَوْمٌ وَلَّوْا أَمْرَهُمُ امْرَأَةً»

“Hawatafaulu watu watakaompa mwanamke mamlaka ya mambo yao” imepokewa na Bukhari. Hivyo basi sababu ya kauli ya hadith hii ni maudhui maalum yaliyo tajwa waziwazi katika andiko la hadith nayo ni utawala yaani mamlaka, na ukadhi sio katika utawala, hivyo basi hadith hii inakuwa ni maalum kwa utawala pekee wala haijumuishi ukadhi…) Mwisho.

2-  Ama kuhusu hali ya pili shariah imeijuzisha dola kuwapa wadhifa wa ukadhi raia wasiokuwa Waislamu (Ahlu al-dhimma) katika mambo yanayowahusu wao kwa wao kulingana na dini zao katika ndoa na talaka na yanayohusiana nayo… makadhi wa Kiislamu hawatahukumu baina yao kwa shariah ya Kiislamu wala kwa sheria zao, bali hukumu baina yao itatolewa na makadhi miongoni mwao yaani wasiokuwa Waislamu, lakini watu hawa watatengewa mahakama maalum, bali watakuwa na vyumba vya mahakama ndani ya majengo ya mahakama za dola na zitakuwa chini ya idara ya mahakama za dola, wala hawataachwa kujiteulia makadhi wenyewe lakini utaratibu huo utakuwa ni wa dola. Hivyo basi, dola ndio itakayo teuwa miongoni mwao makadhi watakaohukumu baina yao katika mambo ya ndoa na talaka na yanayo husiana nayo, kwa mujibu wa dini na sheria zao, kama shariah ilivyo idhinisha.

Ikiwa sheria zao zinaruhusu kadhi mwanamke kuhukumu baina yao katika mambo ya ndoa na talaka basi inawezekana basi kuteuliwa wanawake makafiri kuwa miongoni mwa makadhi ambao dola itawateua kuhukumu baina ya watu wa dhimmi, yaani itawezekana kwa mwanamke kafiri katika hali hii kuwa kadhi atakaye hukumu baina ya watu wa dini yake kulingana na sheria zao…

Nataraji kwamba hili litakuwa ndio jibu la maswali yako, na Mwenyezi Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.

Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

23 Dhul Qi’dah 1441 H
14/07/2020 M

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa Facebook

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa tovuti

 

Maoni hayajaruhusiwa.