Haya Pia Yalipaswa Yasemwe Na Viongozi Wa Kiislamu Ikulu

Karibuni Raisi John Magufuli aliwaalika baadhi ya viongozi wa dini ikulu kwa minajili ya kuwasikiliza kero na dukuduku zao mbalimbali, kama alivyowahi awali kuwaalika viongozi wa juu wastaafu.

Viongozi hao wa kila upande, Waislamu na wasiokuwa Waislamu baadhi waliweza kutoa madukuduku mbalimbali mbele ya raisi, na raisi kujibu baadhi ya kero na changamoto hizo, ikiwemo pia kuwaagiza mawaziri na wasaidizi wake kuchukua hatua za kuzitatua.

Kwa upande wa baadhi ya viongozi Waislamu kuna walioonesha kushamiri kwa janga la kamari, Waislamu kunyimwa haki ya kuwa na majumba ya ibada, wengine walitoa maombi ya kuwepo mawasiliano mazuri baina ya watendaji wa serikali na Waislamu ili kuepuka migongano katika utendaji wa majukumu ya kila siku nk.

Pamoja na kero, dukuduku na changamoto mbali mbali zilizotolewa na baadhi ya viongozi Waislamu kuwa na umuhimu kwa namna moja au nyengine, hata hivyo bado kuna mambo kadhaa ambayo ni nyeti zaidi na zaidi, yanayogusa hisia za kiimani na kibinadamu kwa jumla, kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu yaliyostahili kupaziwa sauti, lakini kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa hayakugusiwa au walau kutajwa kwa mbali.

Tunasema yaliyoachwa yanagusa Waislamu na wanadamu kwa jumla, kwa kuwa Uislamu ni dini iliyoletwa kuwa Rehma kwa wanadamu wote, Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Awali, ni jambo lisilo na tembe ya shaka kwamba tangu nchi changa zilipolazimishwa sheria ya kibaguzi ya kupambana na Waislamu (ugaidi), Waislamu wamekuwa wahanga wakubwa kama sio pekee wa kuswekwa ndani bila ya maelezo, kuteswa na baadhi hadi kuuwawa kinyama. Mfano mzuri ni Ustadh Almas aliyeuliwa kwa dhulma kati eneo la Kurasini Dar, walinganiaji wa Kiislamu waliovamiwa, baadhi kuuliwa na wengine kujeruhiwa wakiwa msikitini maeneo ya Kilwa nk.

Kuna watuhumiwa wengi Waislamu wa kinachoitwa ugaidi wakiwemo masheikh, maustadh, walimu na Waislamu wengi wa kawaida ambao kesi zao zinakata miaka bila ya kusikilizwa, na jambo hili limeshamiri zaidi hapa Tanzania , kinyume na nchi jirani ambapo tunashuhudia kesi za aina hii, amma hufutiliwa mbali au huendeshwa na kumalizika. Kisingizio kinachotumika katika dhulma hii ni kile kile maarufu cha kutokamilika kwa uchunguzi.

Aidha, kuna shehena ya mahabusu Waislamu kwa mamia kama si maelfu ambao hawajui hatima ya tuhuma zao, huku miaka ikisonga mbele, wakiwa vizuizini katika mazingira duni, huku familia zao zikiendelea kuhangaika kwa mashaka ya kijamii na kiuchumi.

Pili, qadhia ya kupotea watu Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika hali ya kutatanisha. Janga hili limewasibu Waislamu karibu 400 katika mkoa wa Pwani hususan maeneo ya Mkuranga, Rufiji na Kibiti. Jambo hili si geni limeshatajwa na wengi katika wanasiasa Bungeni na nje, wanaharakati, viongozi wa dini nk. Bado serikali iko kimya kama hakuna lililotokea, wala haiko tayari kuruhusu uchunguzi huru.

Bila ya kusahau kuna pia waliopotea miongoni mwa wasiokuwa Waislamu katika wanasiasa na waandishi ambao nao maisha yao yana thamani kama wanadamu.
Qadhia ya kupotea watu kiholela tukiifungamanisha na kuokotwa miili inayoelea katika Mto Ruvu na ukingoni mwa bahari ya Hindi ni jambo linaloongeza msumari moto juu ya jeraha hili kubwa na kuongeza shaka yetu tukiwa kama Waislamu na wanadamu, huku serikali ikiwa haitoi majibu yanayokinaisha.

Sisi tunaona hayo ni mambo nyeti zaidi kuliko chochote ambayo yalipaswa kuwa ajenda mama kuliko mengine kwa viongozi wa dini hususan wa Kiislamu. Kwa sababu, unyeti na umuhimu wa uhai kwa Waislamu na wanadamu kwa jumla ni jambo lililoko wazi. Na kimsingi hakuna kinachoweza kutekelezeka kwa Waislamu na wanadamu kwa jumla iwe sheria au ibada bila ya awali kudhamini uhai na ustawi wa huyo mtekelezaji.

Allah Taala Anasema:

مِنْ أَجْلِ ذَلِكَ كَتَبْنَا عَلَى بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنَّهُ مَنْ قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا
“ Kwa ajili hiyo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliyemuuwa mtu bila ya yeye kuuwa au kufanya uharibifu katika nchi, basi ni kama ameuwa watu wote. Na anaemuokoa mtu asiuwawe ni kama amewaokoa watu wote…”
(Al-Maida 32)

Pia Mtume SAAW katika nasaha zake katuonesha damu ya Muislamu ni kitu kitukufu zaidi hata kuliko Msikiti Mtukufu wa Makka (Kaaba) ambao Waislamu ulimwengu mzima kwa mamilioni hutoa gharama kubwa kila mwaka kwenda kufanya ibada ya Hijja. Hii ni kwa sababu ikiwa Muislamu hana dhamana ya uhai na usalama wake, atawezaje kwenda kutekeleza ibada hiyo:

Anasema Mtume SAAW :

‘Ewe (Kaaba) una utukufu gani, damu ya Muislamu ina utukufu zaidi kuliko wewe.”

Ni wajibu Waislamu kuufanyia haki na uadilifu uhai na usalama wa Waislamu kuliko kitu chochote, walau kwa uchache kupaza sauti zao yanapokuwa hatarini mawili hayo. Kwa kuwa hayo (maisha na usalama) ndio msingi wa kila kitu.

Ni wajibu kwa wanaosimamia mambo wasitoe fursa ya kutawaliwa na hisia za chuki, upendeleo na uadui dhidi ya wengine katika majukumu ya usimamizi huo, na badala yake wasimamie juu ya misingi wa haki na uadilifu.

وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُوا اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى (المائدة: 8
“Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutowafanyia uadilifu. Fanyeni uadilifu. Huko ni karibu mno na uchamungu”
(Al-Maida: 8)

21 Jumada al-awwal 1440 Hijri | 27-01- 2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.