Sakata La CAG Na Spika Tanzania: Dhihirisho La Uwongo Wa Demokrasia

Habari:

Vyombo vya habari vimetaarifu kuhusu maamuzi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai kumuamuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Assad kuhudhuria mbele ya Kamati ya Haki, Maadili, na Kinga ya Bunge mnamo tarehe 21/01/2019 kujibu tuhuma zinazomkabili za ‘kuivunjia heshima’ taasisi hiyo ya kutunga sheria kufuatia kauli yake ya karibuni kuwa Bunge ni dhaifu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Maoni:

Kauli ya Spika wa Bunge imezua mjadala wa kisheria, pia alitumia matamshi ya ukali kiasi cha kudiriki kusema kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ajisalimishe katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili, na Kinga ya Bunge kwa khiyari yake, laa si hivyo atapelekwa kwa pingu.

Sakata hili baina ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu linaifedhehi demokrasia kwa kile kinachoitwa mgawanyo wa madaraka na uwajibishaji, kwamba ni urongo wa wazi unaolezwa kwa Ummah, kujaribu kuwaonesha kwamba vitu viwili hivyo (mgawanyo wa madaraka na uwajibishaji) kuwa ni miongoni mwa mihimili miwili muhimu ya demokrasia.

Kwa udhati demokrasia haijawahi kuwa na chochote kati ya hivyo viwili, si mgawanyo wa madaraka wala dhana ya uwajibishaji wa kikweli. Lau kama ndani ya demokrasia kungekuwa na mgawanyo huo wa madaraka na uwajibishaji kikweli, basi Spika angemuacha Mkaguzi na Mdhibiti afanye majukumu yake bila ya kuingiliwa, naye (Spika) atende majukumu yake, kwa kulifanya Bunge kuwa taasisi imara katika kupambana na kufanyia kazi kashfa za ubadhirifu kama zilivyoainishwa na Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu.

Zaidi ya hayo, sakata hili pia linafedhehi uwongo mwengine mkubwa katika demokrasia, nayo ni uwepo wa ‘uhuru wa maoni’ (kujieleza). Maoni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kuhusu kutowajibika na udhaifu wa Bunge yalipaswa kuchukuliwa kama maoni yake binafsi, ambapo Spika angepaswa kuyaheshimu kama maoni binafsi, na hasa kwa kuzingatia unyeti wa afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu.

Katika miaka ya karibuni kumeshuhudiwa wimbi kubwa la kuwepo matumizi ziada ya serikali kama ununuaji wa ndege mpya, matumizi ambayo yapo kando wa bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Kitendo cha Bunge kushindwa kuihoji serikali ipasavyo kuhusiana na matendo hayo na kuchukua hatua stahiki, ndicho kitu ambacho wengi wamekiona kuwa ni udhaifu wa Bunge.

Katika mgogoro huu pameonekana wazi pia udhaifu wa sheria za kutungwa na wanadamu ambao ni viumbe dhaifu. Hilo linazifanya sheria hizo kuwa na mapungufu makubwa kabisa na uwepo wa mgongano. Kwa qadhia hiii kwa upande mmoja Ibara ya 143(6) ya Katiba ya Tanzania inatamka hivi moja kwa moja:

“Katika utekelezaji wa kazi na majukumu yake, kama yalivyotajwa katika vifungu vidogo (2), (3) na (4) vya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kwa namna yoyote hatofungika na amri au maelekezo ya mtu yoyote au Idara ya serikali…..”

Lakini wakati huo huo sheria kuhusu Kinga, Maadili na Haki ya Bunge inampa mamlaka Spika kumwita yoyote kumuhoji, kwa kile alichokitamka kuhusiana na Bunge. Huu ni mkanganyiko wa hali ya juu unaotoa ishara kuwa mwanadamu ni dhaifu na hawezi kutunga sheria zenye ufanisi, na hivyo hana budi mwanadamu huyo ila kujisalimisha kwa sheria za Muumba.

Katika Uislamu, viongozi hawana sifa za kimalaika, huwajibika kusimamia na kuyaangalia mambo ya Ummah, katika kutekeleza, kulinda na kuutangaza Uislamu, ilhali raia wote wana haki ya kuwahesabu/ kuwawajibisha, na kuwaangazia kwa makini utendaji wao kwa mujibu wa sharia ili kuhakikisha wanasimama juu ya mstari imara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Imeandikwa na Said Bitomwa
Mjumbe wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.