Uharibifu Wa Mazingira: Ubepari Ndio Chanzo

بسم الله الرحمن الرحيم

Siku ya tarehe 5 Juni ya kila mwaka huadhimishwa kuwa Siku ya Mazingira Duniani (World Environmental Day). Licha ya maadhimisho haya na matamko ambayo hutolewa katika maadhimisho haya, bado ulimwengu unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kimazingira hususan mabadiliko ya tabia, suala linalohitaji tafakuri pana juu ya namna ya kukabiliana.
Kumekuwa na mipango ya kupunguza upunguzaji wa hewa chafu inayotokana zaidi na matumizi ya nishati, uchomaji wa misitu nk.ambayo hutajwakuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la joto linalopelekea ongezeko la ukame, moto wa misituni, mafuriko nk.
Kumekuwa na mapendekezo kadhaa katika kupambana na hali hii,mfano inapendekezwa kusitisha utumiaji wa makaa ya mawe, kuongeza uwekezaji katika nishati mbadala na rafiki kwa mazingira, kuanza matumizi ya magari ya umeme badala ya mafuta na uwekezaji katika kudhamini juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira katika nchi mbalimbali.
Mabadiliko ya tabia ya nchi hata hivyo ni sehemu ya majanga ya kimazingira yanayoendelea kuzikumba sehemu nyingi duniani leo hii hususani nchi masikini. Kupotea kwa baadhi ya aina za wanyama na mimea, mmomonyoko wa ardhi, uchafuzi wa hewa, kuchafuliwa kwa bahari, maziwa, na mito kwa sumu za taka na kutupwa kwa mamilioni ya tani za plastiki, nguo, nk. na matatizo yanayoikabili ardhi kiujumla.
Uharibifu huu wa mazingira unaugharimu ulimwengu kiasi kikubwa, unaathiri afya za watu, unasababisha kukwama kwa kilimo na ufugaji, kuhamahama kwa watu, kiwango duni cha maisha na kuongeza umasikini katika mataifa mbalimbali.
Jumuiya ya kimataifa inadai kuwa eti inatafuta utatuzi wa mgogoro huu wa mazingira. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na makubaliano, mikataba na matamko tofauti tofauti ya kimataifa kuhusu mazingira kwa mfano Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira wa mwaka 1992 (United Nations Framework Convention on Climate Change), Makubaliano ya Kyoto ya mwaka 1997 (Kyoto Protocol) na Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 (The Paris Accord)
Hata hivyo, wengi wanaona kuna mabadiliko kidogo yanayofanyika katika kukabiliana na changamoto za mazingira zinazoukabili ulimwengu hivi sasa. Hii ni kwa sababu masuluhisho na majadiliano kuhusu mazingira yameshindwa kutibu mzizi au tatizo msingi linalopelekea changamoto za mazingira. Masuala yanayotafutiwa masuluhisho mfano matumizi makubwa ya nishati ya taka, taratibu duni za kilimo, ongezeko kubwa la uzalishaji na utumiaji wa bidhaa, kuharibika vyanzo vya maji kutokana na viwanda nk. ni dalili tu au matokeo ya tatizo na si tatizo msingi. Hivyo, masuluhisho yeyote kuhusu masuala haya hayataleta tija, na tatizo msingi halitotatuliwa.
Sababu Kuu ya uharibifu mkubwa wa mazingira tunaendelea kuushuhudia leo hii ni mfumo wa kibepari unaojali maslahi ya kimada ambao ndio unaosimamia siasa, uchumi na maisha ya kijamii ya watu leo hii. Mfumo huu umetengeneza uwiano kinzani wa uzalishaji na utumiaji wa bidhaa katika mataifa ili kupata mapato zaidi na faida za kiuchumi bila kujali mahitaji mengine ya kibinadamu ikiwemo kulinda mzingira.
Kuendelea na kujirudiarudia kwa uharibifu wa mazingira na kuibuka kwa matatizo ya kimazingira ni matunda ya mfumo huu fisidifu. Kwahiyo, ili kukabiliana na changamoto za mazingira kiuhalisia ni lazima kukabiliana na kuondoa mfumo wa ubepari ambao bila ya kuondolewa utaendelea kuleta majanga na uharibifu, ardhini na majini kwani hauna sifa ya kumsimamia binadamu katika maisha yake.
(ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ)
“Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyoyatenda mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonjeshe baadhi ya waliyoyatenda. Huenda wakarejea ” [Ar-Rum: 41]
Risala ya Wiki No. 133
19 Shawwal 1443 1443 Hijri / 19 Mei 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.