Eda ya Mwanamke Aliyefiwa na Mumewe

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:                                                                      

Assalamu Alaykum – Mwalimu mmoja wa soshiolojia ameibua swali kuhusu eda (eda ya kufiwa na mume ambayo ni miezi minne na siku kumi). Anasema falsafa iliyo nyuma ya kipindi hiki ni kujua kuhusu ujauzito wa mwanamke baada ya kifo cha mumewe, je ikiwa kihospitali itathibitishwa kwamba mjane huyo hana mimba kipindi cha eda kitapunguzwa kwa mujibu wake (huo uchunguzi wa kihospitali)?

Nahitaji jibu lako na muongozo.

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh,

1-Asili katika eda ya mwanamke aliyefiwa na mumewe ni kauli yake Taala: “Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, wasubiri nafsi zao hawa wake kwa miezi minne (wakae eda miezi minne), wakimaliza muda wao (huo wa eda) basi hapana dhambi juu yenu kwa yale wanayoyafanyia nafsi zao kwa wema, na Allah kwa yale mnayoyatenda ni mwenye habari”. Ni wazi katika Ayah hii kwamba eda ya mwanamke aliefiwa na mumewe ni miezi minne na siku kumi. Na Aya (nass) hii ni yenye hukmu jumla (amm) kwa kila mwanamke aliyefiwa na mumewe, akiwa ni mja mzito au si mja mzito…

2-Kuna Aya nyengine “na wale waja wazito muda wao (wa eda) ni kujifungua”  hii inafanya maalum ujumla wa Aya iliyotangulia kwa asiyekuwa mja mzito aliyefiwa na mumewe, yaani asiyekuwa mja mzito aliyefiwa na mumewe eda yake ni miezi minne na siku kumi. Na ama mja mzito aliyefiwa na mumewe basi eda yake ni kujifungua… Kwahiyo, ikithibitika kwamba mwanamke aliyefiwa na mumewe si mja mzito eda yake ni miezi minne na siku kumi, kauli moja. Yaani yule ambae amekwambia wewe itakapothibiti kwamba mwanamke asiyekuwa mja mzito kuwa hana eda itakuwa huyo ameifanya kinyume hukmu, basi ima atakua ni mjinga hafahamu vipi ahkam huchukuliwa na huvuliwa (tustambat), au atakuwa ni msekula anaufanyia vitimbi Uislamu kwa kubadilisha ahkam kwa maana ya kuudhalilisha…

3-Hakika tumebainisha hayo katika kitabu cha Shakhsiyyah Juzuu ya tatu, Mlango wa nafasi ya Sunna katika Quran Uk (77), imeelezwa:

(Kuifanya maalum (takhswiis) ile ya jumla yake Quran (‘aamuh): Katika Quran zimekuja ahkam za jumla kadhaa (umuumaat), na Sunna ikaja kuzifanyia takhswiis hizi umuumaat… Na katika hizo ni kauli yake Taala: “Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, wasubiri hao wake (wakae eda) kwa miezi minne na siku kumi”. Aya hii imetoa dalili ya eda ya kufiwa. Na ikafanyiwa takhswiis Aya hii kwa hadith ya Sabiiat Al-Aslamiyya, pale alipojifungua baada ya kufa mumewe kwa siku ishirini na tano, Mtume (SAAW) akampa habari kuwa ameshahalalika (ameshamaliza eda yake), ikabainika hapo kwamba Aya hii ni makhsuus kwa asiyekua mja mzito).

4-Vilevile, tumesema katika kitabu hicho hicho, katika mlango wa takhswiis Quran kwa Quran  Uk (256), imeelezwa:

(Inajuzu kufanya takhswiis Quran kwa Quran (yaani Aya kwa Aya); kwasababu zote hizo umekuja wahyi kwa lafdhi na kimaana, kwahiyo inafaaa moja kuwa mukhaswis wa nyengine, na kwasababu imetokea hasa takhswis katika Quran kwa Quran, miongoni mwao ni kauli yake Taala: “Na wanawake wajawazito muda wao (wa eda) ni kujifungua”. Hakika Aya hii imekuja kufanya tahkswis  kauli yake Taala: “Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, wasubiri hao wake (wakae eda) kwa miezi minne na siku kumi”  

5-Yaani mwenye kufiwa na mumewe eda yake ni miezi minne na siku kumi, na akiwa mja mzito basi eda yake ni kujifungua. Na hii ni rai ya Jamhuri yaani mafuqahaa wengi…Na iko rai yenye kutiliwa nguvu wameisema baadhi ya mafuqahaa, nayo ni kuwa eda katika hali hii ni kipindi kilichokuwa kirefu zaidi kati ya viwili baina ya kujifungua na miezi minne na siku kumi… Ama yale aliyokwambia mtu huyo ya kwamba ikithibiti kuwa mwanamke si mja mzito kuwa hana eda hiyo haisihi kwa hali yoyote, bali ni kama tulivyotangulia kusema (Yaani yule ambae amekwambia wewe itakapothibiti kwamba mwanamke asiyekuwa mja mzito kuwa hana eda itakuwa huyo ameifanya kinyume hukmu, basi ima atakua ni mjinga hafahamu vipi ahkam huchukuliwa na huvuliwa (tustambat), au atakuwa ni msekula anaufanyia vitimbi Uislamu kwa kubadilisha ahkam kwa maana ya kuudhalilisha…)

6-Na linapatikana hilo katika Tafsiri zinazotambulika sana, na inatosha mimi kutaja moja tu katika hizo:

Imeelezwa katika Tafsiri ya Ibn Kathir kwenye tafsiri ya Aya tukufu:”Na wale ambao hawajapata hedhi na wajawazito muda wao (wa eda) ni kujifungua”

Na kauli yake Taala: “Na wajawazito muda wao (wa eda) ni kujifungua”. Anasema Taala  na mwenye kua mjamzito eda yake ni kujifungua, na hata ikiwa baada ya talaka au mauti katika jihadi katika kauli ya Jamhuri ya wanavyuoni waliotangulia na waliokuja baadae, kama ilivyo Nass ya Aya hii tukufu na kama ilivyoeleza kwalo Sunna ya ki-Utume.

Na imepokelewa kutoka kwa Ali na Ibn Abass (RA) kwamba walikwenda katika aliyefiliwa na mumewe kuwa atakaa eda ya kipindi kilichokuwa kirefu zaidi kati ya viwili cha kujifungua au cha miezi (minne na siku kumi), kwa kuifanyia kazi Aya hii tukufu ambayo imo katika Surat Al-baqara. Na amesema Bukhar: (Ametuelezea Sa’ad bin Hafs, ametuelezea Shaiban, kutoka kwa Yahya amesema: Amenipa habari Abu Salma kasema: Alikuja mtu kwa ibn Abass – na Abu Huraira amekaa – akasema: Nipe habari kuhusu mwanamke aliyejifungua baada ya mumewe kwa masiku arobaini., Ibn Abasss akasema: kipindi kilichokuwa kirefu zaidi kati ya viwili, nikasema mimi: “Na wajawazito muda wao (wa eda) ni kujifungua” , Abu Huraira akasema mimi niko pamoja na mtoto wa ndugu yangu – yaani Aba Salma. Ibn Abass akamtuma kijana wake Kuraib kwa Umm Salama akamuulize akasema: Aliuliwa mume wa Sabii’a bin Al-Aslamiyyah na hali yakuwa yeye mjamzito, akajifungua baada ya kifo chake kwa masiku arobaini, akaposwa, akamuozesha Mtume (SAAW), na Abu Al-Sanaabil alikuwa ni kati ya waliomposa). Hivi ndivyo alivyopokea Bukhar hadithi hii hapa kwa ufupi. Na Muslim ameipokea kwa lafdhi:

(Amenieleza Abu Al-Tahir, ametupa habari Ibn Wahab, amenieleza Yusuf bin Yazid kutoka kwa Ibn Shihab, amenieleza Ubaidullah bin Abdillah bin Utba: Kwamba baba yake alimuandikia Umar bin Abdillah bin Al-Arqam Al-Zuhri akimuamrisha aende kwa Subai’a bint Al-Harith Al-Aslamiyyah amuulize kuhusu hadithi yake na kuhusu aliyoelezwa na Mtume (SAAW) pale alipomuuliza amfutie, Umar bin Abdillah akamuandikia akimueleza kwamba Subai’a alimueleza kwamba yeye alikua mke wa Sa’ad bin Khaula – ambae alikuwa katika walioshuhudia Badr – akafishwa katika Hijjatul Wada’a na yeye (Subai’a) mja mzito, hakukaa muda mrefu akajifungua baada ya kufa mumewe, na alipojinyanyua mwenyewe akajipamba kwa ajili ya posa, Abu Al-Sanabil bin Ba’akak akaenda kwake akamwambia: Una nini mbona umejipamba? Labda unatarajia ndoa. Naapa kwa Allah hakika wewe huwezi kuolewa mpaka ikupitie miezi minne na siku kumi, Subai’a akasema: Aliponiambia mimi hayo nikakusanya nguo zangu nilipofikiwa na jioni nikamuendea Mtume (SAAW) nikamuuliza kuhusu jambo hilo akanijibu kwamba hakika mimi nimeshahalalikiwa pindi nilipojifungua  na akaniamrisha ndoa ikinitokezea).

Ufupisho:

Kwamba eda ya mwanamke mwenye kufiwa na mumewe imebainishwa katika Kitabu cha Allah na Sunna ya Mjumbe wake (SAAW), nayo:

1-Akiwa si mja mzito eda yake ni miezi minne na siku kumi kwa mujibu wa Aya ya Surat Al-Baqara “Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, wasubiri hao wake (wakae eda) kwa miezi minne na siku kumi”, na akiwa mja mzito eda yake ni mpaka ajifungue (itakua imemalizika), kwa mujibu wa Aya ya Surat Al-Talaq: “Na wajawazito muda wao (wa eda) ni kujifungua”. Kwa namna tulivyobainisha punde tu.

2-Ama yule  aliyekwambia wewe itakapothibiti kwamba mwanamke asiyekuwa mja mzito kuwa hana eda itakuwa huyo ameifanya kinyume hukmu, na kama tulivyosema punde tu  (basi ima atakua ni mjinga hafahamu vipi ahkam huchukuliwa na huvuliwa (tustambat), au atakuwa ni msekula anaufanyia vitimbi Uislamu kwa kubadilisha ahkam kwa maana ya kuudhalilisha…)

Ndugu yenu Ata Ibn Khalil Abu Rashta

7, Shaban, 1440H

13, April 2019

Maoni hayajaruhusiwa.