Ramadhani Msingi Wa Khofu Kwa Muumba na Tabia ya Ukweli

بسم الله الرحمن الرحيم

Alhamdulillah! tupo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi uliosheheni kheri nyingi kwa viumbe wote na zaidi Waislamu.
Jamii yetu leo imekosa mambo mengi mazuri ikiwemo kubwa na la msingi nalo ni kupotea kwa ukweli na kukosekana watu wakweli wakiwemo viongozi wakweli.
Badala yake jamii leo imejaa hadaa, ulaghai, utapeli na kila namna ya uongo. Kwa sababu itikadi ya ubepari na nidhamu yake ya kidemokrasia inayotawala ulimwengu, ambayo ndiyo kitegemeo cha kuibua na kuelekeza fikra za mtu, ni itikadi dhaifu ya kiuwongo na isiyo sahihi. Itikadi hiyo kwa inajenga khofu kwa viumbe badala ya Muumba, kiumaumbile huzalisha uwongo na usanii ili kumridhisha kiumbe.
Unapojenga khofu kwa viumbe ambao ni jambo la dhaifu kwa kila nyanja, lazima khofu hiyo itakuwa maangamizi kwa mwenye khofu hiyo. Na kwa kuwa mwanadamu ana udhaifu, ni rahisi kumuhadaa, kumdanganya na kumtapeli.
Kwa hali ilivyo ni wazi kwa mwenye madaraka kwa kuwa anaogopewa anaweza kujenga hali ya kuaminika na kuonekana ni mkweli kuliko watu wote kwa sababu tu ya khofu au uwezo wa kudhibiti taarifa zake kujulikana ambazo hataki zifahamike.
Kwa itikadi hii ya kibepari ni wazi kila mwanasiasa mkubwa huonekana kana kwamba ni mkweli na mwenye haki na busara kuliko wote kwa kuwa vyombo vya habari vyake na taarifa huonesha hivyo.
Ndiyo maana akida ya Kiislamu inamjengea mtu khofu kwa Muumba tu, na humuandaa na kumlea kivitendo afikie hadhi hii. Moja ya nyenzo kubwa na msingi kwa ujenzi wa ukweli na khofu kwa Muumba ni Swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ramadhani imekuja na ibada maalum ya Swaumu. Amri ya kufunga ni sawa na amri za ibadat nyingine kwa kuwa zote ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu swt, Muumba na Mmiliki wa kila kitu. Lakini funga ya Ramadhani ni tofauti na ibada nyingine kwa namna Mwenyezi Mungu Mwenyewe Alivyoikadiria tofauti na nyingine.
Ameweka wazi Mwenyezi Mungu kupitia Hadithi mashuhuri :
Imesimuliwa kutoka kwa Abuu Huraira r.a kwamba Mtume saw amesema;
“Kila amali njema ya Mwanadam italipwa maradufu. Kila jambo jema litalipwa mara kumi au zaidi kufikia mara mia saba au zaidi kadri Mwenyezi Mungu Atakavyotaka. Mwenyezi Mungu Anasema: “Isipokuwa Swaumu, ambayo ni Yangu, na Nitailipa” (Bukhar).
Swaumu ni ibada ya siri hasa, ambayo fungamano la mja kutenda kwa ajili ya Muumba Wake huwa la kiwango cha juu sana kimsingi. Ni kwa sababu Muislamu anajizuiya kufanya baadhi ya vitu vya halali kwa muda maalumu hali ya kuwa ana uwezo wa kuvipata na pia anaweza kuigiza kwa kufanya kwa siri na binadamu wenzake wasijue kwamba hakufunga. Lakini hawezi kujificha au kuficha chochote kwa Mwenyezi Mungu Muumba.
Ndiyo maana swaumu ni fungamano la ndani kabisa baina ya kiumbe (mwanadamu) na Muumba (Mwenyezi Mungu), na ndiyo maana kiwango cha malipo (thawabu) hakijawekwa wazi kwa kuwa bila shaka ubora wa swaumu hutofautiana baina ya watu.
Swaumu inampa mfungaji funzo la kitabia la kuwa mkweli na kumukhofu Allah Taala pekee, ukweli ni suala lililochafuliwa sana katika jamii hususan na wanasiasa wa kibepari wa kidemokrasia.
Ufisadi unaoendelea kushuhudiwa leo hii kwa watu binafsi, viongozi na nchi ni matokeo ya kukosekana ukweli, khofu kwa Muumba na kutokuwepo fungamano la matendo ya watu (viumbe) na Mwenyezi Mungu swt.
Hivyo, Ramadhani kwetu Waislamu tuibebe kuwa msukumo wa kutubadilisha binafsi katika tabia na kuwa wakweli na iwe ni kigezo cha kubaini wasio wakweli katika maisha yetu kwa sababu madhara ya uongo, hadaa na ulaghai ni makubwa hasa yakifanywa na viongozi.
Abu Nuthtaq – Hamza
Risala Maalum ya Ramadhani
11 Ramadhani 1443 Hijri
12 Aprili 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

 

Maoni hayajaruhusiwa.