Kufaa Kuweka Akiba Kwa Haja Maalum Hakuondoi Wajibu wa Zakat

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Akiba iliyopitiwa na miaka kadhaa bila ya kutolewa zakat. Je hutolewa kwa kila mwaka au mara moja tu katika umri? Na utoaji inafaa kutoa thamani? Ahsante.

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh,

1-Kabla ya kujibu swali lako ningependa kutoa angalizo kuwa kuweka akiba ya dhahabu na fedha (silver) na pesa bila ya haja huhesabiwa kuwa ni kuzuia (kanz) hata kama atatoa zaka yake, na kuzuia (kanz) ni haramu. Na miongoni mwa dalili za uharamu wake ni:

-Kasema Allah Mtukufu:

﴿وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ * يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْنِزُونَ﴾.

 “Na wale wanaozuia dhahabu na fedha (silver)  na wasizitoe katika njia ya Allah wape habari ya adhabu kali. Siku ambayo zitaunguzwa katika moto wa jahanam na wababuliwe kwayo mapaji yao ya uso, mbavu zao na migongo yao (waambiwe) haya ndio yale mliyoyazuia kwa ajili ya nafsi zenu, basi onjeni yale mliyoyazuia”

Amepokea Ahmad kwa sanad sahihi kutoka kwa Abi Umamah amesema: (Alikufa mtu katika Ahli Sufa, ikakutikana katika shuka yake dinari moja, akasema Mtume (SAAW): “Mbabuo mmoja”. Akasema: Kisha akafa mtu mwengine zikakutwa dinari mbili katika shuka yake. Mtume (SAAW) akasema: “mibabuo miwili”. Na akaegemeza Tabari kwa Abi Umamah Albahily mfano wa hayo. Hii ina maana moja kwa moja uharamu wa kuzuia dhahabu na fedha hata ikiwa dinari mbili au dinari moja, muda wa kwamba ni kuzuia (kanz), yaani hazina ya mali bila ya haja inayokusudiwa  kutumika, na Mtume (SAAW) amesema hayo kuhusu watu hawa wawili kwasababu wao walikuwa wakiishi kwa kutegemea sadaka na ikawa wana dhahabu. Akasema Mtume (SAAW): “Mbabuo mmoja” na akasema: “Mibabuo miwili” akiashiria kauli yake Allah Taala: “Siku itakapo yeyushwa katika moto wa jahannam yababuliwe kwayo mapaji yao nyuso na mbavu zao”  [Tawba:35] ambayo ni sehemu ya Aya ya kuzuia (kanz) . Kwahiyo hii ni dalili ya kuharamisha uzuiaji (kanz) uharamu wa moja kwa moja. Ni sawa sawa ikiwa imefikia kiwango cha zakat au haijafikia, na ni sawa ikiwa ametoa zakat au hajatoa. Uzuiaji (kanz) wote ni haram.

Ama kuweka akiba kwa haja maalumu hiyo inafaa na wala haihusiani na dalili za kuzuia (kanz). Tofauti baina ya kuzuia na kuweka akiba ni, kuzuia maana yake ni kukusanya pesa nyingi bila ya haja, yaani kuzuia pesa zisiingie sokoni. Ama kuweka akiba ni kuhifadhi pesa kwa ajili ya haja miongoni mwa haja, kama vile kukusanya pesa ili kujenga nyumba, kuoa, kununua kiwanda, kufungua biashara au yasiyokua hayo…”

2-Mtu anapoweka akiba ya dhahabu bila ya haja huwa anapata madhambi kwasababu hiyo huwa ni kuzuia dhahabu nayo ni haramu… Pamoja na hayo, itakua ni juu yake kutoa zaka ya dhahabu ambayo ameiweka bila ya haja kwasababu kuzuia (kanz) ambako ni haramu hakuondoi uwajibu wa zaka…Na pia suala la kuweka akiba kwa haja hilo halijaharamishwa, lakini anaefanya hivyo lazima atoe zaka yake ikiwa imeshafikia nisab na ikapitiwa na mwaka, kwasababu kufaa kuweka akiba kwa haja hakuondoi uwajibu wa zaka…

3-Hakika faradhi ya zaka ni faradhi ya mwaka, yaani kila mwaka wa Hijri. Mali ikifikia Nisaab, mfano dhahabu na ikapitikiwa na mwaka huwajibika kutolewa zaka kwa kiwango cha robo ya fungu la kumi, yaani 2.5% humo. Mja akitoa zaka ya mali yake baada ya kupita mwaka hakika atakua ametekeleza lililowajibu kwake, na akiichelewesha zaka akawa hakuitoa kwa mwaka huo, basi wajibu bado unabakia katika dhima yake mpaka aitoe kwa mwaka huo… Na kuitoa kwa mwaka wa Hijriyyah hakuchukui nafasi ya kuitoa mwaka wa Hijriyyah mwengine, kwasababu kama tulieleza punde tu, kuwa hiyo (zaka) ni wajibu wa kila mwaka ambayo hutolewa kwa kila mwaka mpya ukifika muda wa kwamba sababu zake na masharti yake yapo…

Kwahiyo, mwenye kuiweka dhahabu kwa muda wa miaka mitano  ya Hijriyyah kwa mfano, na ikawa dhahabu imefikia Nisaab pale mwanzo anapoiweka akiba, itakuwa ni juu yake atoe zaka ya miaka mitano katika mwisho wa ule mwaka wa tano ikiwa hakutoa zaka ya dhahabu hii kabla, kwasababu zaka ya kila mwezi wa Hijriyyah katika ile miaka mitano ni deni liko kwenye dhima yake ambalo lazima alilipe… Kwahiyo atatoa zaka mara tano kila mara kwa kiwango cha 2.5% kwa dhahabu yake aliyoiweka akiba…Angalizo ni kuwa si wajibu yeye kutoa zaka katika mwaka kwa kiwango kile alichokitoa katika mwaka wa kwanza yaani “2.5%” ndicho alichotoa mwaka wa kwanza, bali atalazimika kutoa katika 97.5% tu kilichobakia katika mwaka wa pili kwa kiwango (mikdar) cha 2.5%… Na hivyo hivyo katika miaka inayofuata, yaani ataangalia katika miaka inayofuata kilichopungua katika mali ile ya kutolewa zaka baada ya kutoa zaka yake ya miaka iliyopita…

4-Ama kutoa (kile kinachotolewa) zaka kutoka katika jinsia nyengine ambayo sio ile inayotolewa zaka (iliyolazimikiwa na kufikia nisab), hilo linajuzu, kama badala ya dhahabu kutoa pesa au fedha au mfano wake…

Imeelezwa katika kitabu cha Amwal katika ukurasa 155 – 156 maneno yafuatayo:

(…Imepatikana katika Sunna kutoka kwa Mtume (SAAW) na Masahaba zake kwamba ni wajibu wa haki katika mali, kisha hubadilishwa kwa chengine ambacho kutolewa kwake ni wepesi zaidi kwa yule mtoaji kuliko kile cha asili (kile kilichofikiwa nisab). Na katika hilo ni barua ya Mtume (SAAW) kwa Muadh huko Yemen kuhusu jizya: “Kuwa ni juu ya kila mtu mzima atoe dinari moja au kinachokua sawa na hiyo dinari moja katika nguo”. Ameipokea Abu Daud. Kwa hiyo Mtume (SAAW) amechukua kitu chengine badala ya kitu chenyewe cha asili, yaani amechukua nguo badala ya dhahabu. Na katika hayo pia ni yale aliyowaandikia watu wa Najran: Kwamba ni juu yao kutoa nguo elfu mbili kila mwaka au kilichokuwa sawa na hicho katika wakia za dhahabu na fedha” Amepokea Abu Ubaid. Na Ibn Qudama ameeleza katika Al-Mughni kwamba Umar (RA) alikuwa anachukua ngamia katika jizya badala ya dhahabu na fedha, kama Ali (RA) alivyokuwa akichukua misumari, kamba, na misumari mikubwa katika jizya badala ya dhahabu na fedha, Mwisho.

Na pia imeelezwa katika kitabu cha Amwal Fii Daulatil-Khilafah, Uk:165 maelezo yafuatayo:

(Na atatoa dhahabu kwa dhahabu, na kwa pesa za karatasi  za niaba na pesa za karatasi wathiqa, na atatoa fedha kwa fedha na kwa pesa za karatasi  za niaba na pesa za karatasi wathiqa. Kama ilivyo kuwa inamfalia kutoa zaka ya dhahabu kwa fedha na kwa pesa za karatasi za ilzamiyya, na pia kutoa fedha kwa dhahabu  na kwa pesa za karatasi za ilzamiyya, kwasababu zote hizo ni pesa na ni thamani. Kwahiyo inamfalia mtu kutoa baadhi yake kwa baadhi nyengine. Na inajuzu kutoa baadhi yake kwa baadhi nyengine kwa kupatikana lengo lake. Na pamepitwa katika mlango wa zaka ya nafaka na matunda dalili za kuchukua thamani badala ya ile mali asili iliyowajibikiwa kutolewa zaka). Mwisho.

Ni wazi kwa yaliyotajwa hapo juu kuwa inafaa kutoa zaka ya dhahabu na fedha kutoa pesa za karatasi zinazotumika kwa mujibu wa bei ya soko la dhahabu na fedha wakati wa kutoa zaka.

Natarai kwa majibu haya imetosheleza.

Ndugu yenu Ata Ibn Khalil Abu Rashta

01, Ramadhani, 1440H

06, May 2019

Maoni hayajaruhusiwa.