Ushindi wa Bondia Hassan Mwakinyo ‘Farasi wa Uzalendo’

Karibuni jina la Bondia wa Tanzania Hassan Mwakinyo limevuma na kuenea kila mahala kutokana na ushindi mkubwa alioupata katika pambano lake la ndondi nchini Uingereza.

Ushindi wa Hassan Mwakinyo (23) ulitokana kwa kumshinda bondia maarufu wa Uingereza Sam Eggington (24) katika Ulingo wa Arena Birmingham, uwanja mkubwa zaidi wa ndani (indoor arena) kuliko uwanja wowote nchini Uingereza.

Bondia Hassan Mwakinyo si bondia maarufu lakini aliweza kumshinda mpinzani wake Eggington aliyeonekana kuwa na matumaini makubwa ya kushinda kwa wepesi, ikizingatiwa haiba ya chini ya Hassan Mwakinyo, matayarisho duni na ya muda mfupi. Bondia Hassan Mwakinyo alitangazwa mshindi katika raundi ya pili tu katika pambano lililotarajiwa kuwa la raundi kumi, kwa mshangao mkubwa wa wengi Hassan Mwakinyo alidiriki kumshinda Bondia Sam Eggington ambaye tangu mwaka 2012 alikwishaingia ulingoni kwa mapambano 27, kando na lake, na kushindwa mapambano 4 tu.
https://en.wikipedia.org/wiki/Sam_Eggington

Qadhia ya ushindi wa Bondia Mwakinyo ilipazwa juu na kudandiwa kwa haraka ya ajabu hususan na wanasiasa, licha ya kuwa Bondia Mwakinyo hakupatiwa msaada stahiki awali kufikia hapo alipofika. Wanasiasa na watetezi wa uzalendo na utaifa, kauli zao kuanzia hapo zikawa “Hassan Mwakinyo ni mtanzania mwenzetu na kaliletea taifa sifa kimataifa.”

Wanasiasa wakatayarisha mapokezi kwa ajili ya bondia huyo, akapewa fursa ya kwenda bungeni kukutana na wabunge, kuchangiwa kiasi fulani cha fedha na wabunge hao, na serikali kuahidi kumjenga na kumuwezesha zaidi ili aweze kukuza ndoto zake.

Dhamira yangu sio kujadili tasnia ya ndondi, bondia Mwakinyo, wala udhati wa ushindi katika pambano lake. Bali kuonesha udhaifu, uwongo na sura mbili / unafiki wa fikra potofu ya uzalendo kama inavyodhihirika wazi wazi katika qadhia hii.

Uwongo wa ‘uzalendo’ unadhihirika wazi wazi kwa kuwa dhana ya uzalendo imeibuka pale tu bondia huyo alipokuja na ushindi, baada ya bondia huyo kupita katika hali na mazingira magumu ya kupapatua kibinafsi bila ya msaada stahiki hata katika safari ya kwenda kwenye pambano lenyewe. Kama bondia huyo alivyoonesha hisia zake za masikitiko yake aliponukuliwa akisema:

‘Katika vitu sitavisahau ni kwamba mimi nilisafiri kutokaTanzania kama mfungwa, nilikosa kibali na nikaondoka kama mkimbizi, nimeondoka mimi kwa kuazima ada ya mwanafunzi anasoma, tumekopa ada yake ya shule ili tukalipie VISA. Hii imeniuma ingawa leo kila mtu anajitokeza na kunisifu.”..

http://bongo5.com/bondia-aliyemdunda-muingereza-niliondoka…/

Matokeo/ natija haya ni jambo la kutarajiwa, kwa kuwa asili fikra ya uzalendo ni fikra dhaifu, duni, ya muda isiyo na fungamano la dhati na thabiti baina ya wanadamu. Mwanachuoni mkubwa na mwanasiasa mahiri Sheikh Taqiudin Nabahan (Allah Amrehemu) aliwahi kudokeza kuwa fikra ya uzalendo ni fikra duni na ya muda tu, watu hudhihirisha fungamano na umoja wao katika hali fulani hususan zinazohusisha tishio la uvamizi wa nje:
https://hizb.or.tz/wp-conte…/…/2018/05/1.NidhamuYaUislamu.pdf.
Lakini pia hudhihirika hata katika furaha amma ushindi uliopatikana kwa kumshinda mtu au nchi ya nje.

Tunashuhudia wakati timu za mpira iwe Yanga au Simba inapocheza na timu ya nje, hutolewa mwito wa uzalendo kuiunga mkono timu ya Tanzania. Na mara mashindano dhidi ya timu ya nje yakimaliza, washabiki huendelea kuunga mkono timu zao kama kawaida. Au lau ushindi huu wa bondia Mwanyiko angemshinda mtu wa ndani, bila ya shaka kusingekuwa na shamra shamra kama zilizoonekana.

Hivyo, ni wazi uzalendo ni fungamano la muda na kipindi fulani tu, halizingiri sehemu kubwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Na kwa upana wake tuseme ni fungamano tete bila ya mashiko.

Zaidi ya hayo, fikra ya ‘uzalendo’ hutumika kimaslahi na watawala kama kaulimbiu ya uwongo kulenga maslahi ya kuungwa mkono kisiasa, kuwanyamazisha na kuwadhibiti wanaowawajibisha watawala kwamba ‘hawana uzalendo’. Pia hutumika kulazia wananchi na kuwatuliza kama pale zinapongezwa kodi, kuuzwa rasilmali za Umma nk. Kwa yote hayo, raia huambiwa wawe wazalendo.

Historia inatuonesha pia Firaun alivyocheza karata ya uzalendo kimaslahi, katika kujizatiti kisiasa, ili kuungwa mkono zaidi na kuhalalisha mapambano yake dhidi ya Nabii Mussa As.

قَالَ أَجِئْتَنَا لِتُخْرِجَنَا مِنْ أَرْضِنَا بِسِحْرِكَ يَامُوسَى

(طه: 57 ).

“Akasema (Firaun): Ewe Mussa ! hivi umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?”

Huo ndio uzalendo, fikra duni isiyo na uhalisia na hatari kwa ustawi wa wanadamu, kiasi cha James Branch Cabell (1879 – 1958) mwandishi wa vitabu wa kimarekani kuipachika jina fikra ya uzalendo kuwa “ni dini ya motoni”

https://www.brainyquote.com/quot…/james_branch_cabell_380141

Uislamu umeharamisha kwa ukali fikra ya uzalendo na mafungamano yote mfano wake kama utaifa, urangi, umajimbo, ukabila nk. Kwa kuwa yote hayo ni mafungamano dhaifu, ya muda, kitapeli, yanayoleta husuma baina ya watu na hutumika kijanja ili kufikia maslahi fulani fulani bila ya kuwa na ukweli wowote ndani yake.

Ni mafungamano ambayo hayana kufuli ya kimaumbile kuwafunga watu pamoja na kikweli. Ni mafungamano finyu, yanayozingatia kijieneo kidogo sana, yanayodumaza uoni wa mwanadamu na yasiokuza upeo mpana, zaidi ya kuzingatia urangi, ukabila, eneo unaloishi nk. ilhali wanadamu ni wengi na ardhi ya Mwenyezi Mungu ina wasaa.

Fungamano imara na thabiti la kuwafunga wanadamu kiukweli maishani ni fungamano la ki- mfumo pekee. Na mfumo maana yake ni uwepo wa itikadi ya ki-akili, na kutokana na itikadi hiyo pakazaliwa nidhamu.

Na itikadi/aqeeda hii huwa ni fikra inayotoa ufafanuzi juu ya ulimwengu, ubinadamu na uhai, na yale yaliopo kabla ya maisha ya duniani, na yale yatakayojiri baaada ya maisha haya, na mahusiano ya vitu hivyo, pamoja na mahusiano yao kabla na baada.

Kuhusiana na nidhamu zinazotokana na aqeeda hii, hizi ni taratibu mbalimbali ambazo ni masuluhisho ya matatizo mbalimbali ya mwanadamu iwe katika siasa,ibada, jamii, uchumi, mahusiano ya nje nk. Na pia ndani ya nidhamu hizo hupatikana pia muongozo wa namna ya utekelezaji wa masuluhisho hayo, kuhifadhi na kueneza mfumo huo.

Mfano mzuri wa fungamano la kimfumo ni namna wamarekani, wafaransa, wajerumani, waingereza, wahispania, wareno nk. hawa wote hutofautiana kijografia, kiasili, kilugha na hata muonekano lakini kwa kuwa ni waumini wa mfumo mmoja wa kidemokrasia/ kibepari, ambao nchi zao wanautabikisha/ kuutawalisha, hapana shaka wote watakuwa wanabeba vipimo, maono na mtazamo unaofanana kimsingi, kwa mujibu wa mfumo wao wa kidemokrasia. Japo kwa udhati mfumo wa ubepari ni mfumo batil usiowafikiana na maumbile halisi ya mwanadamu.

Watakuwa wamefungwa na fungamano moja la mfumo wa kidemokrasia. Licha ya kuwa wanasimamiwa na serikali tofauti za kidemokrasia. Kwa kuwa, mfumo wa kidemokrasia huruhusu uwepo wa serikali zaidi ya moja.

Aidha, Muislamu anayeishi Tanzania na yule wa Indonesia au pengine popote, licha ya umbali wa kijografia, rangi, asili, lugha nk. Lakini bado Waislamu hao huwa ndugu kwa kuwa wamefungwa kwa mfumo wa Kiislamu, ambao huwafanya wote kuwa na mwelekeo, uoni na vipimo sawa vya ‘halali’ na ‘haramu’. Licha ya kuwa leo kwa bahati mbaya Waislamu hawa hawatawaliwi kwa nidhamu ya Kiislamu. Lakini fungamano lao utaweza kulihisi hata kwa kile kiwango kidogo cha kushikamana na mfumo wao.

Na lau dola ya Kiislamu ya Khilafah inarudi tena kuwatawalia watu hao inakuwa wepesi zaidi kuongeza nguvu tu ya fungamano lao la mfumo wa Kiislamu baina yao.

Fungamano ambalo halijawahi kudhihirika mithili yake katika tareekh ya Uislamu na ubinadamu kwa jumla kwa kuwa linatokamana na mfumo wa haki, sahihi na unaowafikiana na maumbile ya mwanadamu. Allah Sw Anasema:

وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الأَرْضِ جَمِيعًا مَا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَكِنَّ اللَّهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

(الأنفال: 63).

‘Na akaziunganisha nyoyo zao. Na lau wewe ungetoa vyote vilivyomo duniani usingeliweza kuwaunganisha, lakini Allah ndie Aliyewaunganisha. Hakika Yeye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikma’

#UislamuMfumoMbadala

Masoud Msellem

17 Septemba 2018

Maoni hayajaruhusiwa.