Vita Dhidi ya Madawa ya Kulevya Havitafaulu chini ya Mfumo wa Kirasilimali

Mnamo Ijumaa, 18 Oktoba 2019, ripoti ya uchunguzi iliyopeperushwa na Runinga ya France 24 ilifichua kwamba Mji wa Mombasa umepatikana kuwa ndio kitovu cha usafirishaji wa madawa ya kulevya na ni njia ya heroin na cocaine kuelekea duniani. Miezi michache nyuma, Waziri wa Ndani na Mipango ya Serikali ya Kitaifa Fred Matiangi aliwaonya viongozi wa Pwani dhidi ya kuhusishwa na madawa ya kulevya. Onyo hilo ilitolewa baada ya magenge ya vijana waliobeba mapanga na kuwashambulia wakaazi wa Kaunti ya Mombasa na kuwajeruhi watu 14 hivyo kumpelekea Waziri kuanza upya vita dhidi ya madawa ya kulevya ndani ya mji wa Pwani. Katika hotuba yake alisema, “Litakuwa zoezi chungu lakini ninafuraha viongozi wa kisiasa wa eneo wamekubali kutunusuru. Nimejadiliana nao mikakati yetu na wameiridhia.” Ili kuonekana kwamba anayafanyiakazi matamshi yake mnamo 13 Agosti 2019 vyombo vya habari viliripoti kwamba timu ya mjumuiko wa vikosi vya kupambana na madawa ya kulevya vilikuwa vimetoa ilani ya kumkamata na walitarajiwa kuvunja na kuingia katika nyumba ya mfanyibiashara wa Mombasa Ali Punjani kwa madai ya usafirishaji wa madawa ya kulevya.

Hakika, huku Kenya ikiwa ndio mfano wa kuzingatiwa, vita dhidi ya madawa ya kulevya havikuanza leo. Mnamo 2017, ndugu wawili waliodaiwa kuwa wakuu wa madawa ya kulevya walishikwa na kukabidhiwa mamlaka za Amerika ili kushtakiwa kwa mashtaka yanayohusiana na madawa ya kulevya. Na katika sherehe ya mwaka ya kilimo huko Mombasa katika mwaka wa 2015, kiongozi wa serikali alitangaza, “Sasa nina furaha kwamba vijana wako makini na wanaweza kufanyakazi… Vita sasa lazima viwe juu ya madawa ya kulevya,” Tangazo hilo lilitolewa baada ya kushikwa na kuharibiwa kwa meli iliyoshukiwa kubeba heroin yenye thamani ya milioni Ksh28. Katika mwaka wa 2013, watawala wapya walioingia madarakani walitabban sera ya kuwafurusha wakuu wa madawa ya kulevya ambapo raia wa Nigeria alifurushwa haraka kwenda Nigeria na kusababisha mzozo wa kidiplomasia baina ya Kenya na Nigeria. Ama kuhusu mwaka 2012 ndani ya serikali ya muungano, ubalozi wa kigeni ulitoa ripoti kuhusu madawa ya kulevya na wakuu wa madawa ya kulevya ikiwahusisha wanasiasa tajika, wafanyibiashara na wanachama wa familia zilizoko uongozini. Waziri wa Usalama wa Ndani alitangaza uchunguzi kwa wale waliotajwa katika ripoti na kabla tu kutoa orodha hiyo bungeni, alipatikana amefariki kwa ajali ya ndege.

Hivyo basi kupitia mipango hii na mengine kama ya kubuni kitengo cha polisi cha kupambana na madawa ya kulevya ndani ya mataifa ya kirasilimali yameonekana yakitumia rasilimali na juhudi nyingi kupigana dhidi ya matumizi na usafirishaji wa madawa ya kulevya. Ama kuhusu uhalisia wa madawa ya kulevya, kwa mujibu wa ripoti ya Global Financial Integrity (GFI) iliyotolewa mnamo 27 Machi 2017 –soko ya dunia ya madawa ya kulevya ilikadiriwa kuwa kila mwaka ina thamani ya baina ya dolari bilioni 426 na dolari bilioni 652. Hivyo basi, ikiifanya kuwa ndio soko kubwa haramu lililotathminiwa baada ya lile la bidhaa ghushi. Hivyo basi kwa kuzingatia msingi wa kirasilimali unaosema kwamba, ‘kitu chochote kinachovutia kina manufaa, na kitu chochote chenye manufaa ni kitu cha kiuchumi,’ ni wazi kwamba kiwanda cha madawa ya kulevya kinayo thamani ya kiuchumi na hivyo basi itakuwa vigumu kupambana na kuipiga marufuku ndani ya mfumo wa kisekula wa kirasilimali.

Kuhusiana na matunda ya madawa ya kulevya, kiongozi wa zamani wa afisi ya UN ya madawa ya kulevya na uhalifu, Antonio Maria Costa alisema, “baada ya kuanguka kwa soko la kifedha la dunia mnamo 2008, katika mifano mingi, fedha kutoka katika madawa ya kulevya ndio ilikuwa uwekezaji wa pekee wa kimitaji. Katika nusu ya pili ya 2008 mtaji ulikuwa ndio tatizo kuu la nidhamu ya benki na hivyo mtaji ukawa ndio kigezo muhimu,” Napia akasema, “Mikopo baina ya benki ilidhaminiwa kwa fedha zilizotokana na madawa ya kulevya na amali nyingine haramu…kulikuwepo na ishara kwamba baadhi ya benki zilinusuriwa kupitia njia hiyo.” Hivyo basi kwa mujibu wa matamshi ya afisa mkuu wa UN, ni kimaumbile kukatikiwa kwamba matunda ya madawa ya kulevya yanacheza dori muhimu katika uchumi wa mataifa ya kirasilimali.

Kwa kufupisha tangu kutangazwa kwa vita dhidi ya madawa ya kulevya badala ya kuona kupunguzika kwa matumizi ya madawa ya kulevya kinyume chake ndio kinachotokea! Mnamo 1988 afisi ya UN ya madawa ya kulevya na uhalifu iliandaa kongamano lake la kwanza la kimataifa kuhusiana na madawa ya kulevya kwa kichwa, ‘DUNIA HURU ISIYOKUWA NA MADAWA YA KULEVYA INAWEZEKANA’. Ni zaidi ya miongo mitatu tangu wakati huo na dunia bado haijakuwa huru kutokana na madawa ya kulevya. Haswa kinachoendelea tangu wakati huo ni kwamba dunia inakoloniwa na wakuu wa madawa ya kulevya. Felipe Calderon, mkuu wa serikali ya Mexico aliwahi kusema, “Kusitisha matumizi na usafirishaji wa madawa ya kulevya ni zoezi lilsilowezekana… naam lilikuwa sio lengo. Kwa vikosi vya polisi kusitisha kitu ambacho hakiwezekani kusitisha, ambacho ni matumizi na usafirishaji wa madawa ya kulevya.”

Iko wazi kwamba mataifa ya kirasilimali yamefeli kusitisha janga la madawa ya kulevya kwa kuwa tokea mwanzo hawalioni kuwa ni janga. Ama kuhusu yale tunayoyaona kutoka kwa mataifa ya kirasilimali juu ya vita dhidi ya madawa ya kulevya na wakuu wa madawa ya kulevya, kiuhakika tutaendelea kuona filamu hizo kwa kuwa ni vitendo vya kiusanii vilivyo zinduliwa ili kuyadanganya macho ya wapiga kura kwamba kuna vita dhidi ya madawa ya kulevya. Ni wazi bila shaka kwamba lengo la vita dhidi ya wakuu wa madawa ya kulevya na matumizi ya madawa ya kulevya ni kupigana na washindani wa kibiashara pamoja na kudhibiti soko la madawa ya kulevya.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ لاَ تُفْسِدُوا فِي الأَرْضِ قَالُوا إِنَّمَا نَحْنُ مُصْلِحُونَ

Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji.”

Khamis Mwangemi (Abu Leila)

Inatoka Uqab: 35 https://hizb.or.tz/2019/12/01/uqab-35/

Maoni hayajaruhusiwa.