Mikataba Iliyoinyonga Khilafah

Madola ya Magharibi chini ya Uingereza hayakutosheka kugawana ngawira baada ya Vita vya Kwanza vya dunia. Bali waliendelea na mkakati kabambe wa kuhakikisha wanaivunjavunja kabisa athari ndogo iliyobakia ya dola ya Khilafah Uthmania.

Uingereza kwa tathmini na umahiri wake iliona kinachohitajika ni kuibana mbavu zaidi Khilafah kisiasa, kisheria kwa kupitia mikataba ya dhulma, kwa msukumo wa nguvu ya kijeshi na kusaidia wimbi la ndani kwa kupitia vibaraka wake wa kiarabu na kituruki na hatimae Khilafah itamomonyoka kuelekea katika kifo cha kikawaida.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba wakati huo Khilafah Uthmania ilikuwa katika kilele cha kugubikwa na udhaifu na unyonge uliosababishwa na kudorora katika ufahamu wa Kiislamu, mapungufu katika utabikishaji wa sheria na upeo mdogo kisiasa. Kwa hivyo, baada ya Vita vya Kwanza mkakati ulikuwa ni kuilazimisha Khilafah kwa nguvu kusaini mkataba unaojuulikana kama ‘Mkataba wa Sevres’ (Sevres Treaty) uliotiwa saini katika mwezi wa Agosti mwaka wa 1920. Khalifah Mohammed VI. Alituma maafisa wake wa juu kuwakilisha katika Mkutano wa mkataba huu wa hatari. Na kwa bahati mbaya wakaukubali. Lengo kuu likiwa ni kuibena, kuinyonga na kuinyofoanyofoa Khilafah.

Mkataba huu ulikusudia kuzikata ardhi za Khilafah vipande vipande kwa kuzipa mamlaka kamili, kuidhoofisha Khilafah kijeshi na kiuchumi na kuiweka katika udhaifu ambao katika siku za mbele kidogo itakuwa rahisi kwa kibaraka Mustafa Kamal kufikilia lengo la kuivunja Khilafah. Ikumbukwe hata kabla ya mkataba huu tayari Khilafah ilikwishaporwa baadhi ya ardhi zake kadhaa na madola ya Uingereza, Ufaransa na Urusi.

Mkataba huu wa Sevres ulipelekea rasmi kuzaliwa dola mpya ya Saudia chini ya athari ya Uingereza, kupewa uhuru ardhi ya Armenia, kuyagawa maeneo ya Syria na Lebanon kuwa katika hatamu ya Uingereza na Ufaransa nk. Kwa ufupi kwa mkataba huu Khilafah ilimegwa ardhi yake kutoka kilomita za mraba 613,724 na kubakishiwa kilomita za mraba 174,900. Pia Mkataba huu ulitowa amri kwa nchi Washirika chini ya Uingereza kudhibiti kikamilifu bajeti ya Khilafah kuanzia mapato, ukiwemo ushuru wa forodha na kuzisimamia shughuli zote za kiuchumi kwa ujumla. Kwa upande wa kijeshi mkataba huu uliilazimisha Khilafah kubakiwa na jeshi lisilozidi wanajeshi 50,000, isimiliki boti za kivita zaidi ya sita na marufuku kabisa kumiliki jeshi la anga. Kifungu cha 230 cha mkataba huu kililazimisha Khilafah kumkabidhi kwa madola washirika mtu yoyote watakaemuhitaji kusalimishwa kwao kutokana na kushiriki katika mipango ya kiadui au kuyapiga vita madola yao. Kwa hakika ndani ya mkataba huu kulijaa vitisho na vitimbi vilevile tunayofanyiwa Waislamu leo na madola ya magharibi wakiongozwa na Marekani. Kiasi cha kuzipangia nchi za Kiislamu sera wanazozitaka wao za kijeshi, kuzibana katika kumiliki silaha kali zikiwemo silaha za nyuklia na pia kulazimisha wakabidhiwe raia Waislamu kwa kisingizio cha ‘Vita vya ugaidi’ ili kuwapeleka katika kambi zao za mateso za Guntanamo, Abu Ghuraib, Balgram na kwengineko, kama walivyoilazimisha dola ya Taliban ati iwakabidhi mikononi mwao Shahid Usamah bin Laden- Allah Taala Amrehemu.

Mkataba wa pili uliokuwa msumari wa mwisho wa jeneza la kuizika Khilafah Uthmania ni Mkataba wa Lausanne uliofikiwa ndani ya Switzerland katika mwaka 1922. Masharti ya mkataba huu yaliandaliwa na Uingereza kwa kisingizio cha uhuru wa Uturuki ilhali uhalisia wake ni kuivunja Khilafah. Miezi michache kabla ya mkataba huu Uingereza ilieneza propaganda dhidi ya Khilafah kwa kisingizio cha mkataba wa awali wa Sevres. Ilijifanya hivyo ili kuonyesha uovu wa Khalifah na Waziri wake Mkuu Damad Farid Pasha kwa kuukubali kwao mkataba wa awali. Propaganda hii ya Uingereza ilikusudiwa kumuokowa kibaraka wake Mustafa Kamal ambae kipindi hiki Khilafah ilikabiliana nae kijeshi na kuvunja upinzani wake kwa kiasi kikubwa. Pia alikuwa akikabiliwa na upinzani mkubwa wa raia jumla kwa kuipinga kwake Khilafah waziwazi. Na badala yake ilikusudiwa kuijenga haiba ya kibaraka huyo ili umma umuone mkombozi wa kweli wa Uturuki na umuunge mkono. Kipindi hiki uasi wa Mustafa Kamal dhidi ya Khilafah ulikuwa umefikia kilele, kwa kujifanya mtawala kamili ndani ya jiji la Ankara badala ya utawala halali wa Khilafah ndani ya Istanbul. Madola ya Ulaya yakimpa utambuzi rasmi kwa uasi wake huu, kiasi kwamba katika Mkutano wa London (London Confrence) wa mwaka 1921 muda mfupi kabla ya Mkataba wa Lussanne. Madola ya Ulaya chini ya Uingereza yalimtumia mwaliko rasmi Mustafa Kamal kama mtawala rasmi wa Uturuki.

Ilipofika tarehe 20 Novemba 1922 Mkutano wa Lussanne ukazinduliwa, na ajabu Khilafah ya Uthmania ikiwa dola iliyoshindwa katika vita vya kwanza iliwakilishwa na waasi wa Ankara pekee bila ya serikali halali ya Istanbul. Mkutano huu kinara wake ilikuwa Uingereza chini ya uwakilishi wa Waziri wake wa Mambo ya nje Lord Curzon ambae ndie alietangaza masharti manne rasmi ya kutekelezwa na Uturuki ili ipewe uhuru kamili na kurejeshewa baadhi ya maeneo yanayoshikiliwa na majeshi ya washirika.
Masharti hayo yalikuwa:
1. Kukomesha kabisa Utawala wa Khilafah 2. Kumfukuza Khalifah nje ya mipaka ya Uturuki 3.Kufilisi milki yote ya Khalifah na 5. Kuitangaza rasmi Uturuki kwamba ni dola ya kisekula.

Licha ya upinzani mkali kupitia vitisho, hadaa na kudhoofika kwa Khilafah yenyewe katika mwezi kama huu wa Rajab mwaka 1342 Hijri (24/03/1924 miladi) ikatangazwa rasmi ndani ya Bunge la Ankara kutekelezwa masharti yote haya manne. Mustafa Kamal akatuma kikosi chake ndani ya Istanbul kumfukuza kwa idhilali Khalifah Abdul Majid. Akaondoka na kimkoba cha mkononi, vijipesa kidogo na nguo chache kuelekea Switzerland.

Mkataba wa Lussanne ukatiwa saini rasmi tarehe 24 Julai 1924, nchi washirika wakautambua rasmi uhuru wa Uturuki na kujitowa katika maeneo waliyokuwa wakiyashikilia ndani ya Uturuki. Lord Curzon akajigamba baada ya kuiangusha Khilafah aliposema ndani ya Bunge lao la House of Commons:
‘Nukta ya msingi ni kwamba Uturuki imeshaangamizwa na haitohuwika tena kwa sababu tumeshavunja vunja roho ya nguvu yake: Khilafah na Uislamu”.
Kauli hii ni chungu lakini ina ukweli ambao lazima tuuzingatie hususan katika mwezi huu wa Rajab ulioangushwa Khilafah ya mwisho. Kwani nguvu, izzah na heshima ya umma wetu ni kwa kushikamana na Uislamu wetu pekee, ambao nao ni wajibu uwe chini ya utawala wa Khilafah. Kwa hivyo, ni wajibu sote kujifunga kufanya kazi ya kuirejesha tena Khilafah Rashidah ambayo tayari imeshabashiriwa na Mtume wetu SAW ili kuukombowa umma wetu na ulimwengu kwa jumla.

Maoni hayajaruhusiwa.