Msiba wa Kuangushwa Khilafah na Uwajibu wa Kuirejesha

Dola ya Kiislamu ya Khilafah iliangushwa mnamo tarehe 3 Machi 1924 sawa na  27 Rajab 1342 Hijria. Dola hii ilianzia baada ya kufariki Mtume SAAW, na Khalifah wa mwanzo akawa ni Sayyidna Abubakar (ra). Dola hii iliufanya Uislamu mfumo wake pekee katika kila kipengee na ilibakia na kudumu kuwa dola yenye nguvu na ushawishi ulimwenguni hadi karne ya 18. Hatimae kutokana na kudhoofika kifikra na kuongezeka kwa uadui wa ndani na nje iliweza kuangushwa na kuacha msiba usio na kifani katika ummah wa kiislamu hadi leo.

Baada ya tukio hili la kuhuzunisha, yalifuatia kila aina ya majanga kwa Ummah wa Kiislamu. Miji/ardhi yao ikagawanywa vipande vipande na kuundiwa vijinchi dhaifu dhaifu na kutawalishiwa vibaraka wa kikoloni kuvisimamia. Waislamu kila mahala wamekuwa ni walengwa wa wazi wa nguvu za maadui. Dhulma, mateso, udhalili, unyonge, umasikini, khofu, mauwaji na kila aina ya mabalaa ikiwemo kutukanwa Mtume wetu Mtukufu SAAW, kukashifiwa Quran takatifu, kunajisiwa ardhi tukufu, yametusibu na yanaendelea hadi leo.

Tumeshuhudia mauaji na ukatili usioelezeka wa mayahudi dhidi ya ndugu zetu wa Palestina, pia mauaji dhidi ya ndugu zetu Chechnia, Bosnia, Kossovo, Kashmir, Afghanistan, Burma, Somalia, Kenya, Tanzania, Afrika ya Kati, Misri, Syria, Iraq, Yemen nk.
Kwa hakika madhila, mateso na mauwaji haya kwa Waislamu hayatokoma bila ya kurejesha dola ya Khilafah. Kwa kuwa dola hiyo ndio ngao na kinga ya kweli kama alivyosema Mtume SAAW:
“Kwa hakika Imam (Khalifah) ni ngao, hupiganwa nyuma yake na hupatikana kinga kupitia kwake”.

Kimsingi kila anayechukizwa na ukafiri kumtawalia maisha yake, na kupendezwa na Uislamu kuwa ndio mfumo wake maishani ili apate radhi za Allah SWT, basi hana budi kufanya kazi ya kumsimamisha Khalifah atakaepewa bay’ah. Kwa kitendo hicho atajiepusha na dhambi kubwa. Kwani Mtume SAAW amesema: “Yeyote anaekufa pasi na bay’ah juu ya shingo yake anakufa kifo cha kijahilia”. Yaani mtu huyo anatenda dhambi kubwa sana. Pia yeyote anaempenda Mtume SAAW kweli na kupenda na kuchukizwa pindi anapokashifiwa na kutukanwa basi na amtii Mtume SAAW kwa kufuata mwenendo kwa kuirejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah itakayowalinda hadhi na heshima ya Mtume SAAW na matukufu yote ya Kiislamu.

Enyi Umma wa Kiislamu
Qadhia ya kurejesha Khilafah ni tukufu na ni dhima kubwa mbele ya Muumba wetu. Hivyo, hapana budi kushirikiana pamoja kufanya kazi kwa bidii kwa njia ya Mtume SAAW bila ya kutumia nguvu au kutekeleza mashambulizi, sio kwa kuogopa makafiri na vibaraka wao, bali kwa kujifunga na njia ya Mtume SAAW. Muda umefika wa kushindana wenye kushindana katika kuikimbilia bishara tukufu ya Mtume wetu SAAW:
..ﺜﻢ ﺘﻌﻭﺩ ﺧﻼﻓﺔ ﻋﻟﻰ ﻤﻨﻬﺎﺝ ﺍﻟﻨﺑﻭﺓ
….’.Kisha itarudi tena Khilafah kwa njia (manhaj) ya Utume’

https://www.facebook.com/HtTanzaniaa

Maoni hayajaruhusiwa.