Nasaha Adhimu Kwa Mahujaji na Waislamu Wote

بسم الله الرحمن الرحيم

Tayari baadhi ya Waislamu kutoka Mashariki na Magharibi wanakusanyika katika mji mtukufu wa Makka kwa ajili ya ibada tukufu ya Hijja. Ibada ambayo ni faradhi kwa kila Muislamu mwenye uwezo.
Kwa wanaobahatika kutekeleza ibada hii hupata fursa adhimu ya kuizuru na kufanya ibada katika nyumba tukufu ya mwanzo iliyoteuliwa na Allah Taala:
اِنَّ اَوَّلَ بَیۡتٍ وُّضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِیۡ بِبَکَّۃَ مُبٰرَكًا وَّہُدًی لِّلْعٰلَمِیۡنَ ﴿ۚ۹۶﴾
“Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka (Makka), iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote” (TMQ 3:96)
Enyi Mahujaji na Waislamu kwa jumla:
Ibada ya Hijja inatufunza kujizatiti vilivyo na majukumu ya Uislamu, kujitolea muhanga, kujifunga vilivyo na kipimo chetu cha halali na haramu katika chumo na matendo yetu, kupambana na kila taratibu, nidhamu, fikra au mfumo wa kishetwani nk. Pia Hijja inatukumbusha uwajibu wa kulinda na kutetea mshikamano wa kweli kwa Umma wetu, kwa Waislamu wa pembe moja ya dunia kujali na kushughulishwa kwa kupambana kuondoa mashaka, misiba na madhila yanayowasibu Waislamu sehemu mbalimbali duniani, kwa kuwa Umma wetu ni Umma mmoja kimaumbile usiogawanyika milele .Aidha, kubwa zaidi ibada hii hutukumbusha uwajibu mkubwa wa kuishi chini ya bendera moja ya dola ya Kiislamu ya Khilafah.
Enyi Mahujaji na Waislamu kwa jumla:
Katika zama tukufu za makhalifa, Umma wa Kiislamu ndani ya Hijja ilikuwa jukwaa kamili la Uislamu ambapo Umma ulipewa risala za ukombozi kwa khutba zinazoonesha masuluhisho ya matatizo kwa mujibu wa Quran na Sunna. Tofauti na leo ambapo khutuba si za namna hiyo. Kama ambavyo serikali ya Saudia kuwahi kuwalingania mahujaji fikra ya dini mseto kupitia mfalme wao Abdullah. Na pia utawala huo kuwaonesha Waislamu suluhisho lisilokuwa la Kiislamu kama kutoka Umoja wa Mataifa (UN) nk.
Enyi Mahujaji na Waislamu kwa jumla:
Umma wetu leo umetiwa uzito, ugumu na vikwazo visivyokubalika katika utekelezaji wa Hijja. urasimu wa ruhusa ati ‘viza’, huduma duni, na udhaifu katika mchakato mzima wa usimamizi, usalama na utekelezaji wake. Hatuna haja kuwakumbusha msiba mkubwa uliowasiba mahujaji kwa kupoteza maisha yao kwa maelefu miaka ya nyuma kutokana na uzembe wa utawala dhalimu wa Saudia. Mahujaji huruhusiwa kubakia ndani ya mji mtukufu kwa masiku machache na yakimalizika hutimuliwa kwa idhilali, kana kwamba ni wageni au wakimbizi wasio na haki kwa mji mtukufu ambao ni kwa ajili ya Waislamu wote wa mbali na wa karibu na kwa wakati wote. Kwa jeuri na kibri Ufalme wa Saudia hutawanya matangazo ya kifedhuli, dharau na vitisho kwa Waislamu watakaozidisha hata siku chache! Hii ni kwa sababu Hijja leo haisimamiwi rasmi na dola ya Kiislamu ya Khilafah kama ilivyokuwa zama za nuru na utukufu za makhalifa. Na badala yake leo husimamiwa kwa mapungufu makubwa ya kiusimamizi kutoka kwa utawala dhalimu wa kitwaghuti na kuhudumiwa na vijumuiya binafsi ambavyo baadhi yao hata havina sifa, uweledi, uwezo wala uaminifu, zaidi ya kujitajirisha.
Hali hii ni changamoto kwetu Waislamu sote ya kufanya kazi ya kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah ili isimamie ibada hii ipasavyo pamoja na ibada nyengine zote.
Tunamuomba Allah Taala Awawezeshe mahujaji wetu kutekeleza ibada hii na kufikia daraja ya kutakabaliwa/Hajj-mabroor. Aidha,Tunamuomba kwa Utukufu wake kuwawezesha Waislamu wengine kupata fursa adhimu ya kutekeleza ibada hii kabla ya kuondoka duniani. Amiin
Risala ya Wiki No. 137
27 Dhu al-Qi’dah 1443 Hijria / 26 Juni 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
#WahyiChimbukoLaThaqafahYetu

Maoni hayajaruhusiwa.