Katika Kumkumbuka Alim Mkubwa Sheikh Taqiudin An-Nabhan (R L)
بسم الله الرحمن الرحيم
Ndani ya mwezi kama huu wa Disemba (Tarehe 11) 1977 alifariki dunia mwanachuoni Mujadid, mwanasiasa mkubwa wa Kiislamu na na Muasis wa Hizb ut-Tahrir Sheikh Taqiudin An-Nabhani
Jina lake kamili ni Muhammad Taqiuddin bin Ismail Bin Mustafa Bin ismail Bin Yusuf An-Nabhani anatokana na kabila la Nabhani, na anatokea katika kijiji cha Ijzim huko Haifa Kaskazini mwa Palestina. Sheikh alizaliwa kijijini hapo mnamo mwaka 1332 Hijri sawa na 1914.
Familia yake ilifahamika kwa elimu na uchamungu. Baba yake Sheikh Ibrahimu, alikuwa faqihi na mwanazuoni wa elimu ya sheria katika Wizara ya Mambo ya Elimu. Mama yake pia alikuwa mjuzi wa elimu ya sheria ambaye aliipata kutoka kwa baba yake Sheikh Yusuf An-nabahani.
Masimulizi kuhusu upande wa babu yake upande wa mama nasabu yake ni kuwa, Yusuf Bin Ismail Bin Yususf Bin Hassan Bin Muhammad An-nabahani Ashafii jina maarufu/kun-ya ni “Abu almahasin” alikuwa mshairi, sufi na mwanazuoni. Alikuwa miongoni mwa maqadhi bora katika zama hizo. Alifanya kazi ya uqadhi katika ukanda unaounganisha Jenin na Nablus. Baadaye akahamishiwa Istanbul na kuwa Qadhi katika eneo la Kavi Sanjaq huko Mosul.
Baadaye akateuliwa kuwa mkuu wa mahkama ya Al-Azqya na Al-Quds. Kisha akasimamia mahkama ya haki ya Beirut. Ameandika vitabu arubaini na nane.
Shakhsiya ya Kiislam ya Sheikh Taqiuddin An-nabahani ni zao linalotokana na familia yake. Alihifadhi Qur’ani yote alipokuwa na umri wa miaka 13. Alivutiwa sana na babu upande wa upande wa mama kutokana na elimu yake na ufahamu wa mambo. Alichukua kutoka kwake bahari ya elimu kiasi alichoweza.
Tangu mwanzo alichukuwa ufahamu wa kisiasa hususan kupitia harakati za kisiasa zilizoasisiwa na babu yake ili kuunga mkono Khilafah Uthmaaniya. Sheikh alinufaika mno na hoja zinazotokana na elimu ya sheria ambazo zilitolewa na babu yake Sheikh Yusuf. Hili lilimsukuma Sheikh Yusuf amshauri baba yake Sheikh Taqiuddin ampeleke mtoto wake chuo kikuu cha Azhar akapate elimu ya Sharia.
Elimu Yake
Sheikh Taqiuddin alisajiliwa daraja la nane katika chuo kikuu cha Azhar mnamo mwaka 1928 na kufaulu mitihani yote ndani ya mwaka. Akatunukiwa shahada iitwayo “Shuhada Al-Ghurba”.
Baada ya hapo akasajiliwa katika Chuo cha sayansi ambacho kilikuwa na mafungamano na chuo cha Azhar kwa wakati huo. Aliendelea kuhudhuria darsa za wanazuoni ambao babu yake alimwelekeza kama sheikh Muhammad Al-Khizar Hussain (Rh). Zamani wanafunzi waliruhusiwa kuhudhuria darsa hizo. Sheikh Taqiuddin aliendelea kung’ara katika chuo cha sayansi ingawa muda mwengine aliugawa kuhudhuria darsa za Sheikh.
Walimu wake walimpenda kwa uhodari wake, fikra yake ya ndani, bidii ya kusoma na hoja zake zenye nguvu alizozitoa katika mijadala iliyofanyika katika chuo cha Azhar na sehemu nyengine za ardhi ya Kiislam.
Sheikh alitunukiwa shahada zifuatazo:
• Mutawastwa kutoka Azhar
• Shahadatal ghurba kutoka Azhar
• Shahada ya lugha na fasihi ya Kiarabu kutoka Daarul Uluum Cairo
• Shahada ya Uqadhi kutoka chuo cha Ma’had al’Aala ambacho ni chuo cha Sheria ni tawi la Azhar
• Vilevile alipata shahadat Alamiah (Masters degree) sheria kutoka Al-Azhar mnamo mwaka 1932.
Kazi Zake
Sheikh alifanya kazi katika Wizara ya Al ma’arifa katika Idara ya elimu kitengo cha sheria mpaka mwaka 1938. Kisha akapandishwa cheo na kuhamishiwa mahakama ya sheria na kuwa qadhi katika mahakama Haifa. Baadaye akapandishwa cheo na kuwa qadhi mkuu msaidizi. Kisha akawa qadhi katika mahakama ya Ramallah mpaka mwaka 1948.
Baada ya Palestina kuchukuliwa na Wayahudi, akahamia Syria lakini mwaka huo huo akarejea Palestina na akateuliwa kuwa qadhi wa Mahkama ya Sheria ya Al-Qudus kisha akafanya kazi kama qadhi wa Sheria wa mahkama kuu mpaka mwaka 1950. Baada ya hapo akajiuzulu na kuwa mwalimu katika chuo cha Uluum Islamiya cha Oman.
Sheikh Taqiuddin alikuwa bahari kubwa na hazina ya elimu katika matawi mengi ya elimu. Alikuwa Mujtahid mkubwa pia alikuwa muhadith.
Vitabu Alivyoandika Sheikh Taqiuddin
• Nidham al Islam
• Attakatul Hizb
• Mafahimu ya Hizb-ut-Tahrir
• Nidhamu ya uchumi katika Uislam
• Nidhamu ya Ijtimai katika Uislam
• Nidhamu hukmu katika Uislamu
• Katiba ya dola ya Khilafah
• Mukhtasari wa katiba
• Dola ya kiislamu
• Shakhsiya ya Kiislamu
• Ufahamu wa kisiasa wa Hizb-ut-Tahrir
• Fikra ya kisiasa
• Mwito wa dhati
• Khilafah
• Attafkir
• Uwepo kwa Akili
• Nukta ya kuondokea
• Kuingia katika jamii
• Lislah Misri
• Al Ittifaqiyat assaniyat al mastiya al Surya wal yumnia
• Hal Qadih Falastin alaa Tariqatal Amrikya wal Inglizia
• Nazra al faragh al syasi Hul mashruizan hawar
Na pia kuna mamia ya makala za kisiasa, kifikra na kiuchumi.
Pindi vitabu vyake na makala zake zilipopigwa marufuku, alichapisha baadhi ya vitabu kwa majina ya wanachama wenzake wa Hizb-ut-Tahrir kama:
• Mfano wa sera ya kiuchumi
• Ubatili wa ukomonist wa Kimax
• Vipi Khilafah iliangushwa.
• Hukmu ya ushahidi katika Uislamu
• Nidhamu ya kuadhibu wahalifu katika Uislamu
• Hukmu za swala
• Fikra ya Kiislamu
Kabla ya kuasisi Hizb-ut-tahrir aliandika vitabu kama
• Ukombozi wa Palestina
• Risala kwa Waarabu
Sifa Zake
Zuhair Kahala, Mwalimu na pia alikuwa mkuu wa utawala katika chuo cha Masuala ya Uislamu, alikuwa ni mwajiriwa chuoni hapo kipindi ambacho Taqiuddin alianza kufanya kazi hapo. Anasimulia: “Sheikh alikuwa ana akili sana mwadilifu na mwenye moyo safi. Alikuwa mukhlisi ana utu na alijipamba kwa shakhsiya ya Kiislamu. Kuwepo kwa mayahudi ndani ya Ardhi tukufu ya Qudus kulimhuzunisha sana.” Anamalizia Zuhair Kahala“alikuwa na kimo cha wastani, mwili imara wenye nguvu, hodari, mchapakazi, mtekelezaji wa kauli zake, akiwa muwazi na mwenye hoja zenye nguvu katika mijadala. Alikuwa ni mtu wa kupigiwa mfano katika kuwasilisha hoja. Kamwe hakurudi nyuma katika jambo aliloamini ni haki. Ndevu zake zilikuwa ndefu kiasi zenye mvi. Shakhsiya yake iliiwaathiri watu wengi. Hoja zake ziliwafanya wengine kubwaga hoja zao. Kamwe hakujitumbukiza katika mapambano yasiyo na lengo kumshambulia mtu binafsi, na kuacha maslahi ya ummah, alichukizwa na watu wanaopotoka katika maisha yao. Daima akishughulishwa na hatima njema ya Ummah,”
Alikuwa mfano halisi wa kauli ya Mtume (s.a.w) ‘siyo katika sisi asiyeshughulishwa na mambo ya Waislamu.” Alikuwa akiirudia hadithi hii mara kwa mara akiiifanya kama dalili. Alieleza masikitiko yake juu ya ukweli kwamba Imamu Ghazali (Rh), mwandishi wa kitabu “Ahyaa al Uluum” alijishughulisha na kuandika vitabu wakati wa vita vya msalaba.
Kuasisi Kwa Harakati Ya Hizb ut-Tahrir
Sheikh Taqiuddin alizifanyia uchambuzi kwa makini harakati na taasisi ambazo ziliibuka baada ya karne ya nne hijriya. Alifanya juhudi kubwa kuzichunguza kwa kina harakati hizo. Kwa jicho la ndani aliangalia mbinu zao, fikra zao, kuvamiwa na sababu za kushindwa kwao. Kwa kuwa Sheikh alijua ulazima wa kuwepo Hizb ambayo itasimamisha Khilafah, kwa hiyo alizisoma harakati hizo kwa msukumo huu.
Baada ya kuangushwa Khilafah kwa mikono ya muovu Mustafa Kamali Ataturk, Waislamu hawakusimamisha Khilafah, ingawa kulikuwa na vikundi vingi vya Kiislamu vya harakati. Kuchukuliwa Palestina na mayahudi mwaka 1948 na waarabu kutotoa msaada wowote kwa watu wa Palestina mbele ya Wayahudi ambao walipewa nguvu na Serikali zilizo kuwa vibaraka wa Muingereza, serikali za Jordan, Misri na Iraqi kulichochea hamasa ya Sheikh Taqiuddin.
Kwa hiyo akajikita kufanya uchambuzi wa sababu zilizowafikisha Waislamu hapo walipo na hatua zipi zitawahuisha.
Katika safari za kuuhuisha Ummah wa Kiislamu kwa mara ya kwanza Sheikh Taqiuddin aliandika vitabu viwili “Ukombozi wa Palestina” na “Risala kwa Waarabu” vilivyochapishwa mwaka 1950. Vitabu hivi vilieleza fikra, Aqidah na ujumbe khasa kwa Ummah wa Kiislamu. Yaani ni Uislamu pekee ndio suluhisho na waarabu watafute suluhisho la matatizo yao kupitia Uislamu siyo Uasabiya, kama nchi za Kiarabu. Fikra ya nchi za kiarabu iliyoenezwa na wakoloni iliuweka Ummah mbali na suluhisho la matatizo yao na ujumbe khasa wa Uislamu. Walijishughulisha na fikra za kimagharibi zinazogongana na Aqeedah ya Kiislamu, na vipimo vya Kiislamu katika kuyaendea mambo.
Sheikh Taqiudin kabla ya kufikia maamuzi, aliwakabili wanazuoni wote aliowajua na aliokutana nao Misri. Akawapa fikra ya kuanzisha Hizb ya kisiasa ili kurejesha maisha ya Kiislam na kurejesha hadhi ya Ummah kama ilivyokuwa zamani. Kwa lengo hili aliizunguka ardhi yote ya Palestina akiwakabili wanazuoni juu ya jambo hili. Amma kwa hakika qadhia ya Khilafah iliushughulisha moyo wake na akili yake.
Aliwakusanya wanazuoni na kuandaa Kongamano ili kujadiliana nao manhaji ya kurejesha Dola ya Khilafah. Aliwaambia waziwazi wanazuoni hao waliohudhuria kwamba njia wanazozifuata hazitazaa matunda na badala yake zitaondoka patupu. Mara nyingi washiriki wa makongamano hayo walikuwa ni viongozi wa harakati mbalimbali za Kiislamu na harakati za kitaifa.
Aidha, alitoa khotuba kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisiasa. Alikhutubia katika Masjid Al-Aqsa, Al-Khalil na sehemu nyenginezo. Aliwaeleza uhalisia wa Arab League kuwa ni chombo cha wamagharibi kikiwa ni miongoni mwa vyombo vingi vya Wamagharibi. Chombo hiki kimemakinisha ukoloni wa Wamagharibi katika ardhi za Waislamu.
Sheikh alifichua khiyana na njama za wamagharibi na kudhihirisha hatari yake kwa Uislamu na Waislamu. Akajenga ufahamu wa uwajibu kwa Waislamu kurejesha maisha ya Kiislamu na kuwaita waunde Hizb inayotokana na Aqeedah ya Kiislamu.
Sheikh alisimama kama mgombea katika baraza la wawakilishi, ambalo ni kamati ya ushauri tu na siyo ya utawala. Lakini kutokana na msimamo wake, harakati zake za kisiasa, mapambano yake ya dhati ya kuanzisha Hizb ya kisiasa ambayo imejifunga na Uislamu, serikali ilipindua matokeo dhidi ya Sheikh.
Lakini hili halikumrudisha Sheikh nyuma, wala kumdhoofisha katika dhamira yake ya kazi za kisiasa bali aliendelea kuingiliana na Ummah na mijadala. Kazi yake ilikuwa ni yenye ufanisi kwani Allah[swt] alimpa tawfiq ya kukubaliwa na wanazuoni maarufu, maqadhi na wanasiasa mufakkirina ili kuanzisha Hizb ya kisiasa. Akasaidiana nao kuweka mfumo na muundo wa Hizb ambao umekuwa ni miongoni mwa urathi wenye kuendelea wa Hizb- u-t Tahrir.
Ardhi tukufu ya Quds ndiyo sehemu iliyoasisiwa Hizb-ut-Tahrir. Sehemu ambayo sheikh alikuwa anafanya kazi katika mahakama kuu.
Wakati huo aliwakabili watu maarufu kama Sheikh Ahmad Dawr wa Qalqila, Sayyadan Nimra wa Misri, Daudi Hamdan wa Ramallah, Sheikh Abdulqadeem Zallum wa Al-Khalili (Hebron), Adil Al-Nabulsi, Ghanim Abdu, Munir Shaqir, Sheikh As’ad Bewiz Tamimi na wengineo.
Mwanzoni vikao vilifanyika miongoni mwa waasisi na havikuwa na mpangilio maalum bali vilizingatia mahitaji kwa wakati huo. Vikao vingi vilifanyika Al-Quds au Al-Khalil ambapo mada za kuwalingania watu wajiunge na Hizb zilihudhurishwa na kujadiliwa. Na maudhui nyingi yalikuwa ni yale yatayourudishia Ummah wa Kiislamu utukufu wake. Hali hii iliendelea mpaka mwishoni mwa mwaka 1952 pale ambapo watu hawa walikula qasam (kiapo) cha kuanzisha chama cha kisiasa kwa msingi wa Kiislamu kitakachofanya kazi ya kurejesha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Dola ya Khilafah kwa njia ya Mtume[saw]
Mnamo tarehe 17/11/ 1952, wanachama watano waasisi walimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jordan aelewe kwamba wao wamefuata sheria iliyokuwa ikitumika zama za Khilafah Uthmaniya na wameanzisha chama cha kisiasa kwa msingi wa Uislamu.
Wanachama hao walikuwa:
• Taqiuddin An-Nabahan – Amir
• Daudi Hamdan – Naibu Amir
• Ghanim Abdul – Muweka hazina
• Adil Al-Nabuls – Mwanachama
• Munir Shaqir – Mwanachama
Baada ya hapo, Hizb ikawa imekamilisha taratibu zote za kisheria zilizokuwa zikitumika wakati wa Khilafah Uthmaniya kwa mtu anayetake kuanzisha chama cha kisiasa. (yaani kutoa taarifa siyo kuomba kibali au usajili). Makao makuu yakawa Al-Quds.
Katika chapisho la “Mfumo wa hukmu na kanuni za utawala” kutoka Hizb toleo No. 176 ya gazeti la Al Sarih la tarehe 14/03/1953; Hizb-ut-Tahrir ikawa chama rasmi cha halali cha kisiasa tangu tarehe hiyo, ambayo ni sawa na mwezi 28 Jumadal Awwal 1372.
Kwa hiyo kuanzia hapo, Hizb-ut-Tahrir ikaanza kutekelaza majukumu yake ya kisiasa ambayo ni kwa mujibu wa sheria zilizotumika katika Dola ya Khilafah Uthmaniya. Hata hivyo, serikali iliwakamata na kuwahoji wanachama wote na kuwaweka mahabusu wanne kati yao. Mnamo mwezi 7 Rajabu 1372 Hijri sawa na 23/03/1953 Serikali iliifungia Hizb-ut-Tahrir, kupiga marufuku kazi zake na kumwamuru mwasisi wake asitishe kazi zake mara moja. Mnamo 01/04/1953 mabango na matangazo yake yaliyoibandikwa katika ofisi yake hapo Al-Quds yaling’olewa ikiwa ni hatua za utekelezaji wa amri ya Serikali.
Hata hivyo, Sheikh Taqiuddin alipuuzia kufungiwa huko na akasonga mbele katika amali hii tukufu. Daudi Hamdan na Nimr Misr wakajiengua kutoka katika Uongozi mnamo mwaka 1956. Na nafasi zao kuchukuliwa na Sheikh Abdulqadeem Zallum na Sheikh Ahmad Dawr. Wanazuoni hawa watukufu walitekeleza majukumu yao katika amali hii adhimu.
Hizb ilianza kutoa thaqafa katika maeneo ya mikusanyiko ya msikiti wa Al-Aqsa ili kuhuisha maisha ya Kiislamu. Kutokana na amali hiyo iliyotishia utawala, serikali ya wakati huo ilifanya hila na njama ili kuidhoofisha Hizb isijiunde na kuwa Hizb yenye nguvu. Kutokana na vitimbi hivi Sheikh Taqiuddin aliondoka Palestina karibu na mwishoni mwa mwaka 1953, na alizuiliwa mara mbili asirejea. Mwezi Novemba mwaka 1953 Sheikh Taqiuddin alikwenda Syria, ambapo aliwekwa mahabusu na serikali ya Syria na baadaye akafukuzwa aende Lebanon, ilhali serikali ya Lebanon nayo ilikataa kumpokea. Hata hivyo, alimtaka ofisa anayehusika na kituo cha polisi katika bonde la Al-Harir kumwita rafiki yake. Ofisa huyo alimruhusu. Sheikh Nabahan alimwita rafiki yake Mufti Sheikh Hassan Al’Ala na kumsimulia hali halisi. Sheikh Al’Ala alichukua hatua haraka ya kuwatishia maofisa wale kwamba endapo watamzuia Sheikh Nabahan kuingia nchini mwao yeye atasambaza taarifa kwa Waislamu kwamba serikali inayojinadi ni ya kidemokrasia imemzuia Sheikh aliyefukuzwa kuingia nchini mwao. Serikali ya Lebanon ilifyata mkia kutokana na vitisho hivyo na hatimaye ikamruhusu Sheikh kuingia nchini humo.
Sheikh Taqiuddin alijikita katika kueneza daawah juu ya Khilafah na kupata vikwazo kwa kazi yake mpaka 1958. Pale serikali ya Lebanon ilipohisi hatari ya daawah yake wakaanza kumwandama Sheikh. Sheikh kwa siri akahamia mji wa Tripoli, Lebanon kutoka Beiruti. [Tripoli ya Lebanon siyo ya Libya.]
Mmoja wa rafiki zake wa karibu anasimulia kwamba Sheikh alitumia muda wake mwingi kwa kusoma na kuandika. Akifuatilia habari katika redio na kauli za wanasiasa. Alikuwa mchamungu kama lilivyo jina lake – Taqiuddin.Aliudhibiti ulimi wake na hakuwatazama sana watu. Haijawahi kusikika kwamba amemkashifu Muislamu yeyote, hususan walinganizi wa Kiislamu waliokhtalifiana naye katika ijtihadi.
Ndani ya nchi ya Iraqi Sheikh alijikita zaidi katika kutafuta nusrah. Alisafiri mara nyingi kwenda nchini Iraqi kwa lengo hili akiambatana na Sheikh Abdulqadim Zallum, ambaye alikuawa anawasiliana na watu, pia aliambatana na Abdul Salam Arif na wengineo.
Miongoni mwao hawa walikuwepo katika safari ya mwisho ambayo Sheikh aliwekwa mahabusu na kuteswa mateso makali, kimwili na kiakili. Hata hivyo, waliokuwa wakimtesa na kumhoji waliambulia patupu. Yeye alisisitiza kwamba yeye ni mzee aliyekuja Iraqi kwa ajili ya matibabu.
Amma kwa hakika Sheikh alikwenda kule kuutibu Ummah uhuike yaani wasimamishe Khilafah wafuzu duniani na Akhera.
Baada ya watesaji hao kukata tamaa ya kupata habari zozote kutoka kwa Sheikh walimvunja mkono na kumfukuza nchini mwao. Sheikh aliondoka huku akivuja damu baada ya mateso makali.
Wakati anaondoka, mamlaka ya Ujasusi ya Jordan iliitarifu serikali ya Iraqi kwamba Sheikh Taqiuddin wanayemtafuta ndiye huyo mzee waliyekuwa wanamtesa. Lakini Alhamdullillah! bahati haikuwa yao na Sheikh alikuwa ameshatokomea. Mateso makali aliyoyapata kutoka kwa watawala madhalimu yalisababisha mkono wake kupooza.
Kufariki Kwake
Sheikh Taqiuddin alikuwa na Istiqamah na alijifunga barabara na da’awah yake tangu kuanzishwa kwa Hizb, akiwa na matarajio ya kufikia lengo. Lakini Allah Taala akamwita. Sheikh alirejea mbele ya Mola wake katika maisha ya milele siku ya Jumamosi, tarehe mosi, mwezi wa Muharram 1398AH sawa na 11/12/1977.
Sheikh Taqiuddin alikuwa ni bahari ya elimu, kiongozi shupavu, bila shaka ni mwanazuoni mkubwa wa zama hizi, mhuishaji wa fikra za Kiislamu, mufakir mkubwa zaidi wa karne ya 20, mujtahidi wa kweli na mwanazuoni wa kupigiwa mfano.
Sheikh Taqiuddin alizikwa katika makaburi ya Ozayii huko Beirut. Sheikh hakuonja matunda ya kazi aliyoifanya na kujitolea muhanga kwa ajili yake. Hakuiona Dola ya Khilafah ambayo kwayo Hizb iliasisiwa. Lakini aliacha jukumu kwa Sheikh Abdulqadim Zallum, na yeye kwenda kukutana na Mola wake. Ingawa Sheikh Taqiuddin hakuishuhudia Khilafah kwa macho yake ikisimama lakini jitihada zake zimezaa matunda na Hizb imeeenea kila pembe ya ulimwengu na fikra zake zimekubalika ulimwenguni kote.
Makumi ya mamilioni ya watu wamejifunga na fikra zake ulimwenguni kote. Na maadui wa haki nao wameenea kila pembe ya Ulimwengu wakifanya kazi ya kufa na kupona kuizuiya Khilafah. Magereza ya watawala madhalimu yamejaa wanaharakati wanaobeba daawah iliyoasisiwa na Sheikh.
Allah Taala amtunuku Sheikh pepo ya Fir daus kwa kazii kubwa na mchango adhimu alioutoa katika kuhuisha Uislamu. Amiin
Imetafsiriwa na Ramadhan Njera
Inatokana na makala yenye anuani: ‘Kuondoka kwa Msafara wa Hizb ut Tahrir “Nuru iliyoanzia Masjid Al-Aqswa” http://www.khilafah.com/the-departure-of-the-caravan-of…/
Maoni hayajaruhusiwa.