Tatizo La Njaa Madagascar

بسم الله الرحمن الرحيم

Vyombo vya habari vimeripoti tukio la kuhuzunisha na kushtusha, la vifo kutokana na watu kukosa chakula nchini Madagascar. Shirika la chakula duniani (WFP) limeripoti kuwa watu 1.5 milioni kusini mwa Madagascar wanahitaji msaada wa chakula wa haraka. Hali hiyo inatokana na kiangazi kilichoathiri mazao.
Hali hiyo imepelekea watu wa Madagascar kula mchanga uliochanganywa na ukwaju. Shirika la Habari la AFP limemnukuu mkulima wa eneo linalokabiliwa na ukame bwana Fandilava Noelisona akisema: “Siku hizi hatutafuti tena chakula bali tunatafuta mbinu za kupata kitu chochote cha kushikilia tumbo”.
Kijiografia Madagascar ni kisiwa kilichozungukwa na maji kinachopatikana katika Bahari ya Hindi. Bahari ambayo ina utajiri mkubwa wa samaki kama kitoweo kwa binadamu. Kisiwa hiki maarufu kwa zao la biashara la Vanila na karafuu sehemu kubwa ya eneo lake limezungukwa na milima na hali ya hewa isiyotabirika kutokana na kutokuwa na uhakika wa mvua.
Hali hiyo huifanya nchi hii kutegemea kulima asilimia 5% pekee ambayo hulimwa kwa wakati wowote. Aidha sera mbaya za kikoloni nchini humo sehemu kubwa ya mashamba makubwa hutumika kwa kilimo cha maazo ya biashara kama tumbaku,pamba na katani.
Mwaka 2019 wakati wa maadhimisho ya siku ya chakula duniani yaliyofanyika tarehe16 october 2019 shirika la kilimo la FAO na lile la Chakula WFP kwa pamoja yaliripoti kuwa zaidi ya theluthi moja ya chakula hupotea kila mwaka. (SOFA 2019). Ripoti hiyo iliendelea kufafanua kuwa upotevu huo mkubwa husababishwa na usimamiaji mbovu wa chakula kuanzia shambani kwa mkulima na ukosefu wa zana za kuhifadhia chakula hupelekea sehemu kubwa ya mazao kuharibikia mashambani. Aidha miundombinu duni katika njia za mashambani hasa katika bara la afrika huathiri usafirishaji wa mazao kutoka mashambani mpaka kwenye maghala.
Bila ya shaka hali hii ya kushangaza inatokea leo katika dunia ya sayansi na teknolojia iliyosheheni utajiri mkubwa wa zana za kilimo mifumo thabiti ya kuhifadhi chakula nk. Yote haya yanatokea kwa sababu ya usimamizi mbovu wa nidhamu ya kibepari ambayo hupima matendo yake kwa maslahi.
Kipimo hiki cha kimaslahi ndio kimepelekea tatizo kubwa la upatikanaji wa chakula sio tu Madagascar bali sehemu kubwa katika ulimwengu.Mfumo huu huwekeza kidogo katika kilimo hasa katika mazao ya chakula na huwekeza sana katika mazao ya biashara kwa kuwa huhusisha matajiri wakubwa wenye viwanda vikubwa vinavyohitaji malighafi zao. Kutokana na hali hiyo na sera mbovu za ardhi chini ya ubepari na usimamizi duni wa chakula imepelekea takribani watu zaidi ya milioni 800 kukosa chakula na kusababisha vifo vingi vya watoto vinavyosababishwa na utapia mlo.
Katika upande wa Uislamu katika kuchunga hali za watu hulazimu usimamizi madhubuti kwa kuhakikisha kuwa kila mtu anapata na anawezeshwa kupata mahitajio yake ya msingi kama chakula, mavazi na makazi.
Serikali ya Kiislamu huweka sera nzuri katika kilimo kama vile kuzuia kukodisha ardhi kwa ajili ya ukulima, amesema Mtume SAAW:
“Yule ambaye yuko na ardhi basi ailime au ampe ndugu yake”, kuhimiza kuhuisha ardhi iliyokufa, kukataza kubinafsisha mito na maziwa ili kusahilisha umwagiliaji kwa watu wote nk.
Pia, serikali huweka akiba ya chakula ikibidi kuagiza chakula kwengineko kinakopatikana kama alivyoagiza chakula Khalifah Umar ra. kutoka Masri pindi Madina ilipopatwa na ukame.
Aidha serikali huchukua hatua za makusudi katika kusimamia usalama wa chakula kwa watu wake kwa kuwawezesha wakulima kuwa na mipango thabiti hasa wakati wa ukame kwa kuweka mabwawa makubwa kama alivyofanya Nurddin Zink huko Masri zama za utawala wake.
Ust. Issa Nassib
Risala ya Wiki No. 96
30 Rabi’ al-thani 1442 Hijri 15/12/2020 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

 

Maoni hayajaruhusiwa.