Kuangazia Fikra Batil Ya ‘Haki Za Binadamu’

بسم الله الرحمن الرحيم

Tarehe 10 Disemba ya kila mwaka imetangazwa kimataifa kuwa ndio siku ya ‘Haki za Binaadamu. Ndio siku ambayo ndani ya mwaka 1948 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipolibeba rasmi kivitendo (tabanni) ‘Tamko la Kilimwengu la Haki za binadamu’ (Universal Declaration of Human Rights ).
Fikra hii ya ‘Haki za binadamu’ ni fikra hatari ambayo kwa bahati mbaya huwaghilibu wengi, kiasi cha baadhi kuhisi ni kauli nzuri, tamko lililojaa ukombozi na faraja kwa binaadamu bila ya kuhoji asili, maana ya istilahi hii, chimbuko na kutoka kwa mfumo gani.
Chimbuko, ufahamu na asili ya fikra hii imefafanuliwa vya kutosha kwa kina katika kitabu chetu (Hizb ut-Tahrir) kinachoitwa “Kampeni ya Marekani Kuangamiza Uislamu”.
Tunasisitiza sana kila Muislamu na wanafikra jumla kusoma kitabu hicho.
Kwa faida ya wasomaji wetu tunaweka mada hiyo kama ilivyo ndani ya kitabu hicho.

Haki Za Binadamu

Mwito wa tatu ambao Marekani na wamagharibi wanaulingania na kufanya bidii ya kuwalazimisha Waislamu kuubeba ni “haki za binadamu”. Waislamu wengi wamevutiwa na mwito huu kwa sababu ya ukandamizaji, mateso na uonevu wanayoyapata kutoka kwa watawala wao.
Asili ya haki hizi ni ule mtazamo wa mfumo wa ubepari juu ya maumbile ya mwadamu, mahusiano yake yeye na jamii, mtazamo wao juu ya jamii, na jukumu la serikali.
Katika mtazamo wa mfumo huu juu ya hali ya mwanadamu, mfumo huu unamtazama mwanadamu kimaumbile kama ni mwema na wala si mbaya, kwa hivyo uovu wowote unaotendwa na mwanadamu hutokana na kuzuiwa kwake kutekeleza matakwa yake. Kwasababu hii warasilimali wanalingania kuachwa huru kwa matakwa ya binadamu ili aweze kudhihirisha wema wake wa kimaumbile. Kutokana na mtazamo huu, wazo la “uhuru” likazalika na kuwa fahamu muhimu kwa mujibu mfumo wa kibepari.
Mabepari wanadai kuwa mahusiano baina ya mtu binafsi na jamii hayaambatani. Kwa hivyo, ni lazima kulindwa mtu binafsi kutokana na jamii pamoja na kudhamini na kuhifadhiwa kwa uhuru wake. Hii ni kinyume na hali ilivyokuwa zama za nidhamu ya ‘ubwenyenye wa mashamba’ (feudal system), ambapo maslahi ya jamii yalipewa kipaumbele zaidi juu ya maslahi ya mtu binafsi, ilhali warasilimali hutoa kipaumbele maslahi ya mtu binafsi kiasi cha kusema kwamba jukumu kuu la serikali ni kuhifadhi na kuhakikisha maslahi haya.
Amma kuhusu mtazamo wao wa mujtamaa [jamii], wanasema kwamba mujtama ni mjumuiko wa watu binafsi tu wanaoishi ndani yake. Kwa hivyo, endapo yatadhaminiwa maslahi ya mtu binafsi, basi maslahi ya mujtamaa jumla moja kwa moja yatadhaminiwa .
Bali kwa ukweli yote wanayodai warasilimali kuhusu mwanadamu na maumbile yake, maingiliano baina ya mtu binafsi na jamii, uhakika wa mujtamaa, na jukumu la serikali, si sahihi (bali ni makosa).
Mwanadamu kiuhakika hakuzaliwa na sifa ya wema kama wanavyodai warasilimali, wala sifa ya ubaya kama linavyodai kanisa likifuata falsafa za kizamani zilizojengwa juu ya ufahamu kuwa mwanadamu karithi dhambi ya asili ya Adam.
Mtazamo sahihi kuhusu maumbile ya mwanadamu ni kwamba yeye ana ghariza [hisia za kimaumbile] na mahitaji ya kibaologia [organic needs] ambayo yanataka yashibishwe. Kutokana na akili aliyopewa na Allah (SWT), amepewa pia uwezo wa kuchagua njia ambayo atashibisha ghariza zake na mahitajio yake ya kibaologia. Ikiwa atashibisha mahitajio hayo kwa njia ya sawa, atakuwa amefanya ‘uzuri’; lakini lau atashibisha mahitajio hayo kimakosa amma kinyume na maumbile, atakuwa amefanya ‘uovu’. Kwa hivyo mwanadamu kimaumbile ameandaliwa kuwa tayari kufanya uzuri amma ubaya, na yeye ndiye mwenye kuchagua zuri amma baya kwa khiyari yake. Huu ndio mtazamo ambao Uislamu unabeba na ambao Allah (SWT) anaeleza kwa maneno Yake:
{ونفس وما سواها. فألهمها فجورها وتقواها }
“Naapa kwa nafsi (roho) na Yule aliyeitengeneza. Kisha (Yeye) akaifahamisha uovu wake na wema wake” [TMQ 91:7-8]
{ وَهَدَيْنَاهُ النَّجْدَيْنِ }
“Na Tukambainishia zote njia mbili – (iliyo njema na iliyo mbaya)” [TMQ 90:10]
{ إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا }
“Hakika Sisi tumemuongoa (Tumembainishia) njia (zote mbili hizi; kuwa ndiyo ya kheri na hii ndiyo ya shari). Basi imma atakuwa mwenye shukurani au atakuwa mwenye kukufuru (kukanusha)”
[TMQ Al-Insaan:3]
Pia, kusema kuwa maingiliano baina ya mtu binafsi na jamii ni maingiliano yasioambatana na ni yenye kugongana ni usemi wa kimakosa, sawa sawa imesemwa na mabepari wanaoonelea kutangulizwa maslahi ya mtu binafsi mbele ya jamii, au uwe ni usemi wa zama ya ‘ubwanyenye wa mashamba’ uliolingania kutangulizwa (dhawbaan) maslahi ya mtu binafsi kabla ya mjumuiko (jamii); au kama ilivyoonelewa na wana-ujamaa wa ki-Marxi waliodharau mtu binafsi kiasi cha kumfanya sio chochote zaidi ya spoki katika gurudumu la jamii.
Amma maingiliano sahihi yalivyopangwa na Uislamu, haya ni maingiliano ya kudumu na ya kutoshelezana, na wala sio maingiliano ya kugongana. Mtu binafsi ni sehemu katika jamii kama ulivyo mkono kuwa sehemu ya mwili wa mwanadamu. Vile vile mwili haujitoshelezi bila mkono, kadhalika mkono hauna thamani ukitenganishwa na mwili.
Uislamu umempa mtu binafsi haki kama ilivyoipa jamii haki, wala haki hizi si zile zisizoambatana wala zenye kugongana, bali ni zenye kukamilishiana. Kadhalika Uislamu umewapangia kila mmoja majukumu maalumu na kuitwisha serikali jukumu la kuhifadhi mizani juu ya kila mmojawapo (mtu binafsi na jamii) kwa mwenzake kiasi kwamba mmojawapo asivuke mipaka ya mwenzake.
Kila mmoja lazima apate haki zake na kutekeleza majukumu yake. Mtume (SWT) ameeleza haya kwa ufasaha kabisa kuhusu mangiliano haya baina ya mtu binafsi na jamii kwa kusema:
« مثل القائم على حُدود الله والواقع فيها كمثل قوم اسْتَهَموا على سفينة فأصابَ بعضَهُم أَعْلاها وبعضُهُم أسفلها، فكان الذين في أسفلِها إذا اسْتَقوا من الماء مَرّوا على مَن فوقهم، فقالوا: لو أنّـا خَرَقْنا في نصيبِنا خَرْقاً ولم نُؤْذ مَن فَوْقَنا، فإنْ يتركوهم وما أرادوا هَلَكوا جميعاً، وإنْ أخَذوا على أيديهم نَجوا ونَجَوْا جميعاً »
“Mfano wa yule anayechunga mipaka ya Allah na yule anayekengeuka ndani yake ni kama watu waliopanda jahazi wakawa baadhi yao wako juu yake, na baadhi yao wako chini yake. Wakawa wale walio chini yake wakiwa na kiu ya maji hupata kwa wale wa juu yao. Wakasema(waliochini): ‘Lau kama sisi tutatoboa tundu katika sehemu yetu ili tusiwaudhi wa juu yetu.’ (Walio juu) Wakiwawacha (walio chini) (kutenda) wanalotaka wataangamia wote pamoja, na wakiwazuia wataokoka na kuokoka wote pamoja’.”
Amma kauli ya Mabepari kuwa mujtamaa/jamii si chochote isipokuwa ni mjumuiko wa watu binafsi ambao wanaishi ndani yake, kwa namna yoyote sio sawa. Mujtamaa sio tu mkusanyiko wa watu binafsi, bali unakusanya watu binafsi, fikra na hisia zinazowatawala pamoja na mfumo ambao umesimamishwa juu yao; yaani mujtamaa ni kikundi cha watu binafsi wanaoshirikiana katika maingiliano ya kidaima. Abiria katika jahazi amma gari moshi sio mujtamaa, hata kama idadi yao itafika kuwa ni maelfu, ilhali wanaoishi katika kijiji kidogo ni mujtamaa hata kama idadi yao haizidi mia kadhaa.
Kwa hayo mtazamo wa mfumo wa kirasilimali juu ya mujtamaa, pamoja na ufahamu wake juu ya maumbile ya mwanadamu na maingiliano baina ya mtu binafsi na jamii, ni mtazamo wa kimakosa. Amma ufahamu wake juu ya wajibu wa serikali, makosa yake yako wazi kabisa. Serikali sio tu ni chombo cha kuhifadhi na kuhakikisha maslahi ya mtu binafsi, bali ni chombo ambacho kinatizama na kuangalia mambo ya mtu binafsi, jamii na mujtamaa kwa namna zote; ndani na nje kulingana na mfumo maalumu ambao unadhamini haki na majukumu ya wote; pamoja na kubeba ujumbe wake kwa ulimwengu mzima ikiwa umejengwa juu ya mfumo ambao unawalingania wanadamu kwa sifa yao ya ubinadamu pasina kujali sifa nyengine yoyote ile.
Kwa ufupi, mtazamo wa mfumo wa kirasilimali juu ya maumbile ya mwanadamu, maingiliano ya mtu binafsi na jamii anayotokana nayo na mujtamaa anaoishi, na jukumu la serikali ni katika kuhifadhi na kuhakikisha maslahi ya mtu binafsi; ndio ikasukuma mfumo huo kulingania na kudhamini uhuru wa aina nne kwa mtu binafsi: Uhuru wa kuabudu, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kumiliki na uhuru wa kibinafsi.
Aina hizi za uhuru ndizo msingi uliochipuka kwa “haki za binadamu”, na ndizo chanzo cha balaa katika mujtamaa wa kirasilimali ambazo zimesababisha jamii hizo kugeuka kuwa mbuga za wanyamapori ambapo wenye nguvu wanawamaliza wanyonge na mwanadamu kudidimia daraja yake kuwa kama mnyama, kwa sababu ya kuziachilia huru ghariza na mahitaji yake ya kibaologia.
Watu katika jamii za kimagharibi wanafanana na wanyama kwa kujishughulisha na kiasi kikubwa zaidi cha starehe za kimwili, jambo linalochukuliwa na mujtamaa wa kimagharibi kama ndio lengo lao japokuwa, kinyume na hayo, mujtamaa/jamii hizi hazijui hata ladha ya furaha. Bali zimezidiwa na hali ngumu, fujo na tafrani isiyokwisha.

 

Maoni hayajaruhusiwa.