Mwaka Mpya na Tukio la Hijra
Wakati tukiwa tunaanza mwaka mpya wa Kiislamu wa 1440 Hijria, lazima tukumbuke kwamba kalenda ya Kiislamu iliasisiwa rasmi wakati wa Khilafah ya Umar bin Khatab katika mwaka wa 16AH. Baada ya mashauriano na makubaliano na masahaba wakubwa (ijmaa), wakakubaliana tukio kubwa la ‘Hijra’ ndio liwe nukta kianzio ya kuihesabu kalenda hiyo.
Uchaguzi wa tukio la ‘Hijra’ulifikiwa kwa msimamo mmoja licha ya kuwepo matukio mengine makubwa katika tareekh ya kiislamu kama vile Uzawa wa Mtume SAAW, kupewa Utume, safari ya Israi na Miiraj, kufariki kwake nk. Yote hayo yaliachwa si kwa kuwa si muhimu, lakini lilichukuliwa tukio tukufu la ‘Hijra’ kwa kuwa ndilo lililochora mstari muhimu wa maisha ya Waislamu kuishi chini ya utawala wa kikafiri ndani ya Makkah na kuanza maisha mapya ya kutawaliwa na dola yao tukufu ya mwanzo ya kiislamu ndani ya Madina. Hili ni tukio la safari aliyoifanya Mtume (S.A.A.W) kutoka Makka kuelekea Madina akiwa tayari ametawazwa kuwa kiongozi rasmi wa dola ya mwanzo ya Kiislamu.
Kuielewa kwa dhati ‘Hijra’ hatuna budi kwanza kuelewa kwa kina mazingira ya ulinganizi wa Mtume SAAW yaliyopelekea kutokea kwa tukio hili kubwa. Daawa ya Kiislamu katika mwaka wa tatu wa Utume ilitoka katika hatua ya maandalizi ya kukiandaa chama cha Mtume SAAW kwa siri ili kiweze kutoa wabebaji wazuri wa daawa na kuingia katika awamu ya wazi hadharani kwa mapambano ya wazi ya kifikra na kisiasa dhidi ya ukafiri, kufuatia agizo la Allah Ta’ala:
‘Basi yatangaze uliyoamrishwa na jitenge na washirikina’.
(TMQ 15: 94)
Katika hali kama hiyo ulinganizi wa Kiislamu sasa uliingia hatua nyingine na ulilenga moja kwa moja kuanzisha migongano ya kifikra baina ya Uislamu na Ukafiri. Ukafiri uliokuwa ukishikiliwa kwa nguvu zote na makureishi na mabwanyenye wa Makka, na Uislamu uliokuwa bado na wafuasi wachache.
Hatua hii ilikuwa tofauti na ile hatua ya awali katika nyumba ya Arqam, hatua iliyokuwa siri na kulenga maandalizi ya chama cha Mtume (SAAW) tu, bali hatua ya sasa ililenga kufedhehi na kuweka wazi kwa kubomoa fikra za kikafiri katika upande wa siasa kama vile kuwaumbua (character assassination) viongozi wa kiqureish kama ilivyofanywa kwa Abu Lahab , Abu Jahl, Walid bin Mughira na wengineo. Kuonesha uovu wa uchumi wao kama ilivyokosolewa dhulma yao kwenye vipimo na kujirundikia mali, pia kuonesha ufasiki katika sera zao za kijamii kama kudhulumu mayatima, kuwauwa watoto wa kike bila ya hatia, kuwabeza masikini n.k.
Kadhalika hatua hii ilikusudia kuondosha kabisa haiba na kuvunja moyo watu juu ya imani ovu ya ukafiri na kuwataka wauwache ukafiri huo mara moja na badala yake kuonesha ubora na utukufu wa Uislamu ili kuwataka watu waufuate haraka iwezekanavyo.
Katika awamu hii, licha ya kuwataka watu waingie katika Uislamu pia ilikuwa ni kipindi cha kujenga mtazamo jumla (Public opinion) uwe upande wa Uislamu, hata kama hawatosilimu watu wote wa Makka, lakini walau wautizame Uislamu kwa wema (positive).
Ikumbukwe pia kipindi hiki ndipo ilipoanza kampeni kali na ovu ya vitisho, mateso na mauwaji dhidi ya Waislamu iliyokuwa ikiendeshwa kwa jeuri na kibri kutoka kwa makafiri wa Makka kutokana na kuumbuliwa fikra na matendo yao ya kikafiri. Ilipofika mwaka wa kumi wa Utume, hatua ya mgongano wa kifikra iliambatana na ajenda ya ziada ya utafutaji wa ‘Nusra’ambayo ilikuwa ni amri kutoka kwa Allah Taala. (Bidaya wan Nihayah Vol.3).
Utafutaji wa ‘Nusra’ ni kitendo kinachofanywa kukusudiwa kwa watu wenye nguvu na athari na kwa wakati ule kutoka makabila yenye nguvu, kuwaomba na kuwataka wahamishe hatamu za mamlaka na madaraka yao ya kisiasa na ya kijeshi kwa kupitia kiapo maalum (ba’aya) ili kwa wakati ule kumpatia Mtume SAAW kumuwezesha kusimamisha dola ya Kiislamu.
Hii ni kwa sababu ujumbe wa Uislamu daima hulenga kuwa na mamlaka kamili ya dola, ili uweze kutekelezeka kiukamilifu ukiwa mfumo kamili wa maisha. Ni muhimu ieleweke kwa kina na kwa upana malengo ya ‘Nusra’, kwamba: sio tu kunusuru maisha ya Mtume SAAW pekee. Kwa sababu kama lengo lingekuwa hilo tu, angekwishahama awali na masahaba wake kuelekea Uhabeshi, na pia alikwishadhaminiwa mapema usalama wake ndani ya Makka tangu aliporudi Twaif kwa dhamana na bwana Mutim bin Adiy. Lakini dhamira ilikuwa zaidi ya hayo, nayo ni kunusuru maisha yake na pia kupata nguvu na mamlaka kamili ya madaraka ya kuwa na dola, si kwa lengo la uchu wa madaraka bali kupata mamlaka ya kuutekeleza Uislamu kivitendo kwa ukamilifu wake.
Awali Mtume SAAW aliwakabili jamaa zake maqureish kwa lengo hilo, na walielewa kwa upana wake ajenda hii. Alipowataka waushike Uislamu ili waweze kuwatawala waarabu na wasiokuwa waarabu. Katika moja ya matukio ya kuwafikishia ajenda hii, mmoja kati ya viongozi wakubwa wa maqureishi, Bwana Utbah ibn Rabiah baadae alikwenda kuwaeleza watu wake:
“Enyi watu wangu bora mwacheni kijana huyu! Ikiwa waarabu watammaliza hamtakuwa mashakani, lakini akifanikiwa na kupata ushindi, mamlaka yake yatakuwa kwenu na mtakuwa watu bora kabisa”
Baada ya maqureish kumkatalia katakata kumpa nusra yao, ilimlazimu Mtume (S.AA.W) kuyakabili makabila mengine ya kiarabu nje ya Makka, ama kuyafuata katika maeneo yao kama alivyofanya kwa Bani Thaqif au kuwafuata katika mahema yao siku za Hijja.
Katika mchakato huu wa kutafuta ‘Nusra’ S.AAW alikuwa akiyakabili makabila makubwa tu, akiyasilimisha , akifuatilia kujua idadi yao, kutafiti nguvu zao za kijeshi, kujiridhisha na mbinu zao za kivita na kujua idadi ya vita walivyopigana, kama lilivyoulizwa kabila la Bani Bakr bin Wayl na Bani Shayban kwa kupitia Mafruq (kiongozi wao). Sayyidna Abubakar (R.A) alikuwa wakati mwengine akijumuika na Mtume(S.AAW) katika mchakato huu kwa kuwa alikuwa ‘bingwa’ wa kuyajua makabila mbali mbali.
Kwa hivyo, mawasiliano ya moja kwa moja na viongozi wa makabila yalikuwa yakiasisiwa huku wakidadisiwa ili kupata picha halisi ya nguvu ya kabila husika. Hii ni kwa sababu suala la ‘Nusra’,sharia imelifunga itolewe na watu wenye nguvu tu, na ndio maana (S.AAW) kwa upande wa makabila madogo madogo aliyasilimisha tu bila ya kuwaomba ‘Nusra’ kutoka kwao.
Katika ajenda hii ya ‘Nusra’ Mtume SAAW aliyafuata zaidi ya makabila 40. Makabila maarufu zaidi ni Bani Thaqif waliomkatalia kwa kibri na jeuri na kumpiga mawe ndani ya Twaif, kabila la Amr bin Sasa waliomkubalia kwa sharti akifa Mtume SAAW, utawala ubakie kwenye kabila lao. Pale alipojibu Kiongozi wao Buhairah bin Firras kwa kumweleza Mtume SAAW kwa kusema:
‘Jee tukikupa kiapo na Allah akakupa utawala dhidi ya wapinzani wako utatupa sisi haki ya kurithi utawala baada yako?
Pia wakamueleza zaidi Mtume SAAW kwa kusema kwa kebehi:
‘Tuinamishe shingo zetu kwa panga za waarabu na mara ushindi ukipatikana utawala wende kwa wengine’?
(Ibn Hisham)
Baada ya kabila hili kurudi kwao, mmoja katika wazee (shaykh) wa kabila hili ambaye hakuweza kuja Hijja mwaka ule, aliposimuliwa juu ya mazungumzo (negotiation) baina ya kabila lao na Mtume SAAW, alilaumu vikali uamuzi wa kabila lake na kuwataka wabadilishe msimamo, kwa kuwa wameshaitupa fursa adhimu. (Ibn Hisham,Imam Tabari Vol.6 , Bidaya wan Nihayah Vol.3 p.139)
Katika mchakato huu wa kutaka nusra, kabila la Bani Hanifah walimjibu Mtume SAAW maneno ya kifedhuli na kumkatalia kwa uadui kuliko kabila lolote kama inavyosimuliwa na Kaab bin Malik. Ama kabila la Bani Kinda, kwa mujibu wa mapokezi ya Ibn Shihab al Zuhri , baada ya Mtume SAAW kumkabili kiongozi wa kabila hilo bwana Mulayh nae pia alikataa kata kata kwa niaba ya kabila lake. Kabila la Shaiban bin Thaalabah wao walionesha kuwa tayari kutoa ‘Nusra’ yao kwa sharti la kulindwa mkataba wao wa amani unaowataka kabila hilo kujizuia kuwavamia Mafursi. Kadhalika Bani Bakr bin Wayl, jibu lao kwa Mtume lilikuwa kwamba wanaishi karibu na dola ya Mafursi na hawaruhusiwi na dola hiyo kuingia mkataba utakaoathiri maslahi ya dola hiyo.
Mtume SAAW aliyakataa kata kata masharti yote aliyopewa na makabila hayo. Masharti ambayo kwa udhati wake yanapingana moja kwa moja na Uislamu. Alisimama msimamo huo licha ya kuwa alikuwa muhitaji wa hiyo Nusra, lakini hakuweza kukhalifu hata punje ndogo ya Uislamu. Badala yake alisimama kidete katika jambo hili kwa msimamo mmoja tu kwa makabila yote juu ya kauli mbiu hii:
‘Ya kwamba mniamini, kunisadiki na kunilinda mpaka niweze kubainisha yale aliyonituma nayo Allah.’
Katika mwaka wa 12 wa Utume, baada ya watu wa Madina kufunga kiapo cha mwanzo (Baayatu Nissai) na Mtume SAAW, na kuukubali Uislamu kwa udhati, na kuwa tayari kutowa nusra yao kwa Uislamu. Mtume SAAW alimtuma Swahaba wake maarufu Musab bin Umair ndani ya Madina kukamilisha kazi maalum. Kwanza, alimtaka kuwafundisha Uislamu Waislamu wapya ndani ya Madina. Pili, kusilimisha wapya.Tatu, kuandaa mtazamo jumla (public opinion) wa jamii ya Madina kuupokea Uislamu kwa wema hata kama hawatosilimu watu wote. Na nne, kuwaandaa viongozi wakuu wa makabila (manuqabaa) ya Madina waje Makka kutoa Nusra yao kwa Mtume (S.AAW) ili Mtume SAAW awe kiongozi rasmi wa dola ya mwanzo ya Kiislamu. Musab RA aliyatekeleza hayo yote chini ya usimamizi thabiti na mawasiliano ya mara kwa mara na Mtume SAAW kwa kipindi chote cha mwaka mzima alichokuwa ndani ya Madina. Viongozi hao aliowahitajia SAAW walikuwa wa makabila mawili makubwa ya Aus na Khazraj.
Katika mwaka wa 13 wa Utume, viongozi wa makabila ya Madina walifunga safari kuja Makka kwa ajili ya Hijja na kutoa ‘nusra’ yao rasmi kwa Uislamu. Mtume S.AA.W akaahidiana kukutana nao usiku wa manane ndani ya siku za tashreeq katika vilima vya Aqaba ili kuzungumzia ajenda nyeti ya utoaji ‘nusra.’
Ilikuwa ajenda nyeti sana kiasi kwamba ilifanywa kuwa siri ya hali ya juu ambapo Mtume S.A.A.W alimuru yoyote aliyelala asiamshwe na asiyekuwepo asihudhurishwe. Mtume SAAW alijumuika katika usiku huo na Ami yake Abass RA. katika kikao cha majadiliano hayo mazito.
Baada ya majadiliano marefu na kwa upana yaliyowashirikisha maanswaar 73 akiwemo Bibi Nusaybah bint Kaab na Bibi Asma bint Amr wakafikia muwafaka kwa watu wa Madina kutoa Nusra yao kwa Mtume SAAW bila ya masharti yoyote na wakamtawaza rasmi Mtume S.A.AW kuwa kiongozi ndani ya Madina. Na kwa hivyo wakampa baiya (kiapo cha utii) chenye ahadi ya kumlinda na kumnusuru kwa hali yoyote. Kiapo ambacho katika tareekh ya Kiislamu kimepewa daraja ya kuitwa kiapo cha vita (Baayatul-harb) kutokana na masharti ya kivita waliyokubaliana (terms) dhidi ya yoyote atakayekusudia kumdhuru Mtume SAAW.
Imesimuliwa na Ka’b bin Malik Al-Answar:
‘Al-Bara bin Ma’aroor (Answar) akachukua mkono wa Mtume SAAW kisha akasema: Naam naapa kwa Yule ambae amekutuma kwa haki (kuwa Mtume) kwamba tutakulinda kama tunavyolinda wakaribu wetu.Basi ikubali ba’aya yetu ewe Mtume wa Allah, kwani sisi Wallah ni watoto (wazoefu) wa vita na watu wa kupigana kwa mzunguuko.’
Baada ya kiapo hicho Mtume SAAW akaamuru baadhi ya Masahaba zake waanze kuelekea Madina huku yeye akisubiri amri ya Allah Taala lini aondoke Makka kuelekea Madina.
Makafiri wa kiqureishi ndani ya Makka katika kutapatapa kwao, walipopata taarifa ya mazungumzo baina ya Answar na Mtume SAAW na kuona kuhama kwa masahaba, wakaelewa kwamba tayari Mtume SAAW ameshapewa ‘nusra’ na baadae ataitumia nusra hiyo kuja kuwamaliza. Hivyo wakandaa mkakati kabambe wa kiuadui kumuuwa Mtume SAAW. Lakini Allah Taala akamnusuru. Mnamo ndani ya mwezi wa Safar 27 Mtume S.AAW alitoka kisiri siri na Abubakar RA kuondoka Makka kuelekea Madina. Huku Mtume SAW akimuamuru Ali R.A alale kitandani pake badala yake.
Katika safari hii ya Hijra, miujiza kadhaa ilitokea. Kama vile kuzibwa macho maqureishi waliokusudia kumuuwa SAAW, mabuibui waliojenga katika pango waliyojifichia Mtume SAAW na Abubakar ra, kupitia mikono ya SAAW kutoa maziwa kwa mbuzi dhaifu wa Ummu Maabad, kuzama kwenye mchanga kwa ngamia wa Suraqa bin Malik aliyetumwa na maqureish kumuuwa Mtume SAAW nk. Yote hayo huingia katika upande wa aqeeda na hatuna budi kuyakiri na kuyaamini. Pia kunapatikana vitendo vilivyotendwa katika mzunguko wa kibinaadamu, kama vile kubabaishwa makafiri mwelekeo wa safari, kukodiwa mjuzi wa njia, kujificha kwenye pango siku tatu pia kuwatumia watoto wa Abubakar na mtumwa wake kuleta chakula pangoni, kufuta nyayo za ngamia na kuleta taarifa ya hali inavyoendelea ndani ya Makka. Haya yote hungia katika vitendo vya hukmu ya kisheria ambavyo lazima tuchukuwe mafunzo ya kivitendo.
Mtume (S.AA.W) aliwasili Madina mwezi wa Rabil Awwal mwaka wa mwanzo Hijria. Akapokewa kwa vifijo, nderemo na hoi hoi, kwa kuwa hakuwa mkimbizi kama wengine wanavyodai. Bali alikuwa kiongozi aliyekuwa akisubiriwa kuwasiIi. Akaasisi dola ya mwanzo ya Kiislamu iliyodumu karne zote chini ya Makhalifa baada yake.
Kwa masikitiko makubwa makafiri kwa uadui walidiriki kuiangusha dola ya mwisho ya Kiislamu ya Khilafah Uthmania ndani ya Uturuki. Tukio lililotokea katika mwaka 1924 kutokana na kuanguka kifikra kwa Waislamu na kwa msaada wa vibaraka wa kiarabu na kituruki. Leo tuna wajibu juu ya shingo zetu kuirejesha tena Khilafah ili ije isimamie dini na dunia yetu.
Masoud Msellem
Maoni hayajaruhusiwa.