Vikwazo Katika Ulinganizi Na Namna Ya Kuvitatua

بسم الله الرحمن الرحيم

Anasema Allah(SWT) katika kitabu chake kitukufu Al Quran;

وَأَنفِقُوا۟ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ وَلَا تُلْقُوا۟ بِأَيْدِيكُمْ إِلَى ٱلتَّهْلُكَةِ ۛ وَأَحْسِنُوٓا۟ ۛ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلْمُحْسِنِينَ

“Na tumieni Mali yenu katika Njia ya Allah na wala musijitie kwa mikono yenu katika maangamizi, na mudumu katika kutenda wema kwani Allah Anawapenda watendao wema” (TMQ 2:195)

 

Swahaba mkubwa Abu Ayyub Al- Answari(RA) anasimulia kuwa; “ayah hii iliteremshwa kwa ajili yetu (Maswahaba) pale Allah Taala alipoupa nguvu Uislam na ushindi, tukaaanza kuzungumza baina yetu kwamba hapana haja tena ya kushughulika na jihad na badala yake tushughulike kukuza mali na familia zetu” (Tafsiri ya ibn Kathir).

 

Kuendelea kwa daawah(ulinganizi) wa Uislamu katika jamii zetu hutegemea vitu viwili vikuu, ambavyo ni Rai Amma (kukua na kukubalika kwa daawah katika jamii) na pili kuongezeka kwa walinganizi miongoni mwa Waislamu katika kulingania Uislamu wao.Vitu hivi ni viashiria muhimu vya uhai wa ulinganizi wa Uislamu na kipimo cha kufaulu kwake.

 

Tathmini ya haraka inaonyesha ujumbe wa Uislamu umesikika maeneo mengi na watu wengi wanaendelea kuingia katika dini hii na kuwa ndiyo dini inayokua kwa kasi zaidi ulimwenguni leo hii. Kwahiyo kwa upande mmoja Rai Amma Uislamu umefikia watu wengi hivyo yatupasa kama Waislamu kuendeleza ulinganizi wa dini yetu na kuzuia kushuka kwa ulinganizi huo.

 

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kupelekea kushuka kwa ulinganizi wa Uislamu katika ummah. Baadhi ya sababu hizo ni kama vile kutokuweka kipaumbele katika ulinganizi miongoni mwa walinganizi na ummah kiujumla. Iwapo utafutaji wa riziki utakutufanya Waislamu tushindwe kufanya ulinganizi wa dini yetu basi hili litapelekea kuzorota kwa ulinganizi wa Uislamu. Hivyo ni lazima tuwe makini katika hili.

 

Amma jambo lingine ni upungufu wa elimu na maalumat. Kama elimu na maalumat yatakosekana miongoni mwa walinganizi katika kile wanacholingania katika Uislamu basi itafanya katika ulinganizi wa Uislamu na kusimamisha hoja. Kwahiyo ni jukumu la kila mlinganizi kujiongeza katika elimu na maalumat ili aweze kulingania kwa hoja madhubuti mfumo huu wa Uislamu

 

Kwahiyo, hakuna budi kwa Waislamu na hasa wale wanaofanya ulinganizi, kuongeza juhudi katika ulinganizi na kuzalisha walinganizi wapya ili ujumbe wa Uislamu uwafikie watu wote ulimwenguni, waukubali, kuuitikia, na kuufanya usimamie maisha yao yote. Pia ni muhimu sana kwa Waislamu kujifunza kuhusu dini yao ili waweze kusimamisha hoja nzito katika ulinganizi na hivyo kuwaingiza watu wengi zaidi katika Uislamu na kuongeza walinganizi zaidi.

 

Kihakika kilichopo katika maumbile ni kwamba tone la maji likianguka kwenye mwamba kwa kudumu husababisha shimo kwenye mwamba au kusababisha kupasuka kwake! Sisi Waislamu tukizidisha daawah kwa jamii, basi daawah ya Kiislamu kwa nguvu zake itazidi nguvu ya sururu. Daawah ikibebwa kwa elimu(ufahamu wa ndani), ukweli na maazimio na kwa kukariri na kubisha mlango wa mujtama kwa kudumu basi mlango utafunguliwa na jamii itakubali ulinganizi wa Uislamu na kukubali Uislamu

 

Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Mtume(SAW), aliufungua mji wa Madina kwenye kisiwa cha Uarabuni kilichotawaliwa na ujinga, mji ulikuwa mgumu zaidi kuliko jabali, lakini daawah yake pia ilikuwa na nguvu kuliko nyundo na sisi tunajua kuwa daawah yetu(ulinganizi wa Uislamu) haijui lisilowezekana.

 

Risala ya Wiki No. 149

21 Jumada al-awwal 1444 Hijria / 15 Desemba 2022 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.