Tunachojifunza Kutokana Na Khilafah Ya Bani Ummayyah

بسم الله الرحمن الرحيم

Tarehe 17 Rabiul-Thani 132H ilianguka Khilafah ya Bani Ummayah, Khilafah iliyotawala ulimwengu kwa takribani miaka 91, yaani kuanzia mwaka 41H (661M)mpaka mwaka 132H(750M). Utawala wa Bani Ummayah ulianza kwa Muawiya Ibn Abu Sufiani, maarufu kama Muawiya(I) na kumalizikia kwa Marwan ibn Muhammad ibn Marwan maarufu kama Marwan(ii) ikiwa na jumla ya makhalifah 14.

 

Imeitwa Khilafah ya Bani Ummayah kwa sababu Makhalifah wake wanatokana na ukoo wa Kiqureshi wa Bani Ummayah ambao unatokana na Umayya ibn Abd Shams ambaye ni baba yake na Abu Sufiani Swaghir Ibn Harb na babu yake na Muawiyah-Muawiyah Ibn Abu Sufiani. Makao makuu ya dola hii yalikuwa Sham (Damascus/Syria). Kupitia Khilafah hii ya Banu Ummayah, ummah wa Kiislamu unaweza kujifunza mambo mengi kama ifuatavyo:

 

Ummah wa Kiislamu ni lazima uwe na kiongozi mmoja, Khalifah wa Waislamu wote ulimwenguni. Baada ya kumalizikia kwa Khilafah bora (Khilafah Rashidah) iliyodumu kwa miaka 30 kuanzia mwaka 11H mpaka mwaka wa 41H ikiwa na jumla ya makhalifah 4 ambao ni Abuobakr, Umar, Uthman na Ally Allah awaridhie, Banu Ummayah waliendeleza utawala wa Kiislamu ili kutabikisha sheria za Muumba katika ardhi.

 

Kwahiyo masahaba kama ambavyo hawakukubali kuishi bila uongozi wa Kiislamu baada ya kufariki kwa Mtume(SAW) pia hawakukubali kuishi bila ya uongozi wa Kiislamu baada ya Khilafah bora kwani bila uongozi hakuna utabikishwaji wa hukmu na sheria za Kiislamu na kuridhia kutabikisha hukmu zisizokuwa za Kiislamu ni ukafiri wa wazi. Allah (SWT) anasema:

 

 وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلْكَٰفِرُونَ ﴿٤٤

“Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri”

 

Kupitia  Khilafah ya Bani Ummayah tunajifunza kuwa sifa ya serikali ya Kiislamu na mfumo wa Uislamu ni kujitanua kupitia da’awah na jihad. Katika kipindi cha Khilafah bora (Rashidun) eneo la dola ya Kiislamu lilikuwa takriban 6,400,000 km2 lakini chhini ya Banu Ummayah eneo la Khilafah liliongezeka na kufikia takribani 11,100,000 km2.

 

Khilafah ya Bani Ummayah ilitawala Mashariki ya kati, Asia ya magharibi, Asia ya kati ambayo kwa sasa ni nchi za Uzbekistan, Tajikistan, Kazakhstan, Turkmenistan, Afghanistan na Kyrgyzstan, Afrika ya kaskazini na Kaskazini Magharibi, magharibi ya China na baadhi ya sehemu ya Ulaya kama vile Hispania na Ulaya ya Mashariki. Hii ni kutekeleza maarisho ya Mtume (SAW)

 

 عن ابنِ عُمَرَ رضي الله عنهما أنَّ رسُوَل الله صلى الله عليه وسلم قال: ((أُمِرْتُ أَنْ أُقاتِلَ النَّاسَ حتَّى يَشْهَدُوا أنْ لا إلَهَ إلاَّ اللهُ وأنَّ محمداً رسوُل اللهِ، ويُقِيمُوا الصَّلاَةَ، ويُؤتُوا الزَّكاةَ، فإذا فَعَلوا ذَلِكَ عَصَموا منِّي دِماءَهُمْ وأمْوَالَهُمْ إلا بِحَقِّ الإِسْلامِ، وحِسابُهُم على اللهِ تعالى)) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ   وَمُسْلِمٌ  

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (RA) kwamba Mtume(SAW) amesema: “Nimeamrishwa nipigane vita na watu mpaka washahidie kwamba hakuna anayepaswa kuabudiwa kwa haki ila Allaah  na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah.  Watakapofanya hivyo, watakuwa wamepata ulinzi kwangu wa damu zao, na mali zao isipokuwa  kwa haki ya Uislamu, na hesabu yao itakuwa kwa Allaah Ta’aalaa.” (Bukhaariy &Muslim)

 

Khilafah hii pia inatufundisha uadilifu wa hali ya juu wa serikali ya Kiislamu. Katika utawala wa Khalifah wa 6 wa Khilafah ya Bani Ummayah, Al-Walid ibn Abd al-Malik ibn Marwan, maarufu kama Al Walid(I), Waislamu waliingia Asia ya kati katika Samarkand ambayo ni Uzbekistan ya leo, mwaka wa 83H. Kamanda wa jeshi la Waislamu, Qutaybah Ibn Muslim aliwapiga vita vita watu wa Samarkand na kuwatala bila kiwalingania kwanza.

 

Watu wa Samarkand walishtakia suala hili kwa Khalifah na mara baada ya kusikilizwa kesi, ilihukumiwa kuwa Waislamu wamekosea na waondoke Samarkand mara moja. Wakati Waislamu wanaondoka watu wa Samarkand wakawarudisha na kukubali kutawaliwa na Uislamu. Qadhi aliyesimamia kesi hii alikuwa Umar Ibn Abdulaziz, kabla hajawa Khalifah. (Ally Tantawi: Qasas Min Al Tarikh UK 85)

 

Pia tunajifunza kuwa Uislamu si dini ya kiroho pekee bali ni mfumo kamili wa maisha ya binadamu ulio na masuluhisho kamili ya matatizo yote ya binadamu kiitikadi, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Katika kipindi Khilafah ya Bani Ummayah hususani katika utawala wa Khalifah wa 8 aliyetawala kuanzia mwaka wa 99H, Khalifah Umar Ibn Abdulaziz, dola ya Kiislamu ilifanikiwa kuondoa umasikini kwa kiasi kikubwa.

 

Anasimulia  Yahya Ibn Said,aliyekuwa Wali (governor) wa Afrika Kaskazini katika kipindi cha utawala wa Khalifah Umar Ibn Abdul Aziz, anasema: “nilitumwa na Umar Ibn Abdul Aziz kukusanya zakat Afrika. Baada ya kukusanya nilikusudia kuzigawa kwa masikini. Lakini sikupata masikini wa kumpa, Umar Ibn Abdul Aziz alimfanya kila mtu kuwa tajiri katika kipindi cha utawala wake. Mwisho, niliamua kutumia pesa hizo za zakat kununua watumwa na kuwaacha huru” (Ibn Abd Hakam, Abdullah (1994) Al Khilafat Al Adil Umar Ibn AbdulAziz: Khamis Al Khulafah Al Rashidin, Dar Al Fadilat)

 

Hakika ya kujifunza katika Khilafah hii ni mengi lakini muhimu kabisa ni kuwa ilikuwa Khilafah, ilikuwa utawala wa Kiislamu wa kiulimwengu ambao hauna budi isipokuwa kuwepo. Ni wajibu wetu kama Waislamu kufanya kazi kurejesha utawala wa Kiislamu ulimwengu ili hatimaye Uislamu utabikishwe kivitendo kamili kama dini na mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu.

 

Said Bitomwa

Risala ya Wiki No. 148

15 Jumada al-awwal 1444 Hijria / 09 Desemba 2022 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.