Mazazi ya Mtume Saaw Yatukumbushe Malengo ya Dini Yetu

Kumbukumbu za mazazi ya kuzaliwa Mtume wetu mtukufu SAAW yamepamba moto katika mwezi huu wa Rabiul-awwal. Kama zilivyo jamii nyingine za wanaadamu katika kutukuza matukufu yao, imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya Waislamu kuonesha hisia zao kwa kwa kumbu kumbu ya kuzaliwa SAAW. Jambo hilo ni katika viashiria vya mapenzi yao kwake. Kwani kumpenda Mtume SAAW ni katika imani ya Muislamu na ni katika misingi ya kufanikiwa. Allah SW anasema :

قُلْ إِنْ كُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمْ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ (آل عمران: 31
“Sema ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu Atakupendeni na atakafutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mrehemuvu”(TMQ 3:31)

Ndani ya Ummah wa Kiislamu kumekuwepo na namna tofauti za kuyakumbuka mazazi hayo, yakiwemo makongamano yanayoambatana na mada mbalimbali zinazokumbushia baadhi ya sifa za Mtume SAAW akiwa kama Mtume wa Mungu, mwalimu, binamu, mume, kijana, mfanyabiashara, baba wa familia, kiongozi wa Ummah nk. Ni katika mikusanyiko hii ndipo Waislamu wamekuwa wakishajihishana masuala ya Kiislamu kama vile mshikamano, kujikomboa, kujitambua na kujiendeleza.

Hali hii inatuzindua kwamba Ummah bado una hisia ya aqidah yao, una hitajio la kulinda dini yao, kushikamana na muongozo wao na heshima yao japo umepoteza ubwana /izzah yake kilimwengu.

Ujio wa Mtume SAAW ambao ndio mazazi yake, ni ujio wa mabadiliko msingi kwa mwanadamu na Ummah kwa jumla. Mabadiliko yake yaliambatana na kifikra yaliyozaa mtazamo maalumu wa kimaisha. Katika kuuangalia utu, ushirikiano (maingiliano), jukumu la kila mmoja, ulimwengu, uhai, mwaadamu na maisha kwa ujumla.

Mtume SAAW amekuja na mabadiliko sahihi na ya kweli kwa kuonesha ni kipi cha kubadilisha, na ni vipi kibadilishwe, ili badiliko hilo liwe na tija kwa maisha ya viumbe wote wakiwa hai na hata baada ya uhai. Mabadiliko ya namna ya kuyatazama mambo na kuyatathmini kujua ukubwa, uimara na athari zake kwa jamii.

Ujio wa Mtume SAAW ulikuja wakati ambapo jamii iliyokuwepo imepoteza kabisa sifa za ubinadamu, kama hali ilivyo sasa, jamii ambayo iliona dunia sio tena mahali salama kwa wao kuishi, kama ilivyo leo hii.

Dunia ambayo watu waligawanywa katika makundi ya kipato, nafasi na kabila kama tuonavyo ulimwengu wa leo wa kibepari. Inatosha kusema heshima na thamani ya mtu haikutokana na utu wake kama kiumbe bora kiasili, bali kwa vigezo vingine kama mali na nasabu. Ummah wa leo thamani ipo kwa alichonacho mtu, mali humfanya mtu kuwa zaidi ya kiumbe na kujipa au kupewa sifa za Muumba hadi kuabudiwa na wengine kwa kumtegemea katika rizq.

Mtume SAAW akiwa kiongozi wa walimwengu tuna mengi ya kujifunza kutoka kwake. Yeye alitekeleza majukumu yake kiuwanaadamu ambapo baada ya kuchukizwa na hali ilivyokuwa mbaya katika jamii, ‘aliamua’ kufanya juhudi za makusudi katika kuubadilisha Ummah ule. Mtume SAAW akiamini kwamba binaadamu hapaswi kuathiriwa na zama, bali yeye ndie awe mwenye kuziathiri zama hizo. Hivyo aliutazama ulimwengu kama kijiji kimoja na watu wake wakiwa sawa katika mahitajio yote msingi.

Nukta msingi aliyoilenga katika mabadiliko yake ni kuanza kubadili fikra juu ya mitazamo inayohusu hadhi ya mtu. Fikra ambayo ilikuwa ni kuwafanya watu wabadili ufahamu wa kinachopasa kuabudiwa na kunyenyekewa. Yaani ni badiliko la ghariza ya kuabudu, iliyofanya watu waache kuabudu viumbe na warudi kumuabudu Muumba kama ilivyokuwa kwa Mitume As waliotangulia.

Athari ya badiliko hili ni kukua kwa thamani ya utu na kila mmoja kwa waliopata athari ya harakati za Mtume SAAW alibaini kwamba binadamu wote ni viumbe kama vilivyo vitu vingine. Viumbe vyenye udhaifu wa kimaumbile kama kuwa na kikomo maalumu nk. Hali hii iliwafanya waliokuwa wakidharauliwa miongoni mwa wanajamii kupata nguvu ya kiakili na kuona walioonwa kama wakuu si lolote si chochote na wakaanza kuwapinga kwa upinzani msingi wenye tija, kifikra na kwa hoja madhubuti.
Wakapoteza athari zao ‘wakubwa’ wale kwa kukataliwa na walio wengi, wakafanya vitimbi zaidi kwa kupambana kinguvu badala ya hoja. Lakini athari ya kifikra iliyokita katika mabongo ya waliomkubali Mtume SAAW ilikuwa imara na katu Waislamu wale hawakurudi nyuma bali waliendelea mbele mpaka ‘wababe’ wale wakaangamia na wakabaki tu kutajwa katika historia. Hatimae ikapatikana katika jamii heshima ya utu wa mtu.

Athari hii ikadumu kwa miaka zaidi ya 1200 mpaka ikaiteka dunia, na kuwa mabadiliko ya ukombozi kwa walimwengu wote. Unyang’anyi ukakoma, ukandamizaji ukaisha, uonevu ukapotea na hofu ikatoweka. Kisha amani, utulivu na ustawi vikatamalaki.

Kisha ukaibuka uzorotevu uliotokana na kujisahau kwa Waislamu, uliopelekea kutoa nafasi kwa wakorofi kupata nafasi tena. Ndio leo hii hali mbaya imerejea na maisha yamekuwa kama porini, wizi hadi katika majumba ya ibada, nyumba huwekwa kuta za kuizingira, sio kwa ajili ya stara bali kwa hofu ya wizi. Bila ya kutaja kuwa watawala katika nchi za Waislamu ndio wezi wakuu, wanaendekeza tawala za dhulma na manyanyaso kwa Waislamu wakirithishana katika mstari wa familia za ‘watawala’ ili kulindana katika uovu.

Katika mwezi huu tuwe na mazingatio ya msingi juu ya ujio wa Mtume SAAW na kazi kubwa na tukufu aliyoifanya kuusimamisha Uislamu kama mfumo kamili wa kimaisha wa kiulimwengu kwa wanaadamu wote.
Tunamuomba Mola wetu Ajaalie maadhimisho haya ya mazazi yawe yakubadili fikra zetu zielekee katika usahihi wa dini yetu, tuwe chanzo cha mabadiliko ya kweli chini ya dola ya Kiislamu ya Khilafah Rashidah. – Amiin

Hamza Sheshe

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Maoni hayajaruhusiwa.