Kuangazia Mabadiliko ya Sheria Ya Vyama Vya Siasa

Kupitishwa kwa muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2018 na wabunge wengi licha ya kuonekana una vifungu vyenye utata na kandamizi unatoa uhalisia wa demokrasia kama ifuatavyo:

Kwanza, panadhihirika udhaifu wa kauli mbiu ya “wengi wape” ambapo wengi hushinda katika demokrasia hata kama wanachosimamia si sahihi. Lau kama kungekuwa na kipimo kingine sahihi tofauti na kura ya wengi wape ni wazi muswada huu usingepita, kwa sababu una mambo mengi yaliyopigiwa kelele sana na kulalamikiwa na upande wa upinzani.
Kwa mfano, kipengele cha 3 C cha muswada huo kinampa mamlaka Msajili kufuatilia na kuchukua hatua kuhusu chaguzi za ndani za vyama, kifungu cha 26 kinazungumzia kufutwa kwa chama endapo Msajili atabaini kuwa wahusika walitoa taarifa za uongo wakati wa usajili. Kifungu hicho badhi ya wabunge wanadai walikubaliana katika kamati kifutwe, na serikali iliwasilisha jedwali la marekebisho kuwa wamekifuta, lakini kiukweli hakikufutwa.

Pili, kupitishwa kwa muswada huu ambao utakuwa sheria mara baada ya Raisi kuweka saini, inaonesha wazi uhalisia wa sheria hizi kuwa ni maagizo na matakwa ya mtawala kwenda kwa watawaliwa. Ni fedheha na urongo wa wazi kama inavyodaiwa na demokrasia eti watu wote hushiriki kutunga sheria. Hapa tunaona wazi kuwa muswada huu hautakuwa sheria mpaka Raisi atakapoweka saini. Hivyo, sheria hii na nyenginezo si matakwa ya wananchi bali ni matakwa ya Raisi.

Tatu, mfumo wa demokrasia, msingi wake ni maslahi binafsi kwa wanasiasa na matajiri na kamwe na si maslahi ya Ummah kama wanavyolaghai watu wademokrasia. Katika kupitishwa muswada huu pameonekana Wabunge wa chama tawala wakitetea muswada, na upinzani wakipinga. Wabunge wa chama tawala wametetea muswada huo ili kulinda vyeo vyao na kukhofu kukemewa na watawala. Na lau raisi ataonesha kuupinga muswada huo nao watageuka kama walivyoonekana katika suala la kanuni za mafao ya mifuko ya jamii. Na kwa upande mwengine si ajabu kuwa hata upinzani wanaupinga kwa khofu ya kuingiliwa katika vyama ambavyo baadhi yao kimsingi ni milki za watu binafsi ila vina taswira ya Ummah kinje.

Nne, sheria hii inadhihirisha udhaifu mkubwa wa sheria za kibinadamu ambazo wanasiasa huzichezeazea kwa mujibu wa maslahi yao. Jambo hili ni la kutarajiwa, kwa kuwa binadamu ni kiumbe chenye tabia ya kuvutia maslahi upande wake. Bila ya kutaja udhaifu na mipaka ya mwanadamu katika utambuzi wa mambo. Marekebisho haya ya uwekaji viraka vipya ni kukiri kwa mawanadamu kuhitajia sheria za Muumba wa ulimwengu ambazo ziko thabiti milele, kwa kuwa Yeye ni Mjuzi wa kila kitu, kila zama na kila hitajio la wanadamu.

قُلْ أَنزَلَهُ الَّذِي يَعْلَمُ السِّرَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ إِنَّهُ كَانَ غَفُورًا رَحِيمًا (الفرقان: 6.

“Sema Ameyateremsha haya (sheria) ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (Al-Furqan: 6)

Mabadiliko haya yamekuja nchi ikiwa inakabiliwa na uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu 2019, na uchaguzi mkuu mwakani 2020. Hii imechukuliwa na wengi kuwa ni mbinu ya chama tawala kudhibiti vyama vya upinzani na hivyo kujihakikishia ushindi kiurahisi katika chaguzi hizo, ikizingatiwa mwenendo wa uchumi, hali za maisha, na upinzani mkubwa unaotarajiwa kuungana pamoja.

Huo ndio undumilakuwili wa mfumo wa kidemokrasia, uko kama kinyonga, unabadilika kwa mujibu wa maslahi ya wanasiasa, na kamwe haupo kumtumikia mwanadamu na kumletea ufanisi na furaha ya kweli. Wanadamu wanahitaji mfumo wa Kiislamu chini ya dola yake ya Khilafah ili waweze kupata mafanikio ya kweli na kuunusuru ubinadamu na kila aina ya uovu na unafiki wa ubepari na siasa zake za kidemokrasia.

30 Jumada al-awwal 1440 Hijri | 05-02- 2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.