Katika Ubepari, Hata Kamari Nayo Ati Ni ‘Bidhaa Yenye Faida’
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Kumekuwa na kupazwa sauti sana juu ya kuongezeka na kushamiri kupita mipaka kwa vitendo vya uchezaji kamari nchini Tanzania, kiasi cha kuenea kila mahala na kuwaghilibu vijana wengi kujitosa
Wanaoendesha shughuli za vitendo vya kamari wanafanya hivyo kihalali, miradi yao hiyo imesajiliwa rasmi na serikali, wanalipa kodi na tozo nyengine za serikali ambazo ni sehemu ya mapato ya serikali.
Vitendo vya kamari vina madhara makubwa sio tu kimaadili, bali vinaangamiza fedha, kuhamasisha uvivu miongoni mwa watu, kuleta husuma na migogoro katika familia, kwa kuwa baadhi ya wazazi kujitosa katika kamari badala ya shughuli za uzalishaji, bila ya kutaja kuwalevya vijana wengi kuishi maisha ya ndoto za mchana zenye matarajio ya uwongo wa kutajirika kwa wepesi.
Serikali inapata mavuno makubwa kimaslahi na faida kutokana na kamari. Ndio maana inajifanya kana kwamba haijui kinachoendelea, huku ikihamasisha vitendo vya kamari kuongezeka zaidi na zaidi. Takriban vyombo vyote vya habari vimekuwa vikipigia debe uhamasishaji wa kamari ikiambatana na kuwahadaa vijana kwamba kwa kucheza kamari kuna njia ya mkato ya utajiri na ukombozi wa kiuchumi
Ndani ya 2014/15 serikali ilikusanya kutokana na kamari kiasi cha Sh15.3 bilioni, ndani ya mwaka 2015/16 mapato yaliongezeka mpaka Sh24.4 bilioni, na mapato hayo kupaa hadi kiasi cha Sh36.8 bilioni katika mwaka 2016/2017.
https://www.mwananchi.co.tz/…/Bahati-nasibu-sekta-inable-wa… need-take/1597592-4390516-format-xhtml-bptu4wz/index.html
Katika kuwepesisha zoezi la ukusanyaji wa mapato yatokanayo kamari, serikali kwa kupitia Sheria ya Fedha Na. 4 ya mwaka 2017, lilitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya Bahati Nasibu Sura Na. 166 , kwa kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la kukadiria na kukusanya kodi kwenye mapato yatokanayo na kamari.
Kushamiri kwa vitendo rasmi vya kamari kunafedhehi maumbile ya mfumo wa kiuchumi wa kibepari unaoigwa na nchi changa ikiwemo Tanzania. Mfumo ambao katika miamala yake huzingatia kitu kimoja tu, cha kujiongezea maslahi kwa hali yoyote, hata kama kwa gharama ya kudhuru watu mmoja mmoja kibinafsi au jamii kwa ujumla.
Kimsingi, serikali zote zinazofuata mfumo wa kibepari sio tu huzingatia suala la maslahi, bali huwa ndio kipaumbele chake cha kukimbilia daima. Ni wazi kwa maumbile hayo ya ubepari, mfumo huo hauna huruma wala utu kwa walimwengu, na umekosa kabisa sifa ya kuutumikia na kuutawala ulimwengu.
Kupambana kweli na janga la kamari kunahitajika mfumo wa Kiislamu ushike hatamu, ambao kipimo cha sharia zake ni ‘halali’ na ‘haramu’ tu, na kamwe hauzingatii kipimo cha maslahi wala faida.
Sharia za Kiislamu licha ya kuwa ni ibada, lakini pia zinadhamini kulinda uhai, mali, heshima na ustawi wa wanadamu. Kwa mfano, zimekataza ulevi, zinaa, riba nk. hata kama kwa uoni wa kibinadamu upo uwezekano katika hayo kupatikana maslahi.
Zaidi ya hayo, Uislamu umeharamisha miamala ya kamari moja kwa moja bila ya kuzingatia lolote la kimaslahi kutokana nayo. Na kwa hakika kila mtu makini anajua na kuona wazi kwamba kamari inaleta bughdha, uadui , kuchochea husuma baina ya watu, na kuwafanya watu waishi katika ndoto za mchana za matarajio ya kujipatia utajiri kiurahisi.
. ﴿إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَنْ يُوقِعَ بَيْنَكُمْ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَعَنْ الصَّلاَةِ فَهَلْ أَنْتُمْ مُنتَهُونَ﴾
‘Hakika Shetani anataka kuweka baina yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuiyeni na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi jee mtakatazika’ (Al- Maida 91)
Hii ni changamoto ya wazi kwa Waislamu , ambao wamepewa wajibu wa kufanya kazi usiku na mchana ili mfumo wa Kiislamu chini ya dola ya Khilafah utawalie miamala yote, na kwa wasiokuwa Waislamu wakati umefika kwao kutafiti Uislamu kwa undani kama mfumo mbadala wa ubepari. Kwa kuwa Uislamu una vigezo vyote vya kuokoa ubinadamu kutokana na minyororo ya uovu wa ubepari.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Kumb: 1440 / 03
Jumatano, 01st Jumada II 1440 AH
06/02/2019 CE
Email: info@hizb.or.tz
Hizb ut Tahrir Official Website
www.hizb-ut-tahrir.org
Hizb ut Tahrir Central Media Office Website
www.hizb-ut-tahrir.info
Maoni hayajaruhusiwa.