‘Bait-Ul Ajab’ Kielelezo cha Athari ya Uislamu na Waislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Taarifa za leo ni kuwa jengo la kihistoria la Bait el-Aajab la Mji Mkongwe, Zanzibar limeporomoka na baadhi ya watu kufukiwa na kifusi. Wakati tukiwafariji wahanga na wote walioathirika kwa namna moja au nyengine kutokana na kuporomoka jengo hilo, pia tunakumbushia makala iliyoandikwa miaka nane iliyopita (Disemba 2012) na Masoud Msellem, Mwakilishi Kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania, wakati huo jengo hilo likiwa linaanza kuporomoka baadhi ya sehemu yake.
Endelee kusoma kwa makini:
Karibuni tumeshuhudia kuporomoka sehemu ya jumba la Bait-ul ajab (Jumba la ajabu). Jengo kongwe, maarufu la kihistoria lililopo kati kati ya kitovu cha mji mkongwe Zanzibar, ukingoni mwa Bahari ya Hindi.
Inaaminika kwamba Jumba hili lilipewa jina hilo kwa kuwa kwa zama zake lilikuwa jumba la mwanzo kuwa na umeme ndani ya Zanzibar na pia ndio jengo la mwanzo ndani ya Afrika Mashariki kuwa na ‘kipandishia watu’ (lift). Bait-ul ajab lilijengwa na Sultan Barghash bin Said, sultan wa pili, ndani ya mwaka 1883 likiwa miongoni mwa qasri zake. Mara baada ya mapinduzi ya 1964 likanyakuliwa kuwa katika himaya ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar. Na ndani ya miaka ya 2000’s likazinduliwa rasmi kuwa miongoni mwa makumbusho ya kihistoria.
Licha ya jengo hili zaidi kunasibishwa na tareekh/historia ya watawala wa kisultani na wakaazi wa Zanzibar na kutumika kama chapuo ya kukuza fikra batil na haramu ya uaswabia/ubaguzi ya ‘uzanzibari. Ukweli ambao watu wengi husahaulishwa ni kwamba kumbukumbu ya jengo hili na nyingi zilizojaa ndani ya Afrika Mashariki linabeba athari muhimu ya Uislamu kwa kiasi fulani, na pia ni kielelezo cha kuwepo kwa thaqafa ya Kiislamu iliyokita kwa kiasi fulani kwa makarne ndani ya Zanzibar na Mwambao wote kwa ujumla. Pamoja na ukweli kwamba sehemu kubwa ya ukanda wetu huu, Uislamu haukutawala moja kwa moja katika kiwango cha dola, lakini ulikuwa na athari kubwa katika muamala wa maisha ya kila siku.
Kwanza, jina la jengo hili ni kielelezo tosha kwamba lugha ya kiarabu ilikuwa na nafasi muhimu katika maisha ya kila siku ya Waislamu hususan waliokuwa wakiishi Zanzibar ambayo ndiyo iliyokuwa Makao Makuu ya Usultani na kwa mwambao wote kwa ujumla. Hilo huthibitika zaidi kwa kuwa nyaraka zote muhimu chini ya masultani zikiandikwa kwa lugha hiyo. Na hadi kudiriki lugha hii ya kiarabu kuiathiri lugha ya kiswahili kwa kiasi kikubwa, licha ya leo kuwepo kampeni kali ya kiuadui ya kufuta kabisa athari hiyo na kukigubika kiswahili kikamilifu kwa guo la ‘ubantu’. Si hivyo tu, kwa kuwa kiarabu ilikuwa ni lugha ya mapema zaidi na yenye fungamano na wakaazi wa maeneo haya, iliwalazimu Waislamu, kimaandishi kuitumia katika mawasiliano yao ya kila siku, kwa kuandika lugha ya kiswahili kwa kutumia herufi za kiarabu.
Kwa maneno mengine, hali hiyo ilipelekea kukosekana wimbi kubwa la hali ya kutojua kusoma na kuandika (illiteracy), kwa sababu Waislamu wengi wakisoma na kuandika kiswahili kwa kutumia herufi za lugha yao ya kiarabu. Hali hiyo iliendelea mpaka Uingereza ilipomakinisha elimu yake ya kimagharibi na maandishi ya herufi za kilatini na kuipotoa kwa makusudi dhana ya kutojuwa kusoma na kuandika, sasa ikawa ni ile hali ya kutojua kusoma na kuandika kwa herufi zao za kilatini. Na hatimae kukomeshwa kabisa rasmi matumizi ya kiarabu katika miamala ya kila siku na kudhoofisha elimu ya dini na lugha ya Kiarabu. Kwa Zanzibar ilihusisha kwa kuondosha masheikh weledi katika Chuo cha Muslim Academy, kama vile Sheikh Suleiman Alawi, Sheikh Ahmed Zein (Yemen) Said Ahmed Al-Kindy (Oman) na Sayyid Ali Badawi (Lamu). Si hivyo tu, hatimae kukifunga kabisa chuo hicho cha Kiislamu katika miaka ya sitini na kukigeuza nyumba ya kulelea watoto (Forodhani). Akieleza kwa masikitiko Sheikh Ali Muhsin Al-Barwan (ambae alikuwa na nafasi nyeti katika serikali ya Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya 1964) kuhusiana na qadhia ya kutupwa lugha ya Kiarabu, katika kitabu chake cha ‘Kujenga na kubomolewa Zanzibar’ anasema: “Kutokana na amri hii ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ( ya Waislamu kujua kiarabu) nikaona ni wajibu wangu kupigia mbio ili tuweze kuwa nayo mipango ya masomo ya Kiarabu katika marhala zote. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu tukaweza kuwa na masomo ya Kiarabu kuanzia kwa watoto wadogo (chekechea), yakafuatia na wakubwa wao, Arabic speaking, ikafuatilia hii (chuo cha) Muslim Academy na kuendelea ikawa ni ule mpango wa Chuo Kikuu cha Waislamu Afrika Mashariki na Kati. Ziada ya hayo ni ule mpango wa watoto wetu kupelekwa Misri kwa marhala mbali mbali , pamoja na ile ya Al-Azhar. Ilivyokuwa haya ndio nyenzo ya kukuza Uislamu, mara tu baada ya mavamizi ya nchi yetu( mapinduzi) la mwanzo walilolifanya ni kuvuruga mipango yote hii ya masomo ya Kiarabu, hivi ni pamoja na kule kuchoma moto mas-hafu na mashine za kuchapia Kiarabu. Wamefanya haya yote ili (kwa fikra zao) kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu-Uislamu lakini hawatoweza kufanya hivyo”. (“Kujenga na Kubomolewa Zanzibar” uk.187)
Pili, baadhi ya milango ndani ya jengo la Bait-ul Ajab imenakshiwa vizuri mno kwa baadhi ya aya za Quran Tukufu. Cha kushangaza licha ya kuwepo picha mbali mbali za kulitangaza jengo hilo kwa watalii kupitia mitandao mbali mbali, ni nadra sana kuona picha zinazoonesha milango hiyo iliyosarifiwa kwa aya hizo za Quran Tukufu ndani ya jengo hilo. Na hii ni dalili kuwa utalii wa nchi zetu katika kuwaridhisha wageni hutulazimu tujikatae. Kimsingi, kuwepo kwa aya hizo za Quran Tukufu katika jengo hilo ni dalili ya kuwepo athari ya Uislamu kwa makarne katika Zanzibar na Mwambao kwa ujumla.
Licha ya ukweli kwamba watawala wa Kisultani walikuwa chini ya Himaya ya Uingereza, kama walivyo vibaraka watawala wa leo katika nchi zote za Waislamu.
Milki kama hizi katika fiqhi ya Kiislamu huitwa “Al-Sawafi”. Mali ambazo huhusisha milki zote za watawala kabla ya kusimama Khilafah, mali zilizopatikana katika ardhi zilizofunguliwa na kubakia bila ya mmiliki baada ya wamiliki wa asili kutoroka, au mali zilizokuwa milki ya dola iliyofunguliwa, watawala wake, wakiwemo maafisa wote katika ngazi za utawala, wapambe wao, mali za waliouliwa katika vita, au waliokimbia vita na kuziacha nyuma (ngawira) nk. Na huingia mali hizi moja kwa moja kuwa miongoni mwa mali za serikali /State property, na zitahifadhiwa katika hazina ya bait-ul mal. Khalifah atasimamia kwa makini utunzaji wa mali hizi, kwa kuwa yeye pekee ndie dhamana/mas’-ul wa serikali na Waislamu. Na ni yeye pekee mwenye mamlaka ya kuamuru namna ya matumizi/tassaruf ya mali hizi kwa mujibu ijtihadi yake na kwa maslahi ya Uislamu na Waislamu.
Aidha, kwa upande mwengine kwa kuwa mali kama hizi ni miongoni mwa turathi/legacy za Waislamu, Uislamu unatutaka tujifunze yanayotokamana na turathi hizi, na kujiepusha na maovu yanayofungama nazo hata kama ni kutoka kwa jamaa au akraba zetu, na kamwe tusijifakhiri na uovu na dhambi ya waliyotutangulia. Kwa kuwa Muislamu hajifakhiri na haramu wala uovu. Bali daima Muislamu hujinasibu na kujifakhiri na kushikamana na turathi nzuri kutoka kwa wa kabla yetu na kujipamba nazo:
وَاتَّبَعْتُ مِلَّةَ آبَائِي إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ مَا كَانَ لَنَا أَنْ نُشْرِكَ بِاللَّهِ مِنْ شَيْءٍ ذَلِكَ مِنْ فَضْلِ اللَّهِ عَلَيْنَا وَعَلَى النَّاسِ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لاَ يَشْكُرُونَ (يوسف: 38
“Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Ishaq, na Yaa’qub. Hatuna haki ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu, na juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru”(TMQ 12:38)
Na kwa upande mwengine, Uislamu unatuamrisha turekebishe kila penye turathi mbaya na makosa yaliyotangulia kwa kufanya mbadala kwa marekebisho na kuondoa mapungufu hayo:
فَمَنْ خَافَ مِنْ مُوصٍ جَنَفًا أَوْ إِثْمًا فَأَصْلَحَ بَيْنَهُمْ فَلاَ إِثْمَ عَلَيْهِ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ (البقرة: 182).
“Na mwenye kumkhofia muusiaji kwenda kombo au kupata dhambi akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na ddhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu” (TMQ 2: 182)
Turathi kubwa na yenye thamani zaidi ni ile tuliyoachiwa na Mtume SAAW na makhalifa waliotangulia, nayo ni utawala wa Kiislamu /Khilafah ambao makafiri wametupokonya.Turathi hii ndio kinga ya kweli ya turathi nyengine zote, kuanzia aqiida ya Uislamu, thaqafa yake, sha’air zake, majengo ya athari zake nk. Ni wajibu kujipinda usiku na mchana kuirejesha turathi hii ili irudi kudhamini na kuzilinda turathi nyengine zote katika biladi zetu.
Masoud Msellem
Rejea:
1.Al-Barwan, Ali Muhsin-Kujenga na Kubomolewa Zanzibar (Kumbukumbu) uk. 186-187
3. Hizb ut-Tahrir- Zaloom, Abdul Qadeem, Funds in Khilafah State uk.83

Maoni hayajaruhusiwa.