Demokrasia Yaangamiza Neema Adhimu ya Akili

بسم الله الرحمن الرحيم

Tume ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya (UNCND) mwanzoni mwa mwezi huu (Disemba 2020) ilitangaza kuiondoa bangi katika orodha ya madawa ya kulevya. Hatua hiyo ni baada ya wanachama wa tume hiyo kupiga kura na kupatikana ushindi mwembamba. Tume ya (UNCND) ilichukuwa hatua hiyo kutokana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kutaka bangi itumike kwa wanachodai matumizi ya kitabibu.
Taarifa za kuondolewa bangi katika orodha ya madawa ya kulevya zilisambaa kila mahala na kuzuka mijadala kwa watu binafsi na katika vyombo vya habari. Hatua hiyo inamaanisha kuwa bangi sio katika dawa za kulevya za kupigwa vita katika jamii. Yaani madhara yanayosababishwa na bangi kwa afya ya mtumiaji na jamii yamekwisha.
Tangazo la namna hii ni moja kati ya mengi yanayoonesha namna jamii inavyoangamizwa na mfumo wa kidemokrasia. Jambo hili ni kilele cha mchakato wa muda mrefu ambapo nchi kadhaa zilishaweka sheria ya kuruhusu matumizi yake.
Msingi wa demokrasia ni watu kujiundia muongozo wa maisha yao kwa kutumia akili zao na matamanio /hawaa yao. Ndipo kukawepo mabunge na mabaraza ya kutunga sheria ambayo majukumu yao hasa ni kuhalalisha na kuharamisha vitu na matendo ya watu.
Mwaka 2016 katika Bunge la Tanzania, mbunge mmoja kwa jina maarufu, Msukuma, alitamka hadharani kwamba : “hata humu ndani (yaani ndani ya bunge) wapo wanao tumia (bangi) .” https://www.youtube.com/watch?v=FvzB93f2irM
Mbunge Msukuma alitoa kauli hiyo baada ya kuibuka mjadala wa kwamba bangi iruhusiwe au iendelee kupigwa marufuku.
Pia tarehe 3. Februari 2020 bungeni Dodoma, serikali ilisema “tayari imepata wawekezaji wawili ambao wanaotaka kuwekeza kiwanda cha kuchakata mafuta ya bangi nchini yanayotumika kwa matibabu” https://mtanzania.co.tz/serikali-kuanzisha-kiwanda-cha…/
Bunge ni chombo cha kutunga sheria za nchi, lakini ukweli unabakia kuwa hata kwa mujibu wa vipimo vyao, wabunge wengi wamekosa sifa za kuyakabili mambo kitaalamu ikiwemo hilo la kutunga sharia.
Ujio wa bangi kama moja ya dawa za kawaida kutaongeza watumiaji kwa kiwango kikubwa na hivyo kutarajiwa madhara zaidi. Yaani kama katika utumiaji kwa kificho hali ilikuwa ile, itakuaje hali kwa sasa kuwa bangi ni ‘halali’?
Kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu kwa kulima bangi duniani https://habarileo.co.tz/habari/2020-02-045e393d38afb1f.aspx
Pia ni nchi ya 5 katika kutumia bangi nyingi Afrika, ambapo watu milioni 3.6 hutumia ulevi huo:
Akili ni tunu aliyopewa mwanadamu na Muumba wake na inamboresha yeye kwa viumbe wengine. Aidha, tunu hii ndiyo hasa inayotegemewa na mwanadamu katika ustawi wake na ndio iliyomtofautisha kiuhalisia binadamu na viumbe wengine. Bali hata binadamu kwa binadamu mwengine.
Jukumu la serikali la kulinda raia haliishii tu katika kulinda miili yao na mali zao bali pia na akili zao. Kwani kilema mwenye akili timamu ni bora kuliko taahira mwenye viungo kamili katika taifa.
Akili imekuwa kigezo cha hukumu kwa matendo ya mtu, sio kwa Muumba tu bali hata katika vyombo vya kisheria vya wanaadamu wakiwemo wanademokrasia wenyewe.
Demokrasia katika kuchanganyikiwa kwake imefanya vitu vya kuharibu na kuangamiza akili kuwa ni sehemu muhimu ya wanachokiita ‘haki za binadamu; ikiwemo kuhalalisha vilevi vya aina mbalimbali kama vile pombe, kasumba na sasa bangi.
Msingi wa ubepari ni kutazama chenye faida bila kujali madhara. Ndipo utakuta huharamishwa pombe ya gongo / chang’aa na kuhalalishwa pombe ya konyagi, hali ya kuwa kiwango cha ulevi (alcohol) ni kikubwa zaidi katika konyagi. Msingi wa kuiharamisha gongo ni kutokuchangia kodi kwa kuwa inazalishwa kienyeji sana. Na hivyo, kila kitakachodhibitiwa katika namna ya kwamba kinaweza kuingiza kodi, kitahalalishwa. Sababu nyingine zitakazotolewa ni ziada tu.
Kamwe huwezi kuliona kwa udhati suala la ulinzi na thamani ya akili katika mfumo batil wa kidemokrasia usiozingatia sharia za Muumba
Uislamu huthamini hali ya akili, ili kulindwa, kutunzwa na kulelewa kwa umakini ili isidhurike.
Aidha, katika fiqhi ya Kiislamu na chini ya serikali yake ya Khilafah, miongoni mwa sifa inayozingatiwa kwa mtu kupewa jukumu la kisheria na kuhukumiwa kwa makosa ni uwepo akili timamu ya mtu. Mtu kuwa ‘mukalaf’ (anayelazimishwa na sharia kutenda jambo au kuliacha) ni katika sharti kuwa na akili timamu.
Ndipo alipoweka wazi Mtume (saw) kwa kusema kwamba:
“Kalamu (ya kuandika malipo na adhabu) husimama (haifanyi kazi) kwa watu watatu (watu katika hali tatu); Mtoto mpaka atakapobalekhe, aliyelala mpaka anakapoamka na mwenda wazimu mpaka atakaporejewa na akili”
Msingi hapa ni mtu kuwa na ufahamu wa anachokifanya, nayo ni kuwa na akili iliyomurua.
Kuondoa Bangi katika kundi la madawa ya kulevya ni dhihirisho la upungufu wa mifumo ya maisha anayoiunda mwanadamu, na kwa sasa ni mfumo wa kidemokrasia, na kamwe mfumo huo hauwezi kumuhakikishia mwanadamu huyu ustawi wake kibinafsi wala kijamii.
Kilichofanya bangi iharamishwe awali ni viambata vyake (ingridients) ambavyo bila shaka havijabadilika na bado vipo, tofauti ni akili za wanaoamua, huenda nao ni wahanga wa hiyo bangi.
Hali hii ni wazi inaonesha hitajio la kuwepo mfumo mbadala wa kumuongoza, kumsimamia na kumpatia sharia mwanadamu zisizotokamana na akili finyu ya kibinadamu. Mfumo huo ni Uislamu chini ya dola yake thabiti ya Khilafah Rashidah.
Abu Nuthutaq
Risala ya Wiki No. 97
08 Jumada al-awal 1442 Hijri 23 Disemba 2020 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

 

Maoni hayajaruhusiwa.