Karibu Mwaka Mpya Wa Kiislamu Wa 1443 Hijria
بسم الله الرحمن الرحيم
Alhamdullilah, tumeingia mwaka mpya wa Kiislamu wa 1443 Hijria. Mwaka mpya wa Kiislamu huitwa mwaka wa ‘Hijria’ kwa kuwa una fungamano moja kwa moja na tukio kubwa na adhimu la Hijra.
Ni jambo muhimu sana katika wakati huu kuwakumbusha Waislamu unyeti wa tukio kubwa na adhimu la Hijra na kuwafafanulia kwa kina ufahamu thabiti wa tukio hilo, fungamano lake na kalenda yetu na mahusiano yake na maisha yetu ya kila siku hususan katika kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa kupitia Khilafah Rashidah.
Kwanini tukio la Hijra liwe na Uhusiano na kuingia mwaka mpya wa Kiislamu?
Tukio la hijra lina uhusiano wa moja na kuingia mwaka mpya wa Kiislamu, kwa sababu katika zama za Khilafah ya Umar Ibn Al-Khattab Ra. Masahaba kwa mawafikiano yao (ijmaa) walifikia uamuzi wa kuanzisha hesabu ya kalenda ya Kiislamu, na nukta kianzio ya kuhesabu kalenda hiyo waliteuwa kuanzia tukio la hijra
Kwa nini Masahaba waliteua tukio la Hijra kuanzia kuhesabu kalenda hiyo?
Naam, licha ya kuweko matukio mbalimbali makubwa kama vile uzawa wa Mtume SAAW, Kupewa Utume, Safari ya Israi na Miiraj, Kufariki SAAW nk. Bado Masahaba walifikia muwafaka wa kuanza kuhisabu kalenda hiyo kuanzia tukio la hijra. Kwa sababu tukio hilo ndilo lililoweka mstari wa kutenganisha baina maisha ya awali ya Waislamu ndani ya Makka katika utawala wa kikafiri, na kuelekea katika maisha matukufu ya utawala wao wa Kiislamu chini ya kivuli cha dola yao tukufu ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madina.
Jee uteuzi wa tukio la Hijra unaashiria kitu gani kwa Waislamu?
Uteuzi wa Masahaba wa tukio la hijra kuwa nukta kianzio ya kalenda ya Kiislamu maana yake ni kutuonesha uwajibu wa kuwa na dola ya Kiislamu. Masahaba walikusudia kubakisha ufahamu huo thabiti katika bongo na kumbukumbu za Waislamu mpaka siku ya Kiyama. Na hili ndio funzo kuu na mama ambalo Umma unahitaji kukumbushwa kila unapoingia mwaka mpya wa Kiislamu.
Mambo gani mengine ziada yanayopatikana katika tukio la Hijra?
Katika tukio hili kunapatikana mafunzo mengi kama vile:
1. Mtume SAAW hakutoka Makka kwa woga wala kama mkimbizi, kwa kuwa awali alishafikia na viongozi wa maanswar juu ya kupewa nusra na kukabidhiwa hatamu za uongozi ndani ya Madina. Lakini pia hata mapokezi aliyopatiwa Madina ni dalili kuwa sio mkimbizi. Bali ni ya kiongozi aliyetarajiwa kuwasili.
2. Umuhimu na ulazima wa nusra katika ulinganizi wa Uislamu, na pia utukufu mkubwa wa Ansar. Kwa kuwa wao ndio waliompa Mtume SAAW kiapo cha nusra, na jambo hilo likamfanya Mtume SAAW kuelekea Madina akiwa tayari kiongozi wa dola.
3. Muhanga wa Mtume SAAW na masahaba zake mbali mbali katika mchakato wa safari hii. Kama Ali bin Abi Talib, Abubakar Swidiq nk.
4. Kuyakinisha uwezo mkubwa wa Allah Taala na kutokata tamaa na nusra Yake. Uwezo huo hudhihirika katika miujiza mbalimbali iliyotokea katika tukio hili. Haya yote huingia katika upande wa sisi kuamini na kukinai nusra ya Allah Taala hata hali ikiwa ni ngumu kiasi gani.
5. Pamoja na kukinai uwezo mkubwa wa Allah Taala na kuwa na uhakikia wa yakini wa kupata nusra yake, bado sharia ya Kiislamu inatufunga kutenda mipango ya kibinaadamu katika mambo yetu. Kama vile Mtume SAAW katika tukio hili la Hijra alivyoipangalia safari kabambe katika hatua za kibinadamu. Kuanzia muda wa kuondoka, kujificha pangoni, kukodi bingwa, mtaalamu na mweledi wa kuzijua njia, kuwababaisha maqureish kwa kutumia njia isiyokuwa maarufu, kuwa na mtu maalumu kumletea taarifa nyeti juu ya kinachojiri ndani ya Makka nk.
Tunamuomba Allah SWT ajaalie uwe mwaka wa kheri, barka, nusra na ushindi ili kuunusuru Umma wetu mtukufu wa Kiislamu na ubinadamu kwa jumla.
Amiin
01 Muharram 1443 Hijria / 9 Agosti 2021 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.