Nidhamu Bora ya Mtume (saaw) Katika Kuondoa Umaskini

Mapinduzi ya kimfumo yaliyoletwa na Mtume (saaw) yalinyanyua upeo wa kifikra na utatuzi thabiti uliotokana na itikadi safi ya Kiislamu na  kuwa ndio msingi uliojengewa fikra zote, zikiwemo za kijamii, kisiasa,  kiuchumi nk.

Kwa kuwa uchumi unachukua sehemu nyeti na kubwa katika maisha ya binadamu, na kwa kuwa Mtume SAAW alitumwa kuwa nuru kwa ulimwengu na kutatua matatizo yote ya wanadamu, bila shaka eneo hili la uchumi Mtume SAAW aliliangazia vya kutosha. Mtume SAAW alionesha wazi katika msingi wa kiuchumi kwamba fikra asili mali ni  milki ya Allah (swt),  na kuhimiza kuitoa mali hiyo kwa njia nzuri kuwasaidia wenye shida, mafukara na masikini, kwa kuwa mali hiyo ni amana kutoka kwa Muumba.

Amesema Allah Ta’ala:

وَأَنْفِقُوا مِمَّا جَعَلَكُمْ مُسْتَخْلَفِينَ فِيهِ (الحديد: 7

“Na toeni katika yale aliyokupeni Allah” (Al-Hadid:7)

وَآتُوهُمْ مِنْ مَالِ اللَّهِ الَّذِي آتَاكُمْ

“Na wapeni katika mali ya Allah aliyokupeni” (An-Nuur: 33)

Pia Mtume (saaw) katika kuwahimiza na kuonyesha faida kubwa inayopatikana kwa kuwasaidia wenye shida anasema:

“Hakuna Muislamu mwenye kumkopesha Muislamu mkopo mara mbili ila huwa ni sadaka mara moja.”  (Ibn Hibban ).

Katika kuhakikisha kuwa suala la kuondoa umasikini linashughulikiwa kwa uzito unaostahili, Uislamu ukaweka taratibu za kuwasaidia raia mafukara na masikini ndani ya jamii. Ukafanya hilo kwanza ni jukumu kwa watu wa karibu (aqraba) katika ndugu au jamaa. Ikiwa hawapo au hawana uwezo basi dola kupitia fungu la zaka au kwa ruzuku nyengine hutolewa kwa ajili yao. Lau ikiwa hakuna cha kutosheleza katika zaka au Baytul Maal, basi matajiri miongoni mwa raia hutakiwa kutoa kiasi fulani cha kuwatosheleza mafukara na masikini kwa ajili ya mahitaji yao ya msingi kupitia usimamizi wa dola.

Allah Taala anasema:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ (التوبة: 60……

“Hakika zaka (swadaka) ni kwa ajili ya mafukara na masikini”

  (At-Tawba: 60).

وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ (الذاريات: 19).

“Na katika mali zao kuna haki maalumu kwa wanaoomba na wenye kujizuilia (Adhariyat: 19)

Aidha, Mtume (saaw) amesema katika yale yaliyopokewa kutoka kwa Allah (swt):

 “Hajaamini yoyote yule anayelala ameshiba na jirani yake ubavuni mwake ana njaa na yeye analijuwa hilo” (Bazzar kutoka kwa Anas).

Mtume (saaw) na Makhalifah waliomfuatia walionyesha kivitendo juu ya usimamizi wa jukumu hili la kuondoa umasikini. Kwa mfano, Mtume  (saaw) aliwataka Answar kutoa msaada wa kimali kuwapa ndugu zao Muhajirun walio mafukara.  Imepokewa pia kuwa  Mtume SAAW alimpatia mtu katika Maansar nyenzo za kufanyia kazi kumuwezesha kwenda kukata kuni na kuuza ili kuondokana na umasikini na kuomba.

Aidha, imepokewa kuwa Sayyidna Umar (ra) katika Khilafah yake aliwapatia mali wakulima wa Iraq kutoka Baytul Maal ili waitumie katika kugharamia shughuli zao za kilimo.

Katika kutoa fursa za kujiendeleza kiuchumi kwa raia, Mtume (saaw) amezuwia suala la kuyaacha mashamba kukaa bure bila ya kulimwa. Akakataza kukodisha mashamba kwa ajili ya ukulima kwa kusema:

“Mwenye ardhi ailime au ampe zawadi ndugu yake, akikataa basi ardhi yake ichukuliwe.” (Bukhari). Mtume (saaw) pia alihimiza kufufua ardhi, na pindi inapofufuliwa, mfufuaji huwa milki yake. Bila ya kusahau kuwa Mtume SAAW alitowa ardhi na mali kadhaa za Dola kwa watu binafsi ili waweze kujiendeleza kiuchumi.

Uislamu pia umekataza kata kata njia chafu za kumiliki mali zikiwemo riba, kuhodhi (hoarding), ukiritimba na udanganyifu kwa kuwa zinadhoofisha mzunguuko wa kiuchumi. Pia Ukazuwia umilikaji wa mali ya Umma kwa watu binafsi, na kuweka kanuni na sheria za kudhibiti na kuhakikisha kuwepo kwa fursa sawa za kiuchumi katika jamii, bila ya  wengine  kuzitumia rasilmali na fursa kwa maslahi yao kibinafsi.

Kupitia sera hii Mtume (saaw) aliweza kujenga msingi wa uzani sawa wa kiuchumi (economic balance) ambao unahakikisha na kudhamini mzunguko wa mali baina ya wanajamii wote, kama alivyotaka Allah (swt) akasema:

كَيْ لاَ يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ (الحشر:

“Ili (mali) isizunguke baina ya matajiri tu miongoni mwenu”

(Al-Hashr:7).

Suala la ugawanyaji wa mali likawa limetatuliwa na nidhamu hii bora ya kiuchumi iliyotokana na Mfumo bora wa Uislamu aliokuja nao Mtume SAAW.

Nidhamu hii ya Mtume SAAW iko kinyume kabisa na mfumo wa kibepari kwani wao maslahi ndio lengo lao, na huyafikia  maslahi hayo kwa njia zozote zile bila kujali uhalali na uharamu. Msingi wao wa ‘uhuru wa kumiliki’ (freedom of ownership) katika nidhamu ya kiuchumi ya kibepari unakinzana na upatikanaji fursa sawa kwa raia, na hivyo hupelekea kuongezeka kwa tabaka la masikini dhidi ya matajiri. Sehemu kubwa ya utajiri humilikiwa na watu wachache katika jamii hivi leo, hali inayosababisha kuzuka pengo kubwa baina ya walichonacho na wasiokuwanacho kila kukicha.

Kwa kuwa Mtume wetu SAAW aliyetumwa kuwa nuru kwa ulimwengu hatuna budi kuuchukua mfumo na masuluhisho aliyotuletea, hivyo kunahitajika kuirejesha tena dola ya Khilafah katika ulimwengu, ili isimamie nidhamu bora ya kiuchumi itakayoleta ustawi kwa jamii ya Waislamu na walimwengu kwa ujumla.

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Habib Abdulla

Maoni hayajaruhusiwa.