Uzawa wa Mtume (saw) Utukumbushe Ufikishaji wa Risala Yake

Ni katika mwezi kama huu wa Rabi ul Awwal amezaliwa kipenzi chetu, Mtume wetu mtukufu ( rahma na amani ziwe juu yake) ambaye katumwa kuja kuiongoza dunia. Kwa idhini ya Mola wake ametumwa kuwatoa watu katika kiza cha ujahiliya(ujinga na ukafiri) na kuwapeleka katika haki na uadilifu (Uislamu).

Mtume(SAW) ni kigezo chema kwa Ummah  kwa kila kipengele ikiwemo katika amali ya kufikisha risala(ujumbe) aliopewa na Mola wake. Hivyo, sisi wafuasi wake (Waislamu) ni jukumu letu umfuata katika kufikisha risala yake kwa wengine ulimweguni kote.

Suala la kumfuata Mtume SAAW katika kila kitendo chetu na kufikisha risala yake kwa ulimwengu ni mambo muhimu sana kuyazingatia wakati huu tukiwa tunaukumbuka uzawa wake. Na kimsingi  hii ndiyo tafsiri sahihi ya kuwa sisi ni wafuasi wake.

Ni muhimu kukumbuka kuwa yeye Mtume wetu Muhamad (SAW) ni Mtume wa mwisho, na vivyo hivyo ujumbe wake ni ujumbe wa mwisho na kwa ulimwengu mzima, na leo hii dunia nzima ina kiu ya risala hii ya ukombozi (Uislamu) kutokana na kushindwa wazi wazi kwa mfumo wa Kibepari/Kidemokrasia unaotawala ulimwengu sasa, ambao umemtia binadamu katika dhiki kubwa katika nyanja zote za maisha yake.

Ubepari unazidi kuongeza janga la  umasikini duniani, kwa mfano idadi ya masikini katika  Afrika ilikuwa milioni 280 mwaka 1990 lakini imeongezeka na kufikia milioni 330 mwaka 2012 na inazidi kukua kila mwaka (Africa Poverty Report, 2016).

Hiki ni kielelezo cha ni hatari kubwa katika kipindi hiki ambacho teknolojia imekuwa na namna ya kukabiliana na mazingira imekuwa rahisi kwa binadamu, sasa iweje umasikini uongezeke kila kukicha badala ya kupungua. Jibu ni moja tu kuwa mfumo wa kibepari umeshindwa kutawanya rasilimali kwa watu na hatimaye umemilikisha rasilimali nyingi sana katika mikono ya watu wachache sana. Ikitarajiwa wakiwa waroho na mabepari.

Mfano mwingine ni katika suala la njaa na ukosefu wa chakula, inakadiriwa takribani watu milioni 815 walikabiliwa na njaa mwaka 2016 na iliongezeka na kufikia milioni 821 mwaka 2017 (WHO, 2017). Hali hii haitarajiwi kupungua kutokana na kuongezeka kwa ukame duniani  na  vita vya kutengenezwa kama Syria na Yemen, Iraq, Afghanistan nk.

Hili  pia linasikitisha sana kuona katika ulimwengu huu wa leo ambapo inawezekana hata kulima mazao kwa muda mfupi sana vipi kuwe na njaa, haiingii akilini kabisa, na jibu rahisi ni kutojali kwa mfumo wa kibepari.

Hiyo ni mifano michache katika mingi, bila ya kusahau kupotea amani na utulivu kila mahala katika ulimwengu, kunakosababishwa na madola ya kibepari na uporaji wao wa rasilmali katika nchi changa na kuhodhi uchumi wa nchi hizo kwa kisingizio cha uwekezaji nk.

Ni muhimu wakati tunakumbuka uzawa wa Mtume (SAW) kuona uwajibu wa kubeba jukumu la kufikisha risala ya Mtume SAAW kama alivyoifikisha yeye wakati wa uhai wake, ili kuukomboa ulimwengu kutokana na mfumo thakili wa kibepari, na kurejesha furaha, amani na matumaini kwa Waislamu na wanadamu kwa jumla.

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Said Bitomwa

Maoni hayajaruhusiwa.