Mapambano ya ‘Kisanii’ Dhidi ya Ukimwi
Siku ya tarehe 1 Disemba ya kila mwaka imetangazwa kimataifa kuwa ‘Siku ya Ukimwi’. Maradhi ambayo mpaka sasa bado hayana kinga wala tiba, huku yakiwa miongoni mwa maradhi yanayogharimu maisha ya watu wengi ulimwenguni. Siku hii ya Disemba Mosi hufanywa ni siku ya kukumbuka maafa na madhara makubwa yanayoletwa na ukimwi, uhamasishaji wa kupima, kuelimishana juu ya athari yake, na zaidi kutoa msisitizo wa kuwatunza waathirika wake. Wagonjwa wa mwanzo wa maradhi ya ukimwi waligunduliwa mnamo tarehe 5/6 /1981 ndani ya jiji la Los Angeles, Marekani.Wakiwa ni watu wanatokana na jamii ya mabaradhuli, makahaba na watumiaji madawa ya kulevya. Wote walikuwa wakikabiliwa na maradhi ya ajabu yaliyoambatana na maumivu makali ya kifua, maradhi ya ngozi, kupungua uzito na kukonda sana.
Kwa upande wa Tanzania, mgonjwa wa kwanza alithibitika Tanzania Bara katika mwaka 1983 na Zanzibar wagonjwa watatu wa mwanzo waligundulika mwaka wa 1986 katika Hospitali kuu ya Mnazi mmoja. Siku ya tarehe 1 Disemba ilichaguliwa kuwa Siku ya ukimwi kufuatia Tamko la Mkutano wa Mawaziri wa Afya kuhusu Ukimwi uliofanyika mwaka 1988. Kwa sababu siku hiyo (1 Disemba) ndiyo siku iliyogundulika kirusi cha ugonjwa huo. Inakadiriwa kwamba karibu watu14,000 huambukizwa ukimwi kila siku. Sehemu mbili kati ya tatu ya wenye ukimwi duniani wanaishi katika Bara la Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara. Asilimia 95% ya maambukizi yanatokea katika nchi changa zenye pato la wastani. Na zaidi maradhi haya yanaathiri wenye umri baina ya miaka 15- 49 ambao ndio nguvu kazi muhimu kwa ustawi wa wanaadamu.
Qadhia ya ‘mapambano dhidi ya ukimwi’ imekuzwa kiasi kikubwa na ‘kupigiwa debe’ sana. Pamoja na ukweli kwamba siyo maradhi pekee yanayoangamiza maisha. Kumeundwa kamati za ukimwi kila nchi na vitengo vyake kuanzia sehemu za kazi, maskulini, vyuoni katika shehia, kata, wilaya, mkoa, kiwango cha taifa nk. Umoja wa Mataifa nao umeunda taasisi maalum ya kushughulikia suala la ukimwi.
Aidha, katika nchi mbalimbali duniani kama si zote zimeundwa Tume maalum katika kiwango cha Taifa kwa lengo la kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukimwi. Maradhi haya yamefikia kiwango cha kupachikwa ‘lakabu’ ya janga la kitaifa na kimataifa, na jitihada kubwa hufanywa usiku na mchana kuhamasisha kila mtu katika jamii kujihusisha kikamilifu na mapambano dhidi ya maradhi haya.
Kwa hakika mfumo wa kidemokrasia umefanikiwa kuidandia na kuitumia vyema ajenda ya mapambano dhidi ya ukimwi katika kufikia malengo ya kimfumo. Malengo ya kuutangaza mfumo wao kuulinda na kupambana na mfumo mwengine. Kwa upande wa kujitangaza, wanademokrasia kiurahisi sana kwa kupitia kampeni dhidi ya ukimwi wameweza kufikisha thaqafa/mila yao chafu kwa umma wa kiislamu na wanaadamu kwa jumla.Thaqafa inayotokamana na fikra zao za ‘uhuru’ (freedoms), kwa kusambaza uchafu wa zinaa kiurahisi kwa mbinu ya kusambaza mipira ya kondomu na kuhamasisha magoma na miziki ati uhamasishaji dhidi ya ukimwi. Wamefanikiwa pia kiasi fulani kuwatia shaka Waislamu katika aqeeda yao kwa kuwaeleza ati dawa (ARVs) zinarefusha maisha nk. Wanayaeneza haya dhidi ya Uislamu zaidi, kwa sababu Uislamu pekee ndio unaogongana na fikra zao na vitendo vyao vichafu. Fikra hizi za hatari zinapenyezwa kwa watoto wa umma wa kiislamu maskulini, vyuoni nk. kwa kisingizio cha ‘kinga ya ukimwi’. Upande wa pili katika kutangaza mfumo wao wakituonesha kiujanja namna wanavyosimama kidete katika kutatua matatizo ya wanaadamu.
Mbinu hii ni kujikuza na kuukweza mfumo wao na pia kujificha ‘gongo wazi’ juu ya kushindwa dhahir shahir kwa mfumo wao huo wa kikafiri. Kwa upande wa mapambano yao dhidi ya mfumo mwengine ambao kwa leo ni Uislamu pekee, wamefanikiwa kiasi fulani kuondoa fikra ya msingi ya kiislamu kwa kuwafanya Waislamu kutoyaangalia matatizo ‘kimfumo’. (kwa upana) Kampeni yao hii ya kupambana na ukimwi wanaikusudia kuwafanya Waislamu kutoangalia suluhisho la tatizo husika kwa mujibu wa Uislamu kimsingi kama mfumo kamili. Na kwa hivyo hubakia baadhi ya Waislamu kupambana na tatizo hili binafsi, na kuifanya dini ya Uislamu ni dini ya suluhisho la ‘kiakhlaq’ tu kama dini nyengine. Badala ya kupambana na mfumo wa kidemokrasia ambao ndio unaozalisha tatizo hili la ukimwi na mengineyo, wameburuzwa kupambana na tatizo moja moja. Pili, katika mapambano haya wanademokrasia kiujanja huwaburuza baadhi ya Waislamu kuwa askari wa kukodiwa kwa kuwabebesha kauli mbiu zao na fikra zao hatari za kikafiri. Mapambano dhidi ya ukimwi yanaendeshwa bila ya kukhalifu tembe ya fikra za kidemokrasia. Kwa maneno mengine kampeni hii inaendeshwa chini ya usimamizi thabiti wa kanuni za ‘Haki za Binaadamu’. Kwa hivyo mwenye kushirikiana nao hapana shaka yoyote atabebeshwa fikra hizo zinazoongoza mapambano hayo.Na ndio maana Sera ya Ukimwi Zanzibar’ na sera za sehemu nyengine zote zimeweka wazi kwamba zinashikamana na ‘Tamko la Haki za Binaadamu’ na Maazimio mengine mbalimbali.
Kwa hivyo, wanaobeba bango la mapambano ya ukimwi lazima waende sanjari na fikra hizo. Maskini! Waislamu wanaojiingiza katika mchakato huu na wengine hata kudiriki kuunda jumuiya za kupambana na ukimwi chini ya usimamizi wa makafiri huwa wanapanda farasi wasiyemjua anakotoka wala anakokwenda. Msiba mkubwa! Bila ya kutaja malengo ya mfumo huu katika uchumi na ‘maslahi’ ambacho ndicho kipimo cha mfumo wao. Hayo hudhihirika kwa kuuza dawa zao za ARVs kwa wingi na kutengeneza mamilioni ya mipira ya kondom kwa ajili ya biashara. Yote hayo wanayafikia kwa kisingizio cha kupambana na ukimwi, ati ‘janga la taifa’ na ‘kimataifa’.
Hapana shaka kwamba ukimwi ni tatizo, lakini ni tatizo tawi lililozaliwa kutokana na tatizo msingi. Nao ni mfumo muovu wa kidemokrasia. Ukiondoshwa mfumo huu tatizo hili litadhibitiwa. Hivyo ni wazi wagonjwa waliopo wnastahiki matibabu na matunzo, na wasiojimudu kwa kufariki kwa mawalii wao wapewe msaada unaostahitahiki. Hata hivyo, mfumo wa kidemokrasia kimaumbile hauna uwezo wa kuyafanya hayo kikamilifu kwa sababu zifuatazo:
Kwanza, ni mfumo wa ‘kimaslahi’ usiokuwa na fungamano la vitendo na maisha yajayo (akhera).
Pili, hauna fikra ya thamani ya kumuongoza na kumtuliza mwanaadamu aliyesibiwa na majanga. Hii ni kwa sababu suala la kumtuliza mwanaadamu aliyesibiwa na majanga lina mahusiano na fungamano baina ya mwanaadamu na Mola wake. Kwa kuwamiongoni mwa sifa za Allah Ta’ala, ni Mwenye kuleta alitakalo na kumsibu amtakae (qadhaa).
Tatu, fikra za ‘uhuru’(freedoms) ambazo ndizo nguzo za mfumo wa kidemokrasia na muongozo katika mapambano dhidi ya ukimwi ndicho kiwanda kikubwa cha kuzalishia vichochezi vinavyopelekea kuongezeka na kukuwa kwa janga hili. Chini ya fikra ya uhuru binafsi (personal freedom) kunahamasishwa kila aina ya uovu na uchafu kama zinaa, usagajii, liwati, nk. Yote haya ni katika haki za msingi kwa wanademokrasia na si ‘dhambi’. Ndio maana hata aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo, Vijana na Jinsia wa Tanzania Dr. Incy Nkya alikutana rasmi na mashoga mwaka 2009 kupanga mikakati ya kupambana na ukimwi, na alisema:
‘Hatuwezi kiudhati kukabiliana na Ukimwi bila ya kuwa na maongezi na makahaba na mabaradhuli,tutashinda vita hii tu ikiwa tutaungana na si zaidi ya hivyo’ (The Weekend African 29-30 Sept. 2009)
Aidha, katika mapambano haya kuna mkakati unaoitwa ‘ABC’ wakimaanisha ‘jizuilie’ (Abstinence), ‘kuwa muaminifu’ (Be faithful) au ‘tumia kondom’. (Use condom). Vipi mtu atajizuilia wakati katika mfumo wa kidemokrasia ngono ni miongoni mwa haki za msingi kwa mwanaadamu, na yuko huru kufanya tendo hilo na anayemtaka? Na vipi mtu awe muaminifu wakati ‘uaminifu’ unafungamana na malipo na maisha yajayo (akhera), kitu ambacho mfumo wa kidemokrasia hauyatambui? Ukweli pekee wanawataka watu watumie kondom.
Fikra za mfumo wa kidemokrasia na dhana ya ‘mapambano ya ukimwi’ ni vitu vinavyogongana wazi wazi na kuyafanya mapambano haya ni mapambano ya ‘kisanii’, kwa kila mwenye macho. Mapambano ya kweli dhidi ya janga hili na mengineyo yatawezekana na mfumo wa Kiislamu chini ya dola yake ya Khilafah Rashidah. Huu si mfumo wa kisanii kama wa kidemokrasia wenye majigambo na kuwadanganya wenye fikra duni. Amesema kweli Ta’ala alipowafedhehi makafiri :
وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَعْمَالُهُمْ كَسَرَابٍ بِقِيعَةٍ يَحْسَبُهُ الظَّمْآنُ مَاءً حَتَّى إِذَا جَاءَهُ لَمْ يَجِدْهُ شَيْئًا
Na waliokufuru matendo yao ni kama sarabi (mazigazi / mirage) uwandani. Mwenye kiu huyadhania kuwa ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote’….. (TMQ 24: 39)
Kutoka Jarida la Khilafah No.19 Muharram 1433 AH / Disemba 211 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.