Zaka ya Washirika katika Mbuzi
بسم الله الرحمن الرحيم
Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir “Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa Facebook wa “Kifiqhi”
Jibu la Swali
Zaka ya Washirika katika Mbuzi
Kwa: Baher Saleh
(Imetafsiriwa)
Swali:
Nimeona katika Jibu la Swali aliloulizwa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kuhusiana na zaka ya pesa za kushirikiana, kwamba hukmu inatafautiana na yaliyokuja katika kitabu cha “Mali katika Dola ya Khilafah” kuhusu zaka ya washirika wa mbuzi. Ambapo katika kitabu cha Al-Amwaal imekuja maneno yafuatayo:
Hukmu ya Washirika katika Mbuzi
“Kushirkiana au kuchanganya mbuzi wanaolisha kunafanya mali za washirika kuwa kana kwamba ni mali ya mtu mmoja katika utoaji zaka. Sawa iwe ni uchanganyaji “a-yaan”: ambapo wanashirikiana hao mbuzi kati yao, kila mmoja akiwa na fungu lake maalum ila lisilotofauti. Kwa mfano: wawe wamerithi fungu, au wamenunua kwa kushrikiana, au wamepewa zawadi, wakabakisha kama ilivyo bila ya kugawanya. Ni sawa iwe ni hivyo ama iwe ni uchanganyaji wa “sifa”: ambapo kila mshirika ana mali zake binafsi halafu wakazichanganya na kushirikiana. Ima wakiwa sawa katika ushirika ama wazidiane katika ulishaji, malisho, fahali, na mahali pa kunywesha wanyama. Kwa hakika, mbuzi wa ushirika au uchanganyaji wanahisabiwa -vyovyote watakavyokuwa wengi washirika au wachanganyaji, pia haijalishi viwango vyao – wakati wa kuchukua zaka hao mbuzi watahesabiwa kana kwamba ni wa mtu mmoja, zitapigwa hesabu moja tu, na watabaki kama walivyo bila kugawanywa au kuchanganywa. Wakiwa wamefika arobaini basi mtoaji zaka atatoa mbuzi mmoja tu. na wakifika mia na ishirini na moja: watatoa mbuzi wawili. Na wakifika mbuzi mia mbili na mmoja, watatoa mbuzi watatu. Na wakifika mia nne basi watatoa mbuzi wanne. Na zaka inayochukuliwa itagawanywa kwa idadi ya washirika au wachanganyaji kulingana na hisa zao kwenye mbuzi. Na aliye na fungu dogo atarudia walio na mafungu makubwa kwa fungu lake. Kwa neno lake Mtume (saw):
«وما كان من خليطين فإنهما يتراجعان بينهما بالسوية» رواه أبو داود
“Ikiwa mali ni shirika nusu kwa nusu baina ya washirika, basi wanapaswa kulipa zaka ya pamoja na watazingatiwa kuwa wote wamelipa Zaka sawa kwa sawa …” Imepokewa na Abu Dawud
Hivyo, je angalizo langu liko mahala pake ama kuna jambo sijalifahamu?
Kwa maana nyengine, je yaliyokuja katika hicho kitabu cha “Mali katika Dola ya Khilafah” kuhusiana na hukmu ya washirika kwenye mbuzi yanahusu tu zaka ya mbuzi, tofauti na aina zengine za zaka? Kwa sababu, nilikuwa kabla nimefahamu kuwa suala linahusiana na sifa ya ushirika na uchanganyaji unaopatikana kwenye huo ushirika, na wala sio kuwa yahusiana na mbuzi peke yake.
Mwenyezi Mungu awabariki na awahifadhi kwa hifdhi yake in shaa allah na atukutanishe sote katika utawala wa Khilafah ongofu hivi karibuni.
Ndugu yenu, Baher Saleh 17/8/2020 M
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakaatuh.
Bila shaka wakusudia jibu la swali ambalo tulilitoa tarehe 19 Dhul Hijjah 1441H sawia na 9/8/2020 M kwa anuwani “Zaka ya Pesa za Ushirika” na mukhtasari wake ni kwamba, ushirika katika pesa hauna athari yoyote kwenye zaka. Bali kila mmoja katika washirika atajitolea mwenyewe ikiwa mali yake itafikia kiwango, na ikazungukiwa na mwaka, kulingana na hukmu za kisheria zinazohusiana nazo… na umenukuu kutoka katika kitabu cha “Mali katika Dola ya Khilafah” ambapo kwa kifupi chasema kwamba, ushirika na uchanganyaji kwenye mbuzi una athari katika zaka ya mbuzi. Na waulizia ikiwa hii hukmu yakusanya pesa pia? Kinyume na yaliyokuja kwenye jibu letu liloashiriwa, ama ni inahusu mbuzi tu?
Na jibu ni kama ifauatavyo:
1- Bila shaka, zaka kimsingi ni ibada ya kibinafsi inayohusiana na mali binafsi. Na hilo ni kwa kuwa dalili za zaka zimekuja kuelekezwa kwa mwenye mali, pindi mali yake inapofikia kiwango na kuzungukiwa na mwaka. Yaani… ni kwamba, hukmu ya zaka inahusiana na mali ya kibinafsi peke yake, wala haikufungamana na mali za mwengine pamoja naye. Na miongoni mwa hizo dalili ni:
- Imekuja katika Hadith ndefu iliyopokewa na Muslim kutoka kwa Zaid bin Aslam, kwamba Abu Swaleh Dhakwan alimhadithia kuwa alimsikia Abu Huraira (r.a) akisema: amesema Mtume (saw):
»مَا مِنْ صَاحِبِ ذَهَبٍ وَلَا فِضَّةٍ، لَا يُؤَدِّي مِنْهَا حَقَّهَا، إِلَّا إِذَا كَانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ، صُفِّحَتْ لَهُ صَفَائِحُ مِنْ نَارٍ، فَأُحْمِيَ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ …
قِيلَ: يَا رَسُولَ اللهِ، فَالْإِبِلُ؟ قَالَ: «وَلَا صَاحِبُ إِبِلٍ لَا يُؤَدِّي مِنْهَا حَقَّهَا، وَمِنْ حَقِّهَا حَلَبُهَا يَوْمَ وِرْدِهَا، إِلَّا إِذَا كَانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ، بُطِحَ لَهَا بِقَاعٍ قَرْقَرٍ، أَوْفَرَ مَا كَانَتْ، لَا يَفْقِدُ مِنْهَا فَصِيلًا وَاحِدًا، تَطَؤُهُ بِأَخْفَافِهَا وَتَعَضُّهُ بِأَفْوَاهِهَا، كُلَّمَا مَرَّ عَلَيْهِ أُولَاهَا رُدَّ عَلَيْهِ أُخْرَاهَا….
قِيلَ: يَا رَسُولَ اللهِ، فَالْبَقَرُ وَالْغَنَمُ؟ قَالَ: «وَلَا صَاحِبُ بَقَرٍ، وَلَا غَنَمٍ، لَا يُؤَدِّي مِنْهَا حَقَّهَا، إِلَّا إِذَا كَانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ بُطِحَ لَهَا بِقَاعٍ قَرْقَرٍ، لَا يَفْقِدُ مِنْهَا شَيْئًا، لَيْسَ فِيهَا عَقْصَاءُ، وَلَا جَلْحَاءُ، وَلَا عَضْبَاءُ تَنْطَحُهُ بِقُرُونِهَا وَتَطَؤُهُ بِأَظْلَافِهَا، كُلَّمَا مَرَّ عَلَيْهِ أُولَاهَا رُدَّ عَلَيْهِ أُخْرَاهَا..«…
“Hakuna yeyote mwenye dhahabu wala fedha na akawa haitolei haki yake, isipokuwa siku ya Kiyama atatandikiwa matandiko ya moto na kuteketezwa katika moto wa Jahannam… Kukaulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je mwenye ngamia? Akasema: Hakuna yeyote mwenye ngamia asiyewatolea haki yao -na miongoni mwa haki yao ni kuwakamua siku ya kwenda kunyweshwa maji – isipokuwa siku ya Kiyama atawekwa chini kwenye ardhi pana na tambarare, halafu ngamia wote watamkanyaga na kwato zao na kumng`ata kwa meno yao, kila akikanyagwa na wa mwisho huanza kukanyagwa tena na wa mwanzo wao
Kukaulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je mwenye ng`ombe na mbuzi vipi? Akasema: Hakuna yeyote mwenye ng`ombe wala mbuzi na akawa hawatolei haki yake isipokuwa siku ya Kiyama atawekwa chini kwenye ardhi pana na tambarare, halafu wote bila kukosekana hata mmoja, walio na pembe zilizojikunja, wasio na pembe, waliovunjika pembe, wote watamdunga na kumkanyaga kwa kwato zao. Kila akikanyagwa/kudungwa na wa mwisho huanza tena wa mwanzo wao …”
– Amepokea Bukhari kutoka kwa Ibn Abbas (ra) kwamba Mtume (saw) alimtuma Muadh kwenda Yemen, akamwambia:
«فَأَعْلِمْهُمْ أَنَّ اللَّهَ افْتَرَضَ عَلَيْهِمْ صَدَقَةً فِي أَمْوَالِهِمْ تُؤْخَذُ مِنْ أَغْنِيَائِهِمْ وَتُرَدُّ عَلَى فُقَرَائِهِمْ»
“… basi wajulishe kwamba Mwenyezi Mungu amewalazimishia zaka itakayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kurudishwa kwa mafukara wao”
– Imepokewa pia kutoka kwa Ali ibn Abi Twalib, akipokea kutoka kwa Mtume (saw) amesema:
»فَإِذَا كَانَتْ لَكَ مِائَتَا دِرْهَمٍ، وَحَالَ عَلَيْهَا الْحَوْلُ، فَفِيهَا خَمْسَةُ دَرَاهِمَ، وَلَيْسَ عَلَيْكَ شَيْءٌ – يَعْنِي – فِي الذَّهَبِ حَتَّى يَكُونَ لَكَ عِشْرُونَ دِينَارًا، فَإِذَا كَانَ لَكَ عِشْرُونَ دِينَارًا، وَحَالَ عَلَيْهَا الْحَوْلُ، فَفِيهَا نِصْفُ دِينَارٍ… «
“Ukiwa na dirham mia mbili, na zikazungukiwa na mwaka, basi utapaswa kutoa dirham tano. Na hakuna chochote juu yako – yaani katika dhahabu – hadi pale utakapokuwa na dinar ishirini. Na utakapokuwa na hizo dinar ishirini na zikazungukiwa na mwaka, basi utapaswa kutoa nusu dinar” (imepokewa na Abu Dawud)
Ni wazi kutokana na matamshi yaliyotumiwa kwenye hizi Hadith tukufu kwamba hukmu ya zaka inahusiana na mali ya kibinafsi wala haihusiani na mali yoyote tu. Yaani, zaka inahusu mali anayomiliki mtu binafsi mwenyewe, na wala haihusiani na mali inayomilikiwa na mwengine:
«مَا مِنْ صَاحِبِ ذَهَبٍ وَلَا فِضَّةٍ… وَلَا صَاحِبُ إِبِلٍ… وَلَا صَاحِبُ بَقَرٍ وَلَا غَنَمٍ…»،
«…فَأَعْلِمْهُمْ أَنَّ اللَّهَ افْتَرَضَ عَلَيْهِمْ صَدَقَةً فِي أَمْوَالِهِمْ تُؤْخَذُ مِنْ أَغْنِيَائِهِمْ وَتُرَدُّ عَلَى فُقَرَائِهِمْ»،
«… فَإِذَا كَانَتْ لَكَ مِائَتَا دِرْهَمٍ… وَلَيْسَ عَلَيْكَ شَيْءٌ يَعْنِي فِي الذَّهَبِ حَتَّى يَكُونَ لَكَ عِشْرُونَ دِينَاراً فَإِذَا كَانَ لَكَ عِشْرُونَ دِينَاراً…»
“Hakuna yeyote mwenye dhahabu wala fedha… hakuna yeyote mwenye ng`ombe wala mbuzi…” “basi wajulishe kwamba Mwenyezi Mungu amewalazimishia zaka itakayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kurudishwa kwa mafukara wao …” “Ukiwa na dirham mia mbili…. hakuna chochote juu yako – yaani katika dhahabu – hadi pale utakapokuwa ni dinar ishirini…”
Kwa hiyo, haitahesabiwa kwenye zaka mali inayomilikiwa na mtoto kwenye mali inayomilikiwa na baba wala kinyume chake. Wala mali inayomilikwa na mume haitahesabiwa kwa mali anayomiliki mke, wala kinyume chake… mpaka mwisho. Bali hesabu itakuwa kwa mali anayomiliki mtu binafsi bila kuchanganya na mali inayomilikiwa na wengine. Hivyo, kama atakuwa na mali iliyofikia kiwango na ikazungukiwa na mwaka basi atapaswa kuitolea zaka.
2- Hakitoki kitu kwenye msingi huu uliotangulia kutajwa huko juu kuhusiana na mali za zaka isipokuwa kwa dalili inayojulisha kuvuliwa kwake kutoka katika huu msingi. Na bila shaka, imekuja dalili kutokana na hadith za Mtume (saw) ikivua hukmu ya mbuzi, ikafanya zaka wakiwa ni wa ushirika ama wamechanganywa, na hivyo kufanywa kuwa ni kama mali ya mtu mmoja hata kama washirika/wachanganyaji watakuwa wengi itawajibika kutoa zaka ikiwa kwa ujumla wamefika kiwango, ingawa fungu la kila mmoja wao kibinafsi wakitawanywa haifiki kiwango cha zaka…
Na bila shaka, tumebainisha wazi kwenye kitabu cha “Mali katika Dola ya Khilafah” ufafanuzi wa hukmu za kisheria kuhusu mbuzi waliochanganywa, na maana ya kuchanganya katika mlango wa “hukmu za washirika kwenye mbuzi” kama ifuatavyo:
[kushirikiana au kuchanganya mbuzi wanaolisha kunafanya mali za washirika kuwa kana kwamba ni mali ya mtu mmoja katika utoaji zaka. Ni sawa iwe ni uchanganyaji “a-yaan”: ambao ni wao kushirikiana hao mbuzi kati yao, kila mmoja akiwa fungu lake maalum ila lisilotofauti. Kwa mfano: wawe wamerithi fungu, au wamenunua kwa kushrikiana, au wamepewa zawadi, wakabakisha kama ilivyo bila ya kugawanya. Ni sawa iwe ni hivyo ama iwe ni uchanganyaji wa “sifa”: ambapo kila mshirika ana mali zake binafsi halafu wakazichanganya na kushirikiana. Ni sawa wakiwa sawa katika ushirika ama wazidiane. Katika ulishaji, malisho, fahali, na mahali pa kunywesha wanyama. Kwa hakika, mbuzi wa ushirika au uchanganyaji wanahisabiwa – vyovyote watakavyokuwa wengi washirika au wachanganyaji, pia haijalishi viwango vyao – wakati wa kuchukua zaka hao mbuzi watahesabiwa kana kwamba ni wa mtu mmoja, zitapigwa hesabu moja tu, na watabaki kama walivyo bila kugawanywa au kuchanganywa. Wakiwa wamefika arubaini basi mtoaji zaka atatoa mbuzi mmoja tu. Na wakifika mia na ishirini na moja: watatoa mbuzi wawili. Na wakifika mbuzi mia mbili na mmoja, watatoa mbuzi watatu. Na wakifika mia nne basi watatoa mbuzi wanne.
Na zaka inayochukuliwa itagawanywa kwa idadi ya washirika au wachanganyaji kulingana na hisa zao kwenye mbuzi. Na aliye na fungu dogo atarudia walio na mafungu makubwa kwa fungu lake. Kwa neno lake Mtume (saw):
« وما كان من خليطين فإنهما يتراجعان بينهما بالسوية» (رواه أبو داود)
“Ikiwa mali ni shirika nusu kwa nusu baina ya washirika, basi wanapaswa kulipa zaka ya pamoja na watazingatiwa kuwa wote wamelipa Zaka sawa kwa sawa …” Imepokewa na Abu Dawud
Na mchukuaji zaka atawabakisha mbuzi kama walivyo, na atapiga hesabu kama walivyo, wala haifai kuwatenganisha ili achukue zaidi. Kwa mfano: wakiwa washirika/wachanganyaji watatu wanamiliki mbuzi mia na ishirini kwa jumla, kila mmoja wao anamiliki mbuzi arubaini. Sasa mchukuaji zaka akaamua kuwatenganisha ili apate mbuzi watatu hapo, akichukua mbuzi mmoja kutoka kwa kila mshirika! Hilo halitofaa kwake. Anapaswa awaache kama walivyo na achukue mbuzi mmoja tu kutoka kwao. Kama ambavyo pia haifai kwa hao wenye mbuzi kuwatawanya mbuzi anapofika mchukuaji zaka kwa lengo la kupunguza zaka yao, au ili wasiwatolee zaka. Kwa mfano: washirika/wachanganyaji wakiwa na mbuzi mia moja na mmoja, wakawatawanya ili watoe mbuzi wawili badala ya mbuzi watatu lau wangebaki pamoja kama walivyokuwa. Au mfano: wawe wanamilki mbuzi arubaini, halafu wakawagawanya ili wasitoe chochote baada ya kuwatenganisha!.
Na kama ambavyo haifai kuwatenganisha mbuzi walio pamoja, kadhalika haifai kuwakusanya mbuzi waliotengana, kwa lengo la kupunguza kinachotolewa. Hilo ni kwa mfano: watu wawili wawe na mbuzi thamanini, kila mmoja wao awe na mbuzi arubaini kivyake bila ya kuchanganya/kushirikiana. Kisha anapokuja mkusanyaji zaka wakawachanganya hao mbuzi ili wasitoe ila mbuzi mmoja tu badala ya kila mmoja wao kutoa mbuzi mmoja! na dalili ya kutofaa kuwatawanya mbuzi walio pamoja wala kuwachanganya walio mbali mbali, ni Hadith iliyopokewa na Saad bin Abi Waqas akisema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):
«لا يفرق بين مجتمع، ولا يجمع بين متفرق، في الصدقة. والخليطان ما اجتمعا على الفحل، والمرعى، والحوض»
“Katika zaka hawakusanywi walio mbali mbali, na wala hawatawanywi walio pamoja, na wachanganyaji: ni waliochangia fahali, malisho, na manywesho.” Na katika mapokezi mengine: “na (al-Ra’yi) mchungaji”. (imepokewa na Abu Ubaid)] mwisho wa nukuu kutoka kwenye kitabu cha “Mali katika Dola ya Khilafah”.
3- Na wanyama wengine wote ambao hulazimu kutolewa zaka watakutanishwa na mbuzi katika hii hukmu. kama vile ngamia na ng`ombe, watakapokuwa ni wa shirika au wamechanganywa, kwa namna ambayo wataamiliwa kama inavyoamiliwa mali ya mtu mmoja, hata kama washirika/wachanganyaji ni wengi. Zaka itapasa pindi watakapofikia kiwango kwa ujumla wake, ingawa fungu la kila mshirika/mchanganyaji halijakamilisha kiwango, au wote wakiwa mbali mbali au wakitengana. Na dalili ya hayo ni hiyo Hadith iliyotajwa huko juu, kwa sababu ndani yake kuna maana ya uchanganyaji “Khaleet”,
والخليطان ما اجتمعا على الفحل، والمرعى، والحوض»
“Na wachanganyaji: ni waliochangia fahali, malisho, na manywesho.” na katika mapokezi mengine: “na mchungaji” na hii yaweza kuwa “illah” ya kujulisha. Kwa kuwa ni “sifa inayofahamisha” kwa hiyo itawahusu ng`ombe na ngamia na sio mbuzi tu, kwa sababu imetimia hii “illah”. Ukiongezea na kuwa tamshi lake linaenea kila kinachotawanywa au kukusanywa kukaathiri kwenye zaka:
«…وَلَا يُجْمَعُ بَيْنَ مُفْتَرِقٍ وَلَا يُفَرَّقُ بَيْنَ مُجْتَمِعٍ خَشْيَةَ الصَّدَقَةِ…»
“Katika zaka hawakusanywi walio mbali mbali, na wala hawatawanywi walio pamoja…” na ngamia na ng`ombe ukusanyaji wao au utawanyaji wao pia huathiri kwenye zaka, kwa kuzidisha au kupunguza.
4- Ama mali zengine za zaka kama vile pesa, mazao, na biashara, hizi hakuna dalili ya nguvu kwetu iliyokuja kuzivua kutoka kwenye huo msingi. Kwa hiyo bila shaka – mbali na wanyama – mali zengine zote zaka zitabaki kwenye hukmu ya asili kama ilivyobainishwa katika kipengee cha (1).
Na hii ndio rai ya wanazuoni wengi, kama ilivyokuja katika kitabu cha “Al-Mughni” cha Ibn Qudama Al-Maqdisi:
[(mas-ala: wamechanganya visivyokuwa kuwa wanyama, kama vile dhahabu, fedha, vitu vya biashara, na matunda na mazao)
[1736) Mas-ala: amesema: “Na ikiwa watachanganya visivyokuwa hivi, atachukua kutoka kwa kila mmoja wao kivyake, ikiwa kinachomhusu kinapaswa kutolewa zaka) na maana yake: ni kwamba, wakichanganya visivyokuwa wanyama, kama vile dhahabu, fedha, vitu vya biashara, na matunda na mazao, basi kuchanganya kwao hakutoathiri kitu. Na itakuwa hukmu yao ni kama hukmu ya mtu pweke, na hii ndio kauli ya wanazuoni wengi. Na kuna mapokezi mengine kutoka kwa Ahmad, kwamba “Shirika aina ya `yaan” huathiri kwenye visivyokuwa wanyama. Hivyo, kama watakuwa na kiwango wanachoshirikiana basi watapaswa kutoa zaka… na usawa ni kwamba, uchanganyaji hauathiri kwenye vitu visivyokuwa wanyama, kutokana na kauli ya Mtume (saw): “ وَالْخَلِيطَانِ: مَا اجْتَمَعَ عَلَى الْفَحْلِ وَالْمَرْعَى وَالْحَوْضِna wachanganyaji: ni waliochangia fahali, malisho, na manywesho.” hii kauli ikajulisha kwamba, vitu ambavyo hayo hayatapatikana ndani yake basi hautakuwa uchanganyaji unaoathiri. Na kauli yake Mtume (saw):
«لَا يُجْمَعُ بَيْنَ مُتَفَرِّقٍ، خَشْيَةَ الصَّدَقَةِ»
“Katika zaka hawakusanywi walio mbali mbali, na wala hawatawanywi walio pamoja…” yahusu wanyama tu, kwa sababu wao ndio ambao mara zaka hupungua kwa kukusanywa kwao na mara nyengine kuzidi. Ama mali zengine zilobakia huwa zaka hulazimu katika kinachozidi kiwango kulingana na hesabu yake, kwa hiyo hakuna athari kwa kuchanganywa kwake…”].
5- Kutokana na ufafanuzi huo yadhihirika wazi kwamba, hakuna tofauti wala mgongano kati ya maneno yaliyokuja kwenye Jibu la Swali tulilotoa tarehe 19 Dhul Hijjah 1441 H sawia na 9/8/2020 M kwa anwani: “Zaka ya Pesa za Ushirika” na maneno yaliyokuja kwenye kitabu cha “Mali katika Dola ya Khilafah” katika mlango wa “Hukmu ya Washirika katika Mbuzi” kwa sababu, jibu la swali linahusiana na pesa, ama yaliyokuja kwenye kitabu cha “Mali katika Dola ya Khilafah” yanahusiana na mbuzi, na hukmu ya pesa hutafautiana na hukmu ya mbuzi katika suala la uchanganyaji na ushirika.
Natumai hili jibu limetosheleza, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi Zaidi na Mwenye hekima zaidi.
Ndugu Yenu
Ata Bin Khalil Abu Rashtah
19 Rabi’ al-Akhir 1442 H
Sawia na 4/12/2020 M
Link ya jibu hili kwenye ukurasa wa Amiri wa Facebook
Maoni hayajaruhusiwa.