Waislamu Na Matayarisho Ya Ramadhani

بسم الله الرحمن الرحيم

Bila ya shaka baada ya siku chache InshaAllah Waislamu tutafikiwa na mgeni mtukufu, yaani mwezi wa Ramadhani. Huu ndio mwezi ulioteremshwa Qur-ani yote kuja katika wingu wa kwanza wa dunia.
Ndani yake kuna usiku mtukufu kuliko miezi alfu, hufunguliwa milango ya pepo, na kufungwa milango ya moto. Aidha, ni mwezi wa toba na maghfira kwa Waislamu. Pia Allah Taala humtia kifungoni Iblis aliyelaaniwa. Ni Ramadani tu ndio amali za Waislamu hulipwa maradufu, na nyoyo za Waumini hulainika kwa kupanda juu kwa ucha-Mungu, ukarimu na mapenzi baina yao.
Kwa yote hayo, jee Waumini wana maandalizi yeyote kwa ajili ya mwezi huu mtukufu? Bila shaka Waislamu hawako nyuma katika kujiandaa na Ramadhani katika mambo mbalimbali kama futari, kutafuta nguo za sikukuu, kushiriki mijadala (japo haina tija) juu ya muandamo wa mwezi nk.
Ramadhani inahitaji matayarisho mapana zaidi kwa kila Muislamu mbali na hayo yaliyozoeleka.
Kwanza kabisa, ni kumuomba Allah SW atufikishe kuidiriki Ramadhani, kwani wema waliotangulia (maswahaba) walikuwa ikimaliza tu Ramadhani wakimuomba Allah SW awakubalie funga na ibada zao. Na ukianza tu mfunguo saba walikuwa wakimuomba Allah Taala awafikishe waudiriki mwezi huo wakiwa na afya njema ili wanufaike na manufaa makubwa ambayo hayapatikani katika miezi iliyobakia.
Pili, jambo jingine ni kuhakikisha Waislamu tunaongeza maarifa kuhusu ibada ya Swaum. Yaani tujue mambo yanayobatilisha swaumu, kusihi kwake, dalili zake nk. Ili mfungaji awe na uhakika kielimu na anachokitenda. Na kama Muislamu hujui basi ni lazima ajiegemeze kwa mwanazuoni Mujtahid ili iwe hujjah kwake kuwa katekeleza ibada hiyo kwa elimu. Allah SWT anatukataza kutekeleza jambo tusilo na elimu nalo.
Tatu, Waislamu katika kipindi hiki wanapaswa kujiandaa kwa kujitakasa na madhambi kwa kuhakikisha hawazidhulumu nafsi zao kwa kufanya maovu na badala yake wanaziokoa nafsi zao kwa kuhakikisha kumridhisha Allah Taala pekee kwa kuheshimu matukufu yake. Allah SW anasema:
إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِنْدَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنْفُسَكُمْ (التوبة: 36).
” Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah SW ni kumi na mbili katika hukmu ya Allah tokea kuumbwa kwa mbingu na ardhi, katika hiyo imo minne mitukufu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu ndani ya miezi hiyo…..” (TMQ 9:36)
Na kwa upande wa Ramadhan ni bora zaidi kujiepusha (min baabu awla), kwa kuwa ni mwezi uliopata utukufu mkubwa zaidi kuliko miezi hii. Una usiku mmoja mtukufu kupindukia maelfu ya siku ya miezi hiyo.
Nne, maandalizi ya kifikra kabla ya kuingia Ramadhani, nayo ni kwa kuweka azma ya kweli ya kuifunga Ramadhani yote kwa ikhlasi na unyenyekevu. Huku tukijiweka mbali na shubha zote. Pia tujiepushe kuibeba Ramadhani kama jela au kero fulani. Pia tujiepiushe kufunga tu ilimuradi watu watuone, au kuogopa kusemwa vibaya ndani ya jamii. Mtume SAAW anatufundisha kuwa vitendo vitalipwa kwa kuzingatia nia ya mtendaji.
Tano, kujitayarisha kunahusisha pia kuanza kujizoesha kufanya ibada mbalimbali ili isije kuwa na ugumu kuzitenda ibada hizo itakapoanza Ramadhani. Ni vyema kuanza kufanya baadhi ya ibada kama qiyamul-layli, kusoma qur-ni kwa kuuzoesha ulimi, kufanya dhikri mbalimbali, kutoa sadaka nk.
Bibi Aisha ra. anasimulia kuwa Mtume SAAW alikuwa akifunga zaidi mwezi wa Sha’abani mpaka unadhania hafungui ataunganisha na Ramadhani…” . Sasa kwetu ni vizuri kuiga mwendo huo mzuri, kama ni matayarisho kwa ibada hii hasa, na nyenginezo.
Kwa kumalizia, kwa kuwa Ramadhani ndio mwezi ulioshuka Qur-ani, ni wajibu kwa Waislamu kujitayarisha kuutekeleza Uislamu wote kijumla. Na hasa yaliyo ya faradhi, kwani Allah SWT amewajibisha tuufuate Uislamu wote. Na kwa kuwa hili kwa leo haliwezekani kwa kuwa hatutawaliwi na Uislamu, basi ni wajibu Waislamu waweke maandalizi ya kubeba daawa ili kuutawalisha Uislamu katika kila kipengee cha maisha. Na kwa kuwa kipindi cha Ramadhani uchaji wa Waislamu unaongezeka na nyoyo zao hulainika na kuwa wasikivu, basi ni fursa adhimu kuwafikishia ulinganizi ili tushirikiane nao bega kwa bega kufanya kazi ya kuutawalisha Uislamu kupitia dola ya Kiislamu ya Khilafah na kuung’oa ukafiri na matawi yake yote.
Imeandikwa na Ali Amour
Mjumbe wa Afisi ya Habari- Hizb ut Tahrir Tanzania
Risala ya Wiki No. 152
02 Shaaban 1444 Hijri / 22 Februari 2023 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.