Usanii wa ‘Haki za Binadamu’

Kila tarehe 10 Disemba ni Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Siku kama hiyo mwaka 1948 ndipo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha rasmi (tabanni) nyaraka ya Tamko la Kilimwengu la Haki za Binadamu kwa ajili ya ulimwengu mzima.

Tangu hapo dhana ‘haki za binadamu’ ikaenea na kupigiwa debe kila mahala. Katika makongamano, mikutano na taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa. Kubwa zaidi haki hizi zikaingizwa katika katiba takriban za nchi zote ulimwenguni kwa kupewa vifungu malumu. Vifungu hivyo vinavyochukuliwa kudhamini haki msingi za kibinadamu hujuulikana kwa jina la ‘Bill of rights’. (Vifungu vya haki msingi za binadamu) Hivyo ni vifungu maalum kwenye katiba vinavyokusudiwa ati kudhamini uhuru binafsi, uhuru wa itikadi, uhuru wa umiliki, uhuru wa maoni nk. Pia huhusisha uhuru wa makundi ya watu, haki zao na kuwakinga wasinyimwe haki na kuizuiya dola kuingilia uhuru huo au kupora haki hizo.

Chimbuko la fikra ya ‘haki za binadamu’ ni kutokana na mtazamo wa mfumo wa kibepari juu ya mwanadamu. Mfumo huo humuhisabu mwanadamu kuwa daima ni kiumbe chema kwa sharti tu asiwekewe vikwazo katika kujifaragua na uhuru wake. Mtazamo huu wa kibepari unaotokana na usekula ni wa kimakosa, dhaifu, uliotokamana na akili badala ya wahyi, na kimsingi usiokuwa na mashiko.

Hapana shaka kwamba mtazamo huu ni natija ya mapinduzi makubwa ya kifikra na kisiasa yaliyotokea Ulaya ndani ya karne ya 18 yaliyopelekea kuzaliwa fikra ya kisekula. Yaani fikra ya kutenganisha dini na maisha na kutengwa kanisa kando na mambo ya utawala. Kwa mtazamo huo wanademokrasia waliukhalifu matazamo mkongwe wa kanisa juu ya mwanadamu, na hilo lilitarajiwa kwa kuwa harakati za mapinduzi hayo ya kifikra na hatimae kisiasa ndani ya Ulaya zilikuwa na upinzani dhidi ya kanisa. Imani kongwe ya kanisa ni kuwa mwanadamu ni muovu kwa kuwa ana dhambi ya asili. Mfumo wa kidemokrasia ukaja na mtazamo mpya kwamba mwanadamu atabakia kuwa mwema daima endapo tu hatobanwa uhuru wake.

Mtazamo huu unafafanuliwa vya kutosha katika kitabu cha Hizb ut-Tahrir cha “Kampeni ya Marekani Kuangamiza Uislamu” uk 12.

“Mtazamo wa mfumo huu (ubepari) juu ya hali ya mwanadamu, unamtazama kimaumbile mwanadamu kuwa ni mwema na wala si muovu. Kwa hivyo, uovu wowote unaotendwa na mwanadamu hutokana na kunyimwa kwake kutekeleza matakwa yake. (uhuru wake) Kwa sababu hii warasilimali/mabepari wanalingania kuachwa huru kwa matakwa ya binadamu ili mwanadamu aweze kudhihirisha wema wake wa kimaumbile. Kutokana na mtazamo huu, wazo la “uhuru” likazalikana na ni fikra muhimu kwa mujibu mfumo wa kibepari.”

Uislamu unakosoa mtazamo huu dhaifu wa ubepari juu ya mwanadamu. Na Uislamu ukajiweka mbali na kuchanganyikiwa kwa ukiristo na mfumo wa ubepari katika kumuangalia mwanadamu. Kwa hivyo, Uislamu unaweka wazi mtazamo wake wa kiwahyi kwamba mwanadamu hakuzaliwa na sifa ya wema kama wanavyodai wanademokrasia, wala hana sifa ya uovu kama linavyodai kanisa likifuata falsafa za kizamani zilizojengwa juu ya ufahamu wa mwanadamu kurithi dhambi ya asili ya Adam na Hawa. (As)

Mtazamo sahihi kuhusu maumbile ya mwanadamu ni kwamba mwanadamu ana ghariza [hisia za kimaumbile] na mahitaji ya kibaologia [organic needs]. Kama kula, kunywa, kulala nk. Mahitaji haya yanahitaji yashibishwe, huku mwanadamu akiwa kapatiwa akili na Allah Taala ili kufahamu muongozo wa Muumba wake wa namna ya kushibisha mahitajio hayo. Pia mwanadamu amepewa uwezo wa kuchagua njia gani atatumia kushibisha ghariza zake na mahitajio yake ya kibaologia. Uchaguzi huu sio uhuru, bali ni mtihani kwake.

Kwa hivyo, ikiwa mwanadamu atashibisha mahitajio hayo sawa sawa kwa namna anavyotaka Muumba wake, hapo mwanadamu atakuwa ametenda ‘wema’, lakini lau atashibisha mahitajio hayo kimakosa kwa matamanio yake amma kinyume na maumbile, hapo atakuwa amefanya ‘uovu’.
Kwa hivyo, mwanadamu kimaumbile si mwema wala si muovu, bali yuko tayari kufanya wema amma uovu, na yeye ndiye mwenye kuchagua zuri amma baya kwa khiyari yake.Huu ndio mtazamo sahihi wa Uislamu juu ya mwanadamu. Allah (SWT) Anasema:
{ونفس وما سواها. فألهمها فجورها وتقواها }
“Naapa kwa nafsi (roho) na Yule aliyeitengeneza. Kisha (Yeye) akaifahamisha uovu wake na wema wake” [TMQ 91:7-8]

Licha ya mapungufu ya mtazamo wa ubepari katika kumuangalia mwanadamu ambao ndio uliozalisha fikra ya ‘haki za binadamu’, bado fikra hiyo inalazimishwa kuwa ni ya watu wote (universal) kiasi cha kuasisiwa rasmi Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948 na kusambazwa dunia nzima kama kigezo kwa ulimwengu. Na taasisi za kitaifa, kimajimbo na kieneo nazo kwa kuwa ni wakala tu wa mfumo wa kibepari/kidemokrasia zinaandama nyayo za kuzipigia debe na kuzisambaza fikra hizo kila mahala. Hata kama fikra hizo zinapingana na mila na desturi za walio wengi kama suala la ushoga nk.

Aidha, madola makubwa huzifanya haki za binadamu kuwa ni jukwaa la kudandia kupelekea siasa zao za nje kwa kulazimisha matakwa yao hususan nchi changa. Madola makubwa hudiriki hadi kuwakatia misaada na kuwawekea vikwazo madola dhaifu kwa kisingizio haki za binadamu. Kama tulivyoona awali ilivyotenzwa nguvu nchi ya Malawi ili iwaache huru mashoga waliowafungwa jela . Na kama ilivyoaandamwa Uganda baada ya Raisi Museveni kusaini Sheria ya Kupiga marufuku mashoga.

Kwa upande mwengine, mbali na kuwa fikra ya ‘haki za binadamu’ ni butu katika chimbuko lake. Lakini pia ni uwongo kwa dalili za kiakili, na inadhihirika wazi kuwa ni usanii usiokuwa na uhalisia wowote. Bali zaidi, haki hizi ni kwa ajili ya kuulinda mfumo wa kibepari / kidemokrasia, nidhamu zake na maslahi yao. Na kwa upana wake kiukweli hakuna kitu kinachoitwa ‘uhuru’ katika maisha ya mwanadamu tangu dunia ianze na mpaka itamalizika.

Uislamu kwa kuwa sio dini ya kisanii haitafuni maneno kuhusu jambo hilo, kinyume na ulivyo ubepari namna unavyofanya unafiki wa kutangaza uhuru ilhali ni uhuru wa kulinda mfumo wao kwa mipaka wanayotaka wao.

Mfano mzuri wa kuonesha kuwa dhana ya ‘haki za binadamu’ ni dhana butu ya kimaslahi utaona wakoloni ndani ya Tanganyika wakati wote wa utawala wao hawakutaja fikra ya haki za binadamu katika kuwatawalia watu ndani ya ukoloni wao. Lakini mara walipokusudia kutoa uhuru wa bendera, tahamaki dhana ya haki za binadamu ikawa ajenda ya mstari wa mbele waliyoitaja katika jumba la Lancaster House. Hii ni kwa sababu wakoloniwaliona katika kulinda maslahi, kuhifadhi mali na baadhi ya rasilmali za raia wao watakaobakia katika makoloni ambapo wanakabiliwa na wimbi la harakati za uafrika, lazima haki hizo ziwepo. Na hususan ukizingatia kwamba upande wa usimamizi wa sheria mara baada ya uhuru unabakia kuwa chini ya himaya ya Uingereza moja kwa moja kutokana na kukosekana wanasheria wazalendo wakutosha kushika hatamu za masuala ya kisheria wakati huo.

Kwa hivyo, wakoloni walitaja dhana ya haki za binadamu kwa dhamira ya kimaslahi na sio zaidi. Kwa sababu lau ingalikuwa ni kwa sababu za kibinadamu, kwa nini hawakuweka misingi hiyo kipindi chote cha ukoloni wao. Bali kimsingi kwa haki hizo za binadamu zisingeruhusu kamwe ukoloni wao na zingekuwa tishio kwa maslahi na unyonyaji wa rasilmali katika makoloni yao.

Aidha, Tanganyika chini ya chama kimoja mara baada ya uhuru wa bendera watawala walikataa kuingiza vifungu vya ‘haki za binadamu’ ndani ya katiba. Kwa kisingizio kuwa vifungu hivyo vitaleta migongano baina ya serikali na mahkama. Na katika katiba ya mwaka 1961 pia havikuingizwa. Katika mwaka 1963 Nyerere alipoulizwa kuhusu kuingiza vifungu hivyo alijibu hivi:
“Hiki ni kipindi cha dharura, mpaka tutakapo pata ushindi dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi. Hatuwezi kuruhusu umoja wetu kuvurugwa kwa matamanio ya kufuata kanuni za vitabu vya watu fulani.”

(R. Martin, Personal Freedom and the law in Tanzania Dsm 1973)

Na kwa mara ya kwanza vifungu hivyo viliingizwa katika katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 katika marekebisho yake ya mwaka 1984 (Constitutional Amendment Act, No 15 1984) Hata hivyo vifungu hivyo vya baadhi ya haki za binadamu viliambatana na masharti, mipaka, vizuizi nk. (claw back clauses ). Mipaka, vizuizi na msharti yaliyoambatana na vifungu hivyo vilipelekea mpaka baadhi ya magwiji wa sheria wakaviita vifungu hivyo kuwa ni vifungu vya ‘ shuruti’ na mipaka na sio vifungu vya haki msingi za binadamu.

Ukiangalia kwa makini suala la kuingiza vifungu vya haki za binadamu ndani ya katiba katika mihula yote minne. Kuanzia wakati wa wakoloni, baada ya uhuru wa bendera, kipindi cha mpito ambapo baadhi ya vifungu viliingizwa na katika kipindi cha jaribio lililofeli la maandalizi ya inayoitwa katiba mpya. Kimsingi mihula yote minne inawiana. Wakoloni walikataa fikra za ‘haki za binadamu’ ndani ya katiba kwa maslahi yao ya ukoloni na unyonyaji, na walipozitaka katika kipindi cha kutoa uhuru pia ni kwa ajili ya kulinda maslahi yao. Vivo hivyo watawala wazalendo mara baada ya uhuru wa bendera nao walikataa vifungu hivyo kutokana na uchu wao wa madaraka, wakitoa kisingizio cha kusababisha migongano baina ya serikali na mahkama. Pia hata hapo watawala wazalendo walipokubali kuingizwa baadhi ya vifungu hivyo vya haki hizo walikubali lakini viliwekewa masharti, vizuizi na mipaka mingi kiasi cha kushindwa vifungu hivyo kufanya kazi ipasavyo. Na katika hata katika jaribio lilofeli la rasimu ya katiba mpya, ukiangalia kwa jicho la uadilifu utaona vifungu vyote vilivyoingizwa ati kudhamini zinazoitwa ‘haki za binadamu’ kimsingi hakuna tofauti na katiba ya mwaka 1977 kutokana na kufungwa kwa masharti, mipaka, vizingiti, na vizuizi kadhaa wa kadhaa, isipokuwa vizuzi katika rasimu ya katiba iliyofeli viko tofauti kidogo na katiba ya mwaka 1977, kwa kuwa mipaka, masharti, vizingiti na vizuizi hivyo vya kudhibiti haki hizo vimewekwa katika sura ya kijanja zaidi.

Kwa hivyo, hakuna mahala ambapo ‘haki za binadamu’ zitadhaminiwa kikweli, iwe na madola makubwa ya kibepari, Umoja wa mataifa, mataifa machanga katika katiba zilizotangulia amma zitakazokuja, kwa kuwa fikra yenyewe ni ya uwongo katika msingi wake na katika utekelezaji wake.

Mfumo wa kibepari unajidanganya na unadanganya wanaadamu katika kumangalia mwanadamu kwa ufinyu sana. Wamemuangalia mwanadamu kimakosa na kuzaaa fikra ya haki za binadamu ambayo msingi wake ni wa kimakosa na haikubaliani na uhalisia. Isitoshe haki wanazonadi kuwa haki za binadamu ni zile ambazo sio tishio kwa mfumo wao. Haki ya kuzini, haki ya kuwa shoga, haki ya kulewa nk. Na kila siku haki hizo zinadhirisha unafiki na zinaongezwa mipaka hususan. Mifano hai ni namna nchi za kibepari wanavyopambana na hijabu na niqab ilhali huo ni uhuru wa imani na uhuru binafsi wa mtu, au katika mapambano yao dhidi ya Uislamu kwa jina la vita vya ugaidi. Hakuna haki hata moja inayoheshimiwa.

Upande mwengine, wakati mfumo wa kibepari ukihubiri ‘ haki za binadamu’ unafanya ujanja wa wazi kwa kuweka mianya mbalimbali ili kuweza kuitumia kwa kuzigeuza haki hizi juu chini, chini juu, lau kuna tishio upande wao na serikali zao. Ndio maana ukaona kisingizio cha maslahi ya umma, usalama wa taifa nk vimewekwa tayari tayari kama kinga lau kuna haja ya kukitumia kuuhifadhi mfumo, mtawala na serikali yake.

Uislamu uko wazi kwamba mwanadamu hayuko huru kwa kuwa mahusiano yake na Muumba wake ni mahusiano baina ya Bwana na mtumwa. Kwa hivyo, liliopo juu ya mwanadamu ni kutii tu. Ubepari unanadi kuna uhuru kumbe ni udanganyifu. Uhuru unaonadiwa na demokrasia sio kwa mujibu unavyotaka wewe bali kwa namna unavyotaka mfumo wa kibepari. Ajabu bado unaambiwa uko huru. Uhuru huu anapotukanwa Mtume SAAW ni uhuru wa maoni lakini zinapotolewa siri za nchi huwa sio uhuru tena. Hapo husemwa maslahi ya Umma na usalama wa nchi umehatarishwa.

Umefika muda Waislamu na wanadamu kwa jumla kuuvurumisha mfumo wa kibepari katika jalala la kihistoria kwa mbadala wa mfumo mwengine wa haki ili kujikomboa na uwongo, dhulma, idhilali na ukandamizaji wake usio na mfano.

وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلاَّ فِي ضَلاَلٍ (الرعد: 14

“Na mwito wa makafiri hauko ila katika upotofu” (TMQ 13:14)

#UislamuNdioUfumbuziSahihi

Masoud Msellem

Risala ya Wiki No. 66

13 Rabi’ al-thani 1441 Hijri 10/12/2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.