Ummah Wangu Utagawanyika Makundi Sabiini na Tatu

بسم الله الرحمن الرحيم

Maana ya Hadithi:

«وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً»

“Ummah wangu utagawanyika makundi sabiini na tatu.”

Kwa Abdullah Omar

Swali:

Assalamu Alaykum Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu

Mimi ni Abdullah kutoka Afghanistan, Mwenyezi Mungu akulinde Sheikh wetu,

Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«ستنقسم أمتي إلى ثلاثة وسبعين فرقة وكلها في النار ما عدا واحدا»

“Umma wangu utagawanyika makundi sabini na tatu na yote yataingia motoni isipokuwa kundi moja tu .”

Natumai utaielezea Hadithi hii.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu,

Kwanza: Hadithi unayoiulizia haisimuliwi katika muundo uliowasilishwa katika swali lako, na tulikuwa tumeiweka wazi hadithi hii katika Swali na Jibu lililochapishwa mnamo 24 Rabii ‘ul-Akhir 1439 Hijria sawa na 11/01/2018 Miladia, katika mapokezi kadhaa, ambayo mengine ni pamoja na nyongeza tofauti, na tulihitimisha mwishoni mwa jibu kuwa: (hadithi inayohusu mgawanyiko wa Ummah katika madhehebu 73 bila nyongeza yoyote ni hadithi sahihi… na kwamba hio nit oleo  kwanza:

كلها في النار إلا واحدة “Yote yataingia motoni isipokuwa kundui  moja tu “ imezingatiwa na wengi kuwa ni hasan… ama kuhusu toleo la pili:

كلها في الجنة إلا واحدة “Yote yataingia Peponi isipokuwa moja tu,” wengi wameichukulia ni dhaifu, na wachache tu wameiona kuwa ni sahih au hasan; kwa hivyo, naona ya kuwa yenye uzito zaidi ni rai ya kuwa nyongeza katika mapokezi:

كلها في النار إلا واحدة “Yote yataingia motoni isipokuwa moja” inakubaliwa, ama kwa hile inayoelezea:

كلها في الجنة إلا واحدة “Yote yataingia Peponi isipokuwa moja,”  haikubaliki, hii ni kwa kurejelea yale tuliyotoa katika masimulizi yanayojumuisha nyongeza zote mbili…) Na kulingana na yale tuliyoyataja katika jibu la swali lililotajwa hapo juu. Kati ya masimulizi yanayoweza kutegemewa na kutiliwa maanani ni masimulizi yafuatayo:

– Tirmidhi ameripoti katika Sunan yake kwamba Abu Hurayrah (ra) amesimulia: Mtume (saw) amesema:

«تَفَرَّقَتْ الْيَهُودُ عَلَى إِحْدَى وَسَبْعِينَ أَوْ اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً وَالنَّصَارَى مِثْلَ ذَلِكَ وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً»

“Mayahudi waligawanyika katika makundi sabini na moja au sabini na mbili; na Wakristo waligawanyika mfano wa hivyo; na Ummah wangu utagawanyika katika makundi sabini na tatu.”

”Na katika mlango huo huo, Sa’d na Abdullah ibn Amr na ‘Awf ibn Malik walisema: Abu Issa alisema: Hadithi ya Abu Hurayrah ni Hasan Sahih. Katika riwaya nyingine ya Tirmidhi kwamba Abdullah ibn Amr amesema: Mtume (saw) amesema:

«… وَإِنَّ بَنِي إِسْرَائِيلَ تَفَرَّقَتْ عَلَى ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ مِلَّةً كُلُّهُمْ فِي النَّارِ إِلَّا مِلَّةً وَاحِدَةً قَالُوا وَمَنْ هِيَ يَا رَسُولَ اللَّهِ قَالَ مَا أَنَا عَلَيْهِ وَأَصْحَابِي»

“…Bani Isra’il waligawanyika katika mila (makundi) 72, lakini watu wangu watagawanyika katika mila (makundi) 73, yote yataingia motoni isipokuwa moja tu.” Alipoulizwa ni lipi, alijibu, “Ni lile ambalo mimi na Masahaba wangu tupo.” Abu Issa amesema kuwa Hadithi hii ni Hasan Gharib…

– Al-Hakim katika Al-Mustadrak ameripoti katika sahih mbili kwamba Abu `Amir Abdullah bin Luhay amesema;

حَجَجْنَا مَعَ مُعَاوِيَةَ بْنِ أَبِي سُفْيَانَ… ثُمَّ قَامَ حِينَ صَلَّى الظُّهْرَ بِمَكَّةَ، فَقَالَ: قَالَ النَّبِيُّ ﷺ: «إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابِ تَفَرَّقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً، وَتَفْتَرِقُ هَذِهِ الْأُمَّةُ عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ كُلُّهَا فِي النَّارِ إِلَّا وَاحِدَةً وَهِيَ الْجَمَاعَةُ…»

“Tulifanya Hija na Mu`awiyah bin Abi Sufyan. Tulipofika Makka, alisimama baada ya kuswali Dhuhr na akasema; ‘Mjumbe wa Allah (Salallahu alaihi wasallam) amesema: “Hakika watu wa Kitabu wamegawanyika katika dini yao makundi (millah) sabini na mbili, na umma huu utagawanyika makundi sabini na tatu yote yataenda Motoni isipokuwa moja nalo ni jamaa (kundi kubwa lao)…” Al-Hakim amesema: sanad  hii ya wapokezi ni uthibitisho katika kuainisha hadithi hii kuwa ni Sahih… na Al-Dhahabi amekubaliana naye.

‘Ahlul Kitab waligawanyika katika makundi (mila) sabini na mbili. Ummah huu utagawanyika katika makundi (mila) sabini na tatu, yote yataingia Motoni isipokuwa moja, ambalo ni Jama`ah (kundi kuibwa lao). Baadhi katika Umma wangu utaongozwa na matamanio, kama yule aliyeameambukizwa na kichaa cha mbwa; hakuna mshipa au kiungo kitakachookolewa kutokana na tamaa hizi.’

– Abu Dawud katika Sunan yake, na Ibn Majah pia waliripoti riwaya kama hiyo.

Pili: maana tunayoiona ina nguvu zaidi katika Hadithi hii ni kama ifuatavyo:

 1. Vikundi na migawanyiko ya kiistilahi imetumika sana katika Sharia katika matiki ya mgongano katika Aqidah na katika chimbuko la Dini, na mgongano katika ushahidi wa hakika na wa wazi:

– Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَأُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ)

“Wala msiwe kama wale waliofarikiana na kukhitilafiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakaokuwa na adhabu kubwa.” [Aali-Imran: 105].

– Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(وَمَا تَفَرَّقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَةُ)  Wala hawakufarikiana waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia hiyo bayana.” [Al-Bayyina: 4].

– Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(إِنَّ الدِّينَ عِنْدَ اللَّهِ الْإِسْلَامُ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْياً بَيْنَهُمْ وَمَنْ يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللَّهِ فَإِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ)

Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislam. Na waliopewa Kitabu hawakukhitilafiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwasababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na anayezikataa ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.” [Aali-Imran:19]

– Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعاً لَسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُمْ بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ)

“Hakika walioigawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale waliokuwa wakiyatenda.” [Al-An’am: 159]

 1. “Kundi” hapa katika hadithi hizi inamaanisha watu wa dini ya Uislamu, na maandishi ya kisharia yamewekwa wazi ambayo yanafafanua maana hii, pamoja na Hadithi zilizowafikiwa. Abdullah ibn Mas’oud amesema: Mjumbe wa Allah (saw ) amesema:

«لَا يَحِلُّ دَمُ امْرِئٍ مُسْلِمٍ يَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَأَنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَّا بِإِحْدَى ثَلَاثٍ الثَّيِّبُ الزَّانِي وَالنَّفْسُ بِالنَّفْسِ وَالتَّارِكُ لِدِينِهِ الْمُفَارِقُ لِلْجَمَاعَةِ»

“Si halali kumwaga damu ya Muislam isipokuwa katika hali tatu: mzinifu aliyeowa, nafsi kwa nafsi, na yule aliyeiacha dini yake na kujitenga na jamaa.”

Hii ni riwaya ya Muslim. Katika hadithi hii adhimu, Mtume (saw) alielezea kuwa kujitenga  na kundi ni sawa na kutoka katika Dini na kuitupa kwa sababu alimchukulia yule anaeitupa Dini yake kuwa yupo tofauti na kundi, kwa hivyo kinachofunzwa hapa ni kwamba neno kundi kwa maana hii ni kutoamini na ni sawa na kuacha Dini na Imani (itikadi)…

– Imetajwa katika Fath Al-Bari, Sherhe ya  Sahih Al-Bukhari ya Ibn Hajar, yafuatayo:

[…kauli yake ‘yule anaeitelekeza Dini yake, akaachana na kundi’kama ilivokuja katika kauli ya Abu Dhar kwa Akashmihani na waliobaki, na ‘yule anaejiweka mbali na Dini (Mareq)’, lakini katika mapokezi ya Nasafi, Sarkhasi na Almustmli: ‘kuikataa Dini yake’ Al-Taybi amesema: yule anaeikataa Dini yake ndiye anaeitelekeza; imechukuliwa kutokana na neno “kuiasi” ambalo linamaanisha “kuacha/kutelekeza”. Katika masimulizi ya Muslim: “na yule anayejitenga na dini yake na kuachana na kundi,” na katika mapokezi ya Al-Thawri: “na yule anayeacha dini yake na kujitenga na kundi.” … na kinachomaanishwa kwa neno ‘kundi’ ni wafuasi wa Uislam, yaani amejitenga nao au kuwaacha, ikimaanisha ni muwasi, kwani uasi ni sifa ya yule aliyeondoka au kujitenga… Al-Baydawi alisema: yule anaeiacha Dini yake ni mwenye sifa dhahiri ya “Mareq” yaani yule aliyejitenga na kundi la Waislamu na kuacha safu zao…] MWISHO.

 1. Kauli yake (saw) katika hadithi tofauti: «وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي» “Ummah wangu utagawanyika,” «وَتَفْتَرِقُ هَذِهِ الْأُمَّةُ» “Ummah huu utagawanyika,” «وَإِنَّ هَذِهِ الْمِلَّةَ سَتَفْتَرِقُ» “Mila (imani) hii itagawanyika” zote ziko wazi kuwa Ummah au mila hapa inamaanisha Umma wa Uislam unaoamini dini ya Uislamu, kama Mtume (saw) alivyoongezea katika moja ya mapokezi ya neno Ummah kwake mwenyewe «أُمَّتِي» “Ummah wangu,” «هَذِهِ الْأُمَّةُ» “Ummah huu,” na «وهَذِهِ الْمِلَّةَ» “Mila hii” kwa hivyo ni wazi kwamba Hadithi inazungumzia Ummah mmoja na mila moja, Ummah wa Kiislam…
 2. Kama inavyojulikana, baadhi ya ikhtilafu katika Uislamu ni zenye kulaumiwa na nyengine ni zenye kusifiwa. Ama kwa ikhtilafu zenye kusifiwa, ni ikhtilafu katika maswala ya Ijtihad kutokana na kutofautiana katika ufahamu wa maandiko, kwa kupata kwake ujira mara mbili yule aliepatia (katika hukumu), na kulipwa mara moja kwa yule aliekosea (katika hukmu) kama ilivyotajwa katika Hadithi iliyosimuliwa na Bukhari katika Sahih yake, kwamba Amr ibn Al-Aas alimsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

«إِذَا حَكَمَ الْحَاكِمُ فَاجْتَهَدَ ثُمَّ أَصَابَ فَلَهُ أَجْرَانِ وَإِذَا حَكَمَ فَاجْتَهَدَ ثُمَّ أَخْطَأَ فَلَهُ أَجْرٌ»

“Hakimu anapohukumu akajitahidi na akapatia atapata ujira mara mbili. Anapohukumu akajitahidi kadri ya uezo wake  na kukosea atapata ujira mara moja.” Ama ikhtilafu yenye kulaumiwa, inajumuisha ikhtilafu katika Aqidah, ushahidi na hukumu za kukatikiwa, ni aina ya ikhtilafu inayomfanya mtu auasi Uislamu, aina nyingine ya ikhtilafu hii ni ile inayotokana na matakwa na matamanio kama ikhtilafu kati ya watu wa uzushi (bid’ah), wale ambao hawaamini katika uzushi wao, na pia ni pamoja na kutokubaliana juu ya imamu na utii wake, na pia aina nyengine ya ikhtilafu zenye kulaumiwa ni ambazo muhusika hatoki nje ya Uislam…

Tatu: Kulingana na uchunguzi uliotajwa hapo juu na kwa kuuzingatia, tunaweza kuelewa Hadithi tukufu juu ya mgawanyiko wa Wayahudi na Wakristo na mgawanyiko wa Umma wa Uislamu … na maelezo yake ni kama ifuatavyo:

 1. Allah (swt) alimtuma Musa (AS) na dini ya ukweli kwa Bani Israil, wale waliomwamini na wakawa pamoja naye kwenye ‘Aqidah ya ukweli na Tawhiyd wamekuwa ni watu wa imani moja (millah).. hata hivyo, baadhi ya vikundi vya watu walijitenga na imani hii kila muda ulivyosonga, wakitofautiana nayo katika Dini «إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابِ تَفَرَّقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً» “Watu wa kitabu wamegawanyika katika Dini yao makundi (milla/itikadi) sabiini na mbili,” wakitengana na imani yake, ushahidi na dini wazi ya Musa (AS), wakiiwacha Dini yake na kuwa makafiri. Makundi hayo yalioacha Dini ya Musa yakawa makundi tofauti na yenye maoni tofauti katika uasili wa Dini (aqidah)  «إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابِ تَفَرَّقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً» “Watu wa kitabu wamegawanyika katika Dini yao makundi sabiini na mbili,” wamefikia milla sabini au sabini na moja, ambayo yote ni makundi yasioamini ya watu wa motoni, ama kwa kundi lililobakia kwenye Dini ya Musa (AS), yaani imani ya Musa (AS), ambalo ni kundi la 71 au la 72, ni kundi lililo juu ya ukweli na ni katika watu wa Jannah, na ni kundi lililookoka (Firqa Najiyah) kutoka kwa wafuasi wa Nabii wa Allah, Musa ( AS)…
 2. Pia, Allah (swt) alimtuma Issa (AS) na dini ya ukweli kwa Bani Israil, wale waliomwamini na kukusanyika pamoja naye kwenye Aqidah ya ukweli na Tawhid wakawa ni watu wa imani moja (millah).. lakini, makundi ya watu waliojitenga na imani hii kidogo kidogo, wakitafautiana nayo katika Dini, wakitengana na imani yake, ushahidi na Dini ya wazi ya Issa (AS), wakaiacha Dini yake na kuwa makafiri. Makundi hayo yaliyoiacha Dini ya Issa (AS) na kuwa makundi tofauti yenye maoni tofauti katika asili ya Dini (aqidah) yamefikia makundi sabini na moja, yote ni makundi ya watu wasioamini ya watu wa motoni, ama kwa dhehebu lililobakia juu ya Dini ya Issa (AS), yaani imani ya Issa (AS), ambalo ni kundi la 72, liko juu ya haki na ni katika watu wa Jannah, na limekuwa ni kundi lililookoka (Firqa Najiyah) kutoka kwa wafuasi wa Nabii wa Allah Issa (AS)…
 3. Baadae Mwenyezi Mungu (swt) alimtuma Nabii wake Muhammad (saw) kwa Dini ya haki na ‘Aqidah ya Tawhid, Waislamu walimuamini na wakaungana juu ya ‘Aqidah ambayo Mtume (saw) na masahaba wake watukufu waliiamini, na kwa umoja huu, wakawa Umma wa Kiislam na imani ya Uislamu na Jama’ah (kundi)… lakini makundi yalikengeuka (na yataendelea kukengeuka) kutoka kwa Dini ya Muhammad (saw), na yamejitenga (na yatajitenga) na kile ambacho Mtume (saw) na masahaba zake na Waislamu wengine wameamini katika ‘Aqidah ya Uislamu na Nusus za wazi na dalili za Uislamu … kwa hivyo, kila moja ya madhehebu hayo yaliojitenga na Uislamu limekuwa kundi na imani inayotafautiana na imani ya Uislamu, kwa sababu waliamini imani ambazo ni kinyume na za Uislamu… makundi hayo ambayo wafuasi wao walikuwa Waislamu kisha walijitenga na Uislamu yamefikia au yatafikia makundi/imani 72, na yote ni makundi ya kufr na ni ya watu wa motoni… kundi/imani(millah) ya 73, kundi mama, ambalo ni kundi (jama’ah) na dhehebu la Uislamu ambalo linaamini kile ambacho Mtume (saw) na masahaba watukufu waliamini, wakishikamana na Nusus za wazi na dalili za Uislamu, ni Umma wa Uislamu ambao unamuamini Mwenyezi Mungu (swt), Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, Siku ya Mwisho na Qadhaa Wal-Qadar – kizuri chake na kibaya chake ni kutoka kwa Allah (swt)… ni Ummah wa Uislam kwa jumla, kundi lililookoka (al-Firqa Al-Najiyah ) na ni katika watu wa Jannah, kundi na aqida iliyounganishwa juu ya yale ambayo Mtume (saw) na masahaba wake wameibeba, nalo ni (kundi) Jama’ah.

Nne: Kulingana na ufafanuzi huu wa maana ya hadithi na uhalisia wake, tunaweza kuhitimisha kwa yafuatayo:

 1. Kundi lililookolewa (al-Firqa al-Najiyah) ni Ummah wa Kiislamu kwa maana yake ya jumla, nao ndio uliokusanyika juu ya ‘Aqidah ya Uislamu na uwazi wa Dini na dalili zake, bila kujali tofauti kati ya rai zao, fikra, na madhehebu juu ya masuala yote ya matawi ya imani na matakwa ya Shari’ah… nk, na sababu ya kudumu kwake na kuwa kundi la watu wa Jannah ni imani yao katika ‘Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na ushahidi wake… Na hivyo hivyo:
 2. a) Ahlul-Sunnah wal Jama’ah miongoni mwa watu wa kauli (kalam), kama Ash’ari, Maturidiyya, na mapote yote mengine ya kifikra, pamoja na wale wanaoitwa “Salafi”, watu wa hadithi, na waandishi wengine wa makala na makundi ya fikra za Kiislam… wote ni katika Al-Firqa Al-Najiyah kwa neema ya Mwenyezi Mungu (swt) kwa sababu wao ni wafuasi wa Muhammad (saw), waumini wa ‘Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na ushahidi wake … na tofauti kati yao haziwatoi katika kundi la Uislamu.
 3. b) Na madhehebu tofauti za fiqhi za Hanafi, Maliki, Shafi’i, Hanbali na madhehebu nyengine za fiqhi, na wafuasi wa mujtahidi anuwai … wote hao ni miongoni mwa watu wa kundi lililookolewa, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu (swt), kwa sababu wao ni wafuasi wa Muhammad (saw), waumini wa ‘Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na dalili… na tofauti kati yao haiwatoi katika kundi la Uislamu.
 4. c) Na makundi ya Kiislamu na harakati za Kiislam zinazofanya kazi katika medani za wakati wetu, kama Hizb ut Tahrir, Udugu wa Kiislam, Kundi la Tabligh, makundi ya jihadi, makundi ya Salafi, na mengineo… yote ni kutoka kwa watu wa kundi lililookolewa, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu (swt), kwa sababu wao ni wafuasi wa Muhammad (saw), waumini wa ‘Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na dalili… na tofauti kati yao haiwatowi katika kundi la Uislamu.

Kwa hivyo, sio sahihi kwa kundi lolote la Ummah wa Uislam kudai, kwa msingi wa hadithi hii tukufu, kwamba ni kundi lililookolewa na dhehebu lililookolewa kwa sababu hii itamaanisha kuwa inawaondoa Waislamu wasiokubaliana nayo kutoka kwenye duara la Uislam na kuingia ndani ya duara la wasioamini, na hii sio sawa katika hali yoyote, kwa sababu Waislamu wote ambao wanaamini ‘Aqidah ya Uislamu, wanaozingatia uhakika na ushahidi wake ni katika kundi lililookolewa, kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu (swt).

 1. Mapote yaliyoacha kundi la Uisilamu na wakawa makafiri na hivyo kustahili kuwa makundi ya watu wa Motoni, ni makundi yaliokiuka Dini na kuachana na imani (Aqidah) ya Waislamu na kuvuka mipaka ya Uislamu na uhakika wake na dalili, kwa hivyo wamemshirikisha Mwenyezi Mungu (swt) na vitu vyengine au wakamfuata mtume baada ya Muhammad (saw) au kukataa Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu au mfano wake… kama wa-Druze, wa-Nusayri, ma-Bahai, ma-Qadiani na makundi mengine ya kikafiri nje ya Uislamu… na wenziwao kutoka kwa Mayahudi waliokengeuka kutoka dini ya Musa, amani iwe juu yake, watu waliomfanya ‘Azeez, amani iwe juu yake, mwana wa Mungu, na miongoni mwa wafuasi wa Issa, amani iwe juu yake, waliomfanya kuwa mwana wa Mungu … kwa hivyo watu hao walibadilika katika imani zao dhidi ya imani na dini ya Manabii hawa wawili mashuhuri, kwa hivyo wakawa makafiri.

Natumai kuwa maana ya hadithi imekuwa wazi kwa ufafanuzi huu, na Mwenyezi Mungu (swt) ni mwenye kujua zaidi na ndiye Mwenye Hikima.

Ndugu yako,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta

Maoni hayajaruhusiwa.