Ukombozi (Fathi) wa Andalus

بسم الله الرحمن الرحيم

Moja kati ya matukio makubwa yaliyotokea katika tareekh ya Kiislamu ndani ya mwezi kama huu mtukufu wa Ramadhani ni tukio la Fathi (ufunguzi) wa biladi ya Andalus.
Andalus ni neno la kiarabu lenye kumaanisha maeneo ya Ukanda wa Iberia (Iberian Peninsula), maeneo yanayojumuisha ardhi ya Hispania (Spain) na Ureno (Portugal).

Ilikuwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka wa 93 Hijria sawa na mwaka 711 miladi ndipo Fathi ya Andalus ilipotekelezwa kwa mapana katika zama za Khalifah Al-Walid Ibn Abdul-Malik, mwishoni mwa Khilafah ya Bani Ummayah wakati alipomuagiza Wali (Gavana) wake wa Wilaya ya Afrika ya Magharibi Mussa Ibn Nusayr kutekeleza amali hiyo adhimu. Ibn Nusayr nae akamuamuru Jemadari wake Tariq Ibn Ziyad (ambae awali alikuwa mtumwa wake kabla ya kukombolewa na kuwa huru) kuaandaa jeshi la Waislamu kwa jihadi ya kuifungua Andalus.

Kikosi cha wanajeshi kilichojumuisha Waislamu mbalimbali wakiwemo waarabu, mabar-bara na wengineo chenye askari kati ya elfu kumi na mbili hadi elfu kumi na saba kiliandaliwa kwa jukumu hilo tukufu. Kikosi hicho kilipokuwa safarini kuelekea Andalus wakati kikivuka bahari ya Mediterenia baina ya Afrika na Bara la Ulaya na wakati kamanda wake Tariq Ibn Ziyad alipokuwa kajipumzisha na kuchukuliwa na lepe la usingizi alimuota Mtume (SAAW) akiwa pamoja na maswahaba zake, Muhajirina na Answari wakiwa wamewazunguka na silaha zao (panga na mishale), Mtume (SAAW) akamueleza Jemadari Tariq Ibn Ziyad:

“Kuwa jasiri, ewe Tariq! Likamilishe lengo uliloliazimia”

Baada ya Ibn Ziyad kuzindukana kutoka usingizini kusikia kauli ya Mtume (SAAW) ndani ya ndoto ile alijawa na tabasamu kubwa, kwani alikuwa hana tembe ya shaka kwamba Allah Ta’ala atampa Nusra Yake katika fathi hiyo.
Jeshi la Waislamu chini ya Jemadari Tariq likatia nanga katika mwezi wa Aprili mwaka wa 711 miladi usiku kimya kimya kwa siri na hadhari kubwa bila ya kuonekana na kufikia kwenye mlima uliokuwa karibu na bahari (kama kisiwa) uliokuja kuitwa kwa jina la Jabal al-Tariq (mlima wa Tariq) kwa heshima ya mkombozi huyu, mlima ambao leo umebadilishwa jina na kuitwa ‘Gibraltar’. Waislamu waliufanya mlima huo kuwa nukta kianzio cha mashambulizi (base) yao ya kuifungua Andalus.

Mara baada ya jeshi la Waislamu kushuka kutoka katika mashua zao katika sehemu hiyo, Kamanda Tariq Ibn Ziyad akachukuwa hatua ya kijasiri ya aina yake kwa kuzichoma moto mashua zote walizopanda kufikia hapo na akalieleza jeshi lake bayana kwamba: Chaguo ni moja tu katika mawili. Amma waifungue Andalus au wafe mashahidi katika njia ya Allah Ta’ala.

Mfalme Roderick aliyekuwa mtawala wa Andalus alipopata taarifa juu ya uvamizi huu nae akaandaa jeshi kubwa la askari laki moja (100,000) ili kukabiliana na jeshi la Waislamu. Kwa majivuno na tamaa ya kuliangamiza mara moja jeshi dogo la Waislamu ukilinganisha na jeshi lake kubwa akaamua kulifuata jeshi la Waislamu.

Jeshi la Roderick likasonga mbele na kufunga kambi katika eneo la Qurtuba (Cordoba) ili kumvamia Tariq na jeshi lake. Hata hivyo awali Mfalme Roderick alichukuwa hadhari kwa kutuma majasusi wake mahiri na werevu kufanya ujasusi kwa jeshi la Waislamu ili aweze kugunduwa ukubwa wa jeshi la Waislamu na kiwango cha maandalizi waliyoyafanya. Jemadari Tariq alipopata fununu ya taarifa hii ya Mfalme akatumia mbinu kabambe ya kuwadanganya na kuwaghilibu majasusi wa Mfalme Roderick. Ibn Ziyad kwa umahiri na ushupavu akaliagiza jeshi lake lote wajifanye kama wanachimbua maiti za watu na kujifanya kama wanazila maiti hizo. Baada ya majasusi wa Roderick kuyashuhudia hayo walirudi haraka kwa khofu na kuchanganyikiwa na kumpa taarifa hiyo kwa upana Mfalme wao Roderick ambae nae pia alishtuka na kupatwa na khofu kubwa.

Kabla ya vita kuanza Tariq alilikhutubia jeshi la Waislamu, kwa kuwahimiza, kuwahamasisha na kuwapa moyo wa kupigana Jihad. Yeye binafsi akaweka azma ya kumuua Mfalme Roderick kwa mkono wake. Baada ya khotuba yake, Waislamu wakavaa mavazi ya kivita wakiwa na panga na mishale yao na kujimwaga kwa ujasiri na ushujaa kati kati ya medani ya vita. Yasemekana Tariq alifanikiwa kumuuwa Mfalme Roderick kwa kumrembea mshale na hivyo kuweza kutimiza azma yake aliyoikusudia. Kitendo hichi cha kuuliwa Mfalme Roderick kiliwachanganya vibaya wanajeshi wa kikristo na jeshi lao. Wakaanza kukimbia kimbia ovyo kwa lengo la kuokoa maisha yao. Waislamu wakautumia vyema mwanya na udhaifu huu kwa kushirikiana na baadhi ya raia wa kikiristo na mayahudi waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukandamizaji za mtawala wao. Kwa hivyo Waislamu wakaweza kupata ushindi kiurahisi na kuuchukuwa mji wa Qurtuba, Archidona, Elvira na kusonga mbele hadi mji mkuu wa Toledo. Jeshi la Waislamu likaweza kuingia ndani ya Andalus kiasi cha maili mia mbili na khamsini magharibi ya nchi. Hali hiyo ikapelekea jeshi la Kiislamu kupata machofu na kudhoofika kutokana na safari ndefu. Jemadari Tariq Ibn Ziyad alipowaona askari wake wamechoka taabani akawaeleza:

“Naapa kwa Allah, lau ningekuwa nasukumwa na rai yangu pekee, ningekwenda mchaka mchaka na kusonga mbele hadi katika milango ya Roma au ya Konstantiniya ili tuifunguwe miji hiyo kwa idhini ya Allah, lakini kwa kuwa mumechoka na kudhoofika basi rudini.”

Waislamu si tu wakaiteka Andalus (Spain) lakini katika kipindi cha miaka kumi waliweza kusonga mbele hadi kuichukuwa sehemu kubwa ya kusini mwa Ufaransa mpaka katika mwaka 732 miladi walipozuiwa na kiongozi wa Ufaransa Charles Martel.

Waislamu wakaibadilisha haiba ya Andalus kiasi kwamba chini ya mtawala Abdul-Rahman III waliweza kujenga mji bora kabisa kwa jina la ‘Az-Zahra’, ujenzi uliochukuwa karibu miaka arubaini. Nchi hiyo pia ikafanywa kuwa kituo muhimu na kitovu cha elimu ya dini na ya dunia kiasi cha kupatikanwa wanavyuoni wakubwa na mashuhuri wa Kiislamu kama vile Imam Al-Qurtubi na wengineo. Raia wa nchi mbali mbali hususan bara la Ulaya ambao bado nchi zao zilikuwa kizani walikuja Andalus (Spain) kujifunza elimu mbali mbali kwa Waislamu. Chini ya Mtawala Al-Hakam II kulijengwa maktaba kubwa ndani ya Qurtuba (Cordova) iliyokusanya maelfu ya vitabu. Mtawala Abdul-Rahman I akanunua kwa dinari laki moja za dhahabu Kanisa la zamani la Qurtuba kutoka kwa makasisi wa kikatoliki kwa khiyari yao na kuufanya msikiti mkuu wa Qurtuba uliotanuliwa na watawala mbalimbali waliofuatia.

Raia ndani ya Andalusia walistajaabishwa na kushangazwa sana na namna Waislamu walivyoamiliana nao kwa haki, ukarimu, insafu na uadilifu kinyume na ukandamizaji na dhulma za watawala wa kikatoliki waliotangulia. Wakristo wakaruhusiwa kuendelea na ibada za dini yao bila ya kubughudhiwa ndani ya mipaka ya sheria za Kiislamu na kulipa jizya kwa mwenye uwezo. Kadhalika mayahudi ambao nao awali chini ya utawala wa wakatoliki waliokuwa raia wa daraja duni kwa kuchukiwa, kunyanyaswa na kufanyishwa kazi duni na ngumu za vibarua, sasa chini ya utawala wa Waislamu wakaishi maisha ya furaha na utulivu kiasi cha Profesa Graetz kunukuuliwa kutoka katika kitabu chake ‘History of the Jews’ aliposema:
“..Wakati wakiristo wakiwa katika makanisa yao wakifanya ibada kuomba usalama wa nchi yao na dini yao, mayahudi kwa upande wao walikuwa wakiwafungulia milango mashujaa wa kiarabu, wakiwapokea kwa nderemo wakiona wakati muwafaka wa kulipiza kisasi kutokana na mashaka waliyokuwa wakifanyiwa’.

…Katika hali kama hii mayahudi ambao awali walikuwa vibarua sasa walikuwa mabwana katika miji ya Cordoba, Granada, Malaga na mengineyo.”
(A.Thomson na M. Ata’ur- Rahman, Islam in Andulus, Revised Edition, uk. 20)

Kwa msiba mkubwa baada ya Waislamu kuitawala Andalus kwa karibu karne nane, makafiri wameweza kutunyang’anya ardhi hii nyeti kwa fedheha na idhilali isiyoelezeka kiasi cha msikiti wetu mkubwa wa Qurtuba (Cordova) kufikia kugeuzwa kanisa baada misikiti yote kufungwa. Hayo yaliweza kutokea kutokana na watawala wa Kiislamu ndani ya Andalus kugubikwa na ubinafsi, kushindwa kwa watawala waliofuatia baadae kuwaunganisha vyema raia kwa kuwadogosha Waislamu wasiokuwa ‘waarabu’ na kushughulishwa na starehe za kidunia. Sambamba na kutokea hayo Khilafah iliyotarajiwa kuyatibu kwa haraka na kimsingi nayo ilisibiwa na udhaifu mkubwa, ilibweteka, na kugubikwa na mapungufu makubwa ya kiutawala (maladminstration) kutokana na kuanguka kifikra.

Pamoja na Umma kuporwa ardhi zake ikiwemo Andalus na nyenginezo lakini bado haukufilisika kifikra wala hauna uhaba wa wabebaji wenye ikhlasi. Kwa hivyo jukumu kubwa lililopo mabegani mwetu leo ni kuirejesha tena Khilafah Rashidah ili izikomboe ardhi zetu zote tulizoporwa na kuzilinda imara kwa kuepusha makosa yaliyotangulia yasitokee tena. Na kufungua zaidi na zaidi ardhi nyingine mashariki na magharibi ya Ulimwengu ili kutekeleza lengo la kutumwa Mtume (SAAW) kwetu sote.

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلاَّ رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ
“Na hatukukutuma wewe ila (uwe) Rehma kwa ulimwengu wote” [TMQ 21:107]

21 Ramadhan 1441 Hijria

Muhija Zubeir na Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.